Dola ya Banul-Abbas:
Banul-Abbas wanatokana na Al-Abbas bin Abdul Muttalib bin Hashim ami yake Mtume Muhammad (SAW), sahaba mkubwa ambaye alisilimu kabla ya kutekwa Makka naye ni sahaba wa mwisho kuhamia Madina na kufariki katika Ukhalifa wa Uthman bin Affan na kusaliwa na Uthman na kuzikwa Al-Baqii, Madina.
Alikuwa Al-Abbas ana watoto kumi wanaume na katika hao ni Abdullahi bin Abbas, mwanachuoni mkubwa wa umma huu na ambaye ndiye babu wa Muhammad bin Ali aliyesimama kuleta upinzani dhidi ya dola ya Banu Umayya mwanzo kwa kisiri, kisha kwa kusimamisha vita dhidi yao.
Mwito wa Banul-Abbas:
Baada ya kuuliwa Al-Husein bin Ali huko Karbala, walijikusanya Mashia chini ya uwongozi wa Muhammad bin Ali bin Abi Talib (Ibnul-Hanifiya) na kuanza kuwapinga Mabanu Umayya kisiri, lakini aliposikia habari hii Khalifa Hisham bin AbdulMalik alimwita na kujidai kumkirimu kisha akamtilia sumu, na alipokuwa anarudi Al-Hamima kijiji katika Jordan na kuhisi kuwa atakufa, alimwachia kazi hii Muhammad bin Ali bin Abdullahi bin Al-Abbas.
Muhammad bin Ali alianza mwito wake katika kijiji cha Al-Humaima huko Jordan na kufanya kuwa ndio makao makuu yake na kuweka kituo chengine Khurasan cha kueneza mwito huu wa upinzani, walianza kupeleka watu katika miji mbali mbali ya kiislamu kuueleza mwito wao na kuonyesha dhulma waliyoifanya Mabanu Umayya ya kuwapokonya Banu Hashim haki yao ya Ukhalifa tangu walipouchukuwa kwa nguvu zama za Khalifa wa nne Ali bin Abi Talib.
Banul-Abbas wakisaidiwa na kizazi cha Ali bin Abi Talib waliweza kupata wasaidizi wengi hasa ilivyokuwa dola ya kibanu Umayya ilikuwa na maadui wengi wa makundi mbali mbali. Aidha, katika mambo yaliyowasaidia ni kupigania kuwepo usawa baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu jambo ambalo Banu Umayya walikuwa hawalifanyi.
Kusimama kwa dola ya Banul-Abbas:
Mji wa Al-Kufa ambao ndio ulikuwa mji mkuu wa Ali bin Abi Talib katika Ukhalifa wake, uliendelea kuwapinga Mabanu Umayya, lakini kwa kuwa ulikuwa karibu na Damaskas ulihamia upinzani Khurasan na kuwa ndio kituo cha kueneza mwito huu, na kubaki mji wa Al-Kufa, Iraq kuwa ndio mji wa mawasiliano baina ya Al-Humaima na Khurasan na miji mengineyo.
Sababu ya kuchaguliwa Khurasan kuwa ndicho kituo cha kueneza mwito huu ni kule kuwa mbali na mji mkuu wa Banu Umayya na kule kuchukia watu wa Khurasan Mabanu Umayya kwa ubaguzi wao waliokuwa wakiwatendea wasiokuwa Waarabu katika Waislamu.
Watu walichaguliwa kueneza mwito wa Banul-Abbas huko Khurasani na Al-Kufa na akawa mkubwa wa kueneza mwito huu huko Al-Kufa ni Maysara Al-Abdi na aliendelea na mwito huu kimyakimya mpaka alipokufa katika mwaka wa 105 Hijria, akapewa kazi hii badala yake Bakir bin Mahan ambaye alipitisha juhudi kubwa mpaka alipofariki katika mwaka 127 Hijria.
Muda huu wote Mashekhe na watu fulani walikuwa wakieneza mwito huu vile vile huko Khurasani mpaka alipoingia Abu Muslim Al-Khurasani mji mkuu wa Khurasani katika mwaka wa 130 Hijria na baada ya kupita miaka miwili, miji mingi ya Iraq na Khurasani ilikuwa chini yake.
Katika mwaka 132 Hijria alipeleka majeshi kupigana na Banu Umayya na akaweza kumshinda Marwan Khalifa wa mwisho wa Banu Umayya na kuweza kusimamisha dola ya Banul-Abbas.
Baadhi ya Makhalifa wa ki-Abbasi:
1- As-Saffah - (132H-136H):
2- Al-Mansur - (136H-158H)
3- Al-Mahdi - (158H-169H)
4- Al-Hadi - (169H-170H)
5- Ar-Rashiid - (170H-193H)
6- Al-Amin - (193H-198H)
7- Al-Maamun - (198H-218H)
8- Al-Muutassim billah - (218H-227H)
9- Al-Waathiq - (227H-232H)
Mambo muhimu waliyoyafanya:
Ulidumu Ukhalifa wa kibanul-Abbas miaka 524, kuanzia mwaka 132 wa Hijra ilipovunjika dola ya kibanu Umayya mpaka mwa 656 wa Hijra, lakini dola yao ilikuwa na nguvu na thabiti zaidi katika zama zao za kwanza ambazo ziliendelea kwa muda wa 96, kisha ikadhofu kwa sababu ya kupunguwa nguvu za Makhalifa wao na kutegemea kwao Waturuki na makabila mengine katika kuisimamisha na kuithibitisha dola yao.
Dola ya ki-Abbasi ilifanya mengi katika zama zao na kusaidia sana katika kuenea ustaarabu wa kiislamu katika sehemu nyingi za ulimwengu. Aidha, ilisahilisha biashara baina ya umma na mataifa mbali mbali yaliyokuwa yakiishi katika zama zao kwa ajili ya uhusiano mzuri uliokuwepo baina yao na dola jirani. Vile vile, makabila mbali mbali yaliyoingia kwenye Uislamu katika zama zao yaliweza kushiriki katika kueneza dini ya kiislamu na elimu na ustaarabu wa kiislamu katika miji na nchi zao mbali mbali.
Nidhamu mbali mbali za kiuchumi na kisiasa na kibiashara ziligunduliwa katika zama hizi na vikasimama viwanda na mitambo na mabenki na mashimo ya madini na sanaa mbali mbali. Masoko yakazidi na mashule yakafunguliwa kila upande, na watu wakashughulika na elimu na kufasiri maarifa mbali mbali za umma zilizopita za kiyunani na kirumi na kihindi na kiajemi.
1- Abul-Abbas As-Saffah (132H-136H):
Alizaliwa Abdullahi bin Muhammad bin Ali bin Abdullahi bin Al-Abbas katika mji wa Hamima huko Jordan katika mwaka wa 105 Hijria, na babake ambaye ndiye mwanzilishi wa mwito wa Al-Abbas alikufa katika mwaka 125 Hijria akiwa As-Saffah ana umri wa miaka ishirini tu.
Alikuwa As-Saffah ni kijana mzuri wa sura mweupe na mwenye haiba, mrefu na mtulivu. Alikuwa ni shujaa na karimu sana kufikia hadi kupigiwa mfano kwa ukarimu wake. Aliishi kwa muda wa miaka thalathini na moja tu na alioa mke mmoja tu.
Juu ya kuwa Abul-Abbas As-Saffah alikuwa ni mtu mwema na karimu, lakini kwa ushujaa wake mkubwa alibandikizwa jina la As-Saffah (Muuaji) ambalo liliwasaidia sana Mabanul-Abbas mwanzo kuweza kuuthibitisha utawala wao kwa sababu ya kuingiza khofu ndani ya nyoyo za maadui wao, na juu ya kuwa mwenye jina hili mwenyewe alikuwa si mtu mwenye kupenda ukubwa, lakini jamaa zake ambao walikuwa wakipigania kupata ukubwa huu waliweza kujizatiti wakiwa naye na kuwatenga watu wa kambo kuukaribia utawala huu.
Baada ya kushika Ukhalifa, alichagua As-Saffah mji wa Al-Kufa, Iraq kuwa ndio mji mkuu wake, lakini baadaye akahamia Al-Anbaar na kuufanya kuwa ndio mji mkuu wa dola ya Banul-Abbas. Hakuishi As-Saffah muda mkubwa sana kwani alibakia katika Ukhalifa kwa muda wa miaka minne na miezi tisa kisha akafariki katika mwaka wa 136 Hijria na kabla ya kufa akamchagua nduguye Abu Jaafar Al-Mansur kuwa ndiye atakayechukuwa Ukhalifa baada yake.
2- Abu Jaafar Al-Mansur (136H-158H):
Abu Jaafar Al-Mansur ni Abdullahi bin Muhammad bin Ali bin Abdillahi bin Al-Abbas. Alizaliwa Al-Mansur katika kijiji cha Al-Hamima, Jordan mwaka wa 95 Hijria, na alikuwa ni mtu mwenye busara na hekima na mpole na mwenye tabia njema, lakini vile vile alikuwa na haiba na nguvu na ushujaa mkubwa, naye Al-Mansur anachukuliwa kuwa ndiye muanzilishi hasa wa dola ya Banul-Abbas kwa sababu ya kuweza kuvinyamazisha vita mbali mbali alivyokuwa akipambana navyo na kuwashinda maadui wa dola hii na kuleta amani kwenye dola na kuzithibitisha nguzo zake na kuizatiti misingi yake.
Mambo muhimu aliyoyafanya:
Baada ya kuwashinda maadui na kuleta amani katika nchi, alifanya bidii kuzijenga upya zile ng'ome ambazo zilivunjwa na Warumi, na kuwaweka maaskari ndani yake. Aidha, alijenga mji wa Baghdad katika mwaka wa 145 Hijria na ukawa unajulikana kwa jina la "Darussalam".
Vile vile, alitumia nidhamu ya upelekaji wa barua katika kuwachunguza maliwali na kuwahukumu ikiwa watafanya makosa. Kama vile vile, alivyojishughulisha na mambo mengine ya dola.
Kufariki kwake:
Alifariki Al-Mansur katika mwaka wa 158 Hijria wakati alipokuwa yuko njiani kwenda kuhiji, na alikuwa ameandika kuwa mwanawe Al-Mahdi ashike Ukhalifa baada yake.
3- Al-Mahdi (158H-169H):
Al-Mahdi ni Muhammad bin Al-Mansur, naye alizaliwa katika mwaka wa 126 Hijria, na mamake alikuwa ni Arwa Al-Himyari mwanamke wa kiyemeni, naye alikuwa ni kijana mrefu na hadharani mwenye nywele za mapindi. Alichaguliwa kuwa Khalifa baada ya kufa babake Al-Mansur katika mwaka wa 158 Hijria, akiwa na umri wa miaka 32.
Alikuwa ni kijana mwema na karimu, mwingi wa elimu na fasihi wa maneno, mwenye akhlaki njema na tabia nzuri, shujaa na muadilifu na akipendwa na raia zake kwa sababu ya kuwapigania haki zao na kuzuia wasifanyiwe dhulma. Aliwarudishia watu ambao katika zama za babake walinyanganywa mali zao na kuwapa haki zao na wala alikuwa hawapendelei na kuwapa watu wake mali ya umma.
Alioa Al-Mahdi binti wa ami yake Umm Abdallah bint Saleh bin Ali, na alipokwenda Madina alimuoa Ruqayya bint Amr, na vile alimuacha huru kijakazi wake Al-Khayzuran na kumuoa na alikuwa akimpenda sana na ndiye mama wa wanawe wawili Al-Hadi na Harun ambao waliokuja kushika Ukhalifa baada yake.
Mambo muhimu aliyoyafanya:
1- Alijenga msikiti wa Ar-Rusafa katika mwaka 159H.
2- Aliupanua msikiti wa Makka katika mwaka 167H.
3- Alimchagua Abu Yusuf sahibu wa Abu Hanifa katika mwaka wa 166H kuwa ndiye Kadhi na alikuwa ni katika wanazuoni wakubwa wa zama zake.
Kufariki kwake:
Alifariki Al-Mahdi katika mwaka 169 Hijria akiwa na umri wa miaka 43, na alikaa katika Ukhalifa muda wa miaka kumi na mwezi unusu.
4- Al-Hadi (169H-170H):
Musa Al-Hadi ni mtoto mkubwa wa Al-Mahdi, na babake aliusia ashike Ukhalifa baada yake Al-Hadi kisha Ar-Rashiid, na alipokufa babake alikuwa bado yuko vitani lakini nduguye Harun alimpelekea habari na kumuonyesha utiifu wake kama Khalifa mpya baada ya babake.
Alikuwa Al-Hadi ni mtu shujaa sana na karimu na alikuwa muda mkubwa wa maisha yake katika vita na jihadi, na kwa hivyo alikuwa ni mtu aliyezowea maisha ya taabu na shida. Juu ya hivyo, alisifa Al-Hadi kwa ukarimu mkubwa kufikia hadi kufanya israfu katika kutoa kwake.
Al-Hadi alipambana na matatizo mengi aliyoyawacha babake Al-Mahdi na kwa hivyo alipitisha juhudi kubwa kuondosha matatizo mbali mbali aliyorithi kutoka kwa mzee wake mpaka akashinda.
Kufa kwake:
Ukhalifa wa Al-Hadi haukuendelea muda mkubwa kwani alitawala kiasi cha mwaka na kitu tu kisha akafariki dunia, na siku aliyokufa ni siku ambayo alitawala Harun na kuzaliwa Al-Amin.
5- Ar-Rashiid (170H-193H):
Harun Ar-Rashiid alizaliwa mwaka wa 145 Hijria, na mamake ni mwanamke wa kiyemeni aitwaye Al-Khayzuran, na Harun aliusiwa na babake Al-Mahdi ashike Ukhalifa baada ya nduguye Al-Hadi, ijapokuwa mamake alikuwa anapendelea Harun ashike mwanzo kabla ya Al-Hadi kwa sababu ya uhodari wake na uwezo wake mkubwa wa kuendesha nchi.
Harun alishika Ukhalifa usiku ule ule aliokufa nduguye Al-Hadi katika mwezi wa mfungo sita mwaka wa 170 Hijria. Alikuwa Harun Ar-Rashiid ni mtu mrefu mwenye mwili na mweupe na mzuri wa sura. Aidha, alikuwa akijulikana kwa ufasaha wake na akipenda mashairi na elimu na alikuwa akikaribisha washairi na wanazuoni katika baraza lake na kuwakirimu na kuwapenda sana.
Vile vile, alikuwa Harun Ar-Rashiid mtu mcha Mungu sana, na alikuwa akihiji mwaka na kwenda kupigana jihadi mwaka mwengine, na ndiye Khalifa wa pekee alikwenda kuhiji Makka kutoka Baghdad kwa miguu. Aidha, alikuwa akiwapeleka watu kuhiji kwa mali yake ikiwa yeye hakwenda.
Katika zama zake mji wa Baghdad ulipanuka sana na kuwa mji mkubwa wenye wakaazi wengi na majumba makubwa makubwa na kufikia kipeo kikubwa cha ustaarabu na maarifa na zilikuwa biashara na misafara ya bidhaa zikija kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu. Aidha, utajiri ulizidi na mali yalikusanyika katika Baytul-Mal na kuzidi sana.
Kadhalika, ulikuwa mji wa Baghdad mashuhuri kwa elimu na wanazuoni na mafakihi na washairi, na alikuwa Harun ni mtu mwenye siasa nzuri na dola nyenginezo na kwa hivyo umaarufu wake ulienea kila mahali.
Mambo muhimu katika zama zake:
1- Vita na Michafuko:
Katika zama zake kulitokea matatizo mbali mbali, na katika hivyo ni vita alivyovisimamisha Al-Walid Ash-Shari ambaye alisimama kupigana na majeshi ya Harun na kuyashinda mara chungu nzima na kuteka sehemu mbali mbali za dola ya kiislamu mpaka alipompeleka Harun Yazid Ashaybani kwenda kuukata mzizi huu wa fitna na kumshinda na kumuua.
Aidha, sehemu za Afrika ya Kaskazini yaliendelea makabila ya kibarbari kupigana na majeshi ya ki-Abbasi mpaka alipompeleka Harun kiongozi aitwaye Harthama na jeshi kubwa ambalo liliweza kuwashinda Mabarbari huko, lakini baadaye Ibrahim bin Al-Aghlab liwali aliyewekwa na Harun Ar-Rashiid kuwatia adabu Mabarbari huko alisimamisha dola yake akaiita dola ya Al-Aghaliba na baada ya muda ikawa ni kama dola huru iliyojitenga.
Vile vile, huko Damaskas Sham, kulitokea mchafuko mkubwa baina ya makabila ya Kiyemeni na ya Kihijazi yakaendelea kupigana kwa muda wa miaka miwili tangu mwaka 176 Hijria mpaka alipoingilia Harun na kuzima moto wa vita hivi.
2- Mabarmaki:
Mabarmaki walikuwa ni watu waliokurubishwa sana na Maabbasi na wakati wa Harun Ar-Rashid walikuwa na nguvu na satwa kubwa na alikuwa Khalid bin Yahya Al-Barmaki ndiye Waziri wake na mambo yote ya nchi alikuwa akiyaendesha yeye na watoto wake wanne, na kwa hivyo watu walikuwa wakiwapenda na kuwatungia mashairi na kuwapigia mifano kwa ukarimu wao na wema wao.
Kufa kwake:
Alizidiwa Harun na maradhi na alipoambiwa na tabibu kuwa hana tamaa ya kupona, aliusia ashike mwanawe Al-Amin Ukhalifa na baada yake Al-Maamun, na kuubandika wasia huu kwenye ukuta wa Al-Kaaba huko Makka, kisha akafariki dunia katika mwaka wa 193 Hijria akiwa na umri wa miaka arubaini na nne na miezi minne.
6-Al-Amin (193H-198H):
Muhammad Al-Amin alizaliwa mwaka 170 Hijria, na alikuwa amepishana na nduguye Abdullahi Al-Maamun kwa miezi sita akiwa Abdullahi ndiye mkubwa. Mamake Al-Amin alikuwa ni Zubeyda Al-Hashimiya mwanamke wa kikureshi, na kwa kuwa baba na mama wa Al-Amin walikuwa wanatokana na Banu Hashim, basi yeye alikuwa ni Khalifa pekee wa kibanul-Abbas ambaye alikuwa anatokana na Banu Hashim kwa baba na mama.
Kabla ya kufariki Harun Ar-Rashiid aliusia ashike mwanawe huyu Al-Amin Ukhalifa kisha ndio uende kwa nduguye mkubwa Al-Maamun, na kwa hivyo katika mwaka wa 193 Hijria alipofariki Harun alitawazwa Al-Amin kuwa Khalifa na baada yake ashike Al-Maamun.
Alikuwa Al-Amin ni kijana mwenye sura na umbo zuri na alikuwa ni mrefu mweupe na mwenye nguvu nyingi na ushujaa mkubwa, na ni mtu mwenye akili na aliyesoma sana mwenye kuijua lugha yake uzuri na ufasaha mkubwa na mwenye kuhifadhi mashairi mengi, lakini alikuwa si mtu mwenye siasa na akipenda sana mchezo na starehe na kukaribisha waimbaji na washairi na kuwatumilia mali kwa israfu.
Kwa hivyo, katika wakati wake kukazuka fitina mbali mbali na fujo za hapa na pale na kusababisha vita baina ya Waarabu wenyewe kwa wenyewe. Aidha, alijaribu kumkiuka nduguye na kutaka kumpa Ukhalifa mwanawe badala yake juu ya kuwa babake aliweka ahadi kwenye ukuta wa Al-Kaaba na kuwashuhudisha wanazuoni na raia kuwa Ukhalifa baada ya kufariki Al-Amin uende kwa Al-Maamun.
Jambo hili ambalo lilizidi kutiliwa nguvu na waziri wake Al-Fadhl bin Ar-Rabii lilimpeleka Al-Amin kutuma mtu kwenda Makka na kuuiba mkataba huu uliobandikwa kwenye ukuta wa Al-Kaaba na kuvunja ahadi ya babake, kisha akampelekea ndugu yake barua kumtaka aje Baghdad, lakini Al-Maamun alitambua hila anayotaka kuitumia Al-Amin, hasa ilivyokuwa keshaanza kumuuzulu nduguye mwengine Al-Qasim, na alivyompelekea barua kumtanguliza mwanawe mdogo Musa kushika Ukhalifa baada yake, alisimama Al-Maamun kupigana na nduguye Al-Amin mpaka akamshinda na kuuliwa Al-Amin.
Mwisho wake:
Aliishi Al-Amin muda mdogo tu akiwa ni Khalifa, kwani alitawala kwa muda wa miaka minne na miezi minane na siku tano tu, na kuuliwa akiwa na umri wa miaka 28 katika mwezi wa mfungo sita mwaka wa 198 Hijria.
7-Al-Maamun (198H-218H):
Inaelezwa kuwa siku aliyozaliwa Al-Maamun ndio siku ambayo alikufa Khalifa yaani ami yake Al-Hadi na kutawazwa Khalifa yaani babake Harun Ar-Rashiid, na ulikuwa mwaka 170 Hijria. Mamake alikuwa akiitwa Marajil na alikuwa Al-Maamun ni ndugu wa Al-Amin kwa baba tu, mama zao wakiwa ni mbali mbali.
Kama tulivyoeleza, Harun Ar-Rashiid kabla ya kufariki aliusia Ukhalifa uende kwa Al-Amin kwanza kisha kwa nduguye Al-Maamun, lakini Al-Amin alitaka kupitisha khiyana na kumpa Ukhalifa mwanawe Musa badala ya nduguye Al-Maamun, jambo ambalo lilizusha vita na kusababisha ndugu kuuana.
Baada ya kushindwa Al-Amin katika vita na kuuliwa, watu walimchagua Al-Maamun kuwa ndiye Khalifa wao akiwa bado yuko Khurasan.
Al-Maamun alirudi Baghdad katika mwaka 204 Hijria na kuendelea kutawala mpaka mwaka 218 Hijria, na katika muda huu alifanya mengi na kuleta mambo mengi mapya, naye alikuwa ni katika Makhalifa bora wa kibanul-Abbas na mwenye kupenda sana elimu na maarifa, na alikuwa ni mtu mwenye kupenda kusamehe watu, na hakuwa akipenda starehe na upuzi na alijishughulisha sana na kukusanya vitabu vya elimu vilivyoandikwa kwa lugha mbali mbali na kuamrishwa vifasiriwe kwa lugha ya kiarabu.
Katika zama zake kulizuka vita vingi, katika hivyo ni vita vya Abu Saraya ambaye alianzisha vita baada ya kuchelewa kulipwa mishahara yeye na kikosi chake na kuuzuliwa mkubwa wao, akasimama kuiteka Al-Kufa na nchi jirani yake. Jeshi la Khalifa likasimama kupigana naye mpaka akashindwa na kuuliwa katika mwaka wa 200 Hijria.
Vile vile, kabla ya kuwasili Baghdad, ilipita njama kutawazwa Ibrahim bin Mahdi ami yake Al-Maamun kuwa Khalifa wa Waislamu katika mwaka 202 Hijria naye akakubali, lakini Al-Maamun alitumia hekima na kuanza kuyashinda majeshi ya upinzani akiwa katika safari yake kurudi Baghdad, na kabla ya kufika Baghdad, ami yake aliingiwa na khofu na kukimbia kwenda kujificha na kwa hivyo Al-Maamun akarudi katika utawala wake. Kisha baadaye alikuja akamsamehe ami yake Ibrahim kwa kutaka kumnyang'anya haki yake ya Ukhalifa.
Aidha, katika vita vilivyozuka katika zama za Al-Maamun ni vita vya Nasr bin Shiith ambaye hakupendelea kuona wasiokuwa Waarabu wanapewa mbele kuliko Waarabu, hasa baada ya kumshinda Al-Maamun Al-Amin, na kwa hivyo akakusanya jeshi na kupigana na jeshi la Khalifa, lakini Al-Maamun aliweza kumshinda akasalimu amri na kurudi Baghdad katika mwaka 210 Hijria.
Kadhalika, katika vita vilivyozuka katika zama zake ni vita vya Az-Zutt, watu waitwao An-Nawar wenye asli ya kihindi, waliitumia fursa ya jeshi la Khalifa kushughulika na vita wakawa wanafanya uharibifu na fasadi katika nchi, na ijapokuwa Al-Maamun alijaribu sana kupigana nao na kuukata mzizi huu wa fitina, lakini hakuweza kuwakomesha mpaka aliposhika Al-Muutasim katika mwaka wa 219 Hijria.
Aidha, kulizuka mgogoro mkubwa huko Misri baina ya Waarabu wa Kusini na Waarabu wa Kaskazini, kwa sababu Waarabu wa Kusini (Wayemeni) walikuwa wanamuunga mkono Al-Maamun na wa Kaskazini wanamsaidia Al-Amin, basi hili likaleta zogo na mchafuko na vita baina yao mpaka alipoingilia Al-Maamun yeye mwenyewe na kusitisha vita hivi.
Vile vile, kama zilivyosimama dola za Aghaliba na Adarisa huko Tunis na Morocco katika zama za Harun Ar-Rashiid babake Al-Maamun, zilisimama katika zama zake dola ya Tahiria huko Khurasan na dola ya Az-Ziyadiya huko Yemen, ambazo hatimaye zikajitenga.
Aidha, katika zama zake kulizuka tatizo la Qurani na kujadiliana wanazuoni na mafakihi kuhusu kuumbwa kwake. Baadhi yao wakasema kuwa Qurani ni maneno ya Mwenyezi Mungu na kwa hivyo hayakuumbwa, na wengine wakasema kuwa Qurani kama vitu vyengine vyote imeumbwa, mjadala ambao ulileta mgogoro mkubwa na kusabibisha wanazuoni kuteswa na katika hao alikuwa Ahmad bin Hanbal imamu wa madhehebu ya kihambali.
Khalifa baada yake:
Al-Maamun mwanzo alimchagua Ali bin Musa Ar-Ridha katika kizazi cha Ali bin Abi Talib kuwa ndiye mwakilishi wake baada ya kufa kwake, na kwa hivyo akawa ni Khalifa wa kwanza wa kibanul-Abbas kuchagua katika Alawiyin kuwa Khalifa baada yake, lakini baada ya vita vya Baghdad dhidi ya Ibrahim bin Al-Mahdi ami yake na kufa kwa Ali Ar-Ridha, alimchagua nduguye Al-Muutasim kuwa ndiye atakayekuwa Khalifa baada yake.
Kufariki kwake:
Katika vita vya mwisho alivyopigana Al-Maamun na Warumi katika mwaka 218 Hijria, alishikwa na homa kaskazini ya mji wa Tus na kufariki akiwa na umri wa miaka 48.
8-Al-Muutassim (218H-227H):
Muhammad Al-Muutassim ni mtoto wa Harun Ar-Rashid kwa mkewe mwengine aitwaye Maarida, na kwa hivyo alikuwa ni ndugu yake Al-Maamun kwa baba tu, lakini pamoja na hayo aliahidi Al-Maamun akifa ashike Ukhalifa nduguye huyu Al-Muutassim badala ya kumpa mwanawe Al-Abbas ambaye alikuwa akipendwa sana na majeshi, na akamnasihi akae na raia kwa wema Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika wao.
Baada ya kufariki Al-Maamun katika mwaka wa 218 Hijria, watu walimchagua Al-Muutassim kuwa ndiye Khalifa wao na kuonyesha utiifu wao kwake, na juu ya kuwa jeshi lilipinga mwanzo mwanzo lakini aliposimama Al-Abbas na kumuunga mkono ami yake, jeshi nalo likamkubali.
Alikuwa Muutassim ni mtu mwenye busara na karimu na shujaa, na alikuwa na umbo zuri na mwili wa kujaza wenye nguvu na rangi yake ilikuwa nyeupe iliyovilia wekundu na macho yake yalikuwa ni mazuri na makubwa. Alikuwa ni mwenye kujishughulisha sana na mambo ya vita na mwenye haiba kubwa mbele ya watu, lakini alikuwa akipenda sana maskini na wanyonge na akiwashughulikia na kuwatazama.
Mambo muhimu aliyoyafanya:
1- Aliweza Al-Muutassim kumshinda Babek Al-Kharmi na kuivunja madhehebu yake na kuwaua wengi katika wafuasi wake baada ya kupigana nao kwa muda wa zaidi ya miaka ishirini.
2- Alipigana na majeshi ya kirumi na kuyatia adabu na kuyashinda katika vita mbali mbali.
3- Aliingiza katika jeshi lake Waturuki wengi mpaka wakakithiri na kuanza kuwaudhi raia, mpaka ikambidi kujenga mji aliyouita Samuraa na kuwaondosha majeshi yake Baghdad na kuwaweka huko, na kuhamia yeye mwenyewe huko.
4- Alipambana Muutassim na harakati mbali mbali ambazo zilijaribu kusimama dhidi yake na kupeleka majeshi yake kuzivunja harakati hizi.
Kufariki kwake:
Alifariki Al-Muutassim dunia katika mwaka wa 227 akiwa na umri wa miaka 48 baada ya kushikwa na maradhi kwa muda mdogo.
9-Al-Waathiq (227H-232H):
Al-Waathiq jina lake ni Harun bin Al-Muutassim, naye alizaliwa na mama wa kirumi aitwaye Qaraattis katika mwaka 186 Hijria, na alikuwa tangu utotoni mwake ni kijana aliyekuwa na akili na busara kubwa, na babake akimtegemea sana katika mambo mengi, hata alipohamia Samuraa alimwacha yeye Baghdad ahukumu.
Alikuwa Al-Waathiq akimpenda sana ami yake Al-Maamun na alikuwa akijaribu kumuigiza nyenendo zake na sifa zake na kwa hivyo alikuwa akiangalia raia zake kwa uzuri na kuwashughulikia maskini na mafakiri, na alikuwa hodari na mjuzi na fasihi na mshairi mzuri. Aidha, kama ami yake alikuwa akiunga mkono wanazuoni wenye kusema kuwa Qurani imeumbwa na kwa hivyo alikuwa akiwatesa wanazuoni wenye kwenda kinyume na rai hii.
Al-Waathiq kama babake Al-Muutassim aliingiza Waturuki wengi katika jeshi lake na kuwapa vyeo vikubwa vikubwa na kuufanya mji wa Samuraa kuwa ndio makao makuu ya Ukhalifa, na kwa hivyo nguvu na satwa za Waturuki zikazidi na kupindukia mipaka na Ukhalifa ukaanza kudhoofu na kutegemea sana Waturuki, jambo ambalo lilibadilisha mwenendo wa Makhalifa na kusababisha kuanguka kwa dola ya kibanul-Abbas.
Kufariki kwake:
Alihukumu Al-Waathiq kiasi ya miaka sita na alipokuwa anakufa katika mwaka wa 232 Hijria, alikataa kumchagua mwanawe kuwa Khalifa baada yake kwa kuchelea kuchukua jukumu la umma katika uhai wake na baada ya kufa kwake, na alipofariki ulikuwa Ukhalifa wa kibanul-Abbas umekamilisha karne nzima tangu kusimama, na baada yake walikuja Makhalifa ambao hawakuwa na satwa wala nguvu kwani utawala ulikuwa katika mikono ya Waturuki ambao walikuwa wakimweka Khalifa wampendaye na kumuondosha wampendaye.
Ukhalifa wa Ki-Abbas wa Pili:
Baada ya kufariki Al-Waathiq katika mwaka 232 Hijria, na kukithiri Waturuki katika jeshi la Banul-Abbas, ilianza zama ambayo Makhalifa walikuwa ni kama pambo la dola ya kiislamu, lakini nguvu na satwa ya kweli kweli ilikuwa katika mikono ya Waturuki, wanamueka wamtakaye na wanamuondosha wamtakaye.
Waturuki walianza kuingia katika jeshi la dola ya kiislamu katika zama za Al-Muutassim wakati alipoona kuwa Wafursi walikuwa na nia ya kuutawala ulimwengu wa kiislamu kwa njia ya kizazi cha Ali bin Abi Talib au Al-Alawiyyin, na vile vile alivyoona Waarabu wako dhidi yake, na kwa hivyo akaanza kubadilisha jeshi lake kwa kuwaingiza Waturuki ambao walikuwa ni watu mashujaa sana katika vita na waliokuwa wakisifika kwa ujasiri wao na ukali wao.
Nguvu za Waturuki zilizidi wakati wa Al-Waathiq na satwa yao ikakamilika, hasa ilivyokuwa wao ndio waliokuwa walinzi wa dola na wa Khalifa mwenyewe, na ikawa kila kitu katika mikono yao, na baada ya kushika Al-Mutawakkil katika mwaka 232 Hijria, nguvu na satwa yao zilifurutu ada kufikia hadi kumuua Khalifa Al-Mutawakkil katika mwaka 247 Hijria na kumweka Al-Muntasir katika mwaka 247 Hijria, na baada ya mauaji haya waliendelea Waturuki kufanya wanalotaka kwa Makhalifa ambao walitawala katika zama zao wakitokea kwenda kinyume nao.
Makhalifa waliotawala katika zama hizi za Waturuki (Al-Mamaliik) ni hawa wafuatao:
1- Al-Mutawakkil (232H-247H)
2- Al-Muntassir (247H-248H)
3- Al-Musta'in (248H-252H)
4- Al-Muutazz (252H-255H)
5- Al-Muhtadiy (255H-256H)
6- Al-Muutamid (256H-279H)
7- Al-Muutadhid (279H-289H)
8- Al-Muktafiy (289H-295H)
9- Al-Muqtadir (295H-320H)
10- Al-Qaahir (320H-322H)
11- Al-Raadhi (322H-329H)
12- Al-Muttaqi (329H-333H)
13- Al-Mustakfi (333H-334H)
Pamoja na kuwa Waturuki walikuwa ndio wenye kuendesha dola ya kiislamu na Makhalifa walikuwa ni jina tu, lakini kuwepo kwao kama viongozi wa dola kulikuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu wao ndio waliokuwa wakikubaliwa na raia kuwa ndio viongozi wa kisharia wa dola na kwa hivyo Waturuki walilazimika kuwaweka na kuwasimamisha kama wawakilishi rasmi wa dola ya kiislamu.
Baada ya Waturuki, walishika hatamu ya dola ya kiislamu Buwayhiyun ambao waliendelea kuendesha dola hii tangu mwaka wa 334 Hijria mpaka mwaka wa 467 Hijria na Makhalifa waliokuwa wakitawala katika zama hizi ni hawa wafuatao:
1- Al-Mutti' (334H-364H)
2- Al-Ttaai' (364H-381H)
3- Al-Qadir (381H-422H)
4- Al-Qaim (422H-467H)
Kisha dola ya kiislamu ikawa chini ya uwongozi wa Salaajiqa ambao walishikilia uwongozi tangu mwaka wa 467 Hijria mpaka 656 Hijria ambao hukumu ya Makhalifa wa kibanul-Abbas ilimalizika, na walioshika Ukhalifa katika zama hizi ni hawa wafuatao:
1- Al-Muqtadi (467H-487H)
2- Al-Mustadh-hir (487H-512H)
3- Al-Mustarshid (512H-529H)
4- Al-Rashid (529H-530H)
5- Al-Muqtafi (530H-555H)
6- Al-Mustanjid (555H-566H)
7- Al-Mustadhi' (566H-575H)
8- Al-Nasir (575H-622H)
9- Al-Dhahir (662H-623H)
10- Al-Mustansir (623H-640H)
11- Al-Mustaasim (640H-656H)
Sababu ya kuvunjika dola ya ki-Abbasi:
Kudhofu Ukhalifa wa ki-Abbasi (232H-334H):
Baada ya kushika Al-Mutawakkil Ukhalifa katika mwaka wa 232 Hijria mpaka miaka mia iliyofuatia baada yake, Ukhalifa wa ki-Abbasi ulianza kudhofu na nguvu za Makhalifa kupungua mpaka wakawa ni Makhalifa jina tu, lakini mambo yote yakawa yanaendeshwa na Waturuki, na dola ya kiislamu ikawa kwa hakika inahukumiwa na wao.
Sababu ya haya ni kuwa baada ya kuchaguliwa Al-Mutawakkil kuwa Khalifa, alianza kuwakurubisha Waturuki na kuwapa vyeo vya kijeshi badala ya Waarabu walioisimamisha dola hii na kuipa nguvu, na kwa hivyo Waarabu wakawa hawaiungi mkono dola hii, na kila kitu kikawa kinaendeshwa na Waturuki na Wafursi.
Aidha, dola ya kibanul-Abbas ilipata upinzani mwengine kutokana na Maalawiyyin (Kizazi cha Ali na wafuasi wake) kwa sababu ya kuwapokonya haki yao ya kuhukumu dola ya kiislamu baada ya kuwa wao ndio waliopigana na kusimama kuwapinga Mabanu Umayya mpaka wakawashinda na kuurudisha Ukhalifa katika mikono ya Banu Hashim, lakini Mabanul-Abbas wakatawala wao na kuwanyima haki hii Maalawiyyin ambao ndio waliosimamisha upinzani hasa dhidi ya Banu Umayya.
Vile vile, katika zama hizi kulizuka watu wasioamini Mwenyezi Mungu na wazandiki na wanafiki ambao walikuwa wakidhihirisha imani lakini kwa hakika walikuwa ni Makafiri, na pia kulikuwa na mataifa mbali mbali ya watu ambayo yalikuwa yakihitalifiana katika itikadi na madhehebu, na kusababisha kugawanyika Waislamu katika makundi na mafungu tofauti tofauti, na haya yote yakaleta kudhoofika kwa dola hii na mwisho kuvunjika katika mwaka wa 656 Hijria ilipovamiwa na majeshi ya kitatari.
Al-Mutawakil (232H-247H):
Baada ya kufariki Al-Waathiq, Khalifa wa 9 wa Banul-Abbas, aliondoka duniani bila ya kuagizia mwanawe kushika Ukhalifa baada yake na kwa hivyo, akachaguliwa Al-Mutawakkil nduguye Al-Waathiq kuwa ndiye Khalifa baada yake.
Alizaliwa Jaafar Al-Mutawakkil katika mwaka wa 206 Hijria huko Iraq na alikuwa ni ndugu ya Al-Waathiq kwa baba tu, maana mamake alikuwa ni mwengine si mwanamke wa kiarabu, na alifanya bidii kumlea mwanawe na kumkuza na kumtayarisha awe Khalifa.
Katika zama za Al-Mutawakkil kulikuwepo na makundi mbali mbali ya Waislamu lakini yeye alikuwa akiwapenda Ahlus-Sunna
1- Kutawala Majeshi dola ya kiislamu:
Nguvu za Majeshi zilizidi mpaka wakawa wao ndio wenye kuendesha dola, na kwa hivyo Waturuki waliweza kuhukumu kwa muda wa miaka ya kiasi mia, kuanzia mwaka wa 247 Hijria mpaka 334 Hijria, kisha baada yake zikazidi nguvu za Maaskari wa kibuweyhi ambao walikuwa ni Wafursi na ni Mashia na wakaendelea kuhukumu dola ya kiislamu kwa muda wa zaidi ya miaka mia, tangu 334 Hijria mpaka 447 Hijria. Baada yake yakaja tena majeshi ya kituruki ya kisuljuqi na kuwashinda nguvu Mabuweyhi na kuhukumu wao kuanzia mwaka wa 447 Hijria mpaka 656 Hijria.
2- Kuzuka dola mbali mbali:
Dola ya kiislamu ilikuwa moja tangu ilipoanzishwa na Mtume (SAW) mpaka zama za Makhalifa wanne Waongofu, ndipo ilipotokea fitna na akajitangaza Muawiya kuwa ni Khalifa na kusimamisha vita dhidi ya Ali bin Abi Talib. Chokochoko hizi ziliendelea vile vile zama za Abdullahi bin Zubeyr mpaka wakasimama na kumpiga vita na kumuua katika Ukhalifa wa AbdulMalik bin Marwan. Ukhalifa wa Banu Umayya uliendelea miaka mingi lakini ulipoanguka na wakashika Banul-Abbas ilizuka dola ya Banu Umayya huko Andalus Uhispania, na baada yake dola nyengine zikazuka sehemu za Mashariki na Magharibi na zikajitenga na Ukhalifa wa Banul-Abbas.
3- Kuenea fasadi:
Baada ya kuzidi ukubwa wa dola ya kiislamu na kuenea sehemu kubwa kabisa ya ulimwengu, tokea mipaka ya China na Urusi upande wa Mashariki mpaka mipaka ya Morocco na Uhispania upande wa Magharibi, na baada ya kupungua nguvu za Makhalifa na kujitenga dola mbali mbali ndani ya dola hii kubwa ya Uislamu, Waislamu waliacha Jihadi na kushughulika na neema na mali nyingi furifuri walizozipata kutoka sehemu hizi na wengine wengi wakaingilia mambo ya starehe na anasa, na fasadi ikaenea na ulevi na nyimbo na mambo ya upuuzi, ndipo Mwenyezi Mungu akawabadilishia watu mwenendo wao na kuwaletea mitihani mikubwa na fitna mbali mbali ambazo zilisababisha kuivunja dola hii kubwa ya kiislamu.
4- Njama na vitimbi:
Mayahudi na Manasara na Majusi walivyoona Uislamu unatapaka kila sehemu na dola yao inazidi kupanuka na kuwa na nguvu kubwa, walianza kupitisha njama na vitimbi mbali mbali ili kuidhoofisha dola hii na kuanza kuanzisha harakati za kisiasa na za kidini na za kimadhehebu zenye nia ya kuuchafua Uislamu na kuleta chokochoko baina ya jamii mbali mbali za kiislamu, na zikasababisha harakati hizi migorogoro na michafuko mingi baina ya Waislamu na kuleta fitna na vita ambavyo viliweza kuondosha utulivu na amani katika dola na kusababisha mauaji makubwa baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe. Na katika njia walizozitumia kuvutia watu katika harakati hizi ni mali na wanawake kwa upande mmoja na fasadi na khofu kwa upande mwengine ili kufikia muradi wao.
5- Vita vya Msalaba:
Baada ya kusita Jihadi na kuzidi matatizo baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe, na baada ya dola ya kiislamu kuanza kudhofu, Manasara walichukuwa fursa ya kulipiza kisasi cha kuchukuliwa nchi zao zilizokuwa chini ya utawala wa kirumi huko Asia na Afrika, na kwa hivyo walikutana wakubwa wa kanisa katika mwaka wa 489 Hijria na kuamua kuanzisha vita dhidi ya Waislamu ambavyo vilijulikana kwa jina la vita vya Salibiya au vita vya Msalaba, na akaamrisha Baba Mtakatifu yakutane majeshi katika mji wa Kostantinia (Constantinople), lakini majeshi haya yalipokuwa yanaelekea Kostantinia yalileta mchafuko na uharibifu mkubwa na kuua watu wengi na kunyanga'nya mali na kuharibu miji waliokuwa wakiipita njiani mwao kuelekea huko. Baada ya kukutanika walianza safari yao kuingia katika miji ya kiislamu ambayo yalikumbana na uharibifu mkubwa wa mali na nchi na mauaji yasiyokuwa na sababu wala kikomo mpaka waliposimama Waislamu kila upande kusitisha uovu na uharibifu huu na kupigana Salahuddin Al-Ayyubi na majeshi yake mkusanyiko wa majeshi ya kikristo mpaka akairudisha Baytul-Maqdis kwenye mikono ya Waislamu na kuwashinda Wafalme wa Ulaya waliokusanyika kuihujumu dola ya kiislamu.
6- Mavamizi ya Maghul:
Maghuli ni makabila ya kitatari na kimaghuli yanayotoka sehemu za Uchina na Urusi na Mongolia yaliyojumuika chini ya uongozi wa Jenghis Khan na kuanza kuvamia miji mbali mbali, mwanzo sehemu za karibu karibu na Asia, kisha baada ya ushindi mkubwa walioupata, walipata moyo na kuzidi hamasa kutaka kuteka miji mengine. Makabila haya yalizidi kushajiika kutaka kuvamia dola ya kiislamu walipopata habari kutoka kwa Wafalme wa kizungu kuwa nchi za kiislamu zina kheri nyingi na mali isiyokuwa na kifani. Kwa hivyo, katika mwaka wa 616 Hijria majeshi ya ki-Maghuli yalivuka mto wa Seihun na kumwagika kwenye nchi za kiislamu na kuua watu na kuvunja majumba na kuchoma mashamba na misikiti na maktaba, na kuanza kuteka mji baada ya mji mpaka wakaingia Baghdad katika mwaka wa 656 Hijria na kumuua Holako Al-Mustaassim Khalifa wa mwisho wa dola ya ki-Abbasi na kusababisha kuvunjika kwa dola ya Banul-Abbas.