Bismillahir Rahmanir Rahim

                                   

Bara Arabu:

           

            Bara Arabu katika ramani ya ulimwengu wa kale kabla ya kugunduliwa Umarekani ni sehemu ya ardhi iliyoko katikati baina ya Bara la Afrika na Bara la Ulaya na Bara la Asia.

 

            Kuwepo kwa Bara Arabu kwenye sehemu kama hii kumeipa umuhimu mkubwa kabisa na kuifanya kama moyo kwa kiwiliwili, kwani ni sehemu ambayo imetawala mapitio muhimu sana ya bahari za ulimwengu wa kale. Ili kufika Arabuni au Bara Arabu kama ilivyokuwa ikijulikana zamani, ni lazima kupitia mapitio haya kabla ya kuendelea na safari yako kwenda Afrika, Asia au Ulaya.

 

            Mapitio haya ambayo leo yanaendelea kuwa na umuhimu mkubwa kabisa duniani ni Bahari Nyekundu (Red Sea), na Bahari ya Waarabu (Arabian Sea) ,na Ghuba la Uajemi (Uarabu) (Persian (Arabian) Gulf), na ndio yaliyoifanya Bara Arabu kuwa ni sehemu muhimu kabisa kibiashara, kiuchumi na kisiasa, katika hali ya vita au amani.

 

            Aidha, kwa sababu ya umuhimu mkubwa kama huu ndio maana Mwenyezi Mungu akaijaaliya Bara Arabu kuwa ni shina la biashara, uchumi na dini yake ya Uislamu, na ndio maana vile vile ikawa ni sehemu inayopiganiwa na umma mbali mbali ikiwa hapo zamani baina ya Wafursi na Warumi au sasa baina ya Wamarekani na Wazungu wengineo.

 

Waarabu:

 

            Hapo zamani za kale kulikuwa kuna Waarabu waliokuwa wakiishi Bara Arabu na walikuwa ni watu wenye nguvu nyingi na majenzi ya ajabu kama yale yaliyojengwa na kaumu Hud yenye nguzo ndefu zatiti au yaliyojengwa na kaumu Saleh kwa kuchonga majabali. Kaumu hii ya Hud iliyokuwa ikijulikana kwa jina la A'd na kaumu Saleh iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Thamud ,ziliangamizwa na Mwenyezi Mungu kwa dhambi na maasiya yao na kuleta badala yake kaumu nyengine.

 

            Anasema Mwenyezi Mungu aliyetukuka:

 

            Kwani hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya kina A'di

            Wa Iram, wenye majumba yenye nguzo ndefu?

            Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi?

            Na Thamudi ambao walichonga majabali huko bondeni

            Na Firauni mwenye vigingi? (Mapiramidi?)

            Ambao walifanya jeuri katika nchi?

            Wakakithirisha humo ufisadi?

            Basi Mola wako aliwapiga mjeledi wa adhabu.

            Hakika Mola wako yupo daima macho.

                                                                                      Sura: Al-Fajr:6-14.Fajr

 

            Baada ya kuangamizwa kaumu mbili hizi zilizokuwa zikiishi Bara Arabu, Waarabu wote waliobakia wanahesabiwa kuwa wanatokana na kizazi cha Qahtan ambao asli yao na nchi yao ni Yemen. Waarabu hawa walikuwa wakiishi kwenye sehemu nzuri ya nchi yenye mabustani na mashamba mazuri mazuri na walikuwa katika neema kubwa lakini pia walikufuru na kumfuata Iblisi na Mwenyezi Mungu hamuachi mwenye kukufuru na kudhulumu nafsi yake basi akawaletea adhabu yake baada ya kuwa katika raha na furaha.

 

           

            Hakika kulikuwa na ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika  

            maskani yao: Bustani mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya

            Mwenyezi Mungu, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Msamehevu

            Lakini wakaacha. Tukawapelekea mafuriko makubwa, na   

            kuwabadilishia badala ya bustani zao hizo, bustani nyengine

            zenye  matunda makali machungu, na mivinje, na kidogo katika miti

            ya kunazi Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyokufuru.

            Nasi kwani tunaadhibu isipokuwa anayekufuru?

                                                                                   Sura: Saba:15-17

 

            Waarabu hawa baada ya kuvunjika boma la Maarib lililokuwa likizuilia ziwa kubwa la Maarib na kunyweshea mashamba na mabustani yao, walitawanyika na kuhamia sehemu mbali mbali za Arabuni. Wengine wakaelekea Shamu na wengine wakenda Iraq na Hijaz na Oman kutafuta riziki na maisha mapya.

 

            Miongoni mwa makabila muhimu ya kizazi cha Qahtani ni Himyar na Kahlani na kutokana na Kahlani lilitoka kabila la Azd ambalo watoto wake wenye umuhimu mkubwa katika tarehe ya Uislamu ni Aus na Khazraj ambao makabila yao ndiyo yaliyokuwa yakiishi Madina kabla ya kuhamia Mtume Muhammad (SAW), na kadhalika kabila la Jurhum ambalo lilihamia sehemu za Hijazi na kuteremkia katika bonde la Makka zama za Nabii Ismail.

 

            Kabila la Qureshi linatokana na kizazi cha Nabii Ismaili mwana wa Nabii Ibrahim ambaye alipelekwa Makka yeye pamoja na mamake Hajar akiwa bado mchanga na kuachwa katika bonde kavu lisilokuwa na chochote hapo Makka. Hajar alishangazwa sana na kitendo hiki lakini baada ya kujua kuwa ni amri inayotokana na Mwenyezi Mungu alitulia moyo wake kwa kujua kuwa Mola wake bila shaka hatomtupa. Huku nyuma Nabii Ibrahim aliondoka akiwa na huzuni lakini alikuwa na yakini kuwa Mwenyezi Mungu Mola wake hamtakii ila la kheri kwa mtihani huu, basi akaomba:

 

            Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya kizazi changu

            katika bonde lisilo mimea, kwenye nyumba yako takatifu,

            ewe Mola wetu ili washike Sala. Basi jaalia nyoyo za watu

            zielekee kwao, na uwaruzuku matunda, ili wapate kushukuru.

                                                                                         

                                                                                 Sura: Ibrahim:37

 

            Hajar alibakia na mwanawe mchanga baada ya kuondoka Nabii Ibrahim na kuanza kuangaza huku na huku asaa ataona dalili yoyote ya maji au aina yoyote ya uhai, lakini kwa kuwa ni bonde tupu katikati ya jangwa alianza kukimbia huku na huku akipanda mlima wa Safa na kuangaza kisha akenda mbio mpaka juu ya mlima wa Marwa na kuangalia kama ataona chochote kwa mbali. Alifanya hivi mara saba bila kuona kitu lakini aliporudi kwa mwanawe alikuta chemchemu ya maji iliyotimbuka karibu na miguu ya Nabii Ismaili akafurahi sana na kumshukuru Mola wake. Chemchemu hii ndio hii chemchemu ya Zamzam ambayo mpaka leo inatumika na mamilioni ya wakaazi wa Saudia na mahujaji wanapokwenda kuhiji Makka.

 

            Kabila la Jurhum lililokuwa likipita karibu na bonde la Makka lilistaajabu kuona ishara za uhai katika bonde hili na lilipokaribia na kuona maji lilimuomba Hajar kufanya maskani hapo. Hajar alifurahi sana kupata watu wa kuishi naye na alipokuwa Ismaili mkubwa alioa katika kabila hilo na kuleta kizazi chake ambacho kitakuja kuwa na umuhimu mkubwa hapo Makka na ulimwengu mzima kwa jumla.

 

            Katika kizazi cha Nabii Ismail ni Adnan ambaye ndiye babu wa mababu wa makabila ya kikureshi, na kutokana na Makureshi wanatoka Bani Hashim na kutokana na Bani Hashim wanatoka Bani AbdulMuttalib na katika watoto wa AbdulMuttalib ni Abdullah ambaye ni babake Mtume Muhammad (SAW).

 

Amesema Mtume (SAW(: Hakika Mwenyezi Mungu ameteua kutokana na watoto wa Ibrahim,

Ismail na akateua kutokana na watoto wa Ismail, Kinana na akateua kutokana na Kinana

Qureshi na kutokana na Qureshi Bani Hashim na akaniteua mimi kutokana na Bani Hashim.

                                                                          Imesimuliwa na Muslim

‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎‎Hali ya kimaisha na kisiasa:

 

            Kama ilivyotueleza Qurani Takatifu, Waarabu walitawanyika sehemu nyingi baada ya kuvunjika boma la Maarib na kuanzisha miji mipya sehemu hizo walizohamia. Makabila haya ambayo aghlabu yake yalikuwa ni makabila ya kibedui hayatulii mahali pamoja yalikuwa yakisafiri baina ya miji hii mbali mbali kwa sababu ya kufanya biashara na kutafuta maisha.

 

            Pamoja na hayo, kulikuwepo na makabila mbali mbali ambayo yalitulia katika miji na kusimamisha mamlaka na kuwa na wafalme na maamiri na mashekhe mbali mbali. Katika hayo ni makabila ya Ghasasina yaliyokuwa na wafalme wao katika sehemu za Sham, na makabila ya Manadhira yaliyokuwa na wafalme wao na mamlaka yao iliyokuwa ikiitwa Al-Hira, na aidha mamlaka ya Kinda ambayo iliyokuwa katika Hijazi. Lakini pamoja na kuwa na mamlaka na wafalme wao, Waarabu hawa walikuwa hawishi vita baina yao kwa sababu ya kupigania ardhi na ukubwa na mali.

 

            Makureshi kabla ya kuja Uislamu walikuwa wanahukumu nchi ya Makka na kushughulikia mambo ya mahujaji waliokuwa wakija kuizuru Al-Kaaba na chakula chao na kushughulika na biashara zinazokuja hapo wakati wa Hija au biashara zao zinazoletwa kutoka Sham na Yemen. Hija hii ilikuwa ni masalio ya dini ya Nabii Ibrahim na Nabii Ismail ambayo kwa wakati huu ilikuwa ishachafuliwa sana na kubakia jina tu, kwani kila aina ya masanamu na ibada ya mizimu na majiwe ilikuwa imeshaingizwa ndani yake.

 

            Makabila mengine ya kiarabu yalikuwa yakiishi chini ya wakubwa wa kabila zao na walikuwa wakijulikana kama mashekhe wao, na neno lao ndio hukumu na sheria lazima lifuatwe na kila mmoja katika kabila hilo, na kwa hivyo walikuwa ni kama wafalme kwa watu wao, na walikuwa kukitokea vita basi wao hupewa robo ya ghanima (ngawira) na chochote chengine atakachokipenda na kulikuwa dhulma na zina na ufasiki na maasiya mbali mbali yalikuwa yameenea kila upande.

 

            Pamoja na hayo, mashairi yao na misemo yao na mithali zao zinatuonyesha kuwa kulikuwepo na tabia njema chungu nzima ambazo walikuwa wakijifakhirisha nazo kama ukarimu na ushujaa na kutimiza ahadi na ghera na kujienzi nafsi na kutokubali kuchezewa na mtu, sifa ambazo zimewapelekea kushika zimamu na hatamu za umma na kuongoza wanadamu mpaka wakafikia kutawala ulimwengu mzima wakati ulipokuja Uislamu.

 

Hali ya kidini Bara Arabu:

 

            Aghlabu ya Waarabu, hasa wale waliokuwa wakiishi Bara Arabu walikuwa wakiabudu masanamu kabla ya kuja Uislamu, na hii ni kwa sababu ya mtu mmoja aliyekuja akaleta uzushi huu (bid'a hii) na kuingiza kwenye dini safi aliyowaachia Nabii Ibrahim na Nabii Ismail.

 

            Kama tunavyoelezwa na Qurani Tukufu, Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Nabii Ibrahim na mwanawe Nabii Ismail kusimamisha Al-Kaaba hapo Makka ili iwe ndiyo nyumba ya kwanza kabisa ya kuabudiwa Mola Mmoja ulimwenguni na baada ya kulisimamisha jengo waliwaamrisha kizazi chao na Waarabu wengine kufuata dini hii.

             

           

                    Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Al-Kaaba) iwe mahali pa

                    kukusanyikia watu na mahali pa amani. Na pafanyeni mahali alipokuwa

                    akisimama Ibrahim mahali pa Sala. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail:        
                    Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wenye kutufu na wanaojitenga huko

                    kwa ibada, na wanao inama na kusujudu.

       

                                                                                               Sura:Baqara:125

 

            Waarabu waliendelea kufuata dini hii mpaka alipokuja Amr ibn Lahy mkubwa wa kabila la Khuza'a ambaye alikuwa ni mtu wa dini na mcha Mungu na mtenda mema akapendwa sana na watu na kuheshimiwa na kuchukuliwa kuwa mwanachuoni mkubwa. Huyu Amr alikwenda safari Sham akawakuta Wakristo huko wanaabudu masanamu na kwa kuwa Sham ni sehemu iliyoletwa Mitume na Manabii wengi, alidhani hiyo ndio njia ya haki, basi akarudi Makka na sanamu lake liitwalo Hubal na kumuingiza ndani ya Kaaba.

 

            Watu wakaipenda bid'a hii na wakaifuata na muda si muda kukazuka masanamu mengine yaliyokuwa yakiabudiwa sehemu mbali mbali badala ya Mwenyezi Mungu kama Lata na Manata na Uzza na yakakithiri na kuzidi na kuenea kila mahali mpaka ikawa kila nyumba kuna sanamu. Kama wanavyosema Waswahili kiingiacho mjini si haramu.

 

            Juu ya hivyo, Waarabu wakitambua kuwa kuna Mungu ambaye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi, na kuwa hawa masanamu ni kwa ajili ya kuwakurubisha na Mwenyezi Mungu tu na kuwaombea na kuwasahilishia muradi wao. Lakini baada ya kupita muda, ujahili ukazidi mpaka wakawa wanawaabudu na kuwaomba na kuwataka wawaondoshee shida zao na wakawa wanachinja kwa ajili yao badala ya Mwenyezi Mungu na kuwatolea muhanga na kuwazunguka na kuwaita na kuwasujudia.

 

            Waarabu wengine pembezoni mwa Bara Arabu waliathirika na dini mbali mbali za watu jirani na wao, kukawa kuna Waarabu Manasara sehemu za Shamu na Yemen, Waarabu Mayahudi sehemu za Iraq na Yemen na Palestin, na Waarabu Majusi (Maparisi) sehemu za Fursi (Iran) na Iraq na Bahrain.

 

            Uyahudi na Ukristo wa zama hizo ulikuwa ushaingia takataka nyingi za uzushi (bid'a) na upotofu, na ulipokuja Uislamu ulizikuta dini hizi zilizoletwa na Mitume Mitukufu Nabii Musa na Nabii Isa zishachafuka na kuharibika na kuwa hazina tofauti na dini nyenginezo za ushirikina, na kwa hivyo ukaja kurekibisha na kusahihisha na kunyosha na kurudisha usafi na uongofu wa dini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa wakati wa Mitume hawa na Mtume Ibrahim.

 

Nasaba ya Nabii Muhammad (SAW)

 

            Kama tulivyoeleza hapo nyuma, Mtume Muhammad (SAW) anatokana na kabila la kikureshi ambalo linarudi nasaba yake kwa Nabii Ismail na Nabii Ibrahim. Kutokana na vitabu vya kutegemewa vya sera ya Mtume (SAW), Muhammad ni mtoto wa Abdillahi bin AbdilMuttalib bin Hashim bin Abdi Manaf bin Qusay bin Kilab bin Murra bin Kaab bin Luay bin Ghalib bin Fihr (ambaye jina lake jengine ni Qureysh) bin Malik bin Nadhr bin Kinana bin Khuzayma bin Mudrika bin Ilyas bin Mudhar bin Nizar bin Maad bin Adnan.

 

            Nasaba hii inaendelea mpaka kufika kwa hao mababu zao wakubwa kina Ismail na Ibrahim, lakini wanahistoria wamehitalifiana kuhusu mababu wanaofuatia baada ya Adnan na kwa hivyo nasaba ya Mtume mpaka hapa kwa Adnan husita kwa kuchelea watu kufanya makosa kwa kuzidisha au kupunguza mababu wanaokuja baada ya Adnan.

 

Babu yake:

 

            Babu yake Mtume (SAW) AbdulMuttalib alirithi cheo na kazi za baba yake Hashim ambaye alipewa sharafu ya kulisha na kunywisha Mahujaji wajapo kuhiji Makka na alikuwa mtu karimu sana na akipendwa na kuheshimiwa na kutukuzwa na watu wake Makureshi kuliko hata wazee wake waliomtangulia.

 

            Na katika mambo makubwa aliyoyafanya AbdulMuttalib ni kukigunduwa kisima cha Zamzam kilichokuwa kimefukiwa na kabila la Jurhum walipotolewa Makka, na kukifukuwa tena na kuanzisha kugawa maji yake na kunywesha Mahujaji wanapokuja kuhiji, jambo ambalo linaendelea mpaka hii leo.

 

            AbdulMuttalib alipata watoto kumi wa kiume na sita wa kike. Wakiume ni Al-Harith na Az-Zubeyr na Abu Talib na Abdullahi na Hamza na Abu Lahab na Al-Ghaydaq na Al-Maquum na Saffar na Al-Abbas, na wa kike ni UmmulHakim na Barra na A'tika na Safiyya na Arwa na Umayma.

 

Baba yake:

 

            AbdulMuttalib aligundua mahali kilipo kisima cha Zamzam baada ya kuoteshwa mahali hapo na kuamrishwa akichimbe. Makureshi wakagombana naye wakitaka na wao washirikishwe katika mali yaliyozikwa humo, AbdulMuttalib akakataa na kusema kuwa ni jambo alilohusishwa yeye tu peke yake.

 

            Makureshi wakamchukuwa kwa kuhani awahukumu, lakini njiani Mwenyezi Mungu akawaonyesha dalili kuwa kisima cha Zamzam kimehusishwa AbdulMuttalib peke yake, basi hapo akaweka nadhiri kuwa Mwenyezi Mungu akimjaaliya kupata watoto kumi wa kiume atamchinja mmoja kwenye Al-Kaaba hata ikiwa Makureshi watajaribu kumzuiya.

 

            Basi alipopata watoto kumi na akajua kuwa watajaribu kumzuiya asimchinje mmoja wao, aliwakumbusha nadhiri yake wakamsikiliza, akaandika majina yao juu ya mishale na kurushwa likatoka jina la Abdullah. Basi AbdulMuttalib akamchukuwa Abdullah na kuchukuwa na kisu kikubwa na kuelekea kwenye Al-Kaaba ili amchinje, akazuiliwa na Makureshi, akawauliza na nitafanyaje kuhusu nadhiri yangu niliyoiweka?!!

 

            Makureshi wakamuelekeza ende kwa muaguzi na alipokwenda alimwambia amfanyie kura baina yake na ngamia kumi na kila mara ikitokea Abdullah basi naaongeze kumi. Akafanya hivyo ikawa inatokea Abdullah mpaka walipofika ngamia mia ikatokea ngamia, basi akachinja ngamia mia.

 

            Huyu Abdullah ndiye aliyekuwa mzuri zaidi katika watoto wa AbdulMuttalib na mnyofu zaidi katika wao na alikuwa ni mwenye kujihifadhi na machafu na maovu na ndiye aliyekuwa kipenzi cha baba yake. Alipofikia umri wa miaka ishirini na tano, baba yake AbdulMuttalib alimchagulia mke katika wanawake bora kabisa wa kikureshi Amina bint Wahb bin Abd Manaf bin Zuhra bin Kilab, binti mtukufu wa kibanii Zuhra na baba yake ni mkubwa wa kabila lake.

 

            Baada ya ndoa kwa muda mdogo, Abdullah alipelekwa safari na babake AbdulMuttalib lakini alipofika Madina alishikwa na maradhi akafariki dunia. Wakati huu Amina alikuwa tayari ana mimba ya mja wa Mwenyezi Mungu atakayekuja kubadilisha tarehe ya ulimwengu moja kwa moja na kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya binadamu.