Viungo

Fatawa

Masuala

Dua

Tarehe

Sira

Fiqhi

Sunna

Qurani

Maskani

Habari

Elimu

Afya
Nchi
Michezo
Vyakula
Riyadha
Masomo
Nasiha
Kamusi
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
      

 

SERA

 

MAISHA YA MTUME

 

       
       
       
       


8-
 
  Mtume (SAW) amuoa Sauda
9-    Kwenda Taif
10-  Majini wapokea Ujumbe
11-  Majini na Mashetani
12-  Msimu wa kutangaza dini
13-  Kuja kwa watu wa Yathrib
14-  Kumuoa Aisha
 


1-   Kusilimu kwa Hamza na Umar
2-   Msimamo wa Abu Talib
3-   Kupigwa pande Mtume (SAW)
4-   Kuvunjwa mkataba wa dhulma
5-
  
Ujumbe kutoka Manasara wa Habasha
6-
  
Ujumbe wa Makureshi kwa Abu Talib
7-
  
Mwaka wa huzuni

 

Kusilimu kwa Hamza na Umar: 

            Abu Jahl aliendelea kumuudhi Mtume (SAW) mpaka siku moja akapita na kumkuta Mtume (SAW) kwenye jabali la Safa akamuudhi na kumtukana vibaya na kuitukana dini yake lakini Mtume (SAW) akamnyamazia kimya asimtopoe. Kisha akashika njia na kwenda zake kwenye Al-Kaaba katika baraza wanayokutanikia Makureshi na kukaa nao.

            Hamza alipokuwa anarudi kutoka mawindoni alikutana na kijakazi wa Abdullah bin Jud-an akamueleza yale aliyomfanyia Abu Jahl kwa Mtume (SAW) na kuwa Mtume hakumjibu neno. Hamza alikasirika sana na kuingia Al-Kaaba, na kwenda moja kwa moja mpaka mbele ya Abu Jahl bila kuwasalimia Makureshi kama ilivyo ada yake na kumpiga kichwani kwa upinde na kumpasua huku akimwambia: Unamtukana na Mimi niko katika dini yake ninasema kama anayoyasema? Basi nijibu kama unaweza.

            Jamaa wa Abu Jahl kina Banu Makhzumi wakasimama kutaka kumsaidia Abu Jahl, lakini akawazuiya na kuwaambia wamuache kwani yeye amemtukana vibaya mtoto wa nduguye

            Kuanzia hapo Hamza akawa Muislamu na kuendelea kuwa na Muhammad na Makureshi wakajua kuwa sasa Muhammad amepata nguvu na kuwa hawatoweza kumfikia tena maadamu Hamza yuko pamoja naye, basi wakasita kumfanyia baadhi ya maudhiko waliyokuwa wakimfanyia. Kusilimu kwake kuliupa nguvu Uislamu kwani Hamza alikuwa ni kijana mtukufu wa kikureshi na shujaa na mwenye nguvu nyingi.

            Baada yake kwa siku tatu, Mwenyezi Mungu alizidi kuutia nguvu Uislamu kwa kusilimu Umar bin Al-Khattab, jambo ambalo lilibadilisha msimamo wa Waislamu na kuwatia moyo mkubwa hasa madhaifu katika wao.

            Umar alikuwa akijulikana kuwa ni mtu mkali, shujaa na mwenye nguvu nyingi na alikuwa haogopi mtu, na juu ya kuwa akimchukia sana Mtume (SAW) kwa sababu ya kuleta jambo lililokuja kuvunja ada na mila za babu zao, Mtume (SAW) alikuwa akimuomba Mola wake na kusema: Ewe Mola! Utie nguvu Uislamu kwa unayempenda zaidi katika wawili hawa: Umar bin Al-Khattab au Al-Hakam bin Hisham (Abu Jahl). Akawa mwenye kupendwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni Umar.

            Sababu ya kusilimu kwa Umar ni kuwa siku moja alitoka na upanga wake mkononi anakwenda kumuua Mtume (SAW), akakutana na Nuaym bin Abdallah na kumuuliza: Je, za wapi Umar? Akasema: Ninataka kumuua Muhammad. Akasema: Vipi utasalimika na Bani Hashim na Bani Zuhra baada ya kumuua Muhammad? Kwani hurudi kwa watu wako nyumbani na kuwanyosha wao kwanza? Umar akauliza: Watu wangu gani? Akamwambia: Shemegi yako na binamu wako Said na nduguyo Fatma, kwani Wallahi wamesilimu na kumfuata Muhammad katika dini yake, basi anza na wao.

            Pale pale Umar akarudi kuwaendea dada yake na shemegi yake na akamkuta Khabbab bin Al-Arath ambaye alikuwa akiwapitia kuwasomea Qurani, yuko nao ameshika ukurasa imo Sura ya Taha anawasomea, basi alipohisi kuja kwa Umar alijificha khabbab, na Fatma akauchukua ukurasa na kuuficha chini ya paja lake, na wakati huo alikuwa Umar keshamsikia Khabbab akiwasomea, basi alipoingia alisema: Ni mngongono gani huu niliousikia? Wakamwambia: Hukusikia kitu. Akasema: Kwani! Wallahi nimeambiwa kuwa nyinyi mumemfuata Muhammad kwenye dini yake, na akamkamata shemegi yake kumpiga. Fatma nduguye akasimama ili amzuiye asimpige mumewe, akampiga yeye na kumpasua. Alivyofanya hivyo wakamwambia: Naam, tumesilimu na kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtumewe na unalotaka fanya!

            Umar alipoona nduguye anatoka damu alijuta na kumwambia dadake: Nipe huo ukurasa niliokusikieni mnausoma nitazame aliyokuja nayo Muhammad. Nduguye akamwambia: Sisi tunauogopea kwako. Akamwambia: Usiogope na kumuapia kwa miungu yao. Basi aliposema hivyo, aliingiwa na tamaa nduguye kuwa atasilimu lakini akamwambia: Ewe ndugu yangu, wewe ni najisi kwa ushirikina wako na haushiki ukurasa huu isipokuwa tahiri. Basi Umar akenda akaoga na nduguye akampa ukurasa na ndani yake "Taha", akasoma Aya za kwanza na kusema: Maneno mazuri yaliyoje na matukufu!

            Basi aliposikia haya Khabbab alitoka kule alipokuwa amejificha na akamwambia: Ewe Umar, Wallahi Mimi nataraji awe Mwenyezi Mungu amekuchagua kwa dua ya Nabii wake, kwani mimi nimemsikia jana akisema: Ewe Mola, saidia Uislamu kwa Abil-Hakam bin Hisham au kwa Umar bin Al-Khattab, basi Allah Allah Ewe Umar. Hapo Umar akamwambia: Basi nionyeshe Muhammad ewe Khabbab ili nimwendee ili nisilimu. Khabbab akamwambia: Yeye yuko kwenye nyumba katika mlima wa Safa pamoja na kundi la Masahaba zake.

            Umar akachukua upanga wake na kuelekea kwa Mtume (SAW) na masahaba zake na kuwagongea mlango. Waliposikia sauti yake alisimama mmoja wao katika Masahaba na kuchungulia kwenye ufa wa mlango akamuona amebeba upanga wake. Akarudi kwa Mtume (SAW) huku akiwa amefazaika, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, huyo ni Umar bin Al-Khattab amebeba upanga wake. Hamza akasema: Mwache aingie, na akiwa amekuja anataka kheri tutampa na ikiwa anataka shari tutamuua kwa upanga wake. Akasema Mtume (SAW): Mruhusu aingie! Basi akaruhusiwa na Mtume (SAW) akamuinukia na kupambana naye kwenye chumba na kumshika ukosi wa nguo zake na kumvuta kwa nguvu, na kumwambia: Kilichokuleta ewe mtoto wa Khattab, kwani Wallahi sioni kama utasita mpaka Mwenyezi Mungu akuteremshie msiba. Akasema Umar: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nimekujia ili kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtumewe, na kwa yale aliyokuja nayo kutoka kwake. Hapo Mtume (SAW) akapiga takbira wakajua wale Masahaba waliokuwepo nyumbani kuwa Umar amesilimu.

            Masahaba wote wakafurahi na kupata moyo kwa kujua kuwa Umar pamoja na Hamza watamhami Mtume (SAW) na kumkinga na maadui zake. Baada ya kusilimu Umar, kukawa hakuna kificho tena kwani Umar alisimama na kumuuliza Mtume (SAW): Je, sisi hatumo katika haki na Makureshi katika batili. Mtume (SAW) akamjibu: Kwani! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mkononi mwake kuwa nyinyi mumo kwenye haki mukifa au mukiwa hai. Akasema Umar: Basi kwa nini kificho? Wallahi kwa yule ambaye amekuleta kwa haki tutatoka. Basi tukatoka makundi mawili, moja linaongozwa na Mimi na moja linaongozwa na Hamza mpaka tukaingia msikitini (Al-Kaaba) na kuwatazama Makureshi. Walipotuona wakaingiwa na huzuni kubwa na kwa sababu hii Mtume (SAW) akamwita: Al-Faruq - Mpambanuzi baina ya haki na batili.

            Akasema Ibn Masuudi: Tulikuwa hatuwezi kwenda kwenye Al-Kaaba mpaka aliposilimu Umar. Na akasema Abdullahi bin Masuudi: Tangu asilimu Umar tumekuwa wenye nguvu. Uislamu ukadhihiri na nuru yake ikatapakaa na Makureshi wakavunjika nguvu zao kwani Hamza na Umar ni watu waliokuwa wakiogopewa tangu zama za Ujahili. Wakaanza sasa mbinu nyengine za kumvutia Mtume (SAW) na kumrairai awache dini yake. 

Msimamo wa Abu Talib dhidi ya washirikina: 

            Mtume (SAW) aliendelea na kuwafikishia watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kila kukicha watu wengine wakawa wanaingia kwenye dini ya haki. Makureshi walivyoona hivi walimwendea tena Abu Talib na kumtaka amsitishe Muhammad mtoto wa nduguye kutukana miungu yao na kuipiga vita dini ya mababu zao, na kuwa wao wanamwacha kwa sababu ya heshima yake yeye Abu Talib, la si hivyo watampiga vita yeye na mtoto wa nduguye mpaka mmoja wao ashinde au ashindwe.

            Abu Talib, baada ya kuonywa, alimwita tena Mtume (SAW) na kumueleza msimamo wa Makureshi na kuwa yeye hatoweza kupigana na Makureshi wote. Mtume (SAW) akamwambia: Ewe ami, Wallahi, lau wataweka jua kwenye mkono wangu wa kulia na mwezi kwenye mkono wangu wa kushoto ili niwache jambo hili sitaliwacha mpaka Mwenyezi Mungu alidhihirishe au nife. Mtume (SAW) akaondoka akiwa ana huzuni, lakini baadaye Abu Talib akamtumizia mtu aitwe na alipokuja akamwambia: Nenda ewe mtoto wa ndugu yangu na useme unalotaka, wala sitokuwacha ufanye jambo usilolipenda abadan.

            Msimamo huu wa Abu Talib ukawaudhi sana Makureshi na wakaona sasa bora watumie njia nyengine, wakamwendea Abu Talib na kumwambia kuwa watampa kijana yeyote mbora wa kikureshi awape Muhammad wamuue, akastaajabishwa sana na fikra ya kijinga kama hii, akawaambia: Mimi nikupeni mtoto wa ndugu yangu mumuue kisha nimchukue badala yake mtoto wenu nimlishe na kumlea!

            Makureshi wakahizika, kisha baada ya muda wakaona sasa bora tumwendee mwenyewe Mtume (SAW), basi akatumwa Utba bin Rabia naye alikuwa ni katika mabwana wakubwa wa kikureshi, akamwambia: Ewe mtoto wa ndugu yangu, wewe unajua utukufu wako kwetu katika jamaa na mahali pako katika nasaba na wewe umekuja kwa watu wako na jambo zito, ukawafarikisha umoja wao na kuwafanya hawana akili na kuwatia aibu miungu yao na dini yao na ukawafanya mababu zako waliopita kuwa ni makafiri, basi nisikilize mambo ninayokuambia utazame utakayokubali katika hayo.

            Mtume (SAW) akamwambia: Sema ewe baba wa Walid, Mimi nakusikiliza. Akamwambia: Ikiwa unataka, kwa jambo hili, mali basi tutakukusanyia katika mali zetu mpaka uwe mwenye mali nyingi zaidi katika sisi, na ukiwa unataka utukufu, basi tutakuchagua uwe bwana wetu, tusiamue jambo bila wewe, na ukiwa unataka ufalme, tutakufanya uwe mfalme juu yetu, na ikiwa hili linalokujia ni jambo unaloliona akilini mwako huwezi kuliondosha mwenyewe, basi tutakuletea dawa na tutatoa mali zetu mpaka upone, na ikiwa unapenda uzuri basi tutakuoza binti yeyote aliye mzuri zaidi ambaye utamchagua wewe mwenyewe.

            Mtume (SAW) akamjibu: Mimi sitaki mali wala ufalme. Mwenyezi Mungu amenileta muonyaji kwa walimwengu wote na Mimi ninakuleteeni ujumbe wake, basi mkiuamini mtafuzu mpate furaha hapa duniani na Akhera na mkikataa neno la Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yangu na nyinyi!!

            Baada ya haya, Makureshi wakaazimia shari kwa Mtume (SAW) na Abu Talib alivyoona hivyo aliwaita Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib na kuwahadharisha juu ya nia ya Makureshi dhidi Muhammad (SAW) na wao wote Waislamu katika wao na wasiokuwa Waislamu isipokuwa Abu Lahab wakatoa ahadi kumhami Mtume (SAW) na kusimama naye.

Kupigwa pande Mtume (SAW) pamoja na jamaa zake:

            Makureshi, baada ya kuyakinisha kuwa Muhammad hataki kukubaliana nao kwa jambo lolote ili awache kutangaza dini ya Mwenyezi Mungu, na walipoona kuwa jamaa zake Muhammad, kina Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib wamekuwa kitu kimoja kumhami mwenziwao, walikutana kufanya mkataba wa kuwasusia Muhammad na jamaa zake na yeyote atakayejaribu kumlinda asiuliwe

            Kwa hivyo, wakakutana na kuandika mkataba kuwa wasiowane na Bani Hashim wala Bani AbdulMuttalib na wala wasifanye biashara nao, wala wasikae nao, wala wasiingiliane nao, wala wasiingie nyumba zao, wala wasiwasemeshe mpaka wamtoe Muhammad ili wamuue na wasikubali kufanya suluhu na Bani Hashim mpaka wamtoe Muhammad

            Mkataba huu ukaandikwa kwa jina la Mwenyezi Mungu na kutundikwa ndani ya Al-Kaaba. Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib wote Waislamu na wasiokuwa Waislamu wakasimama na Mtume (SAW) isipokuwa Abu Lahab, na wakatoka nje ya mji wa Makka kwenye bonde la Abi Talib usiku wa tarehe mosi Muharram mwaka wa saba tangu kupata Muhammad Utume.  

            Miaka mitatu mizima ikapita ikiwa Waislamu na Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib wako nje ya mji wa Makka hawawezi kufanya lolote, na hapana kitu wanachoweza kukinunua au kukipata isipokuwa kwa siri au kwa sudfa ukitokea msafara umepita pale walipo

Rudi Juu

Kuvunjwa Mkataba wa Dhulma

            Katika mwaka wa kumi tangu Mtume (SAW) kupewa utume na baada ya kupita miaka mitatu tangu kuandikwa mkataba wa dhulma na kususiwa Mtume (SAW) pamoja na wafuasi wake na jamaa zake kina Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib, walisimama watu wa tano katika watukufu wa kikureshi kutaka mkataba huu uliowafarikisha watu na kuwatia jamaa katika mashaka na dhiki uvunjwe.

            Akasimama Hisham bin Amr bin Rabia pamoja na wenzake Zuheir bin Abi Umayya Al-Makhzumi na Mutt'im bin Adiy Al-Nawfali na Abul-Bakhtari bin Hisham Al-Asadiy na Zam'a bin Al-Aswad Al-Asadiy wakawafikiana usiku kuwa lazima wafanye njia ya kuuvunja mkataba huu wa dhulma.

            Asubuhi yake Zuheir alikwenda Al-Kaaba akatufu kisha akawaelekea watu na kusema: Enyi watu! Mnaridhia kula chakula na kuvaa nguo na Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib wanakufa na njaa hawauzi wala hawanunui. Wallahi, sitotulia mpaka uchanwe mkataba huu wa dhulma wenye kukata ujamaa.

            Abu Jahl akasema: Umesema uwongo Wallahi, hauchanwi. Akajibiwa na Zam'a: Wewe Wallahi ni mwongo zaidi! Hatukuridhia kuandikwa kwake wakati ulipoandikwa. Akasema Abul-Bakhtari: Amesema kweli Zam'a haturidhii yaliyoandikwa humo wala hatuyakubali na akasema Mutt'im bin Adiy: Mmesema kweli na amesema uwongo aliyesema kinyume na hayo. Kisha akasimama Mutt'im na kuuchana wakauona wote umeliwa na mchwa isipokuwa sehemu iliyoandikwa jina la Mwenyezi Mungu, na alikuwa Abu Talib amekaa upande mmoja wa msikiti anatazama, kwani Mtume (SAW) alikuwa ameshamuarifu kuwa Mwenyezi Mungu amempasha habari kuwa mkataba wote umeliwa na mchwa isipokuwa sehemu iliyoandikwa jina la Mwenyezi Mungu.

            Basi Makureshi wakawaruhusu Bani Hashim na Bani AbdulMuttalib pamoja na Mtume (SAW) na wafuasi wake kurudi makwao, na juu ya kuwa Abu Talib aliwaeleza Makureshi yale aliyoyasema Muhammad (SAW) kuhusu mkataba waliendelea na inadi yao na kumpinga.

Ujumbe kutoka Manasara wa Habasha:

            Ili kumliwaza Mtumewe baada ya masaibu yaliyomfika ya kususiwa na kutolewa nchi na kunyimwa watu wake kila aina ya starehe za maisha, Mwenyezi Mungu aliwatia imani watu wa Najran wanaotoka Habasha wakaja kwa Mtume (SAW) na kusilimu. Ujumbe huu wa Wakristo wa Najran walisikia habari za Mtume (SAW) kutokana na Masahaba waliohamia Habasha wakaja mbio Makka kutazama sifa zake ambazo zimetajwa kwenye vitabu vyao na walikuwa ni kiasi cha watu ishirini, na baada ya Mtume (SAW) kuwasomea Qurani walitokwa na machozi na kusilimu wote pamoja.

            Abu Jahl aliposikia haya aliwaendelea pamoja na wenzake na kuwaambia kuwa hajaona watu wajinga kuliko wao, mara tu baada ya kukaa na mtu huyu wametupa dini yao na kumfuata. Wakamwambia: Sisi tuna amali zetu na nyinyi amali zenu, amani juu yenu sisi hatujibizani na wajinga.

            Na inasemekana kuwa Aya hizi zifuatazo ima zimeteremshwa juu ya watu hawa kama alivyoeleza Ibn Is-haq katika sera ya Mtume au juu ya watu wa Najashi waliomzuru Mtume (SAW) wakasilimu.

            Wale tuliowapa Kitabu kabla yake wanakiamini hiki.
           
Na wanaposomewa wanasema: Tunaiamini.
           
Hakika hii ni Haki inayotoka kwa Mola wetu.
           
Hakika sisi kabla yake tulikuwa ni Waislamu, tulionyenyekea
           
Basi hao watapewa ujira wao mara mbili kwa walivyovumilia,
           
na wakaondoa ubaya kwa wema, na wakatoa katika tuliyowaruzuku
           
Na wanaposikia upuuzi hujitenga nao na husema:
           
Sisi tuna vitendo vyetu, na nyinyi mna vitendo vyenu.
           
Amani juu yenu! Sisi hatutaki kujibizana na wajinga.

                                                           
                                    Sura:Al-Qassas:52-55

Ujumbe wa Makureshi wa mwisho kwa Abu Talib:

            Makureshi hawakumwacha Mtume (SAW) baada ya kurudi mjini Makka aendelee na kazi yake ya kutangaza dini kwa salama bila ya kumpinga, kwani walikusanyana watukufu wa kikureshi na kumwendea Abu Talib ili amzuiye Muhammad kutukana miungu yao na dini yao na wao vile vile watasita kumpiga vita na kuupinga Uislamu.

            Mtume (SAW) alivyoitwa na Abu Talib na kuelezwa matakwa ya Makureshi aliwaambia: Mimi ninataka waseme neno moja litalowafanya Waarabu wote wawafuate na wawamiliki wasiokuwa Waarabu. Abu Jahl akasema: Ni lipi hilo? Naapa kwa babako, sisi tutakupa neno hilo na kumi kama hilo. Mtume (SAW) akasema: Semeni: La ilaha illa llah na muache kuabudu mwenginewe.

            Wote wakapiga kofi kisha wakasema: Unataka ewe Muhammad kujaaliya miungu mingi kuwa Mmoja tu? Kwa hakika jambo lako ni la ajabu! Kisha wakaambizana: Hakika Wallahi huyu mtu hatokupeni kitu katika hayo mnayoyataka basi nendeni zenu na muendelee na dini ya babu zenu mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yenu na yake, kisha wakenda zao.

            Mwenyezi Mungu akateremsha kauli yake:
           
S'aad, Naapa kwa Qurani yenye mawaidha.
           
Lakini waliokufuru wamo katika majivuno na upinzani 
           
Mataifa mangapi tumeyaangamiza kabla yao, na wakapiga kelele,                     
            lakini wakati wa kuokoka ulikwishapita
           
Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anayetokana nao wenyewe,
           
na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo
           
Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu?
           
Hakika hili ni jambo la ajabu
           
Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia:
           
Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu,
           
kwani hili ni jambo lililopangwa
           
Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho.
           
Haya si chochote ila ni uzushi tu.

                                                           
                                    Sura:Saad:1-7

Mwaka wa huzuni:

            Tukio zito kabisa kwa Mtume (SAW) lilitokea katika mwaka wa kumi baada ya kupewa utume, kwani baada ya kupita miezi sita tangu uvunjwe mkataba wa dhulma Abu Talib alishikika akafa. Mtume (SAW) alijaribu mpaka dakika ya mwisho kumsihi na kumnasihi ami yake asilimu na atamke shahada lakini alishindwa na akafa katika dini ya babu zake, jambo ambalo lilimsikitisha sana Mtume (SAW), lakini ndio kama alivyoeleza Mwenyezi Mungu:

            Kwa hakika wewe humwongozi umpendaye, lakini Mwenyezi Mungu
            humwongoza amtakaye. Na Yeye ndiye anawajua zaidi waongokao.

                                                           
                                    Sura:Al-Qassas:56

            Na kwa nini Mtume (SAW) asisikitike na kuingiwa na huzuni na kama tulivyoona ami yake huyu Abu Talib amesimama naye tangu utotoni mwake na kumlea kwa wema na hisani na kumpenda na kumheshimu na kumtanguliza hata juu ya watoto wake, na muda wote wa maisha yake tangu hakupata utume mpaka alipochaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni Nabii wa umma huu, Abu Talib alikuwa naye akimsaidia na kumhami na kumhifadhi asiudhiwe na Makureshi, na kukubali kila aina ya mashaka na dhiki kwa ajili yake.

            Jeraha la msiba huu lilikuwa bado bichi wakati Mwenyezi Mungu alipomletea mtihani mwengine mkubwa zaidi wa kufiliwa na mtu azizi kabisa na mpenzi wa roho yake, kwani baada ya kupita miezi miwili au mitatu ya kufariki dunia Abu Talib, alikufa Khadija (RA) mkewe, mpenzi wake, na mama wa watoto wake. Kifo chake kilikuwa kizito sana juu ya kifua cha Mtume (SAW) kwani ni bibi aliyesimama naye kwa hali na mali miaka yote kumi na tano waliokuwa pamoja

            Akasema kutaja sifa zake: Ameniamini wakati watu waliponikanusha, na akanisadiki wakati watu waliponikadhibisha, na akanishirikisha katika mali yake wakati watu waliponinyima, na Mwenyezi Mungu akaniruzuku watoto wake na kuninyima watoto wa wengineo. Imesimuliwa na Ahmad katika Musnad yake.

Mwaka huu Mtume (SAW) aliuita mwaka wa huzuni kwa kukusanyika masaibu mbali mbali yaliyompata. Basi baada ya kufa ami yake na mkewe, na udhia na mateso yalipozidi na wakawa Makureshi wanamfanyia kila aina ya vitimbi na vituko na maudhiko, aliamua aondoke Makka na kuelekea Taif asaa watu wa huko wasilimu na wamnusuru, basi akatoka peke yake na kuelekea Taif.

Kumuoa Sauda:

            Mtume Muhammad (SAW) aliishi na Khadija miaka ishirini na tano bila ya kumuolea mwanamke mwengine na katika maisha yake na mke huyu, Mtume (SAW) alituonyesha mfano wa namna mtu anavyotakiwa aishi na mke mmoja. Baada ya kufariki Khadija kwa mwezi au miezi miwili, Mtume (SAW) alimuoa Sauda bint Zam'a ambaye alikuwa ni katika Waislamu wa mwanzo mwanzo ambao waliohamia Habasha pamoja na kundi la pili lililokwenda huko. Alihamia huko pamoja na mumewe Sakran bin A'mr na akafa huko huko.

Kwenda Taif:

            Mtume (SAW) alipowasili Taif aliwaendea wakubwa na watukufu wa Bani Thaqiif ambao ndio mabwana wa nchi hiyo wakati huo, nao ni ndugu watatu Abdu Yalil na Mas'uud na Habib bin A'mr bin Umeir bin Thaqiif akawaeleza ujumbe wa Mwenyezi Mungu aliopewa na sababu ya kuwajia wao ili waunusuru Uislamu na kumsaidia dhidi ya watu wake waliompinga, akasema mmoja wao kuwa yeye ataivuta nguo ya Al-Kaaba na aitupe ikiwa Mwenyezi Mungu amemleta yeye kama mjumbe, na akasema mwengine kwani Mwenyezi Mungu hakupata mwengine wa kumleta isipokuwa wewe, na akasema wa tatu na kuapa kuwa Wallahi sitosema na wewe abadan, kwani ikiwa wewe ni Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama unavyosema, basi wewe ni hatari kubwa sana kwa mimi kukurudishia maneno, na ikiwa unamsingizia uwongo Mwenyezi Mungu basi hainipasi mimi kuzungumza na wewe.

            Aliposikia haya, Mtume (SAW) alivunjika moyo wa kupata kheri yoyote kutoka kwa Thaqiif, basi akaondoka lakini wao wakampelekea watumwa wao na watu wao kumtukana na kumzomea mpaka watu chungu nzima wakamzunguka na kumfanyia ghasia na kumpopoa kwa mawe mpaka wakamtoa madamu, akaingia kwenye bustani moja ya vijana wawili Utba na Sheyba watoto wa Rabia ambao walikuwemo ndani yake, watu wakarudi zao na yeye akenda mpaka chini ya kivuli cha mzabibu akakaa na wale vijana wawili wanamtazama. Basi baada ya kutulia akamuomba Mwenyezi Mungu:

            Ewe Mola! Wewe tu ninakushtakia udhaifu wa nguvu zangu na uchache wa uwezo wangu na kudhalilika kwangu mbele ya watu, ewe Mrehemevu zaidi kuliko wote wenye kurehemu. Wewe ndiye Mola wa madhaifu, na Wewe ndiye Mola wangu, basi unaniachia nani? Unaniachia wa mbali anayenidharau au adui uliyenisalimisha kwake? Basi ikiwa huna hasira yoyote juu yangu mimi sibali lakini msamaha wako ndio ninaotaraji. Ninajikinga kwa nuru ya uso wako ambayo kwayo, giza lote limepambazuka na mambo yote ya duniani na Akhera yametengenea, na kuteremshiwa ghadhabu yako, au kunishukia machukivu yako, nilaumu kwa makosa yangu mpaka uridhike, wala hapana uwezo wala nguvu ila kwako

            Basi wale vijana wawili Utba na Sheyba walivyoona yaliyomfika waliingiwa na imani kwa ujamaa uliokuwepo baina yao na Mtume (SAW) wakamwita mtumishi wao wa kikristo anayeitwa A'ddas na kumwambia: Chukuwa hizi zabibu umpelekee yule mtu ale, na A'ddas alivyompelekea Mtume (SAW) alitia mkono wake na kumpeleka mdomoni huku akisema: Bismillahi, kisha akala. A'ddas akamtazama usoni kisha akasema: Wallahi, maneno haya hayasemwi na watu wa nchi hizi. Mtume (SAW) akamuuliza: Na wewe unatoka nchi gani ewe Addas na nini dini yako? Akasema: Mkristo na mimi ni mtu kutoka Ninawa. Basi Mtume (SAW) akamwambia: Unatoka kijiji cha mtu mwema Yunus bin Matta. A'ddas akamuuliza: Na wewe unamjuaje Yunus bin Matta? Akasema Mtume (SAW) Huyo ni ndugu yangu, alikuwa ni Nabii na mimi ni Nabii, basi A'ddas akawa anambusu Mtume wa Mwenyezi Mungu kichwa chake na mikono yake na miguu yake.

            Wale vijana wawili akawa mmoja wao anamwambia mwenzake: Ama kijana wako keshafisidiwa, na alipokuja kwao wakamuuliza: Ole wako ewe A'ddas! Una nini unabusu kichwa cha yule mtu na mikono yake na miguu yake? Akasema: Ewe bwana wangu, hakuna kitu bora zaidi katika ardhi kuliko hiki, ameniambia jambo hapana alijuaye isipokuwa Nabii. Wakamwambia: Ole wako ewe A'ddas! Asije akakutoa kwenye dini yako, kwani dini yako ni bora kuliko dini yake

            Mtume (SAW) alipotoka kwenye bustani alielekea Makka akiwa amevunjika moyo na kujawa na huzuni, basi alipofika Qarnul-Manaazil aliinua kichwa chake na kuona wingu limefunga juu yake na alipotazama alimuona Jibril (AS) ndani yake, akiwa pamoja na Malaika mwengine, akamwita na kumwambia kuwa Mwenyezi Mungu amesikia maneno waliokujibu watu wako na amekuletea Malaika wa majabali ili umuamrishe unalotaka. Malaika wa majabali akamwita na kumsalimia na kumwambia: Ewe Muhammad! Unataka nini? Ukiwa unataka niwafudikize kwa majabali mawili (yaliyoko Makka) nitafanya. Lakini Mtume (SAW) akamwambia: Bali ninataraji Mwenyezi Mungu atoe kwenye migongo yao wale watakaomuabudu Mwenyezi Mungu aliyetukuka peke yake bila kumshirikisha na kitu chochote.

            Subahanallah! Baada ya yote haya aliyofanyiwa na kuudhiwa na kuumizwa hakutaka jambo lolote Mtume (SAW) isipokuwa hidaya na uwongofu kwa kizazi cha wale wale waliomkataa na kumkanusha. Amesema kweli Mwenyezi Mungu alipomsifu Mtumewe na kusema: Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote. (Q.21:107). Aidha, akasema: Naye ni rehema kwa wanaoamini miongoni mwenu. (Q.9:61).

            Baada ya mkutano huu na Malaika wa mbinguni, Mtume (SAW) alipata nguvu na kutulia moyo wake kwa kujua kuwa Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na yeye, basi akafunga safari na kuelekea Makka mpaka akafika kwenye bonde la Nakhla akasita hapo na kukaa kwa masiku, na hapa Mwenyezi Mungu akamletea kundi la majini ambao walipita na kusikia Qurani Tukufu na ujumbe wa Mwenyezi Mungu ambao umeletwa kwa wanadamu na majini

Rudi Juu

Majini waupokea ujumbe

: 

            Huu ulikuwa ni ushindi mwengine kwa Mtume (SAW) baada ya ule wa kuletewa Malaika na kumuuliza analotaka, kwani Mwenyezi Mungu alimletea majini wakasikiliza maneno ya Mwenyezi Mungu na kuamini kinyume na watu wake ambao walimpiga vita na kumuudhi na kuukataa ujumbe huu. Akasema Mwenyezi Mungu aliyetukuka:    

            Na wakati tulipowaleta kundi la majini kuja kwako kusikiliza Qurani.
            Basi walipoihudhuria walisema: Sikilizeni!
           
Na ilipokwishasomwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya
           
Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa   
             baada ya Musa, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake,
           
na kinachoongoza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyonyoka
           
Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuita kwa Mwenyezi Mungu,
           
na muaminini, Mwenyezi Mungu atakusameheni, na atakukingeni na adhabu kali.
            Na wasio mwitikia Mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hao hawatashinda katika ardhi,
            wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhaahiri.
                                                                                                Sura:Al-Ahqaaf:29-32

            Mwenyezi Mungu akampasha habari ya kumletea kundi hili na majini na namna walivyoupokea ujumbe wake bila taabu na kuufikisha kwa wenziwao, na kuwa kama walivyo wanadamu kuna wema katika wao waliomkubali Mola wao na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake na kuna waovu na wabaya waliomkataa Mwenyezi Mungu na kupotea na hao kama ilivyo wanadamu watapata adhabu ya Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama. Akaambiwa Mtume (SAW) awaambie watu wake vipi majini walivyopokea ujumbe:

Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza        
            na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qurani ya ajabu! Inaongoza kwenye uwongofu,
            kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu.
            Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu umetukuka kabisa; hana mke wala mwana.
            Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema uwongo uliopindukia
            mipaka juu ya Mwenyezi Mungu. Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo
            Mwenyezi Mungu. Na hakika walikuwako wanaume katika watu waliokuwa wakitafuta
            kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi. Na kwa hakika
            wao walidhani, kama mlivyodhani nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume.
            Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo.
            Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa
            anayetaka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia! Nasi hatujui kama wanatakiwa shari
            wale wanaokaa kwenye ardhi au Mola wao anawatakia uwongofu. Na hakika katika sisi
            wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.
            Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka
            kwa kukimbia. Nasi tulipousikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake
            basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa. Na hakika wamo katika sisi Waislamu,
            na wamo kati yetu wanaoacha haki. Basi waliosilimu, hao ndio waliotafuta uwongofu.
            Na ama wanaoacha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu.

                                                           
                                    Sura:Al-Jinn:1-15

Majini na Mashetani:

            Na hapa inataka tufahamu tofauti iliyokuwepo baina ya majini na mashetani, kwani kama tunavyoelezwa kuna mashetani majini na kuna mashetani wanadamu, na shetani ni yeyote muovu katika viumbe viwili hivi, na huyu ndiye aliyemuasi Mola wake na kutoka kwenye rehema yake, na kupata adhabu yake siku ya Malipo. Tunaelezwa katika Qurani kuwa Iblisi alikuwa katika majini na alikuwa daima yuko na Malaika lakini alipomuasi Mwenyezi Mungu kwa kukataa kumsujudia Adam alipoamrishwa na Mola wake, alitoka kwenye rehema ya Muumba wake na kuwa katika viumbe vilivyopotea. Kizazi cha Iblisi katika majini na wanaomfuata yeye katika wanadamu na majini ndio mashetani. Na Mwenyezi Mungu ametufundisha njia ya kujikinga na mashetani na kujiepusha nao kwa kusoma baadhi ya sura za Qurani kama Ayatul-Kursi, Qul Huwa- Llahu Ahad na Qul Audhu birabbil-falaq na Qul Audhu birabbin-Naas:  

            Qurani Tukufu inatueleza:
           
Sema: Ninajikinga kwa Mola wa wanaadamu
           
Mfalme wa wanaadamu, Mungu wa wanaadamu,
           
Na shari ya wasiwasi wa Shetani, Khannas
           
Anayetia wasiwasi katika vifua vya watu
           
Kutokana na majini na wanaadamu

                                                           
                                    Sura:An-Naas:1-6

            Kama tulivyoona, Mwenyezi Mungu hamtupi mja wake mwema na siku zote baada ya dhiki faraji, kwani baada ya dhiki na mashaka aliyoyapata Mtume (SAW) pamoja na watu wake aliposusiwa na kutolewa nchi, Mwenyezi Mungu alimnusuru kwa kuuvunja mkataba wa dhulma kwa kutumia makafiri wenziwao wenyewe na kumrudisha yeye na watu wake makwao na kumliwaza kwa kumletea ujumbe wa Manasara kutoka Habasha na kuja kusilimu, ujumbe ambao utarudi kwao na kuueneza Uislamu. Kisha baada ya kufikwa na msiba wa kufiliwa na ami yake na mkewe na kufukuzwa na watu wa Taif, Mwenyezi Mungu alimnusuru kwa kumletea majini wakasilimu na kurudi kwa watu wao na kuwafikishia ujumbe huu, na kwa hivyo huu ndio mwenendo wa Mwenyezi Mungu katika maisha, baada ya dhiki ni faraji daima ili mwanadamu asikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.

Akasema Mola aliyetukuka:
            Basi kwa hakika pamoja na uzito kuna wepesi,
            hakika pamoja na uzito kuna wepesi.
                                                              
                                                                                            Q.94:5-6

            Kwa hivyo, Mtume (SAW) alipokaribia Makka alikwenda kwenye pango la Hira na kumpeleka mtu kwa Mutt'im bin Adiy kumtaka amhami naye akakubali na kutoka na watoto wake na watu wake wakiwa wamechukuwa silaha na kwenda kwenye Al-Kaaba na kuwaambia Makureshi kuwa yeye amemweka chini ya himaya yake Muhammad (SAW), kisha akatumiza aingie Muhammad (SAW) Makka akaingia mpaka walipofika ndani ya msikiti wa Makka akasema Mutt'im bin Adiy akiwa juu ya farasi wake: Enyi Makureshi! Mimi nimemhami Muhammad basi sitaki mmoja wenu amtaje kwa ubaya. Basi Mtume (SAW) akenda mpaka kwenye jiwe akalibusu na kusali rakaa mbili na kurudi nyumbani. 

Msimu wa kutangaza dini

            Katika mwaka wa kumi kwenye mwezi wa Dhul-Qaada (Mfungo Pili) watu na makabila mbali mbali yalianza kuteremka Makka kama ilivyokuwa desturi ya Waarabu kuja kufanya Hija na kufanya biashara. Mtume (SAW) akaona ni fursa kubwa hii kuitumia kuufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu, basi akawa anazipitia kabila moja moja akiwaeleza habari ya Uislamu na Ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kuzungumza na kila anayepata nafasi kuzungumza naye, lakini hakuna kabila lililosilimu isipokuwa baadhi ya watu binafsi kama Suweid bin Samit na Iyaas bin Mu'adh na Abu Dhar Al-Ghafari na Tufail bin A'mr Ad-Dusi na Dhamaad Al-Azdi.

Kuja kwa watu wa Yathrib:

            Ulipokuja msimu wa Hija wa mwaka wa kumi na moja tangu Mtume (SAW) apewe utume, walikuja Waarabu kama desturi yao kutoka kila upande kwa ajili ya Hija na biashara, na usiku mmoja wakati Mtume (SAW) alipokuwa anapitapita yeye pamoja na Abubakar Assiddiq (RA) na Ali bin Abi Talib (RA) katika kujaribu kuwakinaisha Waarabu kuhusu Uislamu, alisikia Mtume (SAW) sauti za watu wakizungumza, basi akawaendea na alipofika akawakuta vijana sita wanaotoka Yathrib (jina la Madina kabla ya Mtume (SAW) kuhamia huko),wakiwa wote wanatokana na kabila la Khazraj mojawapo ya makabila mawili makubwa yaliyokuwa yakiishi Madina wakati huo.

            Mtume (SAW) akawauliza: Nyinyi ni akina nani? Wakasema: Sisi ni watu wa kabila la Khazraj. Akawauliza: Mayahudi marafiki zenu? (kwa sababu baadhi ya makabila ya kiyahudi wakati huo yalikuwa yakiishi Madina). Wakasema: Naam. Akawaambia: Hamukai nikazungumza na nyinyi? Wakasema: Kwani. Basi wakakaa naye, na yeye akaanza kuwaeleza Uislamu na maana ya ujumbe huu na madhumuni yake, kisha akawaambia waingie kwenye dini ya Mwenyezi Mungu na kuwasomea Qurani. Wakasema baadhi yao: Mnajua nyinyi wallahi, kwa hakika huyu ni Nabii ambaye Mayahudi wanakutishieni (kwani walikuwa wakiwaambia kuwa atakuja Mtume na sisi tutamfuata na kukushindeni), basi wasikutangulieni kwake, na wakafanya haraka kumjibu Mtume (SAW) na kuingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu.

            Hawa vijana walikuwa ni katika watu wenye hekima na busara katika watu Yathrib (Madina) na vilikuwa vita havishi baina yao na kabila la pili lililokuwepo huko liitwalo Aws, na haya makabila mawili asli yake ni watu wanaotokana na kabila moja la Azd linalotoka Yemen kama tulivyoeleza mwanzo wa tarehe ya Waarabu. Lakini uadui baina yao ulikuwa ni mkubwa sana wakawa daima wamo kwenye vita, na hawa vijana waliingiwa na matumaini kuwa Nabii huyu atakuja awaunganishe wawe watu wamoja kama walivyokuwa zamani. Wakasema kumwambia Mtume (SAW): Kwa hakika sisi tumewawacha watu wetu hakuna watu wenye uadui na shari baina yao kama wao, basi asaa Mwenyezi Mungu awaunganishe kwako, nasi tutawaendea na kuwaita kwenye dini yako na kuwatajia yale ambayo tumekujibu wewe kuhusu hii dini, na ikiwa Mwenyezi Mungu atawaunganisha na wewe basi hapana mtu atakayekuwa na nguvu zaidi kuliko wewe. Basi waliporudi watu hawa Madina walirudi na Uislamu na ikawa Madina yote wanazungumza kuhusu Mtume huyu

            Hawa Waislamu wa kwanza wanaotoka Yathrib na wenziwao wengine waliowatangulia walikuwa ndio chanzo cha kuenea Uislamu Madina na kupata nguvu Mtume (SAW) kwani baada yake kwa muda mdogo Waislamu wakaanza hijra yao kuelekea Madina na kuanzisha dola ya kiislamu ambayo itakayokuja baadaye kumiliki ulimwengu mzima. Majina ya Waislamu hawa ni

            As'ad bin Zurara na A'wf bin Al-Harith na Raafi' bin Maalik na Quttba bin A'mir na U'qba bin A'mir na Jabir bin Abdallah bin Riab wote kutokana na kabila la Khazraj lakini matumbo mbali mbali. 

Kumuoa Aysha bint Abibakr (RA(

            Mwaka huu vile vile Mtume (SAW) alimuoa Aysha bint Abubakr Assiddiq akiwa bado yuko Makka lakini hakuingia naye nyumbani ila baada ya kuhamia Madina. Ukawa ni mwaka ambao Mwenyezi Mungu amemsahilishia Mtume wake (SAW) na kumwafikia katika kazi yake na kumliwaza moyo wake.

Rudi Juu

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Mwaka wa Kikristo Mwaka wa Kiislamu

Matukio ya Tarehe ya Kiislamu kwa Ufupi

570 M.K. 53 B.H. Makka ilihujumiwa na Abraha, akiwa na jeshi kubwa pamoja na tembo (ndovu) ili kuja kuibomoa Kaaba hapo Makka, lakini Mwenyezi Mungu alimuangamiza kwa kumletea ndege waliobeba vijiwe kutoka Motoni.

Abdullah, baba yake Mtume Muhammad (SAW) alifariki dunia.

Mtume Muhammad (SAW) alizaliwa hapo Makkah  katika mwezi wa Rabi-al-Awwal tarehe 12, siku ya Jumatatu.

572 M.K. 51 B.H. Kuzaliwa kwa Abu Bakr Assiddiq (RA)
576 M.K. 48 B.H. Kufariki kwa Amina bint Wahb, mamake Mtume (SAW)
577 M.K. 47 B.H. Kuzaliwa kwa Uthman bin Affan (R.A.)
578 M.K. 46 B.H. Kufa kwa Abdul Muttalib, babu wa Mtume (SAW)
583 M.K. 41 B.H. Mtume Muhammad alichukuliwa safari na ami yake Abu Talib kwenda Syria.

Kuzaliwa kwa Omar bin al-Khattab (R.A.)

591 M.K.   Kisra II anateuliwa kuwa mfalme wa Masassani
595 M.K. 28 B.H. Mtume Muhammad (SAW) anamuoa Khadijah (RA), mwanamke mtukufu wa Kikureshi, na mfanyibiashara mkubwa.
  20 B.H. Kuzaliwa kwa Ali bin Abi Talib (R.A.)
610 M.K. 14 B.H. Herakle anatawala Kostantinia (Uturuki leo)

Mtume Muhammad (SAW) analetewa Jibril (AS) kwa mara ya kwanza kumteremshia Wahyi na kumfundisha Qurani. (Q. 96:1-5)

Khadijah na Ali na Abubakar wanakuwa watu wa kwanza kuukubali Uislamu.

615 M.K. 9  B.H. Waislamu wanahamia Uhabushia (Ethiopia leo)
  8  B.H. Hamza (R.A.), ami yake Mtume (SAW) anaukubali Uislamu, na kadhalika Omar (R.A.) anaingia katika dini ya Uislamu.
616 M.K. 7  B.H. Kabila la Bani Hashim linapigwa pande na Quraish na kutengwa katika Shuab Ali.
619 M.K. 4  B.H. Mwisho wa kupigwa pande Banu Hashim
Kufariki kwa Abu Talib, na Khadijah, mke wa Mtume (SAW).
620 M.K. 3  B.H. Mtume (SAW) anazuru Taif
Kundi la mwanzo la watu wa Madina wanaukubali Uislamu
621 M.K. 2  B.H. Mkataba wa kwanza wa Aqaba.
Mtume (SAW) anapelekwa safari ya Israa and Miraji. Israa kutoka Makka mpaka Jerusalemu, na Miraji kutoka Jerusalemu kwenda mbinguni kupokea amri ya Sala na kuonyeshwa mambo ya huko.
620 M.K. 1  B.H. Mkataba wa pili wa Aqaba.
614 M.K.   Jerusalem inatekwa na Masassani
622 M.K. 1  B.H. Mtume Muhammad (SAW) na wafuasi wake wanahamia Madina.

Mwanzo wa mwaka wa kiislamu na kuanza kwa tarehe ya kiislamu, tangu kuhama Mtume (SAW) kwenda Madina katika 1.1.01 A.H., siku ya Ijumaa katika mwezi wa Julai 16, 622 C.E.

Mtume Muhammad (SAW) anaweka msingi wa msikiti wa Quba.  Aidha, msikiti wa Mtume wa Madina unajengwa.

Waislamu wanaamrishwa kuadhini, na Bilal (R.A.) anakuwa muadhini wa kwanza wa Mtume (SAW).

  2  B.H. Qibla kinabadilishwa badala ya Waislamu kuelekea msikiti wa Al Aqsa wanaamrishwa waelekee msikiti mtukufu wa Makka

Waislamu wanaamrishwa kufunga mwezi wa Ramadhani.

Vita vya Badr vinapiganwa katika mwezi wa Ramadhani tarehe 17 ya Ramadhan ya mwaka wa pili 2 wa Hijra

Fatima (R.A.) anaolewa na Ali (R.A.)

  3 B.H. Vita vya Uhud
  5 B.H. Vita vya Khandaq
Mtume Muhammad (SAW) anamuoa Zainab bint Jahsh, mtalaka wa Zayd, huru wake na mtoto wake wa kulea.
628 M.K 6 B.H. Mkataba wa amani wa Hudaybiya
Khalid bin Walid na Amr bin al-Aas wanaingia kwenye Uislamu, baada ya mkataba.
Mfalme Najashi wa Habasha (Ethiopia) anaingia kwenye Uislamu.
Mfalme wa Maqipti anampelekea Mtume (SAW) Maria na nduguye Sirin kama zawadi kutoka kwake. Maria anaingia kwenye Uislamu na Mtume (SAW) anamfanya kuwa suriya wake.
Badhan, mkubwa wa Kifursi hukoYemen, anaingia kwenye Uislamu.
629 M.K 7 B.H. Vita vya Khaybar vinapiganwa.
Mtume (SAW) anafanya Umrah pamoja na Masahaba zake
Mtume (SAW) anamuoa Safiya, mwanamke wa Kiyahudi baada ya kulishinda kabila lake katika vita, na yeye kuukubali Uislamu.
630 M.K 8 B.H. Makkah inatekwa,  na Mtume (SAW) anaingia Makka kama mshindi na kusimama kwenye Al Kabah siku ya Ijumaa tarehe 20 ya mwezi wa Ramadhani na kuamrisha kuvunjwa kwa masanamu.
Vita vya Huneyn
  9 B.H. Vita vya Tabuk
Mtume (SAW) anapeleka Masahaba zake kwenda kuhiji, wakiongozwa na Abu bakr (RA).
Wasiokuwa Waislamu wanakatazwa kuingia kwenye msikiti mtukufu wa Makka kuanzia tarehe hii.
632 M.K. 10 B.H. Hija ya mwisho ya Mtume (SAW) ya kuagaa aliyoifanya pamoja na Waislamu 100,000 na kutoa hotuba yake mashuhuri hapo.
632 M.K. 11 B.H. Mtume Muhammad (SAW) anafariki dunia katika mji wa Madina siku ya Jumatatu, tarehe12 ya mwezi wa Rabi-al-Awwal, akiwa na umri wa miaka 63.
Abu Bakr anachaguliwa kuwa ndiye Khalifa wake wa kwanza.

Hamza na Umar wasilimu

Kuitangaza dini kweupe

Kufikisha Ujumbe kisiri

Bishara ya Utume

Safari ya Sham

Nasaba ya Mtume

Zama za Ujahili Bara Arabu

Shambulizi la Uhud Banu Qaynuqaa Kupanga Udugu Mapatano ya Aqaba Israa na Miraji Majini wanapokea Ujumbe

Mkataba wa dhulma

Waislamu waingia Makka Kutangaa kwa Uislamu Shambulizi la Khaybar Kushindwa kwa Ahzaab Mwaka wa Tano Mwaka wa Nne Abu Sufyan ajinaki
Ukurasa 4 Muhtasari Siku za Mtume za mwisho Mtume (SAW) apokea tume Abubakar (RA) ahiji Kikosi cha A'lqama Washirikina watiwa mbioni