|
Wanazuoni wamehitalifiana sana kuhusu tarehe aliyopelekwa Mtume (SAW) safari ya Israa na Miraji kama walivyohitalifiana kuhusu tarehe ya kuzaliwa kwake. Kuna waliosema mwanzo mwanzo baada ya kupewa utume, na kuna waliosema baada ya kupewa utume kwa miaka mitano na wengine wamesema kabla ya kuhajiri kwenda Madina kwa muda mdogo tu, na haya hayana umuhimu mkubwa kama tukio lenyewe ambalo lina uhusiano na nguzo kubwa ya dini ya kiislamu inayomfunganisha mja na Mola wake kwa ibada na maombi, kwani katika safari hii ndio Mtume (SAW) alipofaridhishiwa Sala tano za kila siku.
Mwenyezi Mungu amesema katika
Sura ya Israa: Sura: Al-Israa:1 Kisa cha Israa na Miraji kimeelezwa kwa njia mbali mbali na riwaya tofauti tofauti, na wakahitalifiana wanachuoni kuhusu kwenda safari hii kwa roho au kiwiliwili au ilikuwa ni ndoto tu, na haya si muhimu kwetu na lililokuwa muhimu ni kuwa Mtume (SAW) alipelekwa safari hii na akaonyeshwa mengi ambayo yametufahamisha hali za baadhi ya watu waovu watakavyokuwa na adhabu watakazozipata. Tunaelezwa kuwa Mtume (SAW) alikuwa amelala akamjia Jibril (AS) na kumuamsha na kumtoa nje kwenye mlango wa msikiti wa Makka na hapo akaona mnyama mweupe ukubwa wake baina ya nyumbu na punda kwenye mapaja yake kuna mabawa mawili anayasukumia miguu yake, anaweka mguu wake mwisho wa upeo wa jicho lake. Mnyama huyu ni Buraq naye ni mnyama ambaye Manabii kabla yake walikuwa wakipandishwa. Jibril alipotaka kumpandisha Mtume (SAW) alitutumka na kujitikisa. Jibril akaweka mkono wake juu ya nywele za shingo yake na kumwambia: Je, husitahi hilo unalolifanya ewe Buraq, kwani Wallahi hakukupanda mja kabla ya Muhammad aliyekuwa mtukufu zaidi kuliko yeye. Basi akastahi sana mpaka akamiminikwa na majasho kisha akatulia mpaka Mtume (SAW) akampanda. Basi Jibril (AS) akaruka karibu ya Buraq wakaelekea Baytil-Maqdis hapana mmoja anayempita mwenziwe akiona ishara mbali mbali baina ya mbingu na ardhi, mara akamuona mkongwe amekaa pembezoni mwa njia, akamuuliza Jibril ni nani yule akamwambia aendelee na safari yake. Wakenda muda kisha akaona kitu kinamwita kimejitenga na njia kikamwita Muhammad aje, lakini Jibril akamwambia aendelee na safari yake na wakenda kiasi cha kwenda, akakutana na baadhi ya viumbe vya Mwenyezi Mungu wakamuamkia, na Jibril akamwambia warudishie salamu ewe Muhammad, kisha akakutana nao tena na wakamwambia kama yale ya mwanzo na kisha akakutana nao tena na wakamwambia kama waliyomwambia mwanzo mpaka wakawasili Baitul Maqdis, akaingia ndani na kusali rakaa mbili za kuamkia msikiti, kisha akaletewa vyombo vitatu, chombo kina maziwa na chombo kina ulevi na chombo kina maji, na Mtume (SAW) akasikia mtu anasema wakati alivyopewa vyombo hivi kuwa akichagua chenye maji basi atazama na utazama umma wake na akichagua chenye ulevi basi atapotea na utapotea umma wake na akichagua chenye maziwa ataongoka na utaongoka umma wake, basi Mtume (SAW) akachagua chombo chenye maziwa na kunywa, na Jibril akamwambia: Umeongoka na umeongoka umma wako, na mumeharimishiwa ulevi. Kisha Jibril akamwambia kuwa yule mkongwe aliyemuona umri wake uliobakia ndio kama umri wa dunia uliobakia na kuwa dunia siku zake zilizobakia ni chache tu, na kile kitu kilichokuwa kikimwita ni Iblisi anamwita amfuate ndio maana akamwambia aendelee na safari yake, na wale watu aliowaona wakamtolea salamu akamwambia awarudishie salamu ni Ibrahim na Musa na Isa (amani juu yao). Kisha alipotoka hapo akaonyeshwa ngazi nzuri bila kiasi ya kupandia mbinguni inayoitwa miraji (nayo ndio ngazi anayoitazama maiti wakati anapokata roho), na kupandishwa na Jibril mpaka akamfikisha kwenye mlango katika milango ya mbinguni unaoitwa "mlango wa hafadha" na kumkuta malaika anayeitwa Ismail chini ya uwongozi wake malaika elfu kumi na mbili, na chini ya uwongozi wa kila mmoja wao malaika wengine elfu kumi na mbili, na akasema hapana mwenye kujua idadi ya maaskari wa Mola wako isipokuwa Yeye mwenyewe. Basi nilipoingizwa akasema: Nani huyu ewe Jibril? Akasema: Muhammad. Akasema: Kwani keshapelekwa (kwa umma wake)? Akasema: Naam. Basi akamuombea kheri. Na hivi ndivyo alivyokuwa Jibril akipanda naye mbingu baada ya mbingu na kila mbingu alikuwa akiulizwa suala hilo hilo na wakijua kuwa keshapelekwa kwa umma wake wanamuombea kheri kwa Mwenyezi Mungu na kufurahi naye, isipokuwa alipokutana na malaika mmoja akamuombea na kheri na kumkaribisha lakini hakufurahi wala hakutabasamu. Mtume (SAW) akamuuliza: Ni nani huyo? Akamwambia kuwa huyo ni malaika mshika funguo za Moto, na ingekuwa amecheka na yeyote kabla yako au atacheka na yeyote baada yako basi angecheka na wewe, lakini yeye hacheki kabisa. Basi Mtume (SAW) akamwambia Jibril (AS) ambaye amesifiwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kutiiwa na mwaminifu, amuamrishe amuonyeshe Moto. Akamwambia: Ewe Maalik! Muonyeshe Muhammad Moto. Basi akaufunua ukafurika na kupanda mpaka akadhani kuwa utachukuwa yale anayoyaona. Akamwambia Jibril amuamrishe aurudishe mahali pake. Basi akamuamrisha na akauambia ujifiche ukarudi mahali pake ulipotoka akaufunika. Basi akaeleza Mtume (SAW) kuwa alipoingia kwenye mbingu ya mwanzo ya dunia alimuona mtu amekaa anapitishiwa roho za wanadamu huku akisema kuziambia nyengine: Kheri, roho njema imetoka kwenye mwili mwema, na akionyeshwa nyengine husema: Uff, na kukunja uso wake na kusoma: Roho mbaya imetoka kwenye mwili mbaya. Akamuuliza Jibril, ni nani huyu? Akamjibu kuwa huyu ni babako Adam anaonyeshwa roho za kizazi chake basi ikipita roho ya mwenye kuamini hufurahi na kusema roho njema inatoka kwenye mwili mwema na akipitiwa na roho ya kafiri huipa mgongo na kuichukia na kusema roho mbaya inatokana na mwili mbaya. Mtume (SAW) akamsalimia, naye akamrudishia salamu na kumpokea kwa uzuri na kukiri utume wake. Kisha Mtume (SAW) akapandishwa mbingu ya pili na akakutana hapo na Yahya bin Zakaria na Isa bin Maryam na Isa alikuwa ni mtu mwekundu aliyevilia damu, si mrefu wala si mfupi, ana vitone vingi vyeusi kwenye uso wake, na nywele zake ni za singa ya kulala utafikiri kama ambaye ndio kwanza anatoka kuoga kwa namna ambayo zilivyo majimaji, basi akawasalimia na wao wakamrudishia salamu na kumkaribisha na kukiri utume wake. Kisha akapelekwa mbingu ya tatu na hapo akamuona mtu sura yake kama mwezi ulio kamili kwa uzuri mkubwa aliokuwa nao, na alipomuuliza Jibril huyu ni nani alimwambia kuwa huyu ni ndugu yako Yusuf bin Yaqub basi akamtolea salamu na yeye akamrudishia salamu na kumkaribisha na kukiri utume wake, kisha akampeleka mbingu ya nne akamuona hapo Idris akamsalimia na yeye akamrudishia salamu na kumkaribisha na kukiri utume wake, kisha akampandisha mpaka kwenye mbingu ya tano na hapo akakutana na mtu mzima makamo kichwa chake kimejaa mvi na ndevu zake nyingi na nyeupe na sura yake nzuri sana, na alipomuuliza Jibril akamwambia kuwa huyu ni kipenzi cha watu wake Harun bin Imraan, kisha akampandisha kwenye mbingu ya sita na hapo akakutana na mtu hadharani mrefu mwembamba mwenye pua iliyosimama na nywele za mapindi, na alipomuuliza Jibril akamwambia huyu ni ndugu yako Musa bin Imraan, kisha akampandisha mbingu ya saba na hapo akakutana na mtu mzima makamo amekaa juu ya kiti ameelekea nyumba iliyoamirishwa kila siku wanaingia humo malaika sabiini elfu hawarudi tena hapo mpaka siku ya Kiyama. Akasema Mtume (SAW) kuwa hakuona mtu aliyefanana naye zaidi kuliko huyu, na alipomuuliza Jibril akamwambia huyu ni babako Ibrahim, basi akamtolea salamu na yeye akamrudishia na kumkaribisha na kukiri utume wake, na hapa alipoangalia juu aliona milipuko ya umeme na radi. Kisha Jibril akampandisha mpaka mahali kwenye mkunazi wa mwisho karibu na Pepo na kuonyeshwa yaliyokuwepo hapo, ya rangi za ajabu ajabu asizozijua na vipepeo wa dhahabu na malaika chungu nzima waliofunika huo mti wa mkunazi, na Jibril katika sura yake ya kweli kweli akiwa na mbawa mia sita na mito ya kijani iliyoziba pambizo za mbingu. Kisha akapelekwa mpaka karibu kabisa na Mola wake na hapo Mwenyezi Mungu akamfaridhia Sala na mwanzo zilikuwa sala hamsini lakini alipoteremka akapita kwa Nabii Musa alimnasihi kurudi kwa Mola wake aombe tahfifu kwa kujua kuwa itakuwa vigumu kwa umma wa Muhammad kuzisali Sala zote hizo, basi alikuwa akenda kwa Mola wake na kuomba tahfifu na akipunguziwa kumi kisha akirudi tena na kupunguziwa kumi mpaka mwisho zikabakia rakaa tano na Musa alivyomwambia arudi kwenda kuomba alistahi na kuridhika na tano na Mwenyezi Mungu akajaalia hizo tano kwa thawabu za hamsini. Na katika aliyoyaona huko Peponi ni mito minne ya maji mikubwa sana na kamba za lulu na udongo wa miski ambao ndio udongo wa Pepo na maajabu mengine mengi ya huko, na katika aliyoonyeshwa Mtume (SAW) katika ya adhabu ni adhabu ya wale wenye kula mali ya mayatima kwa dhulma midomo yao kama midomo ya ngamia na katika mikono yao vipande vya mawe ya moto wanavirusha ndani ya midomo yao vikitoka mikunduni mwao, na alipomuuliza Jibril alimuambia hao ni wenye kula mali ya mayatima kwa dhulma. Kisha akaonyeshwa adhabu ya wenye kula riba, watu wenye matumbo makubwa kabisa hajawahi kuona mfano wake hawawezi hata kuondoka hapo walipo, wamekaa kwenye njia wanayopita watu wa Firauni na wanawapita wakiwakanyaga kama ngamia wenye kiu kali na wao hawawezi kutaharaki hivi wala vile, na alipomuuliza Jibril akamwambia hawa ni wale wenye kula riba. Kisha akaonyeshwa watu mbele yao kuna nyama iliyonona nzuri na karibu yake nyama nyengine iliyooza na kunuka uvundo, wanakula ile iliyooza na kunuka uvundo na kuwacha ile iliyonona na nzuri, na alipouliza Jibril alimjibu kuwa hao ni wale wenye kuacha wanawake wa halali na kuwaendea wanawake wa haramu. Kisha akaona wanawake wameninginizwa kwa matiti yao na alipomuuliza Jibril akamwambia hao ni wale ambao wanachukuwa watoto wa watu wa haramu na kuwanasibisha na wanaume wengine, yaani wanazini kisha wakiwabandikiza waume zao watoto wa haramu, na alipoteremka kwenye mbingu ya dini na kuangalia chini aliona vumbi na moshi na ghasia na alipomuuliza Jibril ni nani hao, akamjibu kuwa ni mashetani wanazunguka wakipita mbele ya macho ya binadamu wasifikirie kuhusu ufalme wa mbingu na ardhi, la si hivyo wangeona mengi ya ajabu. Baada ya kurudi kutoka mbinguni aliteremka hapo msikiti wa Baitil Madqis hapo Jerusalemu na kukutanishwa na Nabii Ibrahim na Nabii Musa na Nabii Isa pamoja na manabii wengine wakiwa wamekusanywa kwa ajili yake, na akasimama kuwasalisha kisha akatoka na kupanda Buraq na kurudi Makka usiku ule ule. Amesema Mwenyezi Mungu:
(Mwenyezi Mungu) Akamfunulia mja
wake aliyomfunulia. Sura:An-Najm:10-18 Makureshi wanakanusha Israa: Ameeleza Umm Hani bint Abi Talib (RA) kuwa usiku aliopelekwa Mtume (SAW) Israa alikuwa nyumbani kwangu na baada ya kusali Sala ya Isha alilala na sisi tukalala, kisha kabla ya Alfajiri kwa muda mdogo akatuamsha na baada ya kutusalisha Sala ya Alfajiri aliniambia: Ewe Umm Hani, Mimi nilisali na nyinyi Sala ya Isha kama ulivyoona kwenye bonde hili, kisha nikenda Baytul Maqdis na kusali huko, kisha nikasali na nyinyi Sala ya Alfajiri sasa kama ulivyoona, kisha akasimama anataka kutoka nikamzuiya na kumwambia: Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu usiwazungumzie haya watu wakakuona mwongo na kukuudhi. Akasema: Wallahi nitawahadithia. Basi nikamwambia kijakazi wangu wa kihabushia amfuate ili aende kusikiliza nini atawaambia watu na nini watu watasema. Basi Mtume (SAW) alipowaeleza watu, walistaajabu sana na kufanya stihzai na kejeli, mpaka baadhi ya Waislamu wenye imani dhaifu wakawa na wao hawasadiki. Makureshi wakamuuliza dalili yake na kuwa hawajawahi kusikia jambo kama hili katu. Basi akawaambia kuwa yeye alipita wakati alipokuwa anaelekea Sham msafara wa Bani fulani katika bonde fulani, na ngamia alipohisi kupitiwa na Buraq alitimkwa akakimbia na yeye akawaonyesha alipo, kisha aliporudi kutoka Sham aliupitia msafara mwengine alipofika mahali paitwapo Dhajnan akawakuta watu wamelala na wana chombo kina maji wamekifunika, akakifungua na kunywa maji yaliyokuwemo na kukifunika kama kilivyokuwa, na alama yake ni kuwa msafara wao sasa unaelekea Al-Baydhaa kwenye njia ya jabali la Taniimu wakiongozwa na ngamia mwenye rangi nyeupe na nyeusi amebeba magunia mawili moja jeusi na la pili jeusi-jeupe, basi watu walipoangalia hawakuona isipokuwa yule yule ngamia aliyewatajia Mtume (SAW) ndiye anayeongoza msafara na walipowauliza kuhusu chombo walisema kuwa wao walikiwacha chombo kimejaa maji na kukifunika na walipoamka wakakikuta kimefunikwa kama walivyokifunika lakini hawakupata maji ndani yake, na wakawauliza wengine waliporudi Makka kuhusu ngamia aliyepotea, wakasema amesema kweli wallahi, maana kilitushtua kitu na akatukimbia ngamia kisha tukasikia sauti ya mtu inatuelekeza alipo. Kisha wakataka awaeleze hiyo baytil maqdis imekaaje maana wengine washaiona na wanaijua, basi akawa anaeleza Mtume (SAW) msikiti ulivyo mpaka akababaishika na sehemu zake nyengine, basi Mwenyezi Mungu akamletea sura yake mbele ya macho yake akawa anawaeleza vile ulivyo, basi watu wakasema: Ama kweli umeusifu msikiti sawasawa. Makureshi wakamwita Abubakar na kumwambia amsikilize rafiki yake uwongo wake wa kudai kuwa usiku mmoja kenda baytil maqdis na mbinguni na yale aliyoonyeshwa na Mola wake kisha akurudi usiku huo huo, basi wakamkadhibisha na kumfanyia stihzai na shere, basi Abubakar akasema kuwa ikiwa kweli amesema maneno hayo basi amesema kweli kwani yeye ananiambia yaliyokuwa ya ajabu zaidi ya kuletewa ujumbe kutoka mbinguni, basi Mtume (SAW) akamwita: Assiddiq na kuanzia siku hiyo akawa anajulikana kwa jina la Abubakar Assiddiq. Siku ile alikuja tena Jibril na kumfundisha Mtume (SAW) namna ya kuzisali hizi Sala tano na nyakati zake mbali mbali kwani kabla ya hapo Mtume (SAW) alikuwa akisali mara mbili tu asubuhi kabla ya kuchomoza jua na jioni kabla ya kuzama jua sala za rakaa mbili mbili na hivi inasemekana ndivyo alivyokuwa akisali Nabii Ibrahim (AS). Jibril akamsalisha rakaa mbili ilipodhihiri Alfajiri, na rakaa nne za Adhuhuri lilipopinduka jua upande wa magharibi na rakaa nne za Alasiri kilipokuwa kivuli kimezidi mara mbili kuliko urefu wa kile kitu, na rakaa tatu za Magharibi wakati jua lilipozama na rakaa nne za Isha wakati yalipopotea mawingu mekundu. Safari hii ilielezwa na masahaba mbali mbali kila mmoja kwa namna yake na hayo yaliyoelezwa hapo juu hayakuja kama yalivyoelezwa na wenyewe kwa njia zao tofauti tofauti, bali tumejaribu kukusanya riwaya mbali mbali ili tuweze kueleza mengi yaliyoelezwa na masahaba hawa kwa njia ambayo kila mmoja atafahamu. Katika walioeleza kisa hiki ni Anas bin Malik, na Umar bin Al-Khattab na Ali bin Abi Talib na Ibn Masuud na Abu Dhar na Malik bin Saasaa na Abu Hureira na Abu Said na Ibn Abbas na Shaddad bin Aws na Ubay bin Kaab na Abdullahi bin Amr na Jabir na Hudheifa na Abu Ayyub na Abu Umama na Samura bin Jundub na Suhayb Ar-Rumi na Umm Hani na Aysha na Asmaa wote Mwenyezi Mungu awe radhi nao. Ulipoingia mwaka wa kumi na mbili wa Hijra na kuja msimu wa Hija, walikuja kutoka Yathrib wanaume kumi na mbili wakiwemo watano katika sita waliokuja kusilimu mwaka uliopita na saba ni wapya, wakakutana na Mtume (SAW) kwenye Aqaba katika Mina na kufanya naye mapatano ya kuwa hawatomshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote, wala hawataiba, wala hawatazini wala hawataua watoto wao, wala hawatazua uwongo wowote ule, wala hawatamuasi katika kufanya mema, na mwenye kutekeleza haya ujira wake kwa Mwenyezi Mungu na mwenye kufanya lolote katika haya akatiwa adabu hapa duniani basi itakuwa ni kafara yake na mwenye kufanya haya Mwenyezi Mungu akamsitiri basi jambo lake liko kwa Mwenyezi Mungu, akitaka atamuadhibu na akitaka atamsamehe. Basi wakakubaliana juu ya haya. Hawa kumi na mbili waliofanya mapatano haya na Mtume (SAW) ni As-ad bin Zurara na Awf bin Al-harith na Raafi' bin Malik na Qutba bin A'mir na Uqba bin A'mir na Mua'dh bin Al-Harith na Zakwan bin Abdil-Qays na Ubada bin Samit na Yazid bin Tha'alaba na Al-A'bbas bin Ubada na Abul-Haytham bin Attayhan na Uweim bin Saaida. Katika hawa kumi na mbili, watano wa mwanzo ni wale waliosilimu mwaka uliopita, na watano wanaowafuatia ni wenziwao wa kabila la Khazraj na kwa hivyo wote wanakuwa kumi kutokana na kabila la Khazraj na wawili wa mwisho ndio wa kabila la Aws. Mtume (SAW), baada ya kumalizika msimu wa hija, alimpeleka pamoja na kundi hili la Waislamu, kijana ili awafundishe dini yao na kutangaza Uislamu huko Madina. Kijana huyu ndiye balozi wa kwanza wa kiislamu kupelekwa na Mtume (SAW) naye ni Mus'ab bin U'meir, na Mwenyezi Mungu alimuafikia akafanya kazi nzuri sana ya kutangaza na kueneza dini yake huko Madina, kwani inasemekana kuwa siku moja walikutana Saad na Useid wakubwa wa kabila la Bani A'bdil-Ash-hal akiwa Mus'ab na As'ad bin Zurara wamekaa kwenye kisima ndani ya bustani, Saad akamtumiza Useid kwenda kuwatoa na kuwazuiya wasiingie mtaa wao, akenda Useid akiwa ameshika mkuki wake na akamsimamia Mus'ab na kumuuliza kuwa amekuja kufanya nini kwao? Basi As'ad akamwambia huyu ni mkubwa wa kabila lake, na Mus'ab akamwambia: Mbona hukai basi ukasikiliza, na ikiwa umeridhika na hili jambo likubali na ukilichukia hutoonyeshwa ya kukuudhi. Akasema: Umefanya insafu na kukaa kusikiliza. Mus'ab akamueleza kuhusu Uislamu na kumsomea Qurani na tukawa tunahisi kabla hakutamka kuwa atasilimu kwa namna ya uso wake ulivyofurahi na kubadilika, kisha akasema: Ni mazuri yaliyoje haya! Basi akasilimu. Aliporudi Useid kwa mwezake akamuona amebadilika sivyo alivyoondoka basi akamuuliza umefanya nini? Akamwambia: Nimezungumza nao lakini sikuona kuwa wana ubaya wowote ule. Basi akatoka yeye kwenda na alipofika As'ad bin Zurara akamwambia Mus'ab kuwa anayekuja ni mkubwa wa kabila lake na ikiwa atafanikiwa kumkinaisha basi kabila lake lote litamfuata. Mus'ab akamwambia akae na amsikilize, na baada ya kumuelezea Uislamu na kumsomea Qurani alisilimu na kurudi kwa watu wake na kuwaambia: Enyi bani Abdil-Ash-hal! Mnalionaje jambo langu kwenu? Wakasema: Mkuu wetu na ni mwenye rai bora katika sisi. Akasema: Basi maneno ya watu wenu wanaume na wanawake ni haramu kwangu mpaka mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi haukuingia usiku ila kila mtu, mwanamume na mwanamke, wote walisilimu isipokuwa mtu mmoja tu katika wao alichelewa kusilimu mpaka wakati wa vita vya Uhud akasilimu siku hiyo na kupigana vita na kuuliwa bila kumsujudia Mwenyezi Mungu hata mara moja. Akasema Mtume (SAW): Amefanya kidogo na akaajiriwa ujira mkubwa. Mus'ab akabaki kwenye nyumba ya As'ad bin Zurara anawavutia watu katika Uislamu mpaka watu wote wa Madina wakasilimu isipokuwa nyumba mbili tatu tu ambazo baadaye vile vile zikaja kusilimu, na kabla ya kupita mwaka Mus'ab akawa keshatekeleza kazi yake na kurudi kwa Mtume (SAW) na kumbashiria kufanikiwa kwake na kumueleza habari za watu wa Yathrib. Mapatano ya pili ya Aqaba: Katika msimu wa hija mwengine, ambao ulikuwa ni mwaka wa kumi na tatu tangu Mtume (SAW) kupewa utume, walikuja kutoka Yathrib Waislamu sabiini na tano, wanaume sabiini na tatu, na wanawake wawili, pamoja na wenziwao waliokuwa bado katika ushirikina wao kuja kufanya hija. Katika hao kulikuwepo wanaume sitini na mbili kutoka kabila la Khazraj na wanaume kumi na moja wa kabila la Aws pamoja na wanawake wao wawili. Walikutana na Mtume (SAW) kisiri na kuagana naye kuwa watakutana Aqaba usiku, basi ulipoingia usiku na watu walipokuwa wamelala walianza kutoka mmoja mmoja kuelekea Aqaba na huko wakakutana na Mtume (SAW) akiwa amekuja na ami yake Al-Abbas kuja kushuhudia ijapokuwa yeye mwenyewe alikuwa bado si Muislamu. Baada ya kukusanyika, mtu wa kwanza aliyesimama kusema alikuwa ni ami yake Mtume (SAW) akasema: Enyi Makhazraji! Hakika Muhammad ni katika sisi kama mnavyojua, nasi tumemhami na watu wetu, na yuko katika kuenziwa na watu wake na kuhifadhiwa ndani ya nchi yake, lakini yeye hataki isipokuwa kuwa na nyinyi na kukufuateni nyinyi, basi ikiwa mnaona kuwa mtaweza kumtekelezeya yale ambayo mumemwitia na kumlinda na wale wenye kumpinga, basi nyinyi na jukumu mlilolichukuwa, na ikiwa mnaona kuwa mtamtoa na mtamwacha mkono baada ya kutoka naye kwenda kwenu, basi tangu sasa mwacheni, kwani yeye yuko kwenye enzi na ulinzi na watu wake na nchi yake. Akasema Kaab: Tumesikia uliyoyasema, basi sema Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu na chukuwa unayoyapenda kwa ajili yako na Mola wako. Basi Mtume (SAW) akasema na kusoma Qurani na kumuomba Mwenyezi Mungu na kuwavutia watu katika Uislamu, kisha akasema: Ninapatana nanyi munilinde kama mnavyowalinda wake zenu na watoto wenu. Akasimama Al-Baraa bin Ma'rur na kumpa mkono Mtume (SAW) na kumwambia: Naam, kwa yule ambaye amekuleta kwa haki tutakulinda kama tunavyowalinda wake zetu, basi kubaliana na sisi Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu kwani sisi ni watu wa vita tumevirithi tangu wazee wetu mababu kwa mababu. Na alipokuwa Baraa bado anasema akaingilia maneno Abul-Haytham na kusema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kuna baina yetu na watu wengine (yaani Mayahudi) mikataba na sisi tutaivunja, basi je, ikiwa sisi tutafanya hivyo, kisha Mwenyezi Mungu akakupa ushindi, utarudi kwa watu wako na kutuwacha? Mtume (SAW) akatabasamu na kusema: Bali damu yako ndio damu yangu, na damu utakayoimwaga wewe ndio mimi nitaimwaga. Basi wakafanya mkataba wa pili wa Aqaba na wakachagua viongozi kumi na mbili, kutoka kila tumbo (kabila) mmoja, tisa kutokana na Khazraj na watatu kutokana na Aws nao ni hawa wafuatao:
Kisha Mtume (SAW) akawaambia: Nyinyi mna dhamana juu ya watu wenu, na mimi nina dhamana juu ya watu wangu. Na juu ya kuwa jambo hili lilitimu kwa siri, lakini Makureshi walipata habari na kuingiwa na wasiwasi mkubwa na huzuni kwa kujua kuwa mapatano kama haya yanaweza kuleta mchafuko na kuharibu mambo mengi ambayo yataathiri maisha yao na mali yao na kwa hivyo walipeleka tume kwenye kambi ya watu wa Yathrib ili kupeleka malalamiko yao juu ya mkataba huu, wakasema: Enyi Makhazraji, tumepata habari kuwa mumekwenda kwa huyu mtu wetu (yaani Muhammad) mnataka kumtoa kwetu na kupatana naye kutupiga vita sisi, na kwa hakika tunaapa kuwa hapana mji wa Waarabu ambao tunachukia zaidi kuzuka vita baina yao na sisi kuliko nyinyi. Na ilivyokuwa washirikina katika Makhazraji hawajui kitu kuhusu mapatano haya, kwa kuwa yalifanyika wakiwa wao hawapo na kwa siri, walisimama kuapa na kukataa jambo hili: Hapana lolote lililokuwa na wala sisi hatujui kitu, na ilikuwa kweli hawajui lolote. Kisha wakamwendea Abdullahi bin Ubey bin Salul mkubwa wa Makhazraj lakini si Muislamu naye akasema: Haya ni batili na hayawezi kuwa yametokea, wala watu wangu hawawezi kufanya jambo bila mimi. Ama Waislamu walinyamaza kimya na kutazamana bila ya kusema neno, na kwa hivyo Makureshi wakenda zao wakiwa wamesadiki maneno ya washirikina. Lakini baadaye walikuja kupata uhakika wa jambo hili wakiwa watu wa Yathrib washaondoka na wakatoka kuwafuatia lakini watu wa Yathrib walikuwa washafika mbali, wakaweza kumkamata mmoja wao tu Saad bin Ubada na kumfunga na kumchukuwa Makka, lakini alikuja Mutt'im bin Adiy na Al-Harith bin Harb bin Umayya na kumhami kwa sababu alikuwa akihami misafara yao yalipokuwa yakipita Yathrib, na kumwacha ende zake, akenda na kukutana na wenzake na kurudi Yathrib. Na huu ndio mkataba wa pili wa Aqaba uliowakusanya Waislamu wa Makka na wa Madina na kuanza tarehe mpya kwa Waislamu, kwani baada ya mapatano haya, Waislamu walianza kuhama Makka kwenda Madina na kuanza maisha yao mapya. Kujengwa kwa Msikiti wa Mtume (SAW): Jambo la kwanza ambalo Mtume wa Mwenyezi Mungu alilolifanya baada ya kutulia Madina ni kujenga msikiti wake wa Madina, kwani msikiti kiislamu ndio msingi au kiini cha jamii ya kiislamu, na bila ya msikiti, mambo mengi ya kiislamu yanakuwa hayawezi kufanyika. Msikiti wakati wa Mtume (SAW) ulikuwa ni mahali pa ibada, na pa mikutano mbali mbali ya Waislamu, na pa watu kujifunza elimu na kupata maarifa ya kila aina, na pa kuchukuwa uamuzi tofauti tofauti ukiwa wa mas-ala ya vita au amani au ujenzi au mambo mengineyo ya kimaisha. Kwa hivyo, Mtume (SAW) akanunua ile ardhi ambayo ngamia wake alisita na kukaa chini wakati mwanzo alipowasili Madina, kutokana na vijana wawili mayatima na kuanza kuisafisha kwa ajili ya ujenzi. Mahali hapo kulikuwa na makaburi ya washirikina yakachimbuliwa na kutolewa mafupa ya maiti wao na kuzikwa sehemu nyengine, na mashimo mashimo yakafunikwa, na mitende yakakatwa na kuondoshwa. Ukajengwa msikiti kwa mawe na matufali ya udongo na vigogo vya mitende na kuezekwa kwa majani yake, akishiriki mwenyewe Mtume (SAW) pamoja na Muhajirina na Maansari, huku akiimba mashairi:
Ewe Mola hapana maisha ila maisha ya Akhera
Basi Wasamehe Maansari na Muhajira Msikiti ukamalizika na kikawa kibla chake kimeelekea kaskazini upande wa Baytil-Maqdis, msikiti ulioko Jerusalemu, na karibu yake vikajengwa vyumba viwili, kimoja cha Sauda na cha pili cha Aysha ambao alikuwa wakati huo keshawaowa. Adhana ya kwanza: Umuhimu wa Sala ya Jamaa katika Uislamu ni mkubwa sana, na ndilo jambo linalowakutanisha Waislamu kila siku mara tano ili kujua hali zao na kuweza kusaidiana ikiwa katika wakati wa shida au furaha. Ili Waislamu wakutane wakati wa Sala hizi, Mtume (SAW) aliwaita masahaba zake na kuwashauri wafanye nini na kila mtu akatoa shauri lake. Kuna waliosema kuwa tupandishe bendera kila wakati wa Sala, lakini ikakataliwa fikra hii kwa sababu haitowafaa waliolala wala walioghafilika. Mwengine akasema basi tuwashe moto juu ya kilima, lakini haikukubaliwa fikra hii vile vile. Mwengine akasema kwa nini hatupigi baragumu, na walikuwa Mayahudi wakifanya hivyo. Mtume (SAW) hakuwafikiana na fikra hii, kwa sababu hakutaka kuwafuata Mayahudi. Kisha mwengine akasema basi tupige kengele kama Manasara, nayo vile vile ikakataliwa. Wengine wakasema basi kwa nini hatuiti watu kwa sauti kila ukiwadia wakati wa Sala. Ikakubaliwa fikra hii na akawa mmoja katika watakaoita watu ni Abdullahi bin Zayd Al-Ansari, na alipokuwa amelala alimjia mtu na kumwambia: Je, sikufundishi maneno wakati utakapowaita watu kusali? Akajibu: Kwani! Basi akamfundisha maneno haya yanayotumika katika adhana leo. Alipoamka tu alikwenda kwa Mtume (SAW) na kumueleza, na yeye akamwambia kuwa hio ni ndoto ya haki na kumwambia amfundishe Bilal kwa kuwa sauti yake ilikuwa nzuri kuliko yake, basi akamfundisha Bilal na alipokuwa anaadhini Bilal, akaja Umar bin Al-Khattab na kumwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa na yeye ameoteshwa ndoto kama hiyo. Basi Bilal akawa mmojawapo wa waadhini wa Mtume (SAW), yeye pamoja na Abdullahi bin Ummi Maktum, na akawa akiadhini Alfajiri huongeza "Assalatu khayrun minan-nawm", na Mtume (SAW) akamkubalia. Kisha Mtume (SAW) akaamrisha katika mwezi wa Ramadhani, wakati wa Alfajiri ziadhiniwe Adhana mbili, moja ya kuamsha watu kula daku, na ya pili ya kuingia wakati wa Sala. Ama Adhana ya Ijumaa ya kwanza, hii ilikuwa haiko wakati wa Mtume (SAW) wala wa Abubakar na Umar, lakini aliposhika ukhalifa Uthman, wakawa Waislamu wamekuwa wengi sana, aliamrisha watu waende wakazinduliwe huko sokoni kwa mwito wa Sala. Kisha baadaye katika ukhalifa wa Hisham bin AbdulMalik akaamrisha mwito huu ufanywe juu ya minara na baadaye kugeuzwa kufanywa adhana kamili ndani ya misikiti kabla ya kupanda khatibu kwenye mimbari, na kwa hivyo, adhana hii ya kwanza siku ya Ijumaa ni katika bid'a zilizotumbukizwa katika Uislamu. Kupanga udugu baina ya Muhajirina na Ansari Amesema Ibnul-Qayyim: Kisha Mtume (SAW) akapanga udugu baina ya Muhajirina na Maansari kwenye nyumba ya Anas bin Malik, na walikuwa wanaume tisiini, nusu yao walikuwa Muhajirina na nusu nyengine walikuwa Ansari. Alipanga udugu wa kusaidiana na kurithiana baada ya mauti badala ya jamaa zao mpaka vilivyotokea vita vya Badr, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya za kurudisha urathi kwa jamaa zao watu badala ya kupewa ndugu hawa, akasema: Q.8:75. Udugu huu ulikuwa ni udugu mkubwa, na wakawa Muhajirina na Maansari wanapendana sana kufika hadi kusabiliana kila kitu ili mtu mwenzake aishi maisha mazuri. Amesimulia Al-Bukhari kuwa walipokuja Madina, Mtume (SAW) alipanga udugu baina ya Abdur Rahman na Saad. Akamwambia Abdur Rahman: Mimi ni mwenye mali nyingi zaidi katika Maansari, basi nitaigawanya mali yangu nusu mbili, na nina wake wawili, basi tazama utakayempenda zaidi katika hao umtaje nipate kumwacha, na ikimalizika eda yake utamuoa. Akajibu Abdur Rahman: Mwenyezi Mungu akubariki katika wake zako na mali yako, iko wapi soko yenu? Basi akamuonyesha soko ya Banu Qaynuqaa. Mifano kama hii ya udugu mkubwa kabisa na ya kusalibiana mali na mashamba na hata wake yalikuwa mingi, na hii ni kuonyesha namna gani Maansari walivyowapokea ndugu zao Muhajirina na kuwafadhilisha hata juu ya nafsi zao na kuwapendelea kila la kheri, mpaka Mwenyezi Mungu akawasifu kwenye Qurani yake na kusema: Q. Alhashr:9 Aidha, kupanga huku kwa udugu baina ya Muhajirina na Maansari katika hali ya shida na taabu kama hii, kunaonyesha hekima kubwa aliyokuwa nayo Mtume (SAW) katika kutatua matatizo yaliyokuwa yamewakabili Waislamu mwanzo mwanzo wa kujenga jamii mpya ya kiislamu na kuanzisha dola mpya ya Uislamu. Mkataba baina ya Makabila ya Waislamu: Baada ya Mtume (SAW) kupanga udugu baina ya Muhajirina na Maansari, alifanya mkataba baina ya makabila mbali mbali ya kiislamu ili kuondosha hitilafu zilizokuweko baina ya makabila haya skiu za Ujahili, na kujaaliya Waislamu wote kuwa ni umma mmoja na kitu kimoja, linalomfika mmoja wao ndilo limewafika Waislamu wote. Mkataba huu uliwaunganisha Waislamu wa makabila ya kikureshi, na ya Madina, na wengine wowote wanaotoka kwenye makabila mbali mbali na kuja kujiunga na umma wa kiislamu. Aidha, yaliyoelezwa katika mkataba huu, mbali na kuwa Waislamu wote ni umma mmoja, ni kuwa Waislamu wote wasaidiane dhidi ya Makafiri, na kuwa ni mkono mmoja hata dhidi ya watoto wao wakiwa si Waislamu, na kuwa Muislamu asimuue Muislamu mwenzake, na kuwa wote wasimame dhidi ya dhulma au uadui wowote atakaofanyiwa mmoja wao, na asimnusuru kafiri dhidi ya Muislamu hata akiwa ni jamaa yake, na kawaida hizi ziliwasaidia sana Waislamu kushikamana na kuwa kitu kimoja, na akawa Mtume (SAW) anawafundisha nyenendo nzuri na kuwaelimisha mambo ya kheri na kuwaeleza mambo mapya kila ukiteremka Wahyi kutoka kwa Mola wao. Mayahudi na Wanafiki hapo Madina: Tumeona namna gani Waislamu walivyopata taabu Makka kutokana na Washirikina wa Makka, na vipi walivyokuwa wakiwaadhibu na kuwatesa, mpaka Mwenyezi Mungu akawafariji na kuwapa nchi na watu wenye kuwapenda na kuwashughulikia. Pamoja na hayo, mitihani haikusita kwani hapo Madina walipambana na aina nyengine ya watu ambao walikuwa hawakuridhika na yale waliyokuwa wakifanyiwa Waislamu, ikawaingia hasadi na chuki na kuanza kuwafanyia kila vitimbi na njama. Katika mji wa Madina kulikuwepo na makabila matatu ya kiyahudi: Banu Qaynuqaa, na Banu Qureydha, na Banun-Nadhir, na juu ya kuwa wao walikuwa wakijua kuwa ataletwa Mtume na siku zote wakiwatishia Waarabu wa Madina kuwa atakuja Nabii na sisi tutamfuata tupigane na nyinyi tukushindeni, lakini alipokuja na dalili zote walimkataa kwa chuki na hasadi waliyokuwa nayo. Makabila haya yalikuja kuwaletea Waislamu taabu kubwa katika maisha yao ya hapo Madina mpaka Mtume (SAW) alipolazimika kupigana nao vita na kuwatoa nchi. Kundi jengine lililoleta taabu na shida kwa Waislamu ni baadhi ya Waarabu wa hapo Madina ambao nyoyo zao zilikataa uwongofu na Mwenyezi Mungu akawanyima imani, wakawa wanajidai Uislamu na kudhihirisha imani lakini nyoyo zao zilikuwa zimejaa upotofu na ukafiri. Kundi hili lilikuja kujulikana kuwa ni kundi la Wanafiki na kiongozi wao alikuwa ni Abdullahi bin Ubay bin Salul Al-Khazraji ambaye alikuwa awe kiongozi wa Waarabu wa Madina kabla ya kusilimu watu wa Madina na kumchagua Mtume (SAW) kuwa ndio kiongozi wao. Mkataba na Mayahudi: Kwa sababu ya chuki zao na hasadi waliokuwa nayo Mayahudi, Mtume (SAW) aliona bora afanye mkataba nao ili awafunge kwa mkataba na wazuilike kupanga njama dhidi ya Waislamu, na kwa hivyo akafanya nao mkataba wa kutopigana vita nao, na kutowasadia wale watakaowapiga vita katika makabila mengine, na kukitokea hujuma yoyote dhidi ya Madina, basi wawasaidie kuwapiga maadui, na kuuhami mji wa Madina, na yeye akawakubalia waendelee na dini yao. Uadui wa Wanafiki: Juu ya kuwa Wanafiki walikuwa ni maadui wakubwa zaidi kwa Waislamu kuliko hata Mayahudi, kwa sababu ya kudhihirisha kwao Uislamu na kuishi na Waislamu kama ndugu zao ilhali ni maadui zao, lakini Mtume (SAW) hakuwafanya kitu kwa ajili ya kuwachukulia kwa ile dhahiri yao waliyokuwa wakiionyesha, mpaka aliposimama Abdullahi bin Ubay bin Salul, kiongozi wao, baada ya kupata barua kutoka kwa Washirikina wa Makka ikiwatishia kuwa ikiwa hawatamtoa Mtume (SAW) Madina basi wao watasimamisha vita dhidi yao na kuwachukuwa wanawake wao, na kuwaita Wanafiki wenzake ili wafanye walivyoamrishwa na Washirikina wa Makka. Basi Mtume (SAW) aliposikia haya alikutana nao na kuwaambia kuwa mnataka kuwaua watoto wenu na ndugu zenu kwa ajili ya maneno ya Washirikina wa Makka, basi wakarudi nyuma. Matishio ya Washirikina: Makureshi hawakuwawacha Waislamu kukaa kwa amani huko Madina, kwani waliwapelekea salamu kuwa msifikiri kuwa mumetukimbia kwenda Madina ndio basi, sisi tutakujieni na kukumalizeni huko huko mlipo. Basi Mtume (SAW) akawa anaweka ulinzi mkali usiku wakati Waislamu wanapolala na kuwa daima wanakaa na silaha zao, wakilala wanalala nazo na wakiamka wanaamka nazo.
Jeuri za Makureshi zilipozidi, na matishio yao yalipokithiri, na ujabari wao na kibri kilipopindukia mipaka, Mwenyezi Mungu aliwateremshia Waislamu Wahyi wa kuwaruhusu kupigana na Makafiri wa Makka ikitokea dharura ya vita. Waislamu walipokuwa bado wapo Makka, walikuwa hawana nguvu na hawana dola ya kuweza kufanya matayarisho ya kivita, lakini walipohamia Madina walikuwa na uwezo wa kufanya haya, kwani walikuwa na dola wakati huo, na aghlabu ya watu wa Madina walikuwa pamoja na wao, isipokuwa kikundi kidogo cha wanafiki na makabila ya kiyahudi yaliyokuwa yakiishi huko. Mashambulizi baada ya Badr: Bughudha na chuki zilizidi baada ya ushindi mkubwa ambao Mwenyezi Mungu aliwapa Waislamu katika vita vya Badr, na kukawa na makundi manne yaliyoingiwa na khofu na kuzidi wasiwasi baada ya tukio hili kubwa. Makundi mawili yalikuwepo ndani ya Madina, nayo ni Mayahudi na Wanafiki, na makundi mengine mawili yalikuwa nje ya Madina, moja ni Makureshi wa Makka na jengine ni makabila ya kibedui ambayo kazi yao ilikuwa kunyanganya na kupokonya watu mali zao njiani majangwani. Mabedui hawa walipoona ushindi wa Waislamu na kuzidi kwa nguvu zao, walihisi kuwa kuna hatari na kuwa mambo yakiendelea namna hivi watashindwa siku za mbele kunyanganya watu mali zao. Shambulizi dhidi ya Bani Suleym: Matokeo yake ni kuwa kabila la Bani Suleym lilijizatiti kwenda kuishambulia Madina, na Mtume (SAW) alipopata habari hizi, hakusubiri bali alijitayarisha na jeshi la watu mia mbili na kulihujumu kabila hili ndani ya kijiji chao kwenye sehemu iitwayo Al-Kudr. Bani Suleym wakakimbia na kuwacha nyuma ngamia mia tano ambao Mtume (SAW) aliwachukuwa na kuwagawia wale walioshiriki katika shambulizi hili, kila mmoja akapata ngamia wawili, baada ya kutoa khumsi (sehemu moja katika tano) ambayo ndio sehemu ya Mwenyezi Mungu na Mtumewe. Shambulizi hili lilitokea siku saba tu baada ya kurudi Mtume (SAW) Madina kutoka kwenye vita vya Badr. Mtume (SAW) alimwakilisha Madina Siba'a bin Arqatta alipokwenda kwenye vita hivi. Njama ya kumuua Mtume (SAW): Katika mateka wa Badr ni Wahb bin Umeyr Al-Jumahi ambaye babake alikuwa ni mtu muovu sana katika Makureshi. Siku moja baada ya vita vya Badr, alipokuwa amekaa na Safwan bin Umayya alimwambia: Wallahi, ingekuwa si deni nililokuwa nalo na watoto ninaowaogopea umaskini baada yangu, ningemwendea Muhammad na kumuua, kwani mtoto wangu ni mateka kwao. Safwan akamwambia: Niachie mimi deni lako, na watoto wako ni wangu nitawatazama mimi. Basi Umeyr akachukua upanga wake na kuelekea Madina. Alipofika Madina, Umar ambaye alikuwa amesimama na Waislamu wengine alimuona Umeyr amebeba upanga akasema: Mleteni kwangu! Akamchukua Umar na kumpeleka kwa Mtume (SAW), na alipomuona alisema: Karibia ewe Umeyr. Akakaribia na kumwamkia maamkuzi ya kijahili: Mtume (SAW) akamwambia: Mwenyezi Mungu ametubadilishia maamkuzi sisi na ametupa maamkuzi bora nayo ni Salam. Kisha akamuuliza: Nini kilichokuleta ewe Umeyr? Akasema: Nimekuja kwa ajili ya mateka ambaye yuko kwenu, basi mfanyieni hisani. Mtume (SAW) akasema: Basi upanga wa nini? Akasema: Mwenyezi Mungu azilaani panga kwani zilitufaa nini? Mtume (SAW) akamwambia: Niambie kweli ulilolijia. Akasema: Sikuja isipokuwa kwa hilo. Mtume (SAW) akamwambia: Si kweli, kwani ulikaa na Safwan na kusema kadha wa kadha. Umeyr akasema: Ninashuhudia kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Tulikuwa tukikukadhibisha kwa yale uliyokuwa ukija nayo kwetu ya habari za mbinguni, na wahyi uliokuwa ukiteremshiwa, na jambo hili hakulihudhuria mtu isipokuwa mimi na Safwan, basi wallahi mimi ninajua kuwa hapana aliykuletea jambo hili isipokuwa Mwenyezi Mungu, na ninamsifu Mwenyezi Mungu kwa kunihidi kwenye Uislamu, na kunileta hapa. Basi Mtume (SAW) akasema: Mfundisheni ndugu yenu dini yake, na msomesheni Qurani, na muachieni huru mfungwa wake. Umeyr akarudi Makka na akawa Muislamu mzuri na akasilimisha watu wengi.
|
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|