|
Kubashiriwa kuja kwa Mtume Muhammad (SAW): Kwa kuwa Muhammad (SAW) ndiye Mtume na Nabii wa mwisho hapana mwengine atakayekuja baada yake, na kwa kuwa yeye ndiye Mtume pekee aliyeletwa kwa wanadamu wote ulimwenguni kinyume na waliokuja kabla yake ambao waliletwa kwa watu wao maalumu, na kwa kuwa yeye ndiye atakayekuja kukamilisha ujumbe na dini ya Mwenyezi Mungu duniani, kwa hivyo vitabu vyote vya dini vilivyotangulia vilieleza kuja kwa Mtume huyu mtukufu (SAW) Ikasema Taurati: Nitawaletea Mtume kama wewe (yaani kama wewe Musa), kutokana na ndugu zao (yaani kutokana na ndugu za Mayahudi ambao ni Waarabu, kwani Nabii Musa na Nabii Muhammad wanakutana asli zao kwa Nabii Is-haq na Nabii Ismail ambao baba yao ni Nabii Ibrahim), na nitatia maneno yangu kinywani mwake (yaani hatosema isipokuwa maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo ni Qurani), na atawaambia kila kitu nitakachomuamrisha (yaani atawafikishia ujumbe kamili), na yeyote yule ambaye hatotii maneno yake ambayo atakayoyasema kwa jina langu (yaani atasema kwa jina la Mwenyezi Mungu), basi Mimi nitalitaka neno hili kwake (yaani atamhukumu siku ya Kiyama). Kumbukumbu:18:18 Na ikasema Injili: (Yeye ataueleza ulimwengu kuhusu dhambi na hatia, na kuuongoza kwenye haki na ukweli wote kwani atakuwa hasemi kutokana na yake mwenyewe, bali atasema yote atakayoyasikia). Yohana:16 Yaani atawafahamisha wanadamu kuhusu Sharia yote ya Mwenyezi Mungu wala hatosaza kitu na atawaeleza mema na maovu na ataeleza yale aliyoyapokea kutoka kwa Mola wake tu. Na haya yanathibitishwa ndani ya Qurani wakati inapotuambia kuwa Mtume (SAW) hasemi kwa matamanio yake, bali ni Wahyi kutoka kwa Mola wake.
Naapa kwa nyota inapotua, (kuwa) Sura:An-Najm:1-4 Kwenye Pango la Hira: Miaka ya mwisho kabla Muhammad (SAW) kufikia umri wa miaka arubaini, alikuwa akichukuwa chakula na maji yake na kwenda kwenye pango la Hira katika jabali la Nur kukaa na kufikiri na kutaamali juu ya dunia na pambizo za mbingu zilizomzunguka na maumbile yake. Dunia wakati huo ilikuwa imechakaa kwa madhambi na maasiya, na shirki na ukafiri ulikuwa umezagaa na kuenea kila upande. Mwenyezi Mungu kwa hekima yake alimuongoza aje mahali kama hapa mbali na fujo na ghasia za maisha ili azingatie mambo yaliyomzunguka na atie maanani matatizo yaliyoenea kila sehemu ili roho yake na moyo wake uwe tayari kukabiliana na mazito atakayopambana nayo kwa kusimamia haki na kupiga vita batili. Muhammad (SAW) alikaa katika hali kama hii kwa muda wa miaka mitatu akenda katika hilo pango kutafakari na kutaamali mpaka kinapomalizika chakula chake na maji yake hurudi kwa Khadija na kuchukuwa chakula na maji mengine - mara akikaa huko kwa masiku, mara kwa wiki, na mara nyengine mwezi mpaka Mwenyezi Mungu alipoamua kuteremsha rehema yake juu ya wanadamu ulimwenguni kwa kuwaletea hidaya na uwongofu. Wahyi wa kwanza: Mwenyezi Mungu ili kumtayarisha mja wake kupokea jambo kubwa na zito kama hili la Utume, alikuwa akimletea Muhammad (SAW) ndoto na kila ndoto aliyokuwa akiiona usingizini humdhihirikia waziwazi kama pambazuko la asubuhi. Hizi zilikuwa ni pepesi za mwanzo za Utume. Kisha Mwenyezi Mungu, kwa rehema na fadhila zake, akamtunukia mja wake na kipenzi chake Muhammad (SAW) alipokuwa amejitenga kwenye pango la Hira ufunuo wa kwanza kutoka kwake mbinguni kwa kumletea Mjumbe wake Mtukufu Jibril (AS). Wakati huu Muhammad (SAW) alikuwa keshatimia miaka arubaini, umri wa ukamilifu wa akili na kiwiliwili. Usiku mmoja katika mwezi wa Ramadhani alipokuwa Muhammad (SAW) kwenye pango la Hira alijiliwa na Jibril (AS) na kumwambia: Soma! Muhammad akajibu: Mimi si msomaji. Akamfunika kwa mto mpaka akawa taabani, kisha akamwacha na kumwambia: Soma! Akasema: Mimi si msomaji. Akamfunika tena mpaka akahisi anataka kufa kisha akamwachia na kumwambia: Soma! Akasema: Nisome nini? Akamwambia:
Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba,
Kisha akaondoka Jibril (AS) akiwa Mtume (SAW) ameshayahifadhi maneno haya kama ambayo yameandikwa kwenye moyo wake. Akatoka kwenye pango mbio na alipokuwa katikati ya jabali alisikia sauti mbinguni inamwambia: Ewe Muhammad wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mimi ni Jibril na alipoinua kichwa chake mbinguni alimuona Jibril katika sura ya mtu miguu chini katika pambizo za mbingu anamwambia: Ewe Muhammad! Wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mimi ni Jibril. Mtume (SAW) alirudi mbio kwa mkewe Khadija (RA) na kumueleza Khadija yaliyomtokea na kumwambia: Nilijiogopea nafsi yangu. Khadija (RA) akamtuliza: La abadan, Wallahi, Mwenyezi Mungu hatakudhalilisha abadan. Hakika wewe unatazama jamaa zako, na unamchukuwa kila mtu, na unawapa wasiokuwa na kitu, na unawakirimu wageni na unasaidia katika misiba, basi Mwenyezi Mungu hatowaacha mashetani na mazingaombwe kukutawala, na hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu amekuchagua ili kuwaongoza watu wako. Kisha Khadija (RA) akenda kwa binamu yake Waraqa bin Naufal ambaye alikuwa ni Mkristo na anajua yaliyoandikwa kwenye vitabu vilivyotangulia, akamwambia yaliyomtokea Mtume (SAW) pangoni, akasema: Mtakatifu! Mtakatifu! Na kwa yule ambaye roho ya Waraqa imo mkononi mwake, ikiwa unaniambia kweli Khadija, basi yeye amejiliwa na Malaika Mkubwa ambaye alikuwa akimjia Musa na kwa hakika yeye ni Nabii wa Umma huu! Basi mwambie athibiti. Khadija (RA) akarudi kwa Mtume (SAW) na kumuarifu aliyoyasema Waraqa bin Naufal, na baada ya muda akakutana na Waraqa akamuuliza na yeye akamueleza aliyoyaona naye akamwambia kuwa wewe ni Nabii wa umma huu na laiti nina ujana na uhai wakati watu wako watakapofukuza mji. Mtume (SAW) akamuuliza kwani watanitoa mji? Akasema: Naam, haji mtu katu na jambo kama hili ulilokuja nalo (la haki) isipokuwa atapigwa vita na kufanyiwa uadui na lau nitaiwahi siku hiyo basi nitakusaidia kwa uwezo wangu wote, lakini Waraqa hakukaa muda mkubwa baada ya tukio hilo akafa. Kuteremshiwa Wahyi tena: Alipokwenda Mtume (SAW) kwenye pango la Hiraa kama ilivyokuwa ada na desturi yake alikaa siku za kukaa na baada ya kumaliza siku zake aliondoka kurudi nyumbani akasikia sauti inamwita, akatazama kila upande asimuone amwitaye kisha akapandisha macho yake mbinguni hapo ndipo alipomuona yule Malaika aliyemjia wakati alipokuwa pangoni amekaa katika kiti baina ya mbingu na ardhi, akaingiwa na khofu na kuanguka chini, kisha akarudi kwa mke wake na kumwambia: Nifunikeni! Nifunikeni! Basi wakamfunika guo mpaka akatulia. Na hii ndiyo mara ya kwanza Mtume (SAW) kumuona Jibril (AS) katika sura yake ya kimalaika. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii:
Ewe uliyejigubika! Simama uonye!
Basi Mtume (SAW) akaanza kufikisha ujumbe kwa wale waliokaribu naye na ambao anawaamini katika jamaa zake na marafiki zake. Baada ya kuteremka Aya hizi Wahyi ulichelewa muda mkubwa kiasi cha miaka miwili mpaka Mtume (SAW) akaingiwa na huzuni na kuona dhiki kisha Jibril (AS) akateremshwa na Sura ya Ad-Dhuha na kumliwaza Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kumwambia kuwa Mola wake hakumtupa wala kumchukia na kuwa aliyomwekea Akhera ni mazuri zaidi kuliko ya hapa duniani, na kumkumbusha neema alizompa hapa duniani kwa kumpa wa kumtazama alipokuwa yatima, na kumuongoza katika njia ya haki na kumuondoshea dhiki zake za uhitaji, basi na atazame mayatima na wenye uhitaji na ashukuru neema za Mola wake, akasema Mwenyezi Mungu:
Naapa kwa mchana! Na kwa usiku unapotanda!
Waislamu waliokuwa wamesilimu pamoja na Mtume (SAW) walifurahi sana waliosikia Aya hizi na wakamtukuza Mwenyezi Mungu. Aina za Wahyi: Kama tulivyoona, Mtume (SAW) mara kwanza alipomteremkia Jibril (AS) alikuja kwa sura ya mtu, kisha akamjia kwa sura yake ya kimalaika na hizi ni njia mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu humteremshia mja wake wahyi wake, na kama alivyotueleza ndani ya Qurani, Mwenyezi Mungu hazungumzi na mja wake isipokuwa kwa njia hizi alizozitaja:
Na haikuwa kwa mtu kwamba Mwenyezi Mungu Huja Wahyi kama mlio wa kengele na huwa mzito ukija namna hivi kwa Mtume (SAW) au huteremshwa Jibril (AS) kwa sura ya binadamu au ya Malaika, au Mola wake huzungumza naye kwa nyuma ya pazia kama alivyozungumza naye alivyopelekwa Israa na Mi'raj. Tumeona umuhimu mkubwa sana wa elimu katika Aya za kwanza alizoteremshiwa Mtume Muhammad (SAW) na namna alivyosisitizwa kusoma na kujua na kuzidisha maarifa kwa jina la Mola wake. Hii ni kwa sababu bila elimu mwanadamu anakuwa mjinga na huwa hana tofauti na hayawani na ni mara moja kupotea na kuangamia. Kisha Mwenyezi Mungu alipomteremshia Mtume wake Wahyi kwa mara ya pili alimuamrisha kuzindukana na kuanza kufikisha ujumbe na kumtukuza Mola wake aliyemuumba na kumpa neema ya Uislamu na Imani, na ajitahirishe na kusafisha nguo zake na kujiepusha na kila uchafu na najisi na shirki. Mtume (SAW) akaanza mwanzo kuwaendea watu wake na wale walio karibu naye. Kwa hivyo, watu wa mwanzo kuukubali ujumbe na kuingia katika Uislamu ni mkewe Khadija (RA) na binamu yake Ali bin Abi Talib ambaye alikuwa akilelewa na Mtume (SAW) na huru wake ambaye alimfanya kama mwanawe Zayd bin Haritha na rafiki yake mpenzi Abubakar Assiddiq na Umm Ayman Baraka mlezi wa Mtume (SAW). Kisha wakafuata wengineo ambao walifikishiwa ujumbe kisiri na Abubakar (RA) wakaukubali nao ni Uthman bin Affan na Zubeyr bin Awwam na Abdur Rahman bin A'wf na Saad bin Abi Waqqas na Talha bin Ubaydillah. Aidha, katika masahaba wa mwanzo ni Suhayb Arrumi na Ammar bin Yasir na mamake Sumayya (shahidi wa kike wa kwanza katika Uislamu) na babake Yasir na Abdullahi bin Masoud na Bilal bin Rabah (muadhini wa Mtume) na Abu Ubayda bin Al-Jarrah na Abul-Arqam bin Abil-Arqam na Uthman bin Madhuun na Ubayda bin Al-Harith na Said bin Zayd na mkewe Fatma bint Al-Khattab nduguye Umar bin Al-Khattab. Hawa walisilimu kisiri wakawa wanakutana pamoja na Mtume (SAW) akiwafundisha dini yao na kuwaamrisha wajiepushe na maovu na machafu na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuabudu masanamu, na kuwa hapana wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mmoja tu peke yake.
Ili kufahamu umuhimu mkubwa wa watu wa kwanza waliokubali ujumbe wa Mwenyezi Mungu, na kujua kazi walioifanya katika kuupigania Uislamu na kuusimamisha kwa uwezo wao wote na kuulinda kwa hali na mali mpaka ikawa ndio dini ya Bara Arabu nzima kwa muda mchache kabisa na dini ya ulimwengu wote ndani ya muda mdogo usiokuwa na mfano, inabidi tueleze kwa muhtasari nani hao Waislamu wa mwanzo. Khadija bint Khuwaylid: Khadija bint Khuwaylid alikuwa ni bibi mtukufu kabisa na tajiri sana aliyekuwa akijulikana na wafanyibiashara wengi ambao wakimfanyia biashara zake na kumhudumikia kabla ya kuolewa na Mtume (SAW). Kisha Khadija (RA) akaja akaolewa na Mtume Muhammad (SAW) na akawa ni mke pekee aliyemzaliya watoto wake wote isipokuwa Ibrahim. Bibi huyu alisimama na Mtume (SAW) kwa hali na mali tangu alipoijua haki na kushikamana nayo na akatumia uwezo wake wote katika kupigania haki na kuusimamisha Uislamu, na yeye ndiye mama wa kwanza wa Waislamu wote na ni bibi mtukufu duniani na Akhera na mmojawapo wa wanawake bora kabisa duniani pamoja na Fatma binti wake na Maryam mama yake Isa (AS) na Asya mlezi wa Musa (AS). Ali bin Abi Talib: Binamu wa Mtume Muhammad (SAW) na mkwewe kwa kumuoa binti yake Mtume Fatma, na ni Khalifa wa nne muongofu baada ya Abubakar na Umar na Uthman (RA). Alikuwa mtoto wa kwanza kusilimu na ni mtu wa kwanza kujitolea muhanga kwa ajili ya Uislamu siku alipoamrishwa Mtume (SAW) kuhama kwenda Madina na ni katika wa kwanza aliyetoa upanga wake kupigana na washirikina katika vita vya Badr, na ni mtu ambaye ameshiriki vita vingi vya Jihadi na chini ya uongozi wake imetekwa Khaybar. Alikuwa ni mtu shujaa sana, mwenye elimu nyingi na ufasaha mkubwa kabisa. Mara nyingi masahaba wakitaka shauri lake na uamuzi wake katika mambo mbali mbali ya kidini na kidunia. Amekufa shahidi baada ya kuuliwa na AbdurRahman bin Muljim alipokuwa anaelekea msikitini kwa Sala ya Alfajiri. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. Zayd bin Haritha: Mtumwa aliyenunuliwa na Khadija kisha akampa zawadi Mtume (SAW) naye akamwacha huru na kumfanya kama mwanawe hata akimwita Zayd bin Muhammad kwa namna alivyokuwa akimpenda. Yeye ndiye sahaba pekee aliyetajwa ndani ya Qurani wakati alipoozwa binti wa shangazi lake Mtume (SAW) kwa amri ya Mwenyezi Mungu ili kuweka Sharia ya kuondosha ada ya watu kuchukuwa watoto si wao na kuwapa majina yao kama alivyofanya Mtume (SAW) kwa Zayd, kisha akamuoa yeye huyo bibi Zaynab bint Jahsh ambaye alikuwa ameolewa na Zayd kuonyesha kuwa Zayd si mwanangu kwani ingekuwa mwanawe asingeweza kumuoa baada ya kuachwa na Zayd. Kisha akamuoza mlezi wake Umm Ayman. Amekufa shahidi katika vita vya Muuta. Umm Ayman (Baraka): Bibi huyu alikuwa kijakazi wa kihabushia wa baba yake Mtume (SAW) na ndiye aliyemlea Mtume Muhammad alipokuwa mdogo. Ni katika Waislamu wa mwanzo kabisa. Aliolewa na Zayd bin Haritha huru wa Mtume (SAW) na mama wa Usama bin Zayd katika maamirijeshi na mashujaa wakubwa wa kiislamu. Ukoo wa bibi huyu ulikuwa ukipendwa sana na Mtume (SAW) kwani yeye alikuwa ndiye aliyemlea Mtume na mumewe ni mwana wake wa kulea. Abubakar Assiddiq: Rafiki mpenzi chanda na pete wa Mtume (SAW) na mkwewe kwa kumuoa Mtume (SAW) bintiye Aysha. Ni mtu wa kwanza nje ya ukoo wake Mtume (SAW) kusilimu na wa kwanza kuita watu wengine kwenye Uislamu. Alikuwa ni mshauri mkubwa wa Mtume (SAW) katika kila jambo. Ni sahaba mkubwa kabisa, karimu sana kufika hadi kusabilia mali yake yote kwa ajili ya Uislamu. Ni Khalifa wa kwanza wa Mtume (SAW) na ameshiriki katika vita vingi na kusimamisha vita dhidi ya waliortadi wakatoka kwenye dini ya Uislamu na wale waliotaka kuzuia Zaka wasitoe baada ya kufa Mtume (SAW). Aliwacha watumwa wengi huru baada ya kuwanunua kutokana na makafiri walipokuwa wakiwatesa kwa kusilimu. Mtume (SAW) alimchagua kuwa ndiye waziri wake alipokuwa mgonjwa, na kiongozi wa mahujaji katika Hija ya mwanzo iliyofanywa katika Uislamu na ndiye sahaba alipata hadhi ya kuhama pamoja na Mtume (SAW) kwenda Madina. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. Uthman bin Affan: Katika masahaba wakubwa kabisa wa Mtume (SAW). Aliingia katika Uislamu baada ya kuelezwa na Abubakar Assidiq ukweli na uzuri wa dini hii, na alikuwa wa kwanza kuhama Makka kwenda Habasha (Ethiopia) pamoja na mkewe Ruqayya baada ya mateso aliyoyaona kwa Makureshi. Alikuwa ni katika watukufu wa kikureshi na ni mmojawapo wa matajiri wakubwa wa Makka mwenye mali nyingi na alisabilia mali yake nyingi katika kuusimamisha Uislamu. Mtume (SAW) alimuoza bintiye Ruqayya na alipofariki alimuoza bintiye mwengine Umm Kulthum na kwa sababu hii akaitwa "Dhun-Nurain" yaani mwenye nuru mbili na alipofariki Umm Kulthum alisema Mtume (SAW): Lau ningelikuwa na wa tatu ningemuoza Uthman kwa namna alivyokuwa anampenda. Alikuwa ni mtu mwema sana na ni mwenye haya nyingi mno mpaka Malaika wakimstahi. Alichaguliwa kuwa ni Khalifa wa tatu wa Uislamu baada ya kuuliwa Umar bin Al-Khattab, naye vile vile aliuliwa huku akiwa anasoma Qurani. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. Zubeyr bin Al-Awwam: Aliingia katika Uislamu akiwa bado barobaro kwa kushawishiwa na Abubakar Assiddiq. Yeye ni mtoto wa shangazi lake Mtume (SAW) Safiya bint AbdulMuttalib na baba yake ni ndugu yake Khadija mke wa Mtume (SAW). Ni katika masahaba waliohama kwenda Habasha yalipozidi mateso Makka na wa kwanza kumhami Mtume (SAW) aliposikia amekamatwa na Makureshi na katika waliopigana vita vikali kumhami Mtume (SAW) katika vita vya Uhud. Hapana mashambulizi aliyoyafanya Mtume (SAW) ila yeye alikuwemo ndani yake na daima alikuwa kwenye mstari wa mbele katika kupigania haki. Katika vita vya Yarmuk dhidi ya Warumi alikuwa ni mmojawapo wa maamirijeshi na wakati walipoiteka Misri yeye ndiye aliyeweza kuiteka ngome ya Warumi. Alikufa shahidi. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. AbdulRahman bin Awf: Alikuwa ni wa nane kuingia kwenye Uislamu baada ya kushawishiwa na Abubakar. Alihama kwenda Habasha mateso yalipochacha Makka na kurudi aliposikia Hamza na Umar wamesilimu. Alikuwa mtu mwaminifu sana mpaka Mtume (SAW) akamwita: Mwaminifu duniani na mwaminifu mbinguni". Amehudhuria vita vyote alivyopigana Mtume (SAW) na makafiri na akachaguliwa kuwa amirijeshi wa kikosi kilichopelekwa Duumatul-Jundul, na alikuwa kiongozi shujaa sana na mwanachuoni mkubwa na miongoni mwa masahaba sita wenye kushauriwa na kusikilizwa shauri lao na ulipokuja wakati wa kuchaghuliwa Khalifa baada ya kuuliwa Umar alimchagua Uthman. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. Saad bin Abi Waqqas: Sahaba mkubwa. Anahusiana na Mtume (SAW) kwa upande wa Amina mama yake Mtume (SAW) naye alikuwa akimwita mjomba. Alisilimu kwa kushawishiwa na Abubakar na wakati huo alikuwa bado kijana mdogo akafanya kazi ya kuchonga mishale. Alikuwa ni mtu shujaa na hodari wa kurusha mishale na baada ya kuombewa dua na Mtume (SAW) katika vita vya Uhud alikuwa akirusha hakosi. Alikuwa ni amirijeshi wa jeshi la Waislamu dhidi ya Wafursi katika vita vya Qadisiya ambaye aliweza kulishinda jeshi kubwa kabisa la maadui na kuiteka Madain mji mkuu wa Wafursi, kisha akachaguliwa kuwa liwali wa Kufa, Iraq. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. Talha bin Ubaydillah: Aidha, miongoni mwa waliosilimu mwanzo mwanzo kwa kushawishiwa na Abubakar ni huyu sahaba mkubwa ambaye alibashiriwa na Mtume (SAW) kufa shahidi na kuingia Peponi akiwa bado yu hai. Alishiriki katika vita vingi dhidi ya makafiri katika kuusimamisha Uislamu na katika vita vya Uhud alisimama pamoja na masahaba kidogo waliomzunguka kumhami Mtume (SAW) mpaka akajulikana kama ni "mwewe au kipanga wa Uhud". Alikuwa ni mtu karimu sana aliyesabilia mali yake nyingi kuwasaidia maskini na mafakiri mpaka Mtume (SAW) akamwita "Talha wa kheri: na "Talha Karimu". Aidha, Mtume (SAW) kwa kumpenda alimwita "Rafiki Msaidizi" wake kwani katika vita vya Uhud alimbeba Mtume (SAW) mara mbili juu ya mgongo wake kumkinga na maadui na kumuepusha na hatari. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. Abu Ubayda bin Al-Jarrah: Sahaba huyu alipambana na Abubakar akamshika mkono na kumuonyesha njia ya haki ya Uislamu akasilimu na kuwa kwenye mstari wa mbele katika kuupigania Uislamu, na hapana vita dhidi ya makafiri asivyohudhuria na mara nyingi Mtume (SAW) alimfanya amirijeshi wa baadhi ya vikosi kwa ushujaa wake na kutoogopa lawama ya mtu yeyote katika kusimamisha haki, kwani hata alivyopambana na babake akiwa babake upande wa makafiri alisimama thabiti kupigana naye mpaka akamuua kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Abu Ubayda pamoja na Khalid bin Al-Walid ndio viongozi wa jeshi lililowatoa Warumi kutoka nchi ya Sham na vitongoji vyake. Mtume (SAW) alimwita mwaminifu wa umma huu kwa uaminifu wake mkubwa. Mtume alimbashiria kuingia Peponi. Said bin Zayd: Katika kundi la Waislamu wa mwanzo ni huyu bwana ambaye pamoja na wenzake kumi wengine walibashiriwa kuingia Peponi na Mtume (SAW) hapa hapa duniani kabla hajafa. Baba wa sahaba huyu alikuwa ni mtu wa kheri aliyejitenga na ushirikina na machafu kabla ya Mtume (SAW) kupewa ujumbe kutoka kwa Mola wake. Alikuwa akiwaambia washirikina wa Makka kuwa yeye tu ndiye aliyekuwa akifuata dini ya Nabii Ibrahim (AS). Mkewe Said ni Fatma nduguye Umar bin Al-Khattab na ndiye sababu ya kusilimu kwa Umar. Ameshiriki vita vyote dhidi ya Makafiri pamoja na Mtume (SAW) na alichaguliwa kuwa liwali wa Sham lakini alijiuzulu ili apate kushiriki kwenye jihadi. Alijiepusha na kila aina ya fitina iliyowakabili Waislamu wakati wake na kuishi mcha Mungu mpaka alipofariki dunia. Mbali na hawa waliobashiriwa Pepo, kuna masahaba wengine mbali mbali ambao waliingia katika Uislamu hapo mwanzo mpaka dini hii ikaanza kutangaa na kuenea baina ya watu. Tumeona sifa nzuri kabisa za Waislamu wa mwanzo na mambo waliokuja kufanya katika kuusimamisha Uislamu. Kundi hili thabiti lilikuwa likikutana kisiri na Mtume (SAW) kwenye nyumba ya mmoja wao Al-Arqam bin Abil-Arqam kujifundisha na kufanya ibada. Kundi hili likazidi kuwa kubwa na wakawa wanafanya ibada zao baina ya majabali ya Makka ili wasionekane na washirikina wa Makka. Kisha Mwenyezi Mungu akamuamrisha afikishe ujumbe wake kwa jamaa zake wa karibu akasema:
Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.
Basi baada ya kuteremka aya hii, Mtume (SAW) aliwaita jamaa zake walio karibu kina Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib na kuwaeleza ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kupewa kwake Utume na kuwa kila mmoja atakufa afufuliwe na ahisabiwe na atiwe ima Peponi au Motoni kwa mujibu wa amali yake. Hapa Abu Talib ami yake akamuunga mkono maneno mazuri aliyoyasema na kuwa aendelee na yeye yuko nyuma yake lakini hawezi kuacha dini ya baba yake. Kwa upande mwengine, Abu Lahab, ami yake mwengine, akasema kuwa amekuja na jambo baya sana na lazima azuiliwe kabla ya kuzuiliwa na watu wengine, na Abu Talib akamjibu kuwa watamhami uhai wao. Mtume (SAW) baada ya kuona msimamo mzuri wa ami yake aliyemlea Abu Talib alizidi kupata moyo na baada ya kupita muda alisimama siku moja juu ya jabali la Safa na kuita kwa kelele kwa sauti ya kuonyesha kuwa kuna hatari, na pale pale makabila yote ya kikureshi yakakutanika. Mtume (SAW) akawaambia: Je, nikikuambieni kuwa kuna watu kwenye bonde wanakuja kuwahujumu mtanisadiki? Wakasema: Naam! Sisi hatukuona kwake isipokuwa ukweli. Akasema: Basi Mimi ni monyaji kwenu mwenye adhabu kali. Akasema Abu Lahab: Umeangamia leo nzima! Kwa ajili hii ndio umetukusanya?
Mwenyezi Mungu aliyetukuka akateremsha:
Baada ya kuteremka sura hii kumlaani, Abu Lahab alizidi inda na inadi na kumfanyia Mtume (SAW) kila aina ya vitimbi na udhia yeye pamoja na mkewe kwa kumtupia uchafu mbele ya nyumba yake na kumfuata akimtukana na kumshutumu na kumtuhumu mbele za watu kuwa ni mwongo na akili zake hazimtoshi. Kwa upande mwengine, Abu Jahl aidha alikuwa daima akimuudhi Mtume (SAW) hasa wakati anapokwenda Al-Kaaba kusali hujaribu kumzuiya asisali na kumkera na kumtesa, mpaka Mwenyezi Mungu akamteremshia Aya kumkemea na kumuonya:
Umemwona yule anayemkataza. Mja anaposali?
Pamoja na majabari hawa, kulikuwa na majabari wengine ambao daima walikuwa wakimuudhi Mtume (SAW) na kuwatesa Waislamu na Mwenyezi Mungu aliwaangamiza hapa hapa duniani na kesho Akhera adhabu yao ni kali mbele ya Mola wao. Waislamu wengine ambao walikuwa hawana wakuwahami walipata mazito zaidi na mateso makubwa hasa wale ambao hawana makabila yao hapo Makka au walikuwa watumwa wa washirikina wa Makka. Mfano wa hawa ni Bilal bin Rabah ambaye alikuwa ni mtumwa wa Umayya bin Khalaf. Huyu alikuwa akimtia kamba shingoni na kuwaacha watoto wa Makka wamburute huku yeye akimpiga fimbo, na akimlaza kwenye mchanga umoto siku za joto na kumwekea jiwe zito juu ya kifua chake na kumlazimisha akufuru, naye kwa imani yake kubwa aliyokuwa nayo alikuwa akikataa na kuridhia mateso huku akisema: Ahad! Ahad! yaani Mmoja! Mmoja! mpaka siku moja akapita Abubakar Assiddiq na kumnunua na kumwacha huru. Watumwa wengine waliopata mateso kama haya ni Ammar na babake Yasir na mamake Sumayya mpaka akawa akipita Mtume (SAW) na kuwasikitikia na kuwapa moyo akiwaambia: Subira akina Yasir kwani miadi yenu ni Pepo. Akafa Yasir kwa mateso na Abu Jahl akamchoma mkuki Sumayya na kumuua akiwa ameshikamana na dini ya Mwenyezi Mungu akawa ni shahidi wa kwanza wa kike katika Uislamu. Na mara nyingi Abubakar Assiddiq alikuwa akiwanunua watumwa na vijakazi waliosilimu ambao walikuwa wakiteswa na mabwana zao na kuwaacha huru. Nguzo ya kwanza: Sala: Baada ya kupewa utume Muhammad (SAW) na kufahamishwa nini Imani na nini Uislamu, alikuja Jibril na kumfundisha Mtume (SAW) namna ya kutawadha na namna ya kusali akawa ana sali mara mbili tu asubuhi kabla ya kutoka jua na jioni kabla ya kuzama jua. Akasema Mola aliyetukuka:
Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa
kumsifu Mola wako Na hivi ndivyo alivyokuwa Mtume (SAW) akiwafundisha Waislamu wa mwanzo namna ya kusali kabla ya kuchukuliwa katika safari ya Israa na Miraji wakati alipofaridhishiwa Sala tano za fardhi, kwani amesema Aysha (RA) kuwa mwanzo zilipofaridhiwa Sala zilikuwa ni rakaa mbili mbili tu, kisha baadaye Mwenyezi Mungu akazitimiza baadhi ya Sala kuwa tatu na nne na wakati watu wakiwa wametulia mijini mwao na kubakisha rakaa mbili mbili kwa wale waliokuwemo ndani ya safari. Waislamu wakaendelea kusali kisirisiri baina ya jabali ya Makka na kujificha wasionekane na washirikina wa Makka, lakini siku moja walipokuwa wakisali walipita makafiri wa Makka wakamkuta Saad bin Abi Waqaas na wenzake wanasali wakawa wanawakejeli na kutaka kuwapiga, akasimama Saad na kumpiga mmoja katika washirikina kwa fupa la ngamia akampasua na kumtoa damu, ikawa ndio damu ya kwanza ya makafiri iliyomwagwa katika Uislamu. Idadi ya Waislamu ikawa inazidi kila kukicha na habari za kuingia watu kwenye dini ya Muhammad zikazidi kuwakasirisha Makureshi hasa walivyojua kuwa Uislamu hautofautishi baina ya bwana na mtumwa wake na baina ya Mwarabu na asiyekuwa Mwarabu na kuwa wote mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa sawa kinachowafanya wazidiane na ule ucha Mungu wao kwa Mola wao. Na mwanzo walikuwa wanapuuzisha habari hizi lakini Qurani ilipoanza kuwaponda miungu yao na kuyafanya si kitu na kuwatukana washirikina na kuwafanya hawana akili kwa kuabudu masanamu yasiyofaa wala kudhuru, walizidi kuwatesa Waislamu na kuwakandamiza kwa kila aina, lakini wapi!!! Imani ilikuwa imeshawavaa Waislamu na washajua utamu wake, na kwa hivyo wakawa wanamtanguliza Mwenyezi Mungu na Mtumewe hata zaidi ya nafsi zao. Katika mwaka wa tano baada ya Muhammad (SAW) kupata utume, na mateso ya Makureshi kuzidi dhidi ya Waislamu, liliondoka kundi la kwanza la Masahaba kuelekea Habasha kwa amri ya Mtume (SAW) na ushauri wake, akasema: (Lau mngetoka kwenda ardhi ya Habasha, kwani huko kuna mfalme hadhulumumiwi mtu kwake, mpaka Mwenyezi Mungu akujaaliyeni faraji na njia ya kutokana na haya yanayokufikeni). Wakajitolea Masahaba kiasi kumi wakiwa wengine na wake zao kuhama na kuwacha mji wao na watu wao na shughuli zao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Kundi hili la Masahaba kumi na wanawake wa tano lilikusanya watu kutoka matumbo mbali mbali ya kikureshi na ya Waarabu wengine wa Makka, akiwemo Uthman bin Athman na mkewe Ruqayya binti wa Mtume (SAW), na Abu Salama na mkewe Umm Salama na nduguye Abu Salama kwa mama Abu Sabra na mkewe Umm Kulthum, na Aamir bin Rabia na mkewe Layla na Abu Hudheifa bin Utba na mkewe Sahla na Abdur Rahman bin Awf na Uthman bin Madhuun na Mussab bin Umeir na Suhayl bin Baydhaa na Zubeir bin Awwam. Waliondoka Masahaba hawa wakiwa chini ya uwongozi wa Uthman bin Affan usiku usiku kwa kificho ili wasionekane na washirikina wa Makka na kuelekea baharini ambapo kwa bahati nzuri walipata majahazi mawili wakaondoka nayo kuelekea Habasha na huko walipokelewa uzuri na mfalme wa huko aitwaye Najashi. Watu wa Habasha wakati huu walikuwa ni Manasara na mfalme wao alikuwa ni mtu mwema sana na muadilifu na ndio maana Mtume (SAW) akawaashiria Masahaba zake waende huko. Masahaba walikaa Habasha kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Rajab mpaka Ramadhan kisha wakapata habari kuwa Makureshi wamesilimu basi wakaazimia kurudi juu ya kuwa Najashi alikuwa akiwatazama uzuri sana na kuwapa kila mahitajio yao lakini kuishi ugenini kuna kazi hasa ikiwa idadi ya waliohama ni kidogo, na kwa hivyo wakatamani kurudi makwao. Katika mwezi wa Shawwal (Mfungo mosi) waliwasili Makka kwa kificho lakini walikuta hali ni ile ile na Makureshi wamo katika ukafiri wao ule ule, basi wengine wakarudi Habasha na wengine waliopata wa kuwahami na kuwakinga na mateso ya Makureshi walibaki Makka. Lakini baada ya kurudi Masahaba hawa kutoka Habasha na Makureshi kusikia mapokezi mazuri ya Najashi walizidi kuwakandamiza na kuwaadhibu mpaka Mtume (SAW) akaona bora awaamrishe Masahaba zake kugura tena na kuelekea Habasha. Hijra hii ya pili ilikuwa ni ngumu zaidi kuliko ile ya kwanza kwani Makureshi walikuwa macho wanasubiri lini watahama ili wawazuilie, lakini Masahaba walipanga mpango wakaondoka kisiri na kwa haraka, wakitahamaki Makureshi jamaa washaondoka na ilikuwa idadi yao mara hii imefika thamanini na tatu akiwemo Jaafar bin Abi Talib na mkewe Asmaa bint Umeys na Miqdad bin Aswad na Abdullahi bin Masuud na Abdullahi bin Jahsh na mkewe Umm Habiba bint Abi Sufyan na inasemekana vile vile Ammar bin Yasir alikuwemo. Makureshi walipoona kuwa Masahaba wa Mtume (SAW) wametulia huko Habasha, waliamua wakubwa wao kupeleka ujumbe wa watu wawili wanaotegemewa kwenda kukabiliana na Najashi ili kumuomba awarudishe Masahaba waliohamia kwake na kwa hivyo wakachukuwa zawadi za thamani kumpa Najashi na kila mmoja katika makasisi wake. Wajumbe wawili waliopelekwa na Makureshi Amr bin Al-Aas na Abdullah bin Abi Rabia walipofika Habasha walikutana na makasisi wa Najashi na kuwahonga kila mmoja zawadi yake na kujaribu kuwakinaisha kuwa hawa jamaa wamekimbia kwao na kutupa dini ya watu wao na wala hawakuingia kwenye dini yao ya Ukristo bali wameleta dini mpya wasioijua wao wala hao makasisi, na kuwa wameletwa kwa mfalme kutoka kwa wakubwa wao kuomba warudishwe na kuwatia maneno kuwa Najashi akiuliza na waseme: Ndio hawa wamehalifu watu wao na wamekwenda kinyume na dini yao. Amr na mwenzake walipofika kwa Najashi na kumpa zawadi zake na kumtaka awarudishe Masahaba, makasisi waliunga mkono maneno ya Amr na kusema kuwa watu wao wanajua zaidi aibu zao na kuwa bora awarudishe kwao. Hapo Najashi akakasirika na kusema: La Wallahi! Sitowatoa kuwapa hawa watu, kwani watu ndio kwanza wamekuja kukaa karibu yangu na kuteremka nchini mwangu na kunichagua Mimi badala ya wengine, siwatoi mpaka niwaite ili kuwauliza kuhusu wasemayo hawa vijana wawili juu yao, na ikiwa kama walivyosema basi nitawatoa na ikiwa ni maneno mengine nitawazuiya na wala siwatoi maadamu wako na Mimi. Kisha Najashi akawaita Masahaba waliohamia kwake ili wahudhurie baraza na alipowauliza kuhusu jinsi ya dini iliyowafanya watokane na watu wao, alisogea mbele Jaafar bin Abi Talib na kusema: Ewe mfalme! Sisi tulikuwa watu wa Ujahili, tunaabudu masanamu na tunakula mfu na tunafanya machafu na tunatupa jamaa zetu na kutendea uovu majirani na mwenye nguvu anamuonea mnyonge, na tulikuwa hivyo mpaka Mwenyezi Mungu akatuletea Mtume miongoni mwetu tunayeijua nasaba yake na ukweli wake na uaminifu wake na utahirifu wake, akatuita kwa Mwenyezi Mungu ili tumpwekeshe na tumuabudu na tutokane na tuliyokuwa tukiyaabudu sisi na wazee wetu ya kuabudu mawe na masanamu na mizimu badala yake, na kutuamrisha tuseme kweli na tuifikishe amana na tutazame jamaa na kukaa vyema na majirani na tuwache ya haramu na kuuana na akatukataza machafu na kusema uwongo na kula mali ya mayatima na kuwasingizia uwongo wanawake waliojihifadhi na akatuamrisha tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake tusimshirikishe na kitu chochote, akatuamrisha Sala na Zaka na Saumu, basi tukamsadiki na kumuamini na kumfuata kwa yale aliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Basi watu wetu wakatupiga vita na kutuadhibu na kutufitinisha na dini yetu ili waturudishe kwenye kuabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka, na walipotushinda nguvu na kutudhulumu na kutudhiki na kutuzuilia na dini yetu, tulitoka kuja nchini mwako na kukuchagua wewe badala ya wengineo na kupendelea kuwa karibu na wewe na kutaraji tusidhulumiwe kwako ewe mfalme. Kisha Jaafar akasoma baadhi ya Aya za Qurani Tukufu kutoka mwanzo wa Sura ya Maryam, akaathirika sana Najashi na kulia na wakalia makasisi wake. Kisha Najashi akasema: Hakika haya na yale aliyokuja nayo Isa yanatokana na nuru moja. Nendeni zenu, kwani Wallahi sitowatoa kwenu. Akasema Amr kuwa kesho atamwambia Najashi yale wanayoyasema kuhusu Isa na kuwa ni mtumwa tu wa Mwenyezi Mungu. Basi siku ya pili akasema Amr: Ewe mfalme! Wao wanasema kuhusu Isa jambo zito, basi waite uwaulize nini wanasema juu yake. Basi wakaitwa. Wakakusanyika na kuulizana nini watasema kuhusu Isa wakiulizwa? Wakasema: Wallahi, tutasema aliyoyasema Mwenyezi Mungu na yale aliyokuja nayo Nabii wetu yoyote yale yawayo. Basi walipohudhuria kwa Najashi akawauliza: Mnasemaje kuhusu Isa? Jaafar akajibu: Tunasema juu yake yale aliyokuja nayo Nabii wetu Muhammad (SAW) ya kuwa yeye ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na roho yake na neno lake alilompelekea Maryam. Najashi akakubali kuwa aliyoyasema Jaafar ni haki, na haya ndio yaliyomfanya Najashi asilimu. Hila za washirikina zikaanguka chini na mbinu zao zikapotea bure, lakini vitimbi vyao havikumalizika kwani sasa wakafikiria namna ya kumzuiya Mtume (SAW) asiendelee kutangaza ujumbe wake kwa kupanga njama ya kutaka kumuua na kuzuiya kuenea kwa dini yake moja kwa moja.
|
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|