Dola ya Banu Umayya (41H-133H):

Dola ya kiislamu iliyosimamishwa na Mtume (SAW) na kuthibitishwa nguzo zake na Makhalifa Waongofu ilimalizika baada ya kuuliwa baada ya kuuliwa Khalifa wa mwisho muongofu Ali bin Abi Talib na mmoja katika Makhawarij aitwaye AbdulRahman bin Muljim katika mwaka wa 40 Hijria.

Baada ya kuuliwa Ali alishika Ukhalifa Al-Hasan mwanawe kwa muda mdogo cha kiasi cha miezi sita kisha akajiuzulu katika mwaka wa 41 Hijria na kumwachia Muawiya bin Abi Sufyan ambaye alikuwa akipinzana na babake, ili aondoshe fitna ambayo ilikuwa imewakabili Waislamu, kwa sharti ya kuwa ahukumu kwa mujibu wa Qurani na Sunna za Mtume (SAW) na baada ya kufariki yeye Muawiya, wasimame Waislamu kumchagua Khalifa watakaomridhia wao.

Banu Umayya:

Umayya bin Abdi Shams bin Abdi Manaf alikuwa ni katika mabwana wa Kikureshi na katika matajiri wa Makka, na anahusiana na Mtume (SAW) kupitia mmoja wa babu zake Mtume (SAW) Hashim bin Abdi Manaf ambaye alikuwa ni ami yake Umayya.

Tangu zama za Ujahili, kulikuwa na mvutano baina ya Banu Hashim na Banu Umayya kuhusu uwongozi wa kabila la Kikureshi, na wakawa Banu Hashim wanashughulikia chakula na vinywaji vya Mahujaji na kuiangalia Al-Kaaba, na Banu Umayya walikuwa wanashughulikia amani ya nchi na uwongozi wa jeshi.

Banu Hashim:

Ulipokuja Uislamu na Mwenyezi Mungu akamchagua Muhammad bin Abdillahi bin AbdilMuttalib bin Hashim kuwa ndiye Mtume wake (SAW) kuongoza Umma wa kiislamu, wengi katika Banu Hashim walimkubali na kumsaidia na kumnusuru na kwa hivyo, walizidi utukufu na sharafu kuliko Banu Umayya hasa ilivyokuwa wengi katika Banu Umayya waliukataa Uislamu mwanzo ulipokuja na kuupinga kwa nguvu zao zote wakiongozwa na mkubwa wa kabila lao Abu Sufyan bin Umayya.

Ushindi wa Uislamu:

Baada ya kutekwa Makka na Waislamu katika mwaka wa 8 wa Hijra na kuingia aghlabu ya Washirikina katika Uislamu, waliikubali Banu Umayya dini hii mpya kwa kushindwa nguvu na kukubali kuwa chini ya uwongozi wa Mtume (SAW) ambaye alikuwa ni katika Banu Hashim.

Baada ya kufariki Mtume (SAW) na kuchaguliwa Khalifa kwa mujibu wa mashauriano baina ya Waislamu, alichaguliwa Abubakar kuwa ndio kiongozi wa Umma bila kutazama kuwa ni katika Banu Hashim au katika Banu Umayya, ijapokuwa alikuwa ni katika makabila mengineyo ya kikureshi, na kadhalika wakati wa kuchaguliwa Umar ambaye juu ya kuwa alikuwa ni katika Makureshi, lakini alikuwa si katika makabila haya mawili matukufu.

Alipochaguliwa Uthman kuwa ndiye Khalifa wa Waislamu, lilizuka tena tatizo la ukabila hasa ilivyokuwa yeye ni katika Banu Umayya na mara nyingi alikuwa akiwapa jamaa zake vyeo katika miji mbali mbali. Tatizo hili lilizidi kuwa kubwa na kutumbuka fitna baina ya Waislamu alipouliwa Uthman bin Affan na kudai jamaa zake kuwa lazima kisasi chake kilipizwe.

Ukhalifa wa Ali:

Baada ya kuuliwa Uthman na kuchaguliwa Ali bin Abi Talib bin Hashim na Waislamu kuwa ndiye Khalifa wao, Banu Umayya walimtaka awakamate wauwaji wa Uthman na kuwahukumu, jambo ambalo lilikuwa gumu kwa sababu Uthman aliuliwa na kundi la watu lililotoka miji mbali mbali na kwa hivyo ilikuwa ni muhali kwa Ali kuwakamata na kuwahukumu.

Hili liliwakasirisha sana Banu Umayya, lakini lililokuja kuleta mchafuko zaidi ni kule kuwauzulu Ali maliwali wote walioweka na Uthman, na ijapokuwa wote walikubali amri ya Khalifa wao, lakini Muawiya bin Abi Sufyan bin Umayya ambaye alikuwa ni liwali wa Sham tangu zama za Umar bin Al-Khattab alikataa kujiuzulu, na badala yake alisimama kumpinga Ali bin Abi Talib na kuukataa Ukhalifa wake na kumtaka awalete mahakamani wauwaji wa Uthman bin Affan.

Muawiya ajichagua Khalifa (41H-60H)

Muawiya akisaidiwa na Amr bin Al-Aas na watu wa Sham kwa siasa yake kubwa aliyokuwa nayo, alisimamisha vita dhidi ya Ali bin Abi Talib, na baada ya kushindwa jeshi lake alitumia hekima na hila mpaka akakubali Ali kuhukumiwa na Waislamu baina yake na Muawiya na kuwawacha Waislamu wamchague Khalifa wanayemtaka, na hili lilimpa nafasi Muawiya kumhadaa Ali na kumghilibu na mwisho kusababisha kuuliwa kwake.

Muanzilishi wa dola ya Banu Umayya:

Baada ya kuuliwa Ali na kujiuzulu mwanawe Al-Hasan na kumwachia Muawiya Ukhalifa, alitumia hila na siasa kubwa Muawiya ili Ukhalifa wende kwa mwanawe baada ya kufa kwake, juu ya kuwa sharti ya Al-Hasan ya kujiuzulu ni kuwa baada ya kufariki Muawiya, Waislamu ndio wasimame kumchagua Khalifa wao kwa mashauriano.

Muawiya bin Abi Sufyan:

Alizaliwa Muawiya Makka kabla ya Utume kwa miaka miwili na alisilimu pamoja na babake baada ya kutekwa Makka, na alikuwa ni mtu mwenye akili nyingi na hekima na busara na ufasaha mkubwa. Alikuwa ni mwanasiasa mkubwa mwenye kujua kuendesha mambo kwa njia nzuri, na alikuwa akitumia nguvu wakati inapohitajika nguvu na upole wakati unapohitajika upole, na alikuwa anasifika kwa ukarimu wake mkubwa.

Baada ya kusilimu Muawiya, alishiriki pamoja na Mtume (SAW) katika vita vya Huneyn, na alikuwa ni katika waandishi wake wa Wahyi unapoteremka, na alishiriki yeye katika zama za Ukhalifa wa Abubakar katika kuiteka Sham chini ya uwongozi wa nduguye Yazid, na katika Ukhalifa wa Umar alichaguliwa kuwa liwali wa Jordan, na baada ya kutawala Ukhalifa Uthman, alipewa Sham yote kuitawala yeye na kuendelea kuwa liwali wa Sham zaidi ya miaka ishirini.

Damaskas mji mkuu badala ya Madina:

Alipojitangaza Muawiya kuwa ndio Khalifa wa Waislamu aliigeuza Damaskas kuwa ndio mji mkuu wa dola ya kiislamu na kuthibitisha nguzo za dola kwa kueneza Uislamu na kufanya jihadi dhidi ya Makafiri Magharibi na Mashariki na Kaskazini na Kusini mpaka ikawa dola kubwa kabisa.

Aidha, aliweza Muawiya katika zama zake kwa siasa yake nzuri na kwa msaada wa maliwali wake waliokuwa wakijulikana kwa ujuzi wao mkubwa wa siasa kusitisha vita baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe na kueneza amani kila upande na kushughulikia kuiteka miji mipya ya Makafiri na kueneza Uislamu katika miji hiyo.

Mambo aliyoyafanya:

Mbali na kusimamisha jihadi na kuteka miji na kueneza Uislamu, alishughulika Muawiya na kulikuza jeshi la baharini ili kuweza kupambana na Warumi na kuilinda mipaka ya dola ya kiislamu dhidi ya hujuma zao, na akawa anapeleka majeshi ya wanamaji katika majira ya baridi na ya joto kupigana na maadui, na akajenga merikebu za vita ambazo zilifikia idadi yake katika zama zake merikebu 1700, na kuweza kuviteka visiwa vya Cyprus na Rhodes na vyenginevyo.

Jaribio la kuiteka Kostantinia:

Na katika vita alivyopigana nao ni vile ambavyo viliongozwa na Sufyan bin Awf akifuatana na Masahaba wakubwa na watoto wao kama Abu Ayyub Al-Ansari na Abdullahi bin Abbas na Abdullahi bin Umar na Abdullahi bin Az-Zubeir na kuizingira Kostantinia (Uturuki leo) katika mwaka wa 48 Hijria, lakini alishikwa na maradhi Abu Ayyub na kufariki huko na kuzikwa karibu na kuta za mji huo.

Muawiya alipeleka jeshi tena katika mwaka wa 54 Hijria na kuuzingira mji wa Kostantinia (Istanbul leo) na kubakia hapo jeshi kwa muda wa miaka saba bila kuweza kuuvamia, mpaka alipojiona Muawiya kuwa ajali yake imekaribia akampa uwongozi wa majeshi yake yote Yazid na kumchagua yeye kuwa ndio Khalifa wa Waislamu.

Kuiteka miji ya Afrika ya Kaskazini:

Muawiya baada ya kushika Ukhalifa alifanya kila bidii kuwashinda Warumi waliokuwa wakitawala Afrika ya Kaskazini katika zama zake, na kwa hivyo katika mwaka wa 50 Hijria alimpeleka Uqba bin Naafi' kuelekea Tunis na huko kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu aliweza kulishinda jeshi la kirumi kwa uhodari mkubwa wa kivita aliokuwa nao na kuchagua mahali ambapo alijenga kituo cha kivita ambacho alikiita Al-Qayrawan, na kukitumia kama kituo cha ulinzi wa mipaka ya dola ya kiislamu na mahali pa kuanzia kueneza Uislamu baina ya wakazi wa sehemu hizo.

Aliendeleza Abu Muhajir Dinar ambaye alishika uliwali wa Tunis, vita vya Jihadi baada ya Uqba na kuteka mji wa Talmasan, Algeria na kujaribu kuwavutia Mabarbari kwenye dini ya Uislamu na akaweza kuwavutia wengi kusilimu. Kisha akajaribu kuuteka mji wa Qartaja katika Tunis ambao ulikuwa ndio kituo kikubwa cha Warumi katika Afrika ya Kaskazini lakini alishindwa.

Uqba aliwekwa tena kuwa liwali wa Tunis na akawa Abu Muhajir Dinar chini ya uwongozi wake na katika mwaka wa 60 Hijria alitoka Uqba na jeshi lake na kuelekea Magharibi ya Tunis mpaka akafika ufuoni wa bahari kuu ya Atlantiki, na hapo akasimama kusema: Ewe Mola! Lau ingekuwa si hii bahari, basi ningeendelea kufanya Jihadi kwa ajili yako, na lau ningejua kama kuna ardhi na watu baada yake ningeikata kuwaendea.

Uqba na Abu Muhajir walikufa mashahidi walipokuwa wanarudi zao Tunis kwani njiani walipambana na jeshi kubwa la Mabarbari wakiongozwa na Kusaila, wakiwa wamejumuika na Warumi kuwapiga na baada ya vita vikali waliuliwa Uqba na Abu Muhajir na idadi kubwa ya maaskari wake katika mahali paitwapo Tahwida huko Algeria.

Kisha aliposhika Zuheir bin Qays uliwali wa Tunis baada ya Uqba, aliweza kumshinda Kusaila na wenziwe Mabarbar, lakini baadaye wakati alipokuwa anarudi alipambana na Warumi kwenye mji wa Darna hapo Libya na kukazuka vita vikubwa na kufa Zuheir shahidi katika vita hivyo.

Mambo muhimu aliyoyafanya....

Katika mambo muhimu aliyoyafanya Muawiya ni kuanzisha nidhamu ya Idara na ya Mali ambazo alizichukuwa kutokana na Warumi na kuzitumia katika mji mkuu mpya wa Waislamu hapo Damaskas. Wengi katika wafanyakazi wake walikuwa ni wageni na si Waislamu kwa ajili ya ujuzi wao na kuithibitisha nidhamu hiyo katika dola mpya.

Aidha, alianzisha nidhamu ya bawabu ambaye alikuwa ni mtu mwenye kusimama mlangoni pa Khalifa ili kumuuliza ajae kumuona Khalifa na kumuarifu kabla ya kuingia kumuona, na hili lilibuniwa baada ya jaribio lililofanywa na Khawarij kutaka kumuua Muawiya na Amr na Ali.

Pia katika mambo aliyoyafanya ni kutumia cheo chake na mali yake na siasa yake na maliwali wake kumchangia mwanawe Yazid achaguliwe kuwa Khalifa baada yake, na aliweza kufaulu pakubwa katika jambo hili na akawa wa kwanza kuanzisha nidhamu ya kurithiwa Ukhalifa baada ya kuwa ni nidhamu ya ushauri katika zama za Makhalifa Waongofu.

Utawala wa Muawiya ulidumu miaka ishirini na alipofariki mwaka wa 60 wa Hijra, alishika mwanawe Yazid na kuendelea Ukhalifa kurithiwa na vizazi vya Banu Umayya mpaka mwaka wa 132 wa Hijra na kwa hivyo ulidumu Ukhalifa wao miaka 91.

Makhalifa wa Banu Umayya:

Makhalifa wote waliohukumu dola ya kiislamu wa kibanu Umayya ni 14, nao ni kama wafuatao:

1- Muawiya bin Abi Sufyan - (41H-60H)

2- Yazid bin Muawiya - (60H-64H)

3- Muawiya bin Yazid - (64H-64H)

4- Marwan bin Al-Hakam - (64H-65H)

5- AbdulMalik bin Marwan - (65H-86H)

6- Al-Walid bin AbdulMalik - (86H-96H)

7- Suleiman bin AbdulMalik - (96H-99H)

8- Umar bin AbdulAziz - (99H-101H)

9- Yazid bin AbdulMalik - (101H-105H)

10- Hisham bin AbdulMalik - (105H-125H)

11- Al-Walid bin Yazid - (125H-126H)

12- Yazid bin Suleiman - (126H-126H)

13- Ibrahim bin Suleiman - (126H-127H)

14- Marwan bin Muhammad - (127H-132H)

Mambo muhimu yaliyofanywa na wao:

Katika mambo ambayo walijishughulisha nayo sana Makhalifa wa Banu Umayya ni kupigana Jihadi na kueneza Uislamu, na kwa hivyo katika zama zao dola ya kiislamu ilipanuka kufikia mipaka ya China upande wa Mashariki, na kufikia bahari kuu ya Atlantiki upande wa Magharibi, na kufikia Sudan upande wa Kusini, na kufikia mipaka ya Uturuki upande wa Kaskazini.

Kadhalika, walijishughulisha sana na mambo ya elimu na ustaarabu na kueneza lugha ya Kiarabu, na wakafasiri vitabu kutokana na lugha mbali mbali kwa Kiarabu na kuijaaliya lugha ya Kiarabu ndio lugha ya mawasiliano na maingiliano baina ya watu na ya idara na ya elimu.

Aidha, walijishughulisha na kujenga majumba na majenzi makubwa makubwa na misikiti na madrasa na taasisi za utafiti wa falaki na mahoteli na kuchimba visima na kutengeneza njia na kulima mashamba na kujenga ngome mipakani na vituo vya kijeshi baharini.

Baadhi ya Makhalifa wao:

Yazid bin Muawiya (60H-64H):

Baada ya kushika Yazid Ukhalifa, alisimama Al-Husein bin Ali kumpinga Yazid na kuchukulia kuwa kutawala yeye cheo cha Ukhalifa ni dhulma na unyang'anyi wa haki ya Umma ya kuchagua Khalifa wamtakaye, na kwa hivyo yeye pamoja na Abdullahi bin Az-Zubeir na watoto wengine wa Masahaba walikataa kumkubali Yazid kama Khalifa na kusimama kumpinga kwa vita na silaha, na wakakimbilia Makka ili kujikinga na kupata himaya kwenye msikiti mtukufu wa Makka.

Watu wa Al-Kufa huko Iraq ambao walimsaidia Ali babake Al-Husein, walimpelekea barua kuwa wako tayari kumchagua yeye kuwa ndiye Khalifa wao, na kumsaidia kupigana na Yazid, na kwa hivyo alimpeleka binamu wake Muslim bin Aqil kwenda kuchunguza hali, na alipomjibu kuwa watu wote wako pamoja naye alifunga safari pamoja na jeshi dogo wakiwemo wakeze na wanawe kuelekea Al-Kufa.

Huku Yazid aliposikia habari za watu wa Al-Kufa alifanya haraka kumpeleka Ubeydillah bin Ziyad kumkamata Muslim bin Aqil na wakubwa wa upinzani na kuwatia korokoroni, na alipofika Al-Husein Karbala alizungukwa na jeshi la Ubeydillah na kuuliwa tarehe 10 ya Muharram mwaka wa 61 Hijria.

Ilipomfikia Abdullahi bin Az-Zubeir habari ya kuuliwa Al-Husein, alisimama yeye kumpinga Yazid hasa alivyojua kuwa watu wa Madina wako pamoja naye, na kwa hivyo akajiita Amirul-Muuminin (Kiongozi wa Waislamu) na kubakia Makka kwenye msikiti mtukufu. Yazid aliposikia haya akampelekea jeshi kubwa na likaweza kuwashinda watu wa Madina na kuelekea Makka. Huko waliuzunguka msikiti wa Makka ambamo amejihami ndani yake Abdullahi bin Az-Zubeir na kuupiga mizinga mpaka wakalibomoa Al-Kaaba, lakini mkubwa wa jeshi alipopata habari ya kufa Yazid huko Sham aliondoka na jeshi lake na kurudi Damaskas.

AbdulMalik bin Marwan (65H-86H):

Aliposhika Ukhalifa AbdulMalik katika mwaka wa 65 Hijria ilikuwa dola ya kiislamu katika hali ya mchafuko kutokana na vile vikundi ambavyo vilikuwa vikipinga dola ya Banu Umayya, na kwa hivyo ilimbidi apitishe juhudi kubwa kuondosha fitna hii na kuleta amani na utulivu katika dola, na kwa hivyo alisimama kuendeleza vita alivyovipigana Yazid dhidi ya Abdullahi bin Az-Zubeir na ambavyo viliendelezwa na Muawiya bin Yazid na Marwan bin Al-Hakam babake AbdulMalik.

Vita hivi vilichukuwa muda mkubwa kwani tangu vilivyoanza mwaka wa 64 wa Hijra viliendelea mpaka mwaka wa 73 wa Hijra ndipo Abdullahi bin Az-Zubeir aliposhindwa nguvu na Al-Hajjaj bin Yusuf na kuuliwa na kumakinika AbdulMalik kuthibitisha utawala wake upande wa Hijaz na Misri na Sham. Kisha akampeleka tena Al-Hajjaj kwenda Iraq kupambana na Khawarij waliopanga njama kumuua Muawiya na kufanikiwa kumuua Ali bin Abi Talib, na kwa ushujaa mkubwa na uhodari mkubwa wa kivita wa Al-hajjaj aliweza kuwashinda Al-Khawarij katika mwaka wa 78H na kurudisha amani kwenye dola ya Banu Umayya.

Anachukuliwa AbdulMalik bin Marwan kuwa ni muanzilishi wa pili wa dola ya Banu Umayya kwani kabla ya kushika yeye Ukhalifa dola ilikuwa katika mchafuko mkubwa na aghlabu ya nchi zilikuwa katika mikono ya Abdullahi bin Az-Zubeir au kumchukulia kuwa ndiye Khalifa wa kisharia. Naye AbdulMalik alikuwa ni mtu mwenye elimu kubwa ya dini na sharia.

Mambo aliyoyafanya:

Katika zama zake alipeleka AbdulMalik jeshi kubwa chini ya uwongozi wa Hassan bin Nuuman katika mwaka wa 74 Hijria kwenda Qarttaja, Tunis kupigana na Warumi na aliweza kwa tawfiki ya Mwenyezi Mungu kuvivunja vituo vyao vikubwa huko na kuwashinda, na vile vile kuukomesha uasi wa baadhi ya vikundi vya makabila ya Kibarbari ya huko na kuingia aghlabu yao katika dini ya kiislamu.

Hassan bin Nuuman aliweza baada ya kuwatoa Warumi Afrika ya Kaskazini kuinadhimu nchi na kuitengeneza, na katika mambo aliyoyafanya ni kueneza Uislamu baina ya wakaazi wa miji hiyo na kuwawekea Mafakihi na wanazuoni wa kuwaelimisha dini ya kiislamu, na kuwaingiza wengi wao katika jeshi lake na kushiriki kuendeleza Jihadi mpaka kuweza kuvuka na kufika Andalus (Uhispania na Ureno leo).

Aidha, alijenga Hassan karibu na Qartaja mji mpya ambao ndio mji mkuu wa Tunis leo na kuweka mahali pa ujenzi wa merikebu na msikiti na kituo cha idara ya mambo ya nchi na kambi ya kijeshi.

Baada ya kukomesha chokochoko na michafuko ya ndani ya nchi, alifanya bidii kuitengeneza dola ya kiislamu na kuinadhimu nchi kwa kuiwekea idara mbali mbali na kutumia lugha ya Kiarabu katika idara hizi baada ya kuwa zilikuwa zikitumia Kiyunani (Sham) na Kiajemi (Ufursi) na Kiqipti (Misri).

Abdul-Malik alikuwa wa kwanza...

Aidha, AbdulMalik ndiye Khalifa wa kwanza kujenga nyumba ya kutengenezea pesa katika Afrika ya Kaskazini na kujenga kituo cha jeshi la baharini huko Tunis na kujenga msikiti wa "Kuba la Jabali" huko Jerusalem.

Alifariki AbdulMalik huko Damaskas katika mwaka wa 86 wa Hijra baada ya kumuahidi mwanawe Al-Walid kushika Ukhalifa baada yake.

Al-Walid bin AbdulMalik (86H-96H)/(705-715MK):

Alizaliwa Al-Walid katika mwaka wa 50 Hijria na kushika Ukhalifa katika mwaka wa 86 Hijria baada ya kufariki babake AbdulMalik ambaye alimwachia dola kubwa yenye nguvu na jeshi kubwa na utulivu na amani na mali nyingi sana, na kwa hivyo alipata fursa kubwa ya kujishughulisha na mambo ya ujenzi na kuimarisha nchi na kuikuza dola yake kwa Jihadi na kueneza Uislamu.

Mambo muhimu aliyoyafanya:

Katika zama zake, Al-Walid alimchagua Hajjaj bin Yusuf kuwa liwali wa Iraq na yeye akampeleka Quteiba bin Muslim ambaye alikuwa ni liwali wa Khurasan akiongoza jeshi kwenda sehemu za Turkistan na jeshi jengine kwenda sehemu za Sind chini ya uwongozi wa Muhammad bin Al-Qasim.

Kutekwa miji ya Turkistan:

Aliweza Quteiba kuiteka miji ya Turkistan baada ya vita vikali ambavyo wengi katika Waislamu walikufa mashahidi, lakini kwa uthabiti wa jeshi lake na imani kubwa waliokuwa nayo, waliweza kuiteka Bukhara mwaka wa 90 wa Hijra, kisha Khawarizm na Samarqand na Tashqand katika mwaka wa 93 Hijria, na kwa hivyo miji yote hii iliyotekwa ikawa chini ya dola ya kiislamu.

Baada ya ushindi mkubwa alioupata, aliendelea Quteiba kuelekea China na akaweza kuuteka mji wa Kashgar katika mwaka wa 96 Hijria na kumlipisha jizya mfalme wa China wa wakati huo. Uislamu ulienea katika sehemu hizi na wengi wa wakazi wa miji hii wakaingia katika Uislamu kwa namna Waislamu walivyokaa nao kwa uzuri na kuishi nao kwa wema.

Kutekwa Sind na Hind (India):

Kwa upande mwengine aliweza Muhammad bin Al-Qasim kiongozi wa jeshi akiwa na umri wa miaka kumi na nane tu kuiteka Makran kisha akaiteka Daybul katika mwaka wa 93 Hijria, kisha akaendelea mbele akaingia India na kuuteka mji wao mtukufu katika mwaka huo huo na kuyavunja masanamu yao na kujenga misikiti katika kila miji aliyoiteka.

Waislamu kama ilivyo desturi yao, waliishi kwa uzuri na watu wa sehemu hizi na kuingiliana nao kwa wema na kuwaachia uhuru wa kuabudu wanachotaka kutokana na kawaida ya dini ya kiislamu aliyoiweka Mwenyezi Mungu kwenye Qurani isemayo: "Hakuna kulazimishwa katika dini, uwongofu ushabainika kutokana na upotofu", na kwa hivyo, baada ya kuona haya watu wa miji hii kutoka kwa Waislamu waliingiwa na imani na kuipenda dini hii tukufu na kuingia makundi makundi.

Kutekwa Andalus (Uhispania na Ureno leo):

Katika mwaka wa 92 Hijria alitaka Musa bin Nusayr ambaye alikuwa akitawala Tunis baada ya Hassan bin Nuuman idhini kutoka kwa Al-Walid kuelekea Andalus na majeshi yake, na Al-Walid akamkubalia. Naye alishajiishwa na Tureyf bin Malik ambaye alivuka bahari kuchunguza hali ya nchi na watu huko na kuona kuwa nchi hizo zinastahiki kuendewa na kupelekewa watu wake dini ya Uislamu.

Kwa hivyo, Musa alimchagua Tariq bin Ziyad kwa kazi hii na baada ya kuvuka bahari na kuteremka kwenye jabali ambalo mpaka leo linaitwa kwa jina lake "Jabal Tariq" au "Gibraltar", kisha akavuka na kuingia Andalus ambako alipambana na jeshi kubwa la Zureyq katika Ramadhani ya mwaka wa 92 Hijria na kulishinda vibaya sana na kuendelea kuteka miji ya huko: Qurtuba (Cordova) na Gharnatta (Granada) na Tuleytila (Toledo).

Vile vile, Musa alitoka katika mwaka wa 93 wa Hijra na jeshi kubwa la watu elfu kumi na nane kwenda kumsaidia Tariq na waliweza wote wawili pamoja mpaka kufikia mwaka wa 96 Hijria kuziteka aghlabu ya nchi za Andalus. Majeshi ya kiislamu yalifika mpaka kusini ya Tours, Ufaransa, lakini walishindwa kuendelea mbele walipofika hapo na wakazuiliwa na majeshi ya Wazungu kuendelea kuiteka Ulaya.

Kwa upande mwengine, majeshi ya kiislamu chini ya utawala wa Walid yalisonga mbele sehemu za Mashariki mpaka kufikia kwenye mto wa Indus, na ikawa dola ya kiislamu wakati huo imetanda kuanzia Andalus (Uhispania na Ureno leo) mpaka bara la Hindi.

Mambo muhimu aliyoyafanya:

Katika mambo muhimu aliyoyafanya Al-Walid katika zama zake ni kuwashughulikia mayatima kwa kuwatazama, na kuwawekea viwete na wasiojiweza watu wa kuwaangalia na kuwawekea vipofu watu wa kuwaongoza na kuwaonyesha njia na kuwawekea hawa wote mishahara yao. Aidha, aliwakusanya wakoma na kuwaweka kwenye nyumba moja na kuwawekea watu wa kuwatibu na kuwaangalia.

Aidha, alijishughulisha sana Al-Walid na ujenzi, na katika majenzi mashuhuri aliyoyajenga ni msikiti wa Umawi ulioko Damaskas, na kuupanua msikiti wa Mtume (SAW) ulioko Madina wakati wa uliwali wa Umar bin Abdul-Aziz, na kuutengeneza msikiti wa Al-Aqsa ulioko Jerusalem.

Vile vile alichimba visima na kuweka watu wa kuvishughulikia na kujenga njia na kuzisawazisha. Pia alijenga majenzi ya kifalme sehemu mbali mbali majangwani ambayo alikuwa kila baada ya muda akiyapitia kwa mapumziko, na katika majenzi hayo ni jengo la kifalme liitwalo A'mra katika mji wa Amman hapo Jordan.

Kadhalika, Walid ndiye aliyeitilia nguvu lugha ya Kiarabu kwa kuifanya lugha ya Kiarabu kuwa ndiyo lugha rasmi ya dola, na kuwalazimisha wakaazi wa dola hii kutumia Kiarabu katika mambo yote yanayohusu Idara, na kuwafanya wasiokuwa Waarabu waliokuwa wakiishi kwenye dola hii, wakiwa ni Maqipti au Waajemi watumie lugha hii.

Alipofariki Al-Walid katika mwaka wa 96 wa Hijra aliusia nduguye Suleiman ashike Ukhalifa baada yake.

Suleiman bin AbdulMalik (96H-99H):(674-717MK)

Baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa, Suleiman hakutawala muda mkubwa kwa ukhalifa wake uliendelea tangu 715 mpaka 717 MK ambapo alifariki dunia. Chini ya utawala wake aliweza kuiteka Tabiristan ilioko kwenye milima ya Iran, na vile vile alijaribu kupeleka majeshi kwenda kuiteka Konstantinia lakini hakufaulu.

Suleiman alijitahidi kuhimiza ibada na akachimba visima huko Makka kwa ajili ya mahujaji. Alikuwa akimheshimu na kumpenda sana binamu wake Umar bin Abdul Aziz kwa ajili ya ucha Mungu wake mkubwa na ujuzi mkubwa wa dini, na kwa kuwa Umar alikuwa hapatani na Hajjaj bin Yusuf kwa ukatili wake na kutesa na kuua watu kwa dhulma, Suleiman vile vile alikuwa hampendi Hajjaj, na kwa hivyo alipokufa, aliwakamata wale waliokuwa wakimuunga mkono Hajjaj na kuwafunga, ambao katika hao ni maamiri jeshi wakubwa wa kiislamu ambao walikuwa naye, Musa bin Nusayr, Qutaiba bin Muslim, na Muhammad bin Qassim.

Jambo la kuwafunga viongozi hawa wa jeshi na mwishowe kuwaua, lilitia dosari na doa jina na sifa ya Suleiman, na kuwafanya watu wengi wakereke naye. Aliendelea kutawala kwa muda wa miaka miwili tu kisha akafariki, lakini kabla ya kufariki aliandika wasia wake na kumchagua Umar bin Abdul Aziz kuwa ndiye atakayekuwa Khalifa baada yake. Jambo hili lilikwenda kinyume na ule mwenendo uliowekwa na babu zake wa kurithisha ukhalifa kwa ndugu zake au wanawe, na badala yake alimchagua binamu yake Umar kwa kuchukulia kuwa yeye anastahiki zaidi na ana ujuzi zaidi wa kuhukumu kwa sababu ya elimu yake na ucha Mungu wake, na kwa hivyo akawa amemchagua Khalifa kwa mujibu wa kawaida za sawa sawa zilizowekwa na Uislamu.

Katika zama za Ukhalifa wa Al-Walid na nduguye Suleiman, dola ya kiislamu ilipanuka sana kushinda wakati wowote wa nyuma wa Makhalifa wengine.

Umar bin AbdulAziz (99H-101H):

Umar bin AbdulAziz alikuwa ni mtoto wa kibanu Umayya kutokana na babu yake Marwan bin Al-Hakam, lakini vile vile alikuwa anahusiana na Umar bin Al-Khattab kwa upande wa kuukeni, kwani mamake alikuwa ni mtoto wa Aasim bin Umar Al-Khattab na kwa hivyo aliinukia kuwa mcha Mungu na muadilifu tangu utotoni mwake.

Alipelekwa Umar na babake Madina kwenda kusoma na kujifunza elimu kutokana na wanazuoni na mafakihi wa Madina na akahifadhi Qurani na kujifunza uzuri Sharia, na kwa malezi haya mema aliyoyapata tangu utotoni mwake yalimfanya azidi kuwa mcha Mungu na kusifika kwa wema na uadilifu na elimu mpaka akawa katika wanachuoni wakubwa kabisa wa zama zake.

Katika zama za Ukhalifa wa Al-Walid alimpeleka Madina kuwa liwali wake na huko akaonyesha mfano mwema wa kuishi na raia kwa uzuri na kuwahukumu kwa uadilifu mpaka akapendwa na watu wote huko. Aidha, aliweza kumshawishi Al-Walid alipokuwa liwali wa Madina kuutengeneza na kuupanua msikiti wa Mtume (SAW) kwa kule kuona kuwa umekuwa mdogo na hauna nafasi ya kuchukuwa idadi ya Waislamu inayozidi kila siku.

Aliposhika Suleiman Ukhalifa baada ya Al-Walid, alimchagua Umar bin Abdul-Aziz kuwa ndiye atakayekuwa Khalifa baada yake kwa ule ucha Mungu na elimu kubwa aliyokuwa nayo na uhodari wake wa kuhukumu watu kwa uadilifu, na kwa hivyo alipofariki Suleiman, Waislamu walimchagua Umar kuwa ndiye Khalifa wao. Baada ya kuchaguliwa, alipanda Umar mimbari na kuwahutubia watu na kuwaambia:

Enyi watu! Kwa hakika, Mimi nimetiwa mtihani juu ya jambo hili (la Ukhalifa) bila Mimi kushauriwa wala Mimi kulitaka, wala kushauriwa Waislamu, na Mimi nimekuondosheeni jukumu hili la kunichagua Mimi, basi chagueni wenyewe mnayemtaka. Kisha akaanza Umar kushuka mimbari lakini watu wakampigia kelele na kumwambia kuwa tumekwishakuchagua na wakamsogelea kumpa mikono na kuonesha utiifu wao kwake.

Umar alifuata mwenendo wa Mtume (SAW) na kuchukuwa mithali ya Makhalifa Waongofu hasa Umar bin Al-Khattab katika kuhukumu kwake, na kwa hivyo akachagua maliwali wema na makadhi waadilifu na kuhukumu watu kwa uadilifu na usawa, hata wale wasiokuwa Waislamu katika Mayahudi na Manasara na Majusi. Aidha, akawakurubisha wanazuoni na mafakihi kuwa ndio washauri wake na wenziwe, na akawa anaishi maisha mepesi yasiyo na anasa na kujiepusha na starehe za kidunia.

Jihadi katika Ufaransa:

Waislamu waliendelea na Jihadi yao katika Andalus na kufika mpaka milima ya Barans (Perenes) katika mipaka ya Ufaransa, na katika Ukhalifa wa Umar walisonga mbele mpaka kuingia Ufaransa chini ya uwongozi wa liwali wa Andalus As-Samh bin Malik Al-Khawlani lakini aliuliwa na kufa shahidi kwenye vita vya Tuluz (Tolouse) katika mwaka wa 102 Hijria.

Mambo muhimu aliyoyafanya:

Alichukulia Umar kuwa yale waliokuwa wakiyafanya Makhalifa wa kibanu Umayya ya kujikusanyia mali na kujenga majumba makubwa na kuishi maisha ya starehe ni makosa ambayo mwanadamu atakuja kusailiwa mbele ya Mola wake siku ya Kiyama, na kwa hivyo aliposhika Ukhalifa alijitenga na starehe na kuchagua maisha mepesi mbali na anasa na fahari, na haya yalimpelekea kufanya mambo fulani ili kujikinga na adhabu ya Mola wake:

1- Alizikusanya zile mali ambazo Mabanu Umayya walijikusanyia kwa njia zisizokuwa za kisharia na kuzirudisha kwa wenyewe, na zile ambazo hakuwapata wenyewe alizirudisha katika Baytul-Mal (Nyumba ya Hazina) ya Waislamu.

2- Aliwauzulu Maliwali madhalimu waliokuwa wamewekwa na Makhalifa waliopita na kuweka badala yao Maliwali wema wenye kujulikana na watu kwa uadilifu wao na mwenendo mwema, na akawapandishia mishahara ili wasiwe na tamaa na kuanza kunyang'anya watu mali zao.

3- Akaondosha Jizya (kodi wanaotozwa wasiokuwa Waislamu) kwa wale wanaosilimu katika Makafiri.

4- Alijishughulisha na mashamba na kuamrisha yalimwe na yachimbiwe visima vya maji na kutengenezwa njia na kujenga misafarakhana njiani kwa ajili ya wasafiri.

5- Alijenga misikiti kwenye sehemu mbali mbali.

6- Alijaribu kuzungumza na Khawarij na kuwavutia kwa akhlaki zake njema na ujuzi wake wa dini yake mpaka akaweza kuwarudisha wengi chini ya utiifu wake.

Matokeo ya siasa yake:

Siasa ya Umar bin Abdul-Aziz ya kuishi na raia kwa wema na kuwafanyia uadilifu Waislamu na wasiokuwa Waislamu ilileta matokeo mazuri na kufanya Ukhalifa wake kuwa ni zama nzuri katika maisha ya watu, mpaka watu wakamhisabu kuwa ni katika Makhalifa Waongofu.

Katika matokeo ya siasa hii ni:

1- Kuingia wengi katika Wafalme wa Sind na wa Turkistan katika Uislamu na kufuatiwa na watu wao

2- Kuondosha Jizya juu ya wale wanaosilimu kulifanya wengi katika Maqipti wa Misri, na Majusi wa Ufursi, na Manasara wa Sham kuingia katika Uislamu.

3- Kuwafanyia upole maadui wa dola na kuzungumza nao kwa hekima na kwa mawaidha mema kuliwafanya wengi warudi chini ya utiifu wake na kuwacha kupigana na dola ya kibanu Umayya.

4- Kule kujishughulisha na kuwatengenezea Waislamu nchi yao na kuwatimizia mahitajio yao na kuwashughulikia maskini na mafakiri na mayatima na kila mwenye uhitaji kulifanya maisha yawe mazuri kwa watu wote na kutoweka umaskini katika dola ya kiislamu katika zama zake.

5- Kule kuneemesha watu wote kuliwafanya watu wasiwe na uhitaji na kufanya Zaka inayokusanywa isiwe na maskini wakupewa, na kwa hivyo zikatumika Zaka kununua watumwa na kuwaacha huru na kufanya mengine ya kheri.

Kufariki kwake:

Umar alifariki katika mwaka wa 101 Hijria na kushika Ukhalifa baada yake Yazid bin AbdulMalik kutokana na wasia wa Suleiman bin AbdulMalik.

Yazid bin AbdulMalik (101H-105H):

Aliposhika Yazid Ukhalifa katika mwaka wa 101 wa Hijra baada ya kufa Umar bin AbdulAziz

meli 70 tu kutoka Paris, na hapo kulizuka vita vikali sana vijulikanavyo kwa jina la "Balaattush-Shuhadaa" katika mwaka wa 114 Hijria ambavyo aliuliwa AbdulRahman Al-Ghafiqi na kusita vita hivi hapo.

Kwa upande mwengine, vita vilikuwa vikiendelea huko Armenia chini ya uwongozi wa Marwan bin Muhammad ambaye alikuwa akitawala Armenia baina ya mwaka 105 wa Hijra mpaka 126 Hijria, na alipigana na majeshi ya kirumi na kuyashinda katika vita vyote alivyopambana nao kwa uhodari wake mkubwa wa kivita.

Marwan bin Muhammad (127H-132H):

Baada ya kufariki Hisham alishika Al-Walid bin Yazid kwa muda mdogo tu (125H-126H), kisha akashika Yazid bin Suleiman (126H-126H) na halafu akakamata nduguye Ibrahim bin Suleiman (126H-127H) na mwishowe kukamata Marwan bin Muhammad ambaye ndiye aliyekuwa Khalifa wa mwisho wa kibanu Umayya.

Alikuwa Marwan ni mtu shujaa sana aliyeishi maisha yake yote katika kupigana Jihadi na Warumi na vile vile alikuwa ni mwanasiasa mkubwa. Katika vita vyote alivyopigana na Warumi alipata ushindi mkubwa na kwa hivyo anachukuliwa ni katika viongozi wakubwa wa kivita wa zama zake.

Alishika Ukhalifa katika mwaka wa 127 Hijria, lakini aliikuta dola ya kiislamu ya kiumayya imo kwenye mchafuko mkubwa na fitna kutoka kila upande, na katika makubwa yaliyosababisha fitna hii ni kule kuwacha Mabanu Umayya jambo la kushauriana katika uchaguzi wa Khalifa, na kule kuanzisha kwao nidhamu ya ufalme kwa kurithi, na vita visivyokwisha, na kule kudai kwa Banu Abbasi kuwa Ukhalifa ni haki yao walionyang'anywa na Banu Umayya.

Kumalizika kwa Dola ya Banu Umayya:

Pamoja na kuwa dola ya Banu Umayya imefanya mengi katika miaka 91 ya utawala wake, na kupata kila aina ya ushindi Mashariki na Magharibi, na kufanya matengenezo makubwa makubwa katika mambo ya kijamii na kisiasa na kiuchumi, lakini kulikuwa kuna mambo fulani ambayo daima yalikuwa yakiiandama dola hii na kuitia udhaifu na uhasidi mpaka ikasababisha kudidimia na kuangamia.

Sababu za kuiangusha dola hii:

1- Kutupa Kushauriana:

Moja katika kawaida muhimu sana aliyoiweka Mwenyezi Mungu katika Qurani yake ni kushauriana baina ya Waislamu wakitaka kufanya mambo yao, na ndio Sunna ya Mtume Muhammad (SAW) katika kutekeleza mambo yake na kadhalika mwenendo wa Makhalifa Waongofu baada yake.

Katika mambo muhimu sana ya kuisimamisha dola ya kiislamu na kuithibitisha nguzo yake ni kushauriana wakati wa kumchagua Khalifa wa Waislamu, na haya ndio yaliyokuwa yakifanywa katika zama za Makhalifa Waongofu Abubakar na Umar na Uthman na Ali, lakini alipojinyakulia Ukhalifa Muawiya alibadilisha mwenendo huu na kutumia siasa na hila ili Ukhalifa wende kwa mwanawe baada yake, na ukawa Ukhalifa ni jambo la urathi baada ya kuwa ni la ushauri baina ya Waislamu.

Jambo hili lilileta vita vikubwa baina ya Waislamu na fitna hii iliendelea siku zote mpaka ikawa ni mojawapo wa sababu ya kuanguka dola ya kibanu Umayya.

2- Nidhamu ya kurithi Ufalme:

Baada ya kugeuka Ukhalifa na kuwa ni wa kurithiwa badala ya kuchaguliwa na Waislamu, ilizuka nidhamu ya kumchagua Khalifa nduguye au mwanawe kuwa ndio Khalifa baada yake, na hili lilileta chuki na hasadi baina ya watu wa ukoo mmoja na ikawa akishika huyu humchagua huyu na akishika yule humuondoa huyu na kumweka ampendaye.

Jambo hili lilileta mgogoro baina ya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha matatizo na kuchukiana na mvutano, na kupeleka baadhi ya Makhalifa kujiunga na baadhi ya makabila ili yawanusuru na wengine kujiunga na makabila mengine.

3- Kutegemea Waarabu:

Banu Umayya walikuwa wakitegemea sana kabila za Kiarabu katika utawala wao na kuendesha mambo yao, na hili liliwafanya wasiokuwa Waarabu kuwachukia Mabanu Umayya na kujiunga na vikundi vyengine vilivyokuwa vikiwapinga na kuwapiga vita kama Makhawarij na Mashia.

4- Ukabila:

Aidha, Banu Umayya katika siasa yao, walikuwa wakipendelea baadhi ya Makabila ya Kiarabu kuliko mengine, jambo ambalo lilileta chuki na hasama baina ya Makabila na mwisho kuzuka vita baina yao.

5- Vita visivyokwisha:

Tangu kushika Ukhalifa Mabanu Umayya vilizuka vita mbali mbali baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe na baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na vita hivi vilileta hasara kwa mali na watu na roho na juhudi na wakati na kusababisha udhaifu juu ya dola ya kiislamu ya kibanu Umayya na mwishowe kuivunja na kuiangusha.

6- Mwito wa Banu Abbas:

Watu wa kabila la Banu Abbas walikubaliana na kizazi cha Ali bin Abi Talib (Alawiyyin) kuipinga dola ya kibanu Umayya na kuuondosha Ukhalifa kwenye mikono yao, kwa kuwachukulia kuwa wamechukua haki ambayo si yao, na kuwa lazima haki hii irudi kwa wenyewe Mabanu Hashim ambao ndio wao Banu Abbas na Alawiyyin.

Ulianza mwito huu siri, na akachagua Muhammad bin Ali bin Abdullahi bin Al-Abbas mji wa Al-Hamima huko Jordan kuwa ndio makao makuu ya mwito huu, na kuchagua kituo kingine huko Khurasan cha kueneza mwito huu kwa siri. Kisha wakaanza kupeleka watu katika miji mbali mbali ya kiislamu kuwashawishi watu wafanye upinzani dhidi ya dola ya Mabanu Umayya, na kusababisha mwisho wake kuanguka kwa dola hii.

Hii ni kwa sababu, Banu Umayya, katika miaka 99 ya utawala wao, dola yao ilikuwa ikionekana kuwa ni ufalme wa Banu Umayya, na walipokuja Banu Abbas na kudai kuwa wao wanastahiki zaidi ukhalifa wa dola ya kiislamu kwa kuwa wanatokana na kizazi cha Abbas bin AbdulMuttalib ami yake Mtume (SAW) walipata wafuasi wengi hasa sehemu za Iraq na Khurasani, na kwa hivyo alipotawala Marwan bin Muhammad wa pili, mizizi ya Banu Abbas ilikuwa ishashika sawa sawa na kujizatiti na kwa hivyo walimshinda katika vita na kumuua yeye na wengi wa jamaa zake akina Banu Umayya.

Aliyewahi kukimbia katika wao ni Abdul Rahman bin Muawiyya al Daakhil ambaye aliweza kukimbia na kufika mpaka Moroko na kuvuka kuingia Andalus katika mwaka 756 MK, na kuweza kuanzilisha utawala wa kibani Umayya huko Uhispania na Ureno, nchi ambazo kwa wakati huo zikijulikana kama Andalus.