Fatimiya

Dola ya Faatimiya - Afrika Kaskazini, Hijaz, na Sham:
(297H-567H/(909AD-1171AD):

Mafatimi ni watu wanaojinasibisha na Fatma binti wa Mtume (SAW) nao ni kizazi cha Ali bin Abi Talib (RA). Hawa walikuwa ni vikundi mbali mbali vya kishia waliokuwa wakiona kuwa Ukhalifa ni haki yao ya kijadi na kuwa Banu Umayya waliwanyang'anya.

Baada ya kushindwa Banu Umayya na Banu Abbas kizazi cha ami yake Mtume (SAW), walikhitalifiana Banu Hashim wa kizazi cha Ali na Banu Abbas na kukazuka vita vingi baina yao baada ya kushikilia Banu Abbas Ukhalifa badala ya kizazi cha Ali bin Abi Talib (RA). Mafatimi walipopata ushindi dhidi ya Aghaliba huko Tunis waliendelea kuteka miji mingine ya Afrika ya Kaskazini mpaka mwishowe wakaiteka Misri na Sham na Hijazi.

Kusimama kwa dola ya ki-Fatimi:

Baadhi ya Mashia waliokuwa wakiishi Yemen walipambana na Mahujaji kutoka nchi za Afrika ya Kaskazini na kuwakinaisha kuwa wito wao wa kupigania Ukhalifa ni wa haki na kwa hivyo wakakubali warudi pamoja na wao ili wakatafute njia za kuirudisha haki hii kwao, na alipofika huko aliweza Abdullah Ash-Shi'i kuwakinaisha wakaazi wa Afrika wa Kaskazini kuwa yeye na jamaa zake wamo katika haki.

Kwa hivyo, katika mwaka wa 296 Hijria akiwa pamoja na Ubeidillah Al-Mahdi aliweza kuiteka Raqada makao makuu ya Aghaliba watawala wa Tunis wa wakati huo na kuuondosha utawala wao. Kisha baada ya kujitangaza yeye Abdullah Ash-Shi'i kuwa ndio Khalifa na kiongozi wa Waislamu aliufanya mji wa Qairawan ulioko Tunis kuwa ndio mji mkuu wake mpaka alipoanzisha mji mwengine pwani ya Tunis ambao aliuita Al-Mahdiya katika mwaka wa 303 Hijria na kuhamia huko.

Makhalifa wanne waliokuja baada yake walizidi kutilia nguvu utawala wao huu na kuendelea kuteka miji mingine ya Afrika ya Kaskazini na kuendelea kutangaza wito wao mpaka kufikia Misri na kuhisi watu wa Misri kuwa kweli wamo katika haki, na kupata mapokezi mazuri kutoka kwa Kafur Al-Ikhshidi ambaye alikuwa ni liwali wa Khalifa wa Banul-Abbas pamoja na viongozi wengine wa nchi.

Mafatimi katika Misri:

Baada ya kufa Kafur Al-Ikhshidi alisimama Khalifa wa nne wa ki-Fatimi, Al-Muiz lidini llahi Al-Fatimi na kupeleka jeshi chini ya uwongozi wa Jawhar As-Saqili kuiteka Misri na kwa kuwa Misri ilikuwa imeshakubali wito wa Mafatimi, aliingia Jawhar na kuiteka Misri bila ya vita, na kwa kutekwa Misri ukawa ulimwengu wa kiislamu umegawanyika sehemu mbili: Sehemu moja chini ya utawala wa Makhalifa wa ki-Banul-Abbas na sehemu ya pili chini ya utawala wa Makhalifa wa ki-Fatimi.

Utawala wa ki-Fatimi uliendelea kukuwa na kuenea nguvu zake mpaka kufikia Sham na Hijaz na Yemen, bali katika mwaka 450 Hijria katika zama za Khalifa Al-Mustansir wa ki-Fatimi ulifika utawala wao mpaka Baghdad.

Mambo muhimu walioyafanya:

Ulimwengu wa kiislamu wakati huu ulikuwa unapambana na wazungu waliokuwa wanapigana na Waislamu vita vya msalaba, na kwa kuwa wao wenyewe Mafatimi walikuwa kwenye vita na ndugu zao Banul-Abbas, hawakuweza kufanya jambo kubwa kwa ajili ya ulimwengu wa kiislamu upande wa kivita.

Pamoja na hayo, Mafatimi walisimama kuujenga mji wa Cairo mpaka ukawa unashindana na Baghdad kwa uzuri na ukubwa na wakajenga msikiti mkubwa wa Al-Azhar na kuufanya kuwa ni chuo kikubwa cha kusomesha mambo ya dini kwa madhehebu ya kishia na kuendelea hivyo mpaka alipokuja Salahuddin Al-Ayyubi na kuiteka Misri ndio mambo yalipobadilika na ukawa msikiti wa Al-Azhar unasomesha madhehebu ya kisunni. Leo Al-Azhar ndio Chuo Kikuu kabisa katika ulimwengu wa kiislamu.

Kudhoofu na kuanguka Ukhalifa wa ki-Fatimi:

Katika zama za Khalifa Al-Mustansir yalipungua maji ya mto wa Nile na kuenea ukame nchini mpaka kukazuka njaa na maradhi kila mahali na kusababisha matatizo mengi ndani ya nchi. Jambo hili lilimfanya Khalifa ategemee majeshi kusitisha hali ya fujo, jambo ambalo lililifanya jeshi kuingilia kwenye siasa ya nchi na kushindana baina yao.

Aidha, kwa kuwa utawala wa ki-Fatimi ulikuwa umeshafika mpaka Baghdad katika zama za Al-Mustansir, iliwabidi Mafatimi kupambana na Salaajiqa ambao ndio waliokuwa wakitawala mji wa Baghdad kwa amri ya Khalifa wa Banul-Abbas. Jambo hili liliwafanya Masalaajiqa kusimama dhidi ya Mafatimi na kujaribu kuwatoa Baghdad na sehemu za Sham.

Halikadhalika, miji ya Sham wakati huu yalikuwa yakipambana na wazungu waliokuwa wakipigana na Waislamu vita vya Msalaba na kwa hivyo Mafatimi wakashindwa nguvu na miji yao ya Sham ikatekwa na Masalibi (Wazungu wa Misalaba).

Huko Misri kulitokea ugomvi baina ya viongozi wawili wa Khalifa na kila mmoja akawa anataka kuithibitisha hukumu yake na utawala wake, jambo ambalo liliwafanya wategemee nguvu kutoka nje ya nchi ili kuzatiti utawala wao. Viongozi hawa walikuwa mmoja wao ni Dhirghaam Waziri wa Khalifa na wa pili ni Shaawir liwali wake ambaye alikuwa anataka yeye kuwa waziri.

Dhirghaam alitaka msaada wa Masalibi kupigana na Shaawir naye Shaawir akaomba msaada kutoka kwa Nuruddin Mahmud kiongozi wa Mosul huko Iraq ambaye alikuwa akipigana na Masalibi huko Sham. Nuruddin Mahmud alikuwa amefanya Halab huko Syria ndio makao yake ya kukusanya majeshi dhidi ya Masalibi na alikuwa anatamani nguvu za Misri zichanganyike na za Sham ili zisimame dhidi ya Masalibi ambao vile vile walikuwa wanataka kuivamia Misri.

Nuruddin alipeleka jeshi lake chini ya uwongozi wa Asaduddin Shirko akiwa amefuatana na mtoto wa nduguye Salahuddin ili kupigana na Dhirghaam, na baada ya kumshinda Dhirghaam, aliweza vile vile kumuondosha Shaawir na kuwa yeye ndiye waziri wa Khalifa Al-A'dhid, lakini hakukaa muda akafa na kwa hivyo uwaziri akapewa mtoto wa nduguye Salahuddin.

Baada ya kushika Salahuddin uwaziri na kuwa Khalifa Al-A'dhid ni mgonjwa, alipata nafasi Nuruddin Mahmud ya kuunganisha ulimwengu wa kiislamu dhidi ya Masalibi kwa kumtaka Salahuddin auondoshe Ukhalifa wa ki-Fatimi ambao ulikuwa wakati huo ni dhaifu na kwa hivyo, Salahuddin akawa ameamuru aombewe Khalifa wa ki-Abbasi katika khutba za Ijumaa badala ya Khalifa wa ki-Fatimi, na kwa kuwa Khalifa alikuwa mgonjwa hakujua nini kinachopitikana na kwa njia hii Misri ikarudi chini ya Ukhalifa wa Banul-Abbas, lakini chini ya utawala wa Salahuddin ambaye baadaye alisimamisha dola ya ki-Ayyubi ya kisunni.

Dola ya Salajiqa - Asia, Iran, Iraq, Sham na Turkey:
(Karne ya tano ya Hijria):

Salajiqa ni Maturki wanaotokana na Saljuq bin Daqqaq ambaye aliingia Uislamu yeye na kabila lake na kuhamia miji ya kiislamu iliyokuwa karibu na mto wa Saihun. Huko wakawa wanawahudumikia viongozi wa Maghaznawi ambao walikuwa wakitawala Khurasan na miji iliyoko karibu nao.

Aliposhika uwongozi Tughrul As-Suljuqi alianza kuiteka miji ya karibu mpaka mwisho akamshinda mfalme wa Maghaznawi na kuuteka mji wake mkuu katika mwaka wa 1038AD na kuiteka miji mingine katika mwaka wa 1040AD, na baada ya ushindi mkubwa alioupata aliweza kuiteka Asbahan katika mwaka 1050AD na kuufanya mji huu kuwa ndio mji mkuu wake.

Tughrul aliweza katika mwaka 1055AD kuingia Baghdad na kumsaidia Khalifa Al-Qaim bi amrillah kuwashinda Mabuweyhi ambao walisababisha matatizo na michafuko mengi katika dola na kwa hivyo Masalajiqa wakapata heshima na vyeo mbele ya Khalifa.

Baada ya kufa Tughrul katika mwaka wa 1063AD, alisimama mwanawe Alb Arsalan na kupigana na Warumi baada ya kusikia kuwa mtawala wao amekusanya jeshi kubwa kuja kumpiga. Kwa hivyo, katika mwaka wa 1071AD katika mwezi wa Ramadhani, walikutana Waislamu siku ya Ijumaa kumuomba Mwenyezi Mungu awanusuru, naye akajibu dua zao na likashinda jeshi la Alb Arsalan ushindi mkubwa na kumkamata hata mfalme wao.

Katika vita hivi, majeshi ya kirumi yalishindwa vibaya katika mji uitwao Malaadhkard na jeshi la kiislamu likaweza kuiteka Asia ndogo (Turkiya leo) na kuzivunja nguvu za Warumi na kuurudishia Ukhalifa haiba na nguvu zake.

Baada ya kufa Alb Arsalan katika mwaka 1072AD alipokuwa anakwenda kupigana na baadhi ya kabila za kituruki ambazo bado zilikuwa hazikusilimu, alishika mwanawe Malikshah Nidhamul-Mulk ambaye alihukumu kuanzia mwaka wa 1072AD mpaka 1092AD, na katika muda huu aliweza kuupanua utawala wake na kutawala sehemu kubwa ya ulimwengu wa kiislamu.

Malikshah aliuliwa katika mwaka 1092AD dola ya kisuljuqi ilianza kuvunjika baada ya kuanza Masalajiqa wao wenyewe kwa wenyewe kupigania utawala na Makafiri wakaingiwa tena na tamaa ya kuiteka miji ya kiislamu na hatari ya vita vya Msalaba ikawa inakurubia tena na kutishia kuanguka kwa dola ya kiislamu. Utawala wa Masalajiqa uliendelea mpaka 1307AD katika zama za Sultan A'laauddin III na ulipomalizika walisimama Uthmaniyyun kuuendeleza utawala wa kiislamu mpaka mwaka wa 1924AD baada ya vita vya ulimwengu vya kwanza.