|
Bara Arabu:(Arabuni) Bara Arabu katika ramani ya ulimwengu wa kale kabla ya kugunduliwa Umarekani ni sehemu ya ardhi iliyoko katikati baina ya Bara la Afrika na Bara la Ulaya na Bara la Asia. Kuwepo kwa Bara Arabu kwenye sehemu kama hii kumeipa umuhimu mkubwa kabisa na kuifanya kama moyo kwa kiwiliwili, kwani ni sehemu ambayo imetawala mapitio muhimu sana ya bahari za ulimwengu wa kale. Ili kufika Arabuni au Bara Arabu kama ilivyokuwa ikijulikana zamani, ni lazima kupitia mapitio haya kabla ya kuendelea na safari yako kwenda Afrika, Asia au Ulaya. Mapitio haya ambayo leo yanaendelea kuwa na umuhimu mkubwa kabisa duniani ni Bahari Nyekundu (Red Sea), na Bahari ya Waarabu (Arabian Sea) na Ghuba la Uajemi (Uarabu) (Persian (Arabian) Gulf), na ndio yaliyoifanya Bara Arabu kuwa ni sehemu muhimu kabisa kibiashara, kiuchumi na kisiasa, katika hali ya vita au amani. Aidha, kwa sababu ya umuhimu mkubwa kama huu ndio maana Mwenyezi Mungu akaijaaliya Bara Arabu kuwa ni shina la biashara, uchumi na dini yake ya Uislamu, na ndio maana vile vile ikawa ni sehemu inayopiganiwa na umma mbali mbali ikiwa hapo zamani baina ya Wafursi na Warumi au sasa baina ya Wamarekani na Wazungu wengineo. Hapo zamani za kale kulikuwa kuna Waarabu waliokuwa wakiishi Bara Arabu na walikuwa ni watu wenye nguvu nyingi na majenzi ya ajabu kama yale yaliyojengwa na kaumu Hud yenye nguzo ndefu zatiti au yaliyojengwa na kaumu Saleh kwa kuchonga majabali. Kaumu hii ya Hud iliyokuwa ikijulikana kwa jina la A'd na kaumu Saleh iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Thamud, ziliangamizwa na Mwenyezi Mungu kwa dhambi na maasiya yao na kuleta badala yake kaumu nyengine. Anasema Mwenyezi Mungu aliyetukuka:
Kwani hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya kina A'di?
Sura: Al-Fajr:6-14 Baada ya kuangamizwa kaumu mbili hizi zilizokuwa zikiishi Bara Arabu, Waarabu wote waliobakia wanahesabiwa kuwa wanatokana na kizazi cha Qahtan ambao asli yao na nchi yao ni Yemen. Waarabu hawa walikuwa wakiishi kwenye sehemu nzuri ya nchi yenye mabustani na mashamba mazuri mazuri na walikuwa katika neema kubwa lakini pia walikufuru na kumfuata Iblisi na Mwenyezi Mungu hamuachi mwenye kukufuru na kudhulumu nafsi yake basi akawaletea adhabu yake baada ya kuwa katika raha na furaha
Hakika kulikuwa na ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika
maskani yao: Sura: Saba:15-17 Waarabu hawa baada ya kuvunjika boma la Maarib lililokuwa likizuilia ziwa kubwa la Maarib na kunyweshea mashamba na mabustani yao, walitawanyika na kuhamia sehemu mbali mbali za Arabuni. Wengine wakaelekea Shamu na wengine wakenda Iraq na Hijaz na Oman kutafuta riziki na maisha mapya. Miongoni mwa makabila muhimu ya kizazi cha Qahtani ni Himyar na Kahlani na kutokana na Kahlani lilitoka kabila la Azd ambalo watoto wake wenye umuhimu mkubwa katika tarehe ya Uislamu ni Aus na Khazraj ambao makabila yao ndiyo yaliyokuwa yakiishi Madina kabla ya kuhamia Mtume Muhammad (SAW), na kadhalika kabila la Jurhum ambalo lilihamia sehemu za Hijazi na kuteremkia katika bonde la Makka zama za Nabii Ismail. Kabila la Qureshi linatokana na kizazi cha Nabii Ismaili mwana wa Nabii Ibrahim ambaye alipelekwa Makka yeye pamoja na mamake Hajar akiwa bado mchanga na kuachwa katika bonde kavu lisilokuwa na chochote hapo Makka. Hajar alishangazwa sana na kitendo hiki lakini baada ya kujua kuwa ni amri inayotokana na Mwenyezi Mungu alitulia moyo wake kwa kujua kuwa Mola wake bila shaka hatomtupa. Huku nyuma Nabii Ibrahim aliondoka akiwa na huzuni lakini alikuwa na yakini kuwa Mwenyezi Mungu Mola wake hamtakii ila la kheri kwa mtihani huu, basi akaomba:
Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya kizazi changu Sura: Ibrahim:37 Hajar alibakia na mwanawe mchanga baada ya kuondoka Nabii Ibrahim na kuanza kuangaza huku na huku asaa ataona dalili yoyote ya maji au aina yoyote ya uhai, lakini kwa kuwa ni bonde tupu katikati ya jangwa alianza kukimbia huku na huku akipanda mlima wa Safa na kuangaza kisha akenda mbio mpaka juu ya mlima wa Marwa na kuangalia kama ataona chochote kwa mbali. Alifanya hivi mara saba bila kuona kitu lakini aliporudi kwa mwanawe alikuta chemchemu ya maji iliyotimbuka karibu na miguu ya Nabii Ismaili akafurahi sana na kumshukuru Mola wake. Chemchemu hii ndio hii chemchemu ya Zamzam ambayo mpaka leo inatumika na mamilioni ya wakaazi wa Saudia na mahujaji wanapokwenda kuhiji Makka. Kabila la Jurhum lililokuwa likipita karibu na bonde la Makka lilistaajabu kuona ishara za uhai katika bonde hili na lilipokaribia na kuona maji lilimuomba Hajar kufanya maskani hapo. Hajar alifurahi sana kupata watu wa kuishi naye na alipokuwa Ismaili mkubwa alioa katika kabila hilo na kuleta kizazi chake ambacho kitakuja kuwa na umuhimu mkubwa hapo Makka na ulimwengu mzima kwa jumla. Katika kizazi cha Nabii Ismail ni Adnan ambaye ndiye babu wa mababu wa makabila ya kikureshi, na kutokana na Makureshi wanatoka Bani Hashim na kutokana na Bani Hashim wanatoka Bani AbdulMuttalib na katika watoto wa AbdulMuttalib ni Abdullah ambaye ni babake Mtume Muhammad (SAW). Amesema Mtume (SAW(: Hakika Mwenyezi Mungu ameteua kutokana na watoto wa Ibrahim, Ismail na akateua kutokana na watoto wa Ismail, Kinana na akateua kutokana na Kinana Qureshi na kutokana na Qureshi Bani Hashim na akaniteua mimi kutokana na Bani Hashim. Imesimuliwa na Muslim Hali ya kisiasa na kimaisha: Kama ilivyotueleza Qurani Takatifu, Waarabu walitawanyika sehemu nyingi baada ya kuvunjika boma la Maarib na kuanzisha miji mipya sehemu hizo walizohamia. Makabila haya ambayo aghlabu yake yalikuwa ni makabila ya kibedui hayatulii mahali pamoja yalikuwa yakisafiri baina ya miji hii mbali mbali kwa sababu ya kufanya biashara na kutafuta maisha. Pamoja na hayo, kulikuwepo na makabila mbali mbali ambayo yalitulia katika miji na kusimamisha mamlaka na kuwa na wafalme na maamiri na mashekhe mbali mbali. Katika hayo ni makabila ya Ghasasina yaliyokuwa na wafalme wao katika sehemu za Sham, na makabila ya Manadhira yaliyokuwa na wafalme wao na mamlaka yao iliyokuwa ikiitwa Al-Hira, na aidha mamlaka ya Kinda ambayo iliyokuwa katika Hijazi. Lakini pamoja na kuwa na mamlaka na wafalme wao, Waarabu hawa walikuwa hawishi vita baina yao kwa sababu ya kupigania ardhi na ukubwa na mali. Makureshi kabla ya kuja Uislamu walikuwa wanahukumu nchi ya Makka na kushughulikia mambo ya mahujaji waliokuwa wakija kuizuru Al-Kaaba na chakula chao na kushughulika na biashara zinazokuja hapo wakati wa Hija au biashara zao zinazoletwa kutoka Sham na Yemen. Hija hii ilikuwa ni masalio ya dini ya Nabii Ibrahim na Nabii Ismail ambayo kwa wakati huu ilikuwa ishachafuliwa sana na kubakia jina tu, kwani kila aina ya masanamu na ibada ya mizimu na majiwe ilikuwa imeshaingizwa ndani yake. Makabila mengine ya kiarabu yalikuwa yakiishi chini ya wakubwa wa kabila zao na walikuwa wakijulikana kama mashekhe wao, na neno lao ndio hukumu na sheria lazima lifuatwe na kila mmoja katika kabila hilo, na kwa hivyo walikuwa ni kama wafalme kwa watu wao, na walikuwa kukitokea vita basi wao hupewa robo ya ghanima (ngawira) na chochote chengine atakachokipenda na kulikuwa dhulma na zina na ufasiki na maasiya mbali mbali yalikuwa yameenea kila upande. Pamoja na hayo, mashairi yao na misemo yao na mithali zao zinatuonyesha kuwa kulikuwepo na tabia njema chungu nzima ambazo walikuwa wakijifakhirisha nazo kama ukarimu na ushujaa na kutimiza ahadi na ghera na kujienzi nafsi na kutokubali kuchezewa na mtu, sifa ambazo zimewapelekea kushika zimamu na hatamu za umma na kuongoza wanadamu mpaka wakafikia kutawala ulimwengu mzima wakati ulipokuja Uislamu. Hali ya kidini Bara Arabu: Aghlabu ya Waarabu, hasa wale waliokuwa wakiishi Bara Arabu walikuwa wakiabudu masanamu kabla ya kuja Uislamu, na hii ni kwa sababu ya mtu mmoja aliyekuja akaleta uzushi huu (bid'a hii) na kuingiza kwenye dini safi aliyowaachia Nabii Ibrahim na Nabii Ismail. Kama tunavyoelezwa na Qurani Tukufu, Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Nabii Ibrahim na mwanawe Nabii Ismail kusimamisha Al-Kaaba hapo Makka ili iwe ndiyo nyumba ya kwanza kabisa ya kuabudiwa Mola Mmoja ulimwenguni na baada ya kulisimamisha jengo waliwaamrisha kizazi chao na Waarabu wengine kufuata dini hii.
Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Al-Kaaba) iwe mahali Sura:Baqara:125 Waarabu waliendelea kufuata dini hii mpaka alipokuja Amr ibn Lahy mkubwa wa kabila la Khuza'a ambaye alikuwa ni mtu wa dini na mcha Mungu na mtenda mema akapendwa sana na watu na kuheshimiwa na kuchukuliwa kuwa mwanachuoni mkubwa. Huyu Amr alikwenda safari Sham akawakuta Wakristo huko wanaabudu masanamu na kwa kuwa Sham ni sehemu iliyoletwa Mitume na Manabii wengi, alidhani hiyo ndio njia ya haki, basi akarudi Makka na sanamu lake liitwalo Hubal na kumuingiza ndani ya Kaaba. Watu wakaipenda bid'a hii na wakaifuata na muda si muda kukazuka masanamu mengine yaliyokuwa yakiabudiwa sehemu mbali mbali badala ya Mwenyezi Mungu kama Lata na Manata na Uzza na yakakithiri na kuzidi na kuenea kila mahali mpaka ikawa kila nyumba kuna sanamu. Kama wanavyosema Waswahili kiingiacho mjini si haramu. Juu ya hivyo, Waarabu wakitambua kuwa kuna Mungu ambaye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi, na kuwa hawa masanamu ni kwa ajili ya kuwakurubisha na Mwenyezi Mungu tu na kuwaombea na kuwasahilishia muradi wao. Lakini baada ya kupita muda, ujahili ukazidi mpaka wakawa wanawaabudu na kuwaomba na kuwataka wawaondoshee shida zao na wakawa wanachinja kwa ajili yao badala ya Mwenyezi Mungu na kuwatolea muhanga na kuwazunguka na kuwaita na kuwasujudia. Waarabu wengine pembezoni mwa Bara Arabu waliathirika na dini mbali mbali za watu jirani na wao, kukawa kuna Waarabu Manasara sehemu za Shamu na Yemen, Waarabu Mayahudi sehemu za Iraq na Yemen na Palestin, na Waarabu Majusi (Maparisi) sehemu za Fursi (Iran) na Iraq na Bahrain. Uyahudi na Ukristo wa zama hizo ulikuwa ushaingia takataka nyingi za uzushi (bid'a) na upotofu, na ulipokuja Uislamu ulizikuta dini hizi zilizoletwa na Mitume Mitukufu Nabii Musa na Nabii Isa zishachafuka na kuharibika na kuwa hazina tofauti na dini nyenginezo za ushirikina, na kwa hivyo ukaja kurekibisha na kusahihisha na kunyosha na kurudisha usafi na uongofu wa dini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa wakati wa Mitume hawa na Mtume Ibrahim.ya kisiasa Bara Arabu: Nasaba ya Nabii Muhammad (SAW) Kama tulivyoeleza hapo nyuma, Mtume Muhammad (SAW) anatokana na kabila la kikureshi ambalo linarudi nasaba yak kwa Nabii Ismail na Nabii Ibrahim. Kutokana na vitabu vya kutegemewa vya sera ya Mtume (SAW), Muhammad ni mtoto wa Abdillahi bin AbdilMuttalib bin Hashim bin Abdi Manaf bin Qusay bin Kilab bin Murra bin Kaab bin Luay bin Ghalib bin Fihr (ambaye jina lake jengine ni Qureysh) bin Malik bin Nadhr bin Kinana bin Khuzayma bin Mudrika bin Ilyas bin Mudhar bin Nizar bin Maad bin Adnan. Nasaba hii inaendelea mpaka kufika kwa hao mababu zao wakubwa kina Ismail na Ibrahim, lakini wanahistoria wamehitalifiana kuhusu mababu wanaofuatia baada ya Adnan na kwa hivyo nasaba ya Mtume mpaka hapa kwa Adnan husita kwa kuchelea watu kufanya makosa kwa kuzidisha au kupunguza mababu wanaokuja baada ya Adnan. Babu yake: Babu yake Mtume (SAW) AbdulMuttalib alirithi cheo na kazi za baba yake Hashim ambaye alipewa sharafu ya kulisha na kunywisha Mahujaji wajapo kuhiji Makka na alikuwa mtu karimu sana na akipendwa na kuheshimiwa na kutukuzwa na watu wake Makureshi kuliko hata wazee wake waliomtangulia. Na katika mambo makubwa aliyoyafanya AbdulMuttalib ni kukigunduwa kisima cha Zamzam kilichokuwa kimefukiwa na kabila la Jurhum walipotolewa Makka, na kukifukuwa tena na kuanzisha kugawa maji yake na kunywesha Mahujaji wanapokuja kuhiji, jambo ambalo linaendelea mpaka hii leo. AbdulMuttalib alipata watoto kumi wa kiume na sita wa kike. Wakiume ni Al-Harith na Az-Zubeyr na Abu Talib na Abdullahi na Hamza na Abu Lahab na Al-Ghaydaq na Al-Maquum na Saffar na Al-Abbas, na wa kike ni UmmulHakim na Barra na A'tika na Safiyya na Arwa na Umayma. Baba yake: AbdulMuttalib aligundua mahali kilipo kisima cha Zamzam baada ya kuoteshwa mahali hapo na kuamrishwa akichimbe. Makureshi wakagombana naye wakitaka na wao washirikishwe katika mali yaliyozikwa humo, AbdulMuttalib akakataa na kusema kuwa ni jambo alilohusishwa yeye tu peke yake. Makureshi wakamchukuwa kwa kuhani awahukumu, lakini njiani Mwenyezi Mungu akawaonyesha dalili kuwa kisima cha Zamzam kimehusishwa AbdulMuttalib peke yake, basi hapo akaweka nadhiri kuwa Mwenyezi Mungu akimjaaliya kupata watoto kumi wa kiume atamchinja mmoja kwenye Al-Kaaba hata ikiwa Makureshi watajaribu kumzuiya. Basi alipopata watoto kumi na akajua kuwa watajaribu kumzuiya asimchinje mmoja wao, aliwakumbusha nadhiri yake wakamsikiliza, akaandika majina yao juu ya mishale na kurushwa likatoka jina la Abdullah. Basi AbdulMuttalib akamchukuwa Abdullah na kuchukuwa na kisu kikubwa na kuelekea kwenye Al-Kaaba ili amchinje, akazuiliwa na Makureshi, akawauliza na nitafanyaje kuhusu nadhiri yangu niliyoiweka?!! Makureshi wakamuelekeza ende kwa muaguzi na alipokwenda alimwambia amfanyie kura baina yake na ngamia kumi na kila mara ikitokea Abdullah basi naaongeze kumi. Akafanya hivyo ikawa inatokea Abdullah mpaka walipofika ngamia mia ikatokea ngamia, basi akachinja ngamia mia. Huyu Abdullah ndiye aliyekuwa mzuri zaidi katika watoto wa AbdulMuttalib na mnyofu zaidi katika wao na alikuwa ni mwenye kujihifadhi na machafu na maovu na ndiye aliyekuwa kipenzi cha baba yake. Alipofikia umri wa miaka ishirini na tano, baba yake AbdulMuttalib alimchagulia mke katika wanawake bora kabisa wa kikureshi Amina bint Wahb bin Abd Manaf bin Zuhra bin Kilab, binti mtukufu wa kibanii Zuhra na baba yake ni mkubwa wa kabila lake. Baada ya ndoa kwa muda mdogo, Abdullah alipelekwa safari na babake AbdulMuttalib lakini alipofika Madina alishikwa na maradhi akafariki dunia. Wakati huu Amina alikuwa tayari ana mimba ya mja wa Mwenyezi Mungu atakayekuja kubadilisha tarehe ya ulimwengu moja kwa moja na kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya binadamu. Kuzaliwa kwake: Katika mwezi wa Muharram kabla ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kwa mwezi na kitu, kulitokea tukio kubwa lililoshitua Bara Arabu nzima na kuwaathiri Waarabu wote kwa jumla khususwan Makureshi. Yemen wakati huu ilikuwa inatawaliwa na Mahabushia na Abraha ambaye alikuwa ni mwakilishi wa mfalme wa Habasha alipoona Waarabu wote wanakwenda Makka kuhiji kwenye Al-Kaaba alijenga kanisa kubwa la fakhari hapo Sanaa ili Waarabu wende kuhiji huko. Mtu mmoja wa kabila la Kinana aliposikia haya alikwenda ndani ya kanisa akalichafua, jambo ambalo lilimghadhibisha sana Abraha na akaunda jeshi kwenda kuivunja Al-Kaaba. Kisa hiki kimeelezwa ndani ya Qurani vipi watu wenye ndovu mkubwa walivyotaka kuivunja Al-Kaaba, Mwenyezi Mungu akawapelekea ndege makundi makundi na kuwatupia mawe ya adhabu:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mjawa wa Rehema,
Mwingi wa kurehemu Sura:Al-Fil:1-5 Watu wote wa zama hizo walisikia kisa hiki na kutambua utukufu wa nyumba hii na mahali hapa, na baada ya pilikapilika ya tukio hilo kwa muda mdogo tu ndipo alipozaliwa mbora wa wanadamu, na kwa hivyo wanahistoria wanatueleza kuwa Mtume Muhammad (SAW) alizaliwa katika mwaka wa ndovu kwa mujibu wa tukio hili na mwenyewe Mtume (SAW) anatueleza katika Hadithi Sahihi kuwa alizaliwa siku ya Jumatatu. Baada ya kuzaliwa, mamake alimpelekea habari AbdulMuttalib babu yake na akaja akiwa na furaha kubwa na akamchukuwa kwenda naye kwenye Al-Kaaba, na hapo akamshukuru Mwenyezi Mungu na kumuomba, kisha akampa jina Muhammad, jina ambalo lilikuwa si mashuhuri baina ya Waarabu. Zilipopita siku saba, babu yake alimchukuwa kumpasha tahara kama ilivyokuwa desturi ya Waarabu wakati huo, na akawa mama yake Amina anamnyonyesha siku za kwanza kabla ya kuchukuliwa na Thuwayba kijakazi wa Abu Lahab ami yake Mtume (SAW) ambaye vile vile alimnyonyesha Hamza ami yake mwengine, na akawa Baraka (Umm Ayman) kijakazi wa kihabushia aliyeachiliwa na baba yake Abdullah ndiye aliyekuwa akimlea. Kupelekwa Jangwani: Waarabu wa zama za nyuma walikuwa na desturi ya kuwapeleka watoto wao jangwani ili kuwaepusha na maradhi na hali ya hewa chafu ya mjini, wapate kuishi kwenye hali ya hewa safi na wainukie wakiwa na nguvu na siha nzuri na lugha fasaha. Kwa hivyo, AbdulMuttalib babu yake Mtume (SAW) alimtafutia mwanamke atakayemnyonyesha mjukuu wake akiwa mbali na mji, na walipokuja wanawake kutokana na kabila la Bani Saad bin Bakr, alibahatika Halima Assaadiya kumpata mtoto huyu wa baraka nyingi kurudi naye jangwani, na muda wote alipokuwa huyu mtoto kwao, baraka nyingi ziliwashukia mpaka akatimia miaka minne. Kurudishwa kwa mama yake: Halima, mnyonyeshi wa Mtume (SAW) alikuwa hataki kumrudisha kwa mamake kwa sababu ya baraka nyingi aliyoiona baada ya kumchukuwa mtoto huyu, kwani anaeleza kuwa baada ya kumchukuwa tu maajabu mengi yalitokea. Anasema Halima, kwa mujibu alivyoeleza Ibn Is-haq, kuwa alitoka mji wao na mumewe na mwanawe, pamoja na wanawake wengine wa Bani Saad kutafuta watoto wa kunyonyesha, na ulikuwa ni mwaka mkavu hakuna kitu kwao. Akasema Halima: Tukatoka juu ya punda wangu mweupe pamoja na ngamia mkongwe hatoi tone la maziwa, na tulikuwa hatulali kwa kilio cha mtoto wetu ambaye alikuwa akilia kwa njaa kwani maziwa yangu yalikuwa hayamtoshelezi, na ngamia wetu hatoi chochote, lakini tulikuwa tunataraji faraji. Nikatoka juu ya punda wangu huyo na kumpanda mpaka akachoka kwa udhaifu aliokuwa nao. Tukafika Makka na kuanza kutafuta watoto wa kunyonyesha, na kila katika sisi anayepewa Muhammad (SAW) alikuwa akikataa akiambiwa kuwa ni yatima kwa kujua kuwa maadamu hana baba, basi mama yake au babu yake ataweza kutulipa nini? Wanawake wote waliokuja na mimi walipata watoto isipokuwa mimi, na tulipokuwa tayari tunataka kurudi kwetu, nikamwambia mwenzangu: Wallahi, mimi ninachukia kurudi pamoja na wenzangu bila kuchukuwa mtoto wa kunyonyesha. Wallahi, nitakwenda kwa yule yatima nikamchukue. Mume wangu akaniambia: Hapana neno, asaa Mwenyezi Mungu atujaaliye kwake baraka. Basi nikenda kumchukua na hapana lililonipeleka kumchukua isipokuwa kwa sababu sikupata mwengine. Basi nilipomchukua na kurudi naye kwenye kipando changu, nilimweka mapajani mwangu na kumpa maziwa yangu ambayo alinyonya mpaka shibe yake na akanywa na nduguye (mwanangu) mpaka akashiba na kulala na tulikuwa kabla ya hapo hatulali kwa kilio chake. Huku mume wangu akenda kwa ngamia wetu akamkuta amejaa maziwa akamkamua tukanywa mpaka tukatosheka na kushiba na tukalala usingizi mzuri usiku huo. Asubuhi yake mume wangu akaniambia: Unajua Halima Wallahi, umechukua mtoto wa baraka. Nikamwambia: Wallahi, ninataraji iwe hivyo. Kwa hivyo, Mtume (SAW) akabakia kwa mamake wa kunyonya miaka miwili kisha akamwachisha ziwa na kumrudisha kwa mama yake Amina huku wakitamani abakie kwao kwa baraka nyingi walizoziona, na baada ya kumuomba Amina na kumwambia asubiri mpaka atie nguvu zaidi na kuwa anamuogopea maradhi ya mji wa Makka, alikubali mamake na akabaki kwa Halima kwa muda wa miaka miwili mengine, mpaka lilipotokea jambo ambalo lilimuogopesha sana Halima na kuamua kumrudisha upesi upesi kwa mzazi wake. Kutolewa nyongo: Jambo hili lilimtokea wakati Mtume (SAW) alipokuwa anacheza na nduguze wa kunyonya nyuma ya nyumba yao. Alikuja Jibril (AS) akamchukua na kumlaza chini na kumpasua kifua na kuutoa moyo wake na kuchukua kitu, kisha akasema: Hii ni sehemu ya Shetani kutoka kwako. Kisha akauosha ndani ya tasa la dhahabu kwa maji ya Zamzam na kuurudisha mahali pake. Nduguye wa kunyonya alipoona haya alikimbia kwa wazee wake na kuwaarifu na hapo hapo wazee wake walikimbia kwenda kumtazama wakamkuta mzima lakini amebadilika rangi. Tukio hili lilimtisha na kumshitua sana Halima akaona bora afunge safari kumrudisha mtoto kwao akiwa ni mtoto wa miaka minne. Kufariki kwa mama yake Amina: Baada ya kurudi kwa mama yake, alikaa Mtume (SAW) naye miaka miwili akawa keshafikia umri wa miaka sita. Mama yake akaona bora amchukuwe ende naye Madina kuzuru wajomba wa baba yake Bani Najjar, lakini baada ya ziara wakati wa kurudi, mama yake alishikwa na maradhi njiani akafariki mahali paitwapo Abwa baina ya Makka na Madina. Kuchukuliwa na babu yake AbdulMuttalib: Baada ya kufa mama yake, Mtume (SAW) alichukuliwa na babu yake AbdulMuttalib na kulelewa kwake. Babu yake akawa anampenda sana na kumtanguliza na kumtendekeza kuliko hata wanawe wenyewe, lakini mapenzi haya hayakuendelea kwa muda mrefu kwani baada ya kupita miaka miwili akiwa Mtume (SAW) ni mtoto wa miaka minane babu yake pia alifariki dunia. Kulelewa na ami yake Abu Talib: Ami yake Abu Talib alimchukua mtoto wa nduguye kwa mapenzi yote na kumtanguliza kuliko wanawe kama alivyokuwa akifanya baba yake AbdulMuttalib, na kumpa heshima kubwa, na alikuwa Mtume (SAW) kama alivyoeleza mlezi wake Umm Ayman, tofauti na watoto wengine, hapendi upuuzi, hashughuliki na michezo na ni mtoto aliyekinai sana, hapapii kitu chochote wala hana pupa wala papara, anachopata anashukuru. Ami yake alisimama na Mtume (SAW) katika shida na furaha muda wote wa uhai wake na akampigania katika kila hali mpaka alipofariki baada ya zaidi ya miaka arubaini kupita tangu achukuwe jukumu la kumuangalia mtoto wa nduguye. Abu Talib alipokuwa anataka kwenda Sham kwa ajili ya biashara, aliona taabu kumwacha Mtume (SAW) nyuma, na alivyokuwa ni kijana aliyefikia umri wa miaka kumi na mbili wakati huo, alihisi bora amchukuwe, lakini walipofika mji unaoitwa Busra karibu na Sham, walikutana na mtawa wa kinasara aitwaye Bahira, na alipomuona Muhammad (SAW) alimtambua kwa sifa zake kuwa ndiye Nabii anayesubiriwa aliyetajwa kwenye vitabu vyao vya dini, akamshauri ami yake amrudishe wala asiingie naye Sham maana huko huenda Mayahudi wakataka kumuua. Basi Abu Talib akatumiza baadhi ya vijana wake warudi naye Makka. Inasemekana kuwa Mtume (SAW) alipofikia umri wa miaka kumi na tano au ishirini, kulizuka vita Makka baina ya Makureshi na Qais I'laan. Sababu ya vita hivi ni kuwa Urwa mtu wa kabila la Qais alichukuwa dhamana ya kufikisha bidhaa za Al-Nuuman bin Al-Mundhir kwenye soko la Ukadh huko Makka kwa salama kupitia makabila yote njiani. Akasimama Al-Barradh mtu wa kabila la Kinana la kikureshi na alikuwa ni mtu muovu, akamuuliza Urwa: Utazipitisha bidhaa hata kwa Kinana? Akajibu Urwa: Nitazipitisha kwa watu wote. Alipotoka Urwa na bidhaa, Al-Barradh alimfuata na kumuua kwa khiyana, kisha akapeleka mtu awaambie kabila lake Kinana yaliyotokea na kuwahadharisha kabila la Urwa - Qais I'laan. Huku kabila la Urwa liliposikia tu lilijikusanya kuchukuwa kisasi cha jamaa yao, na tukio hili lilitokea katika mwezi mtukufu ambao haviruhusiwi ndani yake vita wala ugomvi, na kwa sababu hii vikaitwa vita vya fasadi kwa sababu ya kuvunjwa heshima ya mwezi mtukufu na heshima ya mji wa Makka. Qais I'laan wakapigana na Makureshi mpaka viliposhtadi vita, Makureshi wakakimbia na kuingia ndani ya msikiti wa Makka. Hapo Qais wakarudi nyuma na kuahidiana na Makureshi kupambana mwaka ujao kwenye soko la Ukadh. Mwaka ulipoingia lilikuja kabila la Qais pamoja na makabila mengine marafiki zao na Makureshi wakakusanya masahibu zao na kupambana na Qais na mwanzo vita viliwaelemea sana Kinana lakini kisha wakawa wanawashinda Qais mpaka aliposimama mmoja wa Kinana akaomba iwepo sulhu baina ya makabila na kusema kuwa upande wowote utakaopatikana maiti wengi zaidi basi watalipwa dia, makabila yakakubali na Kinana ikabidi walipe wao kwa sababu waliouliwa wengi walikuwa katika kabila la Qais. Mtume (SAW) alishuhudia vita hivi akiwa bado kijana mdogo wa miaka kumi na tano kama alivyoeleza Ibn Hisham au miaka ishirini kama alivyoeleza Ibn Is-haq. Chama dhidi ya dhulma: Baada ya vita hivi, makabila yote ya kikureshi yalikutana kwenye nyuma ya Abdullahi bin Jud'an Attaymi na wakapatana na kuahidiana kuwa wasimkute mtu yeyote kadhulumiwa Makka katika wakaazi wake au wapita njia isipokuwa watamsaidia kumrudishia haki yake. Mapatano haya yalihudhuriwa na Mtume (SAW) na baada ya kupewa utume alisema:
Nilishuhudia pamoja na ami zangu katika nyumba ya Abdillahi bin
Jud'an mapatano Imesimuliwa na Al-Humayriyu Maisha magumu: Tunaelezwa kuwa Mtume (SAW) mwanzo wa ujana wake alikuwa hana kazi maalumu, lakini mara nyingi alikuwa akichunga mbuzi na kondoo wa watu wa Makka kwa vijipesa kidogo mpaka alipofika umri wa miaka ishirini na tano akapata kazi ya kumfanyia biashara bibi mtukufu kabisa wa kikureshi ambaye baadaye atakuja kuwa mkewe. Khadija bint Khuwaylid kama anavyoeleza Ibn Is-haq alikuwa ni mfanyibiashara mwenye mali nyingi sana na alikuwa akiajiri watu kwenda kumfanyia biashara zake na aliposikia uaminifu mkubwa na akhlaki njema za Muhammad (SAW) na ukweli wake, alimtaka aende Sham kumfanyia biashara na atampa ujira mkubwa kuliko aliokuwa akiwapa watu wengine, na Muhammad (SAW) akakubali. Khadija (RA) akamtoa mtumwa wake aitwaye Maysara kufuatana na Mtume Muhammad (SAW) katika safari yake hiyo na waliporudi walirudi na faida kubwa sana na Maysara akamueleza Khadija (RA) yote aliyoyaona kwa Mtume (SAW) ya wema na hisani na tabia njema na uaminifu na baraka kubwa iliyoingia kwa ajili ya uaminifu na uadilifu wake. Khadija (RA) akampenda sana Mtume (SAW) na kutamani aolewe na mtu mwema kama huyu, basi akamtumiza mwenzake amdokeze Mtume (SAW) na alipomwambia alikubali na kuwaambia ami zake, nao wakenda kwa ami yake Khadija kumposa na akakubali na kufungwa akdi kwa kuhudhuria Bani Hashim na wakubwa wa kikureshi, naye ndiye mke aliyekaa naye peke yake bila kumuolea mke mwengine mpaka alipofariki dunia. Khadija (RA) aliolewa na Mtume (SAW) akiwa na umri wa miaka arubaini na Mtume (SAW) miaka ishirini na tano. Alikuwa ndiye mke wa kwanza kwa Mtume (SAW), lakini yeye alikuwa keshaolewa mara mbili, mara ya kwanza na Abu Hala na akazaa naye mtoto wa kiume aitwaye Hind, kisha akaolewa na U'tayyiq na kuzaa naye mtoto wa kike aitwaye Hind vile vile. Ameishi Mtume (SAW) na Khadija miaka ishirini na tano, na akafariki akiwa na umri wa miaka sitini na tano kabla ya kuhamia Mtume (SAW) Madina kwa miaka mitatu. Amezaa na Mtume (SAW) watoto sita isipokuwa mmoja tu ambaye amezaliwa na Maria suriya wake. Alipokuwa na Khadija alikuwa hana mke mwengine na aliishi naye peke yake na kutuwachia mfano wa vipi mtu anaishi na mke mmoja peke yake, kisha alipokufa alioa wake wengi na kutuwachia mfano wa vipi mtu anaishi akiwa na wake wengi. Kujengwa kwa Al-Kaaba: Qurani Tukufu inatueleza kuwa nyumba ya kwanza iliyojengwa kwa ajili ya watu wamuabudu Mwenyezi Mungu Mmoja ni ile iliyoko Makka:
Hakika Nyumba ya kwanza waliowekewa watu kwa
ibada ni ile iliyoko Bakka, Sura: Al-Imraan:96 Qurani Tukufu inatueleza kwamba Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Nabii Ibrahim na Nabii Ismail waitahirishe nyumba yake kwa ajili ya wenye kutufu na wenye kusali na kumtaja Mwenyezi Mungu. Kisha tukaelezwa kuwa Nabii Ibrahim na Nabii Ismail waliinua misingi ya nyumba hii ya Al-Kaaba huku wakimuomba Mola wao awatakabalie kazi yao hiyo ya kuisimamisha Al-Kaaba:
Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni
Nyumba yangu kwa ajili ya wenye kutufu, Sura: Al-Baqara:125
Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua
misingi ya ile Nyumba wakaomba: Sura: Al-Baqara:127-128
Imepokewa kutoka kwa Abi Dhar (RA) kuwa amesema:
Nilisema: Imesimuliwa na Ahmad bin Hanbal Kujengwa Al-Kaaba upya: Kabla ya Utume kwa miaka mitano, Makureshi waliamua kuivunja Al-Kaaba na kuijenga upya kwa sababu ya kuharibiwa na mafuriko na moto ambao ulizichafua kuta zake. Makureshi wakakutana na kushauriana namna ya kuijenga Al-Kaaba kwa sharti isiingie mali yoyote ile ya haramu katika kuijenga, na kwa hivyo wakakataa pesa za riba, na za umalaya na za dhulma. Lakini walikabiliwa na tatizo la kuivunja kwa kuogopa wasije wakadhurika kwa kufanya hivyo mpaka alipoingilia Walid bin Mughira na kuwauliza kwani munaivunja kwa kuiharibu au kuitengeneza na walipojibu Makureshi kuwa wanakusudia kuitengeneza, basi aliwaambia kuwa Mwenyezi Mungu haangamizi wenye kutengeneza na akaanza yeye kuivunja, ndipo walipomfuata walipoona hakufikwa na madhara wala ubaya wowote. Al-Kaaba ikagawanywa sehemu na kila kabila la kikureshi likavunja na kukusanya mawe ya sehemu yake, kisha wakaanza kuijenga upya, na walipofika sasa wanataka kuliweka jiwe jeusi mahali pake wakahitalifiana nani apate heshima na sharafu ya kuliweka jiwe hili tukufu mahali pake, na hitilafu ikageuka kuwa ugomvi mpaka ikafikia hadi kutaka kusimamisha vita baina yao kwenye ardhi tukufu ya Makka. Abu Umayya bin Mughira Al-Makhzumi alivyoona haya aliwapa shauri wakubali uamuzi wa mtu wa kwanza atakayeingia mlango wa msikiti wa Makka wakaridhia, na Mwenyezi Mungu akajaaliya mtu huyo kuwa ni Muhammad (SAW) na wote walipomuona walipiga kelele na kusema: Huyu mwaminifu tumeridhia! Huyu Muhammad! Muhammad (SAW) alipoelezwa tatizo lililowakabili, aliwaambia walete guo na alipoletewa alilichukua jiwe na kuliweka ndani yake na kuwaamuru kila kabila washike sehemu moja na wainue pamoja na walipofika kwenye mahali panapotaka kuwekwa jiwe aliliinua yeye mwenyewe na kuliweka na tatizo likesha. Muhammad (SAW) wakati huu alikuwa na umri wa miaka thalathini na tano, lakini watu wote walikuwa wakimjua kama ni mtu mkweli na mwaminifu kwa sababu ya ukweli wake na uaminifu wake na akhlaki zake njema na upole na ukarimu na uhisani na ujirani mwema na usaidizi. |
|
|||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|