Khalifa wa tatu: 23H-35H
Kabla ya kufariki Umar bin Al-Khattab aliwakusanya Masahaba sita ambao anajua
kuwa Mtume (SAW) amekufa akiwa yu radhi nao, nao ni Uthman na Ali na AbdulRahman
bin Awf na Talha na Az-Zubeyr na Saad bin Abi Waqqas, na kuwataka wamchague
mmoja wao ili awe Khalifa baada yake, na kuwaonya wasipendelee jamaa zao
wakichaguliwa kuwa viongozi.
Umar aliwapa siku tatu kufikia uamuzi kuhusu jambo hili, na kuwaonya kuwa yeyote
atakayeuchukuwa uwongozi kwa nguvu bila kushauriana akatwe kichwa chake, na
akamwita Abu Talha Al-Ansari akae tayari na watu khamsini katika jamaa zake
kuilinda halmashauri isiingiliwe na mtu yeyote mpaka wapitishe uamuzi wao wa
kumchagua mmoja katika wao, na wakishindwa kufikia uamuzi, basi mwanawe
Abdullahi bin Umar achague mmoja katika wao, na kama hawakuridhia uamuzi wake,
basi wawe pamoja na kundi la AbdulRahman bin Awf.
Kwa hivyo, alipofariki Umar walikutana watu hawa sita na kujadiliana kwa muda
mrefu kuhusu nani atakayekuwa Khalifa, na baada ya majadiliano, alikubali
AbdulRahman kujitoa asichaguliwe Khalifa lakini asimamie kuchagua atakayefaa
kuwa Khalifa, na walivyokuwa wengine walimchagua Ali na wengine Uthman, na baada
ya kushauriana na Masahaba wengine alitoka AbdulRahman siku ya nne na kwenda
msikitini asubuhi ambako watu chungu nzima walikuwa wamekusanyika, na baada ya
kutoa hutuba na kuwauliza watu rai zao, alisimama Saad bin Abi Waqqas na
kumhimiza AbdulRahman afanye haraka kuchagua mmoja wao kabla zogo kuzidi ndani
ya msikiti.
Hapo AbdulRahman aliuinua mkono wa Ali bin Abi Talib na kumuuliza kama
ataendesha mambo kwa mujibu wa Qurani na Sunna za Mtume (SAW), na mwenendo wa
Makhalifa wawili waliokuja baada yake, Ali akasema kuwa anatumai kuwa atafanya,
basi AbdulRahman akauacha mkono wa Ali na kuushika mkono wa Uthman na kumuuliza
kama alivyomuuliza Ali, naye akamwambia kuwa:
Inshallah ndiyo nitafanya. Basi AbdulRahman akauinua mkono wa Uthman juu na
kusema: Ewe Mola sikiliza na ushuhudie, kisha akasema: Ewe Mola! Mimi
nimejiondoshea jukumu hili kwenye shingo yangu na nimeliweka juu ya shingo ya
Uthman. Kisha akamchagua Uthman na wote waliokuwepo msikitini wakamkubali Uthman
kuwa ndiye Khalifa wao mpya.
Uthman bin Affan (47KH-35BH):
Uthman bin Affan bin Abil-Aas bin Umayya alizaliwa katika ukoo wa kikureshi na
mamake alikuwa ni Arwa bint Kureyz, naye alizaliwa katika mji wa Taif, na
alifariki babake alipokuwa anakwenda katika mojawapo ya safari zake za Sham
kwenda kuleta biashara na kumwachia mwanawe mali nyingi sana, na akainukia kuwa
mfanyibiashara mzuri na akaweza kukusanya mali nyingi na kuwa katika matajiri
wakubwa hapo Makka, na kuwasaidia watu wake mpaka wakawa wanampenda sana na
kumheshimu.
Alikuwa Uthman ni mtu karimu sana na mara nyingi alimsaidia Mtume (SAW) kwa mali
yake katika kuutangaza Uislamu na kusaidia Waislamu kama aliponunua kisima cha
Ruma kutoka kwa Myahudi ambaye alikuwa akiwatoza pesa Waislamu kwa maji yake na
kuwasabilia wateke bure na vile vile katika kutayarisha jeshi la kwenda kupigana
jihadi na mambo mengine mengi ya kusaidia Waislamu, naye alikuwa ni mwenye haya
nyingi na heshima kubwa mpaka kusema Mtume (SAW) kuwa Malaika wanamstahi Uthman,
na alikuwa akijulikana kwa jina la Dhun-Nurayni kwa kuoa kwake watoto wawili wa
Mtume (SAW) Ruqayya na baada ya kufariki akamuoa Umm Kulthum, na ni mmoja katika
Masahaba kumi waliobashiriwa Pepo na Mtume (SAW).
Sifa zake:
1- Alikuwa katika Masahaba wa mwanzo wa
kusilimu
2- Alikuwa katika Masahaba wa mwanzo kuhama Makka kwenda Habasha.
3- Alikuwa ni mwingi wa kutoa misaada kwa Waislamu wenzake katika mambo ya
Jihadi
4- Alikuwa ni Sahaba aliyebahatika kuoa watoto wawili wa Mtume (SAW):
Ruqayya na Umm Kulthum
5- Alikuwa ni mtu mwenye haya sana
6- Alikuwa katika Masahaba kumi waliobashiriwa kuingia Peponi
Wakeze na wanawe:
Wake wote aliowaoa ni tisa nao ni Ruqayya na Umm Kulthum watoto wa Mtume (SAW),
na Naila na Faakhita na Umm Amr na Fatma na Ummul-Banin na Ramla na Ummu Walad.
Na alizaa nao watoto wa kiume na wa kike, nao ni Abdullahi mkubwa na Abdullahi
mdogo na Amr na Khalid na Abaan na Umar na Al-Walid na Said na Al-Mughira na
Abdul-Malik. Na wanawake ni Maryam na Umm Said na Aisha na Umm Abban na Umm Amr
na Maryam na Ummul-banin, wakiwa wote ni 17, wanaume ni 10 na wanawake ni 7.
Kusilimu kwake:
Uthman alisilimu mapema baada ya Mtume (SAW) kupata utume akiwa ni kijana mwenye
umri wa miaka thalathini baada ya kuzungumziwa ujumbe huu wa Uislamu na Abubakar
Assiddiq. Naye alikuwa ni Muislamu mwema na sahaba mkubwa katika Masahaba wa
Mtume (SAW) na kuhudhuria aghlabu ya vita vya jihadi alivyopigana Mtume (SAW),
na alikuwa ni mfanyibiashara aliyepata ufanisi mkubwa katika biashara zake.
Kuhamia kwake Habasha na Madina:
Uthman alikuwa ni katika Masahaba wa kwanza waliohamia Habasha kwa mara ya
kwanza na mara ya pili, yeye pamoja na mkewe Ruqayya binti wa Mtume (SAW), kisha
ilipotoka amri ya kuhamia Madina, akafunga safari ya kwenda zake Madina na mkewe,
na kwa hivyo amepata fadhila za kuhamia Habasha na Madina pamoja.
Mambo muhimu aliyoyafanya:
Aliendelea Uthman kusonga mbele katika nchi mpya za Makafiri na maadui wa
Waislamu na kupigana nao na kuziteka nchi zao ili kuweka amani kwenye mipaka ya
dola ya kiislamu iliyofika sehemu mbali mbali za ulimwengu wa wakati huo, kwani
alimtuma liwali wake wa Basra Abdullahi bin Aamir kumfuata mfalme wa Ufursi
aliyewahi kukimbia katika vita vya Nahawand na ambaye amejizatiti kupigana na
Waislamu mpaka akampata na kumuua na kulishinda jeshi lake na kuteka Karman na
Sajistaan.
Aidha, katika Ukhalifa wake ilitekwa Tabaristan na Said bin Al-Aas na kuiteka
Takharistan amirijeshi mwengine aitwaye Al-Ahnaf bin Qays na akaiteka liwali wa
Uthman wa Misri, Abdullahi bin Saad bin Abi Sarh mji wa Ifriqiya (Tunis leo) na
Nuba kusini mwa Misri, na akaiteka Habib bin Maslama miji ya Armenia, na kuwa
dola ya kiislamu katika zama hizi inatawala sehemu kubwa sana ya ulimwengu wa
wakati huu.
Vile vile, aliweza Uthman kwa majeshi yake ya baharini na majemadari wake
kuviteka visiwa vya Quprus (Cyprus) na Rodz (Rhodes) na Siqilliya (Cicily) na
Kriti (Crete) katika visiwa viliopo kwenye bahari ya Meditarenean, na kuwashinda
Warumi katika vita vya Dhatas-Sawari na kuitawala bahari yote ya Mediteranean
wao.
Nuskha za Msahafu wa Uthman:
Baada ya kutekwa Armenia, Uthman alimpeleka Hudheyfa bin Al-Yamaan kuwa liwali
wake huko na kulikuwa katika jeshi lililoiteka Armenia watu kutoka Sham na Iraq
na sehemu nyenginezo na alishangazwa na kustaajabishwa kuona watu
wanakhitalifiana katika kisomo chao cha Qurani na kumueleza Uthman habari hii ya
hatari, ndipo alipokusanya Uthman maandishi ya Qurani yaliyokuwa kwenye mifupa
na ngozi na karatasi na mawe na kuchoma moto zote hizi na kuuchukuwa msahafu
ulioandikwa katika zama za Abubakar na ambao ulikuwa kwa Hafsa mkewe Mtume (SAW)
na kuamrisha ziandikwe nuskha kutokana na msahafu huu na kutawanywa katika miji
mikubwa ya kiislamu.
Kuupanua Msikiti wa Makka-29H:
Alipoona Uthman kuwa Msikiti wa Makka umekuwa hauwatoshi Waislamu ambao idadi
yao ilikuwa inazidi kila siku na kutoka kila pande za dola ya kiislamu kubwa,
alisimama kuupanua msikiti huu katika mwaka wa 29 wa Hijra.
Fitna ya pili:
Ilizuka fitna kubwa zama za Ukhalifa wa Uthman wakati watu walipoona kuwa Uthman
anapendelea watu wa kabila lake la Banu Umayya kwa kuwapa vyeo katika miji mbali
mbali ya dola ya kiislamu, na Ali bin Abi Talib alimnasihi sana Uthman kuhusu
hatari ya jambo hili, na ikawa watu wamegawanyika mafungu matatu: Wale waliopewa
vyeo na kujikusanyia mali chungu nzima na kuishi katika anasa kwenye majumba
makubwa makubwa, na wale waliokuwa wakiridhika na kidogo na kuishi maisha
yasiyokuwa na anasa na kujiepusha na starehe za kidunia, na wale ambao walikuwa
na imani dhaifu na ambao ilikuwa nia yao kutia chokochoko na kuchochea fitna
baina ya Waislamu.
Kundi la kwanza lilikuwa ni kundi la Muawiya na jamaa wengine wa Uthman ambao
walikuwa wakiishi katika hali ya juu ya maisha, na kundi la pili ni la Ali
ambalo lilikuwa likipigania watu wote wawe wanashughulikiwa sawa sawa
wasipendelewe hawa juu ya wengine, na kundi la tatu la wachochezi fitna na wenye
kutaka kuwagawanya Waislamu lililokuwa likiongozwa na Abdullahi bin Sabaa
Myahudi kutoka Sanaa aliyejidai kusilimu na kuichochea fitna hii ambayo mwisho
wake ilimpelekea Uthman kuuliwa.
Kuuliwa Uthman:
Ilivyokuwa mali katika Ukhalifa wa Uthman ilikuwa nyingi sana na kukusanyika
katika mikono ya Maliwali na viongozi wa miji na matajiri, alisimama Abu Dhar
Al-Ghafari na kuwanasihi matajiri wa hapo Madina watoe mali zao kuwapa maskini,
na kuendelea kuusia na kunasihi na kwenda huku na huko mpaka akafika Sham na
kutangaza mwito wake wa kuwaomba matajiri wawasaidie maskini.
Mwito huu ulipomfikia Muawiya alimwita na kujadiliana kuhusu jambo hili, lakini
Abu Dhar alishikilia kuwa mali ni mali ya Waislamu na kila mtu apewe haki yake,
basi Muawiya akamwandikia Uthman amwite Abu Dhar Madina na alipokutana naye na
kumuuliza mas-ala haya, alijibu Abu Dhar kuwa haiwapasi matajiri kuzuiya mali ya
Waislamu mikononi mwao, bali inapasa watoe kuwapa wenziwao maskini. Uthman
akamwambia kuwa ni juu yake kutoa katika mali yake tu na kuchukuwa Zaka kutokana
na raiya, lakini si juu yake kuwalazimisha kuishi maisha ya kimaskini na
kujikhini. Abu Dhar akamwomba Uthman ampe ruhusa aondoke Madina ende akaishi
sehemu mbali na Madina, basi akampa ruhusa.
Kwa upande mwengine, alisimama Abdullahi bin Abi Sabaa Myahudi aliyejidai
kusilimu kutia chokochoko katika nchi alizozitembelea, nazo ni Misri na Basra na
Kufa, na kuwachochea watu wawe dhidi ya Uthman kwa hoja kuwa hafanyi uadilifu
baina ya watu na akapata wafuasi wengi, basi wakatoka watu kutoka Basra na Kufa
na Misri kwenda Madina kumtaka Uthman ajiuzulu, lakini alipokataa Uthman
kujiuzulu na kukubali kufanya matengenezo, walikusanyika wapinzani na kuizingira
nyumba ya Uthman na kumzuiya kutoka kwenda kusali na kumnyima maji na chakula.
Wakasimama Masahaba na watoto wao akiwemo Al-Hasan bin Ali na Ibn Abbas na
Muhammad bin Talha na Abdullahi bin Zubeyr na Abdullahi bin Salam na Marwan bin
Al-Hakam na Abu Hureyra na wengi wengineo wanaokaribia watu mia kumhami Khalifa
wao, lakini waasi walikuwa wengi na baada ya kupigana na kuumizwa baadhi ya
watoto wa Masahaba, walichoma moto waasi mlango wa nyumba ya Uthman na kuingia
ndani kwa njia ya nyumba nyengine iliyokuwa imegusana na nyumba ya Uthman na
kumvamia na kumpiga na kumchoma panga na alipojaribu mkewe Naila kumlinda
walimpiga panga wakamkata vidole vyake.
Uthman aliushikilia msahafu wake na kuuweka mapajani mwake na huku waasi
wamemzunguka huyu anampiga teke, yule anamchocha jambia na mwengine anampiga
panga mpaka akaanguka na kukata roho. Masahaba walilia sana kwa kifo chake na
kiwiliwili chake kilikaa siku tatu bila kuzikwa, kisha Ali pamoja na Talha na
Masahaba wengine wakamchukuwa na kumzika.
Uthman ndiye wa kwanza...
1- Kufanya nuskha za Qurani Tukufu na kuzitawanya katika miji ya kiislamu.
2- Kuupanua msikiti wa Makka (Al-Masjidul-Haraam).
3- Kuweka maaskari wa kulinda mji na kuwapa mishahara wanajeshi.
4- Kuweka nyumba hasa ya kadhi ya kuhukumu baina ya watu.
5- Kujenga merikebu za vita na kuanzisha jeshi la kiislamu la baharini.
6- Kuwapa mishahara waadhini kutokana na Baytul-Mal.