Vijidola

 

Kuzuka kwa dola mbali mbali:

Kama tulivyoeleza nyuma tulipotaja sababu za kuvunjika kwa dola ya ki-Abbasi, ilikuwa Dola ya kiislamu ni moja tangu ilipoanzishwa na Mtume (SAW) mpaka zama za Makhalifa wanne Waongofu, ndipo ilipotokea fitna na akajitangaza Muawiya kuwa ni Khalifa na kusimamisha vita dhidi ya Ali bin Abi Talib. Chokochoko hizi ziliendelea vile vile zama za Abdullahi bin Zubeyr mpaka wakasimama na kumpiga vita na kumuua katika Ukhalifa wa AbdulMalik bin Marwan. Ukhalifa wa Banu Umayya uliendelea miaka mingi lakini ulipoanguka na wakashika Banul-Abbas ilizuka dola ya Banu Umayya huko Andalus Uhispania, na baada yake dola nyengine zikazuka sehemu za Mashariki na Magharibi na zikajitenga na Ukhalifa wa Banul-Abbas.

Dola ya Banu Umayya - Andalus (Uhispania): (Kuanzia 138H mpaka 897H)

Bara la Iberia (Uhispania na Ureno) lilitekwa na Waislamu katika zama za Al-Walid bin AbdulMalik katika mwaka wa 92 wa Hijra. Musa bin Nusayr alitaka ruhusa kutoka kwa Al-Walid kulivamia bara la Iberia na baada ya kupanga mipango yake alimchagua Tariq bin Ziyad kijana hodari wa kibarbar kwa kazi hii muhimu.

Chini ya uwongozi mshupavu wa Tariq bin Ziyad jeshi la watu 7000 lilivuka bahari ya Mediterenean na kuelekea kwenye jabali dogo lilioko baina ya Morocco na Uhispania. Jabali hili baadaye likawa linajulikana kwa jina lake (Jabal Tariq au Gibraltar). Jeshi jengine la watu 5000 chini ya uwongozi wa Tarif bin Malik lilifuata kumsaidia Tariq baada ya kuingia Uhispania na Mwenyezi Mungu akawasaidia na wakapata ushindi mkubwa.

Baada ya kushindwa Banu Umayya na Banul-Abbas katika mwaka wa 132 Hijria na kushika wao hukumu ya dola ya kiislamu, alikimbia mmoja katika viongozi wa kibanu-Umayya na kuelekea Morocco na kuvuka bahari na kuingia Andalus (Uhispania). Huko, baada ya kushauriana na wanazuoni, walimkubalia kuwa Khalifa wao na kuanzisha dola ya kibanu-Umayya huko.

Kijana huyu ambaye alipewa jina la Saqr Qureysh (Kipanga wa Maqureshi) alikuwa akiitwa Abdur-Rahman bin Muawiya bin Hisham bin AbdulMalik, na baada ya kuanzisha dola yake huko Andalus aliifanya Qurtuba (Cordova leo) kuwa ndio mji mkuu wake na kujenga misikiti na majumba makubwa na maskuli na madaraja na njia na maktaba kubwa kubwa na kufanya matengenezo mengi katika nchi.

Makhalifa wa kibanu-Umayya katika Andalus walijenga miji mingi na kustawisha sana hali ya maisha na elimu na maarifa katika Andalus, na kuifanya nchi hii kuwa ndio chanzo cha nuru ya elimu na maarifa kwa Ulaya nzima. Waislamu walijitahidi sana kueneza ustaarabu na elimu kote Ulaya na wanazuoni wakubwa wakubwa wa kiislamu kama Ibn Rushd (Averroes) na Ibn Sina (Avicenna) na wengineo ni mashuhuri sana huko Ulaya mpaka hii leo.

Lakini baadaye dola hii ilidhofu kwa sababu ya kutokuwa na umoja baina ya viongozi wake na kugawanyika nchi vipande vipande na kuenea fasadi jambo ambalo liliwapa nafasi Wahispania kuzivamia nchi hizi na kuwatoa Waislamu mji mmoja baada ya mmoja mpaka katika mwaka wa 897 Hijria wakaivunja dola ya kiislamu iliyoendelea katika Uhispania kwa muda wa karibu miaka 800 na kuwatoa Waislamu moja kwa moja katika Andalus.

Kutekwa kwa Andalus:

Andalus (Uhispania leo) ilitawaliwa na wafalme wengi wa kiislamu lakini kulikuwa na mgawanyiko baina yao na kila mmoja akawa anahukumu sehemu fulani ya dola na kwa hivyo Manasara walikuwa daima wanasubiri fursa ili waivamie dola ya kiislamu hii na kuiteka moja kwa moja.

Mfalme wa mwisho wa Andalus Abu Abdallah Muhammad Al-Khain alikuwa ni mtu mwenye tamaa sana na kwa hivyo alipopewa ndugu yake Muhammad bin Saad ufalme na babake katika mwaka 890 Hijria, alisimama kumpiga vita vikubwa, jambo ambalo lilimuudhi sana babake na kumtia hamu na ghamu mpaka akafa.

Muhammad Al-Khain alishirikiana na wafalme wa ki-Nasara Fardinand na Izabella kumpiga nduguye mpaka akashindwa na kutekwa ufalme wake. Lakini jambo ambalo hakulifikiria Al-Khain ni kuwa hawa wafalme watamgeukia na yeye vile vile, kwani baada ya kuteka mamlaka ya nduguye walimgeukia na kupigana naye na kuteka miji yake mpaka mwisho akashindwa na kumpa funguo za mji wa mwisho wa kiislamu huyo Ferdinand.

Hali ya Waislamu chini ya Manasara:

Muhammad Al-Khain alipotoa funguo za miji ya kiislamu ya Andalus alishurutisha Waislamu waishi chini ya utawala wa kiispania wakiwa na uhuru wa kufanya yao na kuabudu Mola wao, na wafalme wa kiispania walikubali na kuwaachilia kufanya haya mwanzo mwanzo, lakini wakubwa wa kidini wa kinasara walianza kuwachochea wanasiasa wawanyang'anye Waislamu haki hii na kwa hivyo baada ya kupita miaka si mingi wafalme walianza kuwakandamiza Waislamu na kuwanyima haki zao na kuwanyang'anya mali zao.

Baina ya mwaka 1609 na 1614 alipokuwa Philip III akitawala Andalus, dhulma na ukandamizaji ulizidi huko Uhispania dhidi ya Waislamu na inasemekana kuwa idadi yao wakati huo ilikuwa kama milioni tano, alianza kuwanyanganya Waislamu mali zao na kuwatoa kwenye miji yao kwa kuwatesa na kuwalazimisha kuingia kwenye dini ya Ukristo na kwa sababu ya kukataa kwao jambo hili, wengi wao waliuliwa.

Waislamu waliobakia Andalus na kuishi kwa kuficha imani yao kwa kubadilisha majina yao na ya vizazi vyao hawakuweza kubakia muda mkubwa kama Waislamu kwani kizazi kilichokuja kilikuwa hakijui chochote kuhusu Uislamu na kwa hivyo wakainukia kuwa ni Manasara na kusahau dini yao na lugha yao ijapokuwa sura zao na maumbile yao yakionyesha kuwa hawa ni watoto wa kiislamu.

Bali jambo hili ni dhahiri kwa yule mwenye kuzuru Uhispania hata leo kwani wengi wao bado wana rangi tofauti na wazungu wengine na kadhalika nywele zao wengi wao ni nyeusi si kama wenziwao wa sehemu nyengine za Ulaya na hii ni kwa sababu Waislamu waliitawala Uhispania zaidi ya miaka 800 na damu zao zilichanganyika sana na watu wa huko, hasa ilivyokuwa wengi katika wafalme wa kiislamu na watoto wao walikuwa wakioa wanawake wa kiispania.

Dola ya Adaarisa - Morocco: (172H-312H)

Katika zama za Ukhalifa wa Harun Ar-Rashiid, alianzisha Idris bin Abdillahi bin Hasan bin Al-Hasan bin Ali bin Abi Talib mji wa Fas mwaka wa 172 Hijria huko Morocco baada ya kusalimika katika vita vya Fakh huko Hijaz katika mwaka 169H na kukimbilia Morocco.
Idris aliendelea kuhukumu dola hii mpaka alipokufa katika mwaka 177 Hijria.

Alipofariki Idris alimwacha mwanawe Idris II bado hakuzaliwa yumo ndani ya matumbo ya mamake, na kwa hivyo dola iliendeshwa na huru wa babake kwa muda na baada ya kufa kwake alishika Abu Khalid mlezi wake mpaka alipokuwa mkubwa akashika mwenyewe katika mwaka wa 188 Hijria.

Idris II alijenga mji mwengine upande wa pili wa mji wa Fas na kuuita Al-Aaliya na kuendelea kuhukumu mpaka alipofariki katika mwaka wa 213 Hijria. Dola hii iliendelea kwa muda lakini kulikuwa na matatizo kati ya kizazi cha Idris wenyewe kwa wenyewe na mwishowe ikamalizika katika mwaka wa 312 Hijria alipoiteka Musa bin Abil-Afiya.

Dola ya Aghaaliba - Tunis: (184H-296H)

Harun Ar-Rashiid alimchagua Ibrahim bin Al-Aghlab kuihami Tunis na mipaka yake ya Magharibi na akawa anaishi mwanzo katika mji mkuu wa Tunis, Qayrawan kisha akajenga mji mwengine akauita Al-Abbasiya na kuhamia huko yeye na maaskari wake na ukoo wake, na kuwa ndio mji mkuu na makao ya utawala wake.

Dola hii ilijitenga na kuendelea ukoo na kizazi cha Ibrahim bin Aghlab kuhukumu nchi hii kwa urathi, lakini walibakia kuwa waaminifu kwa Makhalifa wa ki-Abbasi na watiifu kwao. Dola hii ilikuwa ni msaada mkubwa kwa Ma-Abbasi kwa kuilinda kwao mipaka ya dola na hujuma za Khawarij na Adarisa na Banu Umayya wa Andalus.

Maaghaliba waliweza katika zama zao kukiteka kisiwa cha Sicily katika mwaka wa 212 Hijria, na kuingia wengi katika wakaazi wake kwenye dini ya Uislamu na kujenga misikiti na ngome na majengo mbali mbali ambayo athari yake mpaka leo inaonekana.

Dola hii iliendelea mpaka 296 Hijria kisha akaja Abu Abdullahi Ash-Shii na kuiteka nchi yao na kumalizika hukumu yao.

Dola ya Tuuluniya - Misri: (254H-292H)/(868AD-905AD)

Nguvu na satwa za Waturuki zilizidi baada ya kutawala Ukhalifa Al-Muutasim billahi katika mwaka 218 Hijria mpaka ikabidi awajengee mji wa Samuraa ili kuwaondosha Baghdad, na ikawa baada yake Makhalifa waliokuja wakiwatumia viongozi wa kituruki katika kuendesha mambo ya nchi ya ndani na nje, na kwa hivyo tunaona katika mwaka 254 Hijria anapewa Ahmad ibn Tuulun uwongozi wa kuhukumu Misri, lakini zilizidi nguvu za Ibn Tuulun mpaka akajitenga na Ukhalifa na akawa yeye ndiye mwenye kutawala Misri, bali hakusita hapo lakini aliendelea kuzidisha nguvu zake mpaka akawa anatawala Sham na Libya vile vile.

Ibn Tuulun alijijengea mji mpya hapo Misri kuwa ndio makao yake na akauita Al-Qataai' na kujenga jumba lake na msikiti na hospitali ambayo watu walikuwa wakitibiwa bure. Alikuwa Ibn Tuulun mwanasiasa mzuri na mtu hodari katika kuendesha nchi na kwa hivyo katika zama zake aliweza kuitengeneza nchi yake na kulikuza jeshi lake na kuweka amani katika nchi na kuilinda mipaka yake isivamiwe na watu kutoka nje.

Baada ya kufa Ibn Tuulun katika mwaka wa 280H alitawa mwanawe Khumarawayh dola ya Tuuluniya na kupanua mipaka yake na kufanya uhusiano mwema na Khalifa Al-Muutadhid mpaka akaoa Khalifa binti wa Khumarawaih aliyekuwa akiitwa Qatrun-Nadaa na kufanywa arusi kubwa na kujengewa maarusi majumba makubwa makubwa.

Dola hii haikudumu muda mrefu kwani baada ya kufa Khumarawayh katika mwaka 282 Hijria, majeshi huko Misri walianza fujo na kunyanganya mali za watu na ukoo wa Tuulun haukuweza kuwadhibiti na kwa hivyo Khalifa akapeleka jeshi na kuirudisha dola chini ya utawala wake katika mwaka wa 292 Hijria na ikarudi Misri chini ya hukumu ya Khalifa na kumalizika dola ya Tuuluniya.

Dola ya Hamdaniyyun - Mosul na Halab: (317H-394H)

Hamdaniyyun wanatokana na kabila la Taghlib la Kiarabu lililokuwa likiishi katika mji wa Mosul tangu zama za Ujahili kabla ya kuja Uislamu. Kabila hili wakati wa Ukhalifa wa Al-Mu'tadhid lilisimama kufanya upinzani dhidi ya dola ya ki-Abbasi lakini lilishindwa nguvu kisha likasamehewa na Khalifa.

Baadaye alisimama Al-Hussein bin Hamdan kupigana na jamaa waliojaribu kumpinga Khalifa na kwa hivyo akawa mashuhuri na kupendwa sana na Khalifa, na kabila lake likazidi nguvu na kuwa ni kabila linaloogopwa huko Iraq, na kwa hivyo Khalifa akalitumia kuwatia adabu wale waliokuwa wakijaribu kutokana na utiifu wake.

Katika mwaka 292 Hijria, Khalifa Al-Muqtadir alimfanya Abdallah bin Hamdan kuwa ni liwali wa Mosul na nduguye Ibrahim kuwa liwali wa miji ya Rabia katika mwaka 307 Hijria na nduguye mwengine Said mji wa Nahawand katika mwaka wa 312 Hijria. Kisha watoto wa Abdallah, Al-Hasan na Ali ndio waliokuja kulifanya kabila lao kuwa mashuhuri zaidi wakati waliposimama kupigana na Warumi na kumsaidia Khalifa katika utawala wake, kwani Al-Hasan alipewa uliwali wa Mosul na nduguye akapewa uliwali wa Halab.

Aidha, kabila la Hamdani lilimsaidia sana Khalifa katika kupambana na viongozi wa kijeshi wa kituruki waliokuwa mara kwa mara wakijaribu kutokana na utiifu wa Khalifa na kupitisha dhulma katika nchi, na kwa hivyo Makhalifa wa ki-Abbasi walikuwa radhi na Bani Hamdani na kuwapa vyeo mbali mbali. Kwa hivyo, Khalifa Al-Muttaqi aliposhika Ukhalifa baina ya 329H-333H alimpa Al-Hasan jina la Naasirud-Dawla na nduguye Ali Seifud-Dawla kwa kazi kubwa waliokuwa wakiifanya dhidi ya hawa Maturuki.

Hamdaniyyun waliendelea kuwasaidia Banul-Abbas katika kuendesha dola yao mpaka walipokuja Mabuweyhi wakashikilia mambo ya ndani ya nchi na wakawa wao wameshughulika kupigana na Warumi, na kwa hivyo nguvu zao zikapungua hapo Mosul na badala yao wakashikilia kazi zao Mabuweyhi na ikatoka Mosul chini ya utawala wao.

Waliendelea Hamdaniyyun kupigana na Warumi na kuwatoa kwenye miji mbali mbali mpaka wakawa karibu sana na mji wao mkuu wa Kostantia, lakini baadaye wakajikusanya Warumi na kuanza kuirudisha miji yao mpaka wakafika kuiteka Halab yenyewe makao ya Bani Hamdani na kwa hivyo utawala wao ukesha hasa ilivyokuwa walikuwa wamezongwa upande wa Mosul na Mabuweyhi.

Dola ya Ikhshidiya - Misri: (323H-358H)

Dola ya Aghaliba, baada ya kuwashinda Makhalifa wa ki-Fatimi huko Tunis na kuanza kuiteka miji mingine ya Morocco, walijitayarisha kuiteka Misri kwa kuchukulia kuwa ndio mlango wa kuingia dola za kiarabu za Mashariki. Khalifa wa ki-Abbasi wa wakati huo aliyekuwa akiitwa Ar-Radhi alimchagua Muhammad bin Taghj kiongozi Mturuki kuongoza jeshi dhidi ya Mafatimi huko Misri na katika mwaka 323 Hijria baada ya kuwashinda Mafatimi kuwa ndiye msimamizi wa Wilaya ya Misri.

Muhammad bin Taghj alipewa jina la Al-Ikhshid na Khalifa, ambalo ni lakabu waliokuwa wakipewa wafalme wa Farghana, na baada ya kuwakilishwa Misri alijitahidi kulikuza jeshi lake na kuitengeneza wilaya yake na kujipendekeza kwa raiya zake na akawa anamsaidia Khalifa dhidi ya Maadui zake mpaka akapendwa sana na Khalifa na kuachiwa kuhukumu Misri yeye na kizazi chake.

Muhammad Al-Ikhshidi aliweza kuteka sehemu nyingi za Sham na Yemen na Hijaz na akawa anatawala miji hii yote pamoja na Makka na Madina na kwa ajili ya siasa yake nzuri amani ikaenea na raiya wakawa wanaishi kwa furaha na amani.

Kufa kwake:

Alikufa Muhammad Al-Ikhshidi katika mwaka 334 Hijria na akawacha watoto wawili wadogo, na kwa hivyo akawashikia utawala wao mlezi wao aliyekuwa akiitwa Kafur na kutawala kuanzia 334H mpaka 355H. Watoto wa Muhammad hawakuwahi kutawala kwani walikufa mapema na kwa hivyo aliendelea Kafur kuwa liwali wa Misri mpaka alipokufa na kutekwa na Makhalifa wa ki-Fatimi katika mwaka 358 Hijria.