Mitume na Manabii
Tangu alipoumbwa Adam, baba wa wanadamu wote, Mwenyezi Mungu alimkusudia kuwa awe mwakilishi wake (Khalifa wake) hapa duniani, na kwa hivyo alimfundisha kila kitu na kumtayarishia maisha yake hapa duniani na kumsahilishia njia za kuishi. Kisha alimpa nidhamu ya maisha ambayo aliita dini na kumhimiza kushikamana nayo na kuwafundisha kizazi chake. Kwa hivyo, alipoletwa duniani baada ya makosa aliyoyatenda ya kumuasi Mola wake na kumfuata Iblisi, aliteremshwa duniani pamoja na mkewe na kuchaguliwa kuwa ndiye Nabii wa kwanza kwa wanadamu, baada ya kutubia na kuomba msamaha.
Baada ya kuletwa ulimwenguni na kuanza maisha hapa, waliletwa baada yake Mitume na Manabii chungu nzima ili kuendeleza ujumbe wa Mwenyezi Mungu wa kumpwekesha na kumtukuza na kumtakasa. Mwenyezi Mungu aliendelea kuleta wajumbe wake hawa mpaka wakafikia idadi yao Manabii 124,000, wakiwemo katika hao Mitume 115. Qurani Tukufu imetaja katika hawa 25, na kutueleza kuwa katika hawa 25 kuna 5 ambao walikuwa ni wastahmilivu na wavumilivu.
Wote hawa walikuja kwa watu wao maalumu, na kuleta ujumbe makhsusi kwa kundi au kaumu fulani, lakini alipoletwa Mtume Muhammad (SAW) duniani, ujumbe wake ulikuwa ndio wa mwisho kwa wanadamu na kwa hivyo ukawa ni ujumbe kwa wanadamu wote si kwa kaumu fulani au watu maalumu, bali kwa umma mzima. Yeye tu miongoni mwa Mitume na Manabii walioletwa ulimwenguni ndiye aliyekuwa wa mwisho na wanadamu wote kwa jumla.
Mitume na Manabii waliotajwa ndani ya Qurani:
Adam | Idris | Nuh | Hud | Salih | Lut | Ibrahim | Ismail | Is-haq | Yaqub | Yusuf | Shu'aib |
Ayyub | Dhulkifl | Musa | Harun | Daud | Sulaiman | Ilyas | Ilyas'a | Yunus | Zakaria | Yahya | Isa |
Muhammad |
Watume watano (5) waliotajwa ndani ya Qurani kuwa ni walikuwa wavumilivu na wenye subira kubwa:
Nuh | Ibrahim | Musa | Isa | Muhammad |
Miongoni mwa hawa watano, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa ndiye wa mwisho katika mfululizo wa Mitume na Manabii, na ujumbe wake ndio uliokuwa wa mwisho na kwa wanadamu wote.