|
Muhtasari: Kuhusu Mtume Muhammad (SAW). Maumbile yake: Kama tunavyojua, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa mbora wa viumbe vyote kwa tabia na maumbile, mtukufu katika Mitume na Manabii, na kipenzi cha Mola wake. Maumbile yake kama tunavyoelezwa na wale waliomuona na kuishi naye ni kama yafuatavyo, nayo ni mkusanyiko wa sifa mbali mbali ambazo zimekusanywa kutokana na hadithi za Anas bin Malik, mtumishi wa Mtume (SAW) ambaye ameishi naye miaka kumi, na Ali bin Abi Talib, binamu yake ambaye amelelewa na Mtume (SAW) mwenyewe, na Al-Hasan bin Ali, mjukuu wake Mtume (SAW)). Kutokana na hadithi zao, tutaeleza kwa ufupi maumbile yake Mtume Muhammad (SAW). Alikuwa Mtume (SAW) mzuri sana wa sura. Uso wake ulikuwa wa duwara, na ulikuwa na nuru kama mba la mwezi unapokamilika na kipaji chake kilikuwa kipana na macho yake yalikuwa makubwa na kama ambayo yametiwa wanja, na mboni za macho yake zilikuwa ni nyeusi sana na nyeupe yake ilikuwa imeingiliwa na wekundu wa mbali, na kope zake zilikuwa ndefu, na nyusi zake zilikuwa ni nyingi na ndefu na zimechongeka na kupindika uzuri na zinakaribia kukutana lakini hazikuungana. Pua yake ikionyesha kama ilionyoka moja kwa moja lakini ilikuwa imepinda kidogo kwa katikati na kunyoka uzuri kwenye ncha yake, na mdomo wake ulikuwa mkubwa, na meno yake yalikuwa meupe sana yenye mngaro na mwanya katikati yake, na mashavu yake yalikuwa ni laini, na ndevu zake zilikuwa nyingi. Alikuwa na kichwa kikubwa na nywele nyingi zilizokuwa nyeusi sana, si singa iliyonyoka wala si koto iliyotatizika, lakini zilikuwa za mawimbi zenye mapindi-pindi na zikifika mpaka baina ya masikio yake na mabega yake, na alikuwa akizichana kuzipelekea nyuma kwanza kisha akawa anapasua njia katikati baadaye. Hazikushika mvi nywele zake mpaka utuuzimani akawa ana mvi kidogo katika nywele zake na ndevu zake, na amekufa hanaisipokuwa nywele kidogo za mvi. Mwili wake haukuwa mkubwa sana, maana hakuwa mrefu wala mfupi bali wastani, si mnene wala si mwembamba, bali ni mwenye umbo zuri, shingo yake ilikuwa ndefu iliyonyoka, na kifua chake na maungo yake yalikuwa mapana, hakuwa na tumbo kubwa, bali tumbo lake na kifua chake vilikuwa mfuto mmoja, sehemu ya juu ya kifua chake kilikuwa na nywele lakini chini yake kuanzia maziwani mpaka tumboni kwake alikuwa hana nywele isipokuwa ufito wa nywele hafifu kuanzia kati ya kifua mpaka kitovuni, na kwenye mgongo wake baina ya mabega yake mawili kulikuwa na mkusanyiko wa nywele ukubwa wa yai la njiwa nao ni muhuri wa utume. Kiwiliwili chake kilikuwa kina nguvu sana maana viungo vyake vyote vilikuwa na mafupa mapana. Mikono yake ilikuwa imenyoka uzuri na ina malaika kuanzia mabegani mpaka kwenye dhiraa, na viganja vya mikono yake vilikuwa vikubwa na laini, na vidole vyake nchani vilikuwa vyembamba na miguu yake ilikuwa mizuri iliyonyoka na kulingana na kiwiliwili chake na visigino vyake vilikuwa havina nyama na nyayo zake zilikuwa kubwa na ngumu na zina mvungu mkubwa na vidole vya miguu yake vilikuwa vimenyoka. Rangi yake ilikuwa si nyeusi wala si nyeupe ya kuparara, lakini alikuwa mweupe aliyevilia wekundu inakaribia rangi ya wardi, akifurahi uso wake huzidi nuru, na akihamaki uso wake huvilia damu, na mshipa ulioko kwenye kipaji chake humsimama. Alikuwa hahamaki kwa ajili ya nafsi yake au kwa ajili ya mambo ya kidunia, bali alikuwa akihamaki kwa ajili ya haki na mambo ya Mwenyezi Mungu na alikuwa akimgeuza uso yule anayemhamakia au kumpa mgongo. Alikuwa mara nyingi kucheka kwake ni kutabasamu tu na akitabasamu meno yake hutoa kama mwanga kwa weupe wake, na kufurahi kwake ni kidogo na akifurahi huinamisha macho yake chini, kwani mara nyingi alikuwa katika huzuni na mawazo, hana raha na akikaa kimya muda mkubwa hazungumzi ila kwa haja, na huanza na kumaliza maneno yake kwa jina la Mwenyezi Mungu, na maneno yake yalikuwa ni kidogo yaliyojaa hekima, hayana ziada wala nuksani, si mabaya wala ya kuudhi, daima ni mazuri na yenye faida. Sauti yake ilikuwa kali na yenye nguvu, na akizungumza huzidi kuwa mzuri na akinyamaza huzidi haiba na utulivu, na akiashiria huashiria kwa mkono wake mzima, na akistaajabishwa na jambo huupindua mkono wake, na akizungumza huukutanisha mkono wake wa kulia na wa kushoto na kukishika kidole chake cha gumba cha mkono wa kushoto. Alikuwa mzuri wa sura na umbo, msafi sana wa kiwiliwili na nguo zake, daima akinukia uzuri na harufu yake ni nzuri kuliko harufu ya miski na ambari, na akipita njia huacha nyuma harufu yake anayekuja nyuma yake akajua kuwa Mtume (SAW) amepita hapa. Akitembea hutembea kwa hatua thabiti na kwa kasi kama kwamba anateremka kilima, na mwendo wake ulikuwa wa haraka haraka kama kwamba ardhi inajikunja chini yake na yeyote mwenye kufuatana naye huchoka, lakini yeye hapati taabu wala hachoki. Alikuwa Mtume (SAW) mbora wa wanadamu na mwenye kujawa na utulivu ukimwona kwa mbali, na alikuwa mzuri wao ukimwona kwa karibu. Mwenye kumuona kwa ghafla huingiwa na kicho, na mwenye kuishi naye na kumjua humpenda. Hapana kiumbe bora na mzuri kuliko yeye. Rehema na amani ya Mwenyezi Mungu imshukie. Tabia zake: Mwenyezi Mungu aliyetukuka amemsifu mja na Mtume wake (SAW) kuwa ni mwenye tabia njema zilioje, akasema: Q.68:4 Hii ni kuonyesha kuwa Mtume Muhammad (SAW) amesifika kwa tabia njema na adabu nzuri na akhlaki bora kuliko viumbe vyote ulimwenguni, na yote ni kwa sababu yeye ameletwa awe mfano bora na ruwaza njema kwa wanadamu wote, akasema Mola wake aliyetakasika na kila nuksani na kusifika kwa kila sifa njema: Q.33:21 Kwa sababu hii, Mtume Muhammad (SAW) alikuwa ni mtu mtulivu na mpole, mnyenyekevu na mwingi wa haya, karimu na mwingi wa hisani. Alikuwa ni mtu shujaa na mwingi wa subira, mkweli na muaminifu, mpigania haki na muadilifu, na alikuwa mrehemevu na mwingi wa huruma. Mwenyezi Mungu akamsifu kwa kauli yake: Q.3:159; 21:107 Aidha, Aisha alimsifu mumewe na kusema kuwa zilikuwa akhlaki za Mtume (SAW) kama alivyosifiwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe ndani ya Qurani Tukufu kuwa alikuwa na akhlaki njema kabisa, naye daima alikuwa akifuata mwenendo na tabia za Mola wake ambazo zilikuwa hazina upungufu, kwani yeye alikuwa mnyenyekevu hana kiburi, akiwatembelea wagonjwa na kuhudhuria mazishi na kuzuru makaburi na kuitika mwaliko akialikwa. Alikuwa akipenda maskini na kuwasaidia wenye haja na mafakiri, na mtu yeyote akimuomba humpa anachotaka akiwa nacho au humpa maneno mazuri akiwa hana. Akiwasalimia matajiri na maskini wote sawasawa, na kuanza yeye kuwaamkia na kuwapa mkono, na akimpa mtu mkono hawi wa kwanza kuutoa mkono wake mpaka yule mtu autowe wake, wala hawi wa kwanza kuondoka mpaka aondoke yule mwenzake, na alikuwa akikutana na mtu huanza yeye kutoa salamu, na hukaa pale ambapo watu wamemalizikia sio katikati yao, na huzungumza na kila mmoja na kuwashughulikia wote waliohudhuria, na akizungumza na mtu hamkatizi maneno yake mpaka amalize kusema. Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa hamfanyii mtu uadui, wala akifanyiwa ubaya harudishi ubaya, bali alikuwa akimtendea wema na kumfanyia hisani yule anayemfanyia uovu. Maneno yake yalikuwa ni ya faida na ya hekima na ya busara, na alikuwa hasemi maneno mabaya na machafu, na hazui uwongo hata kwa maskhara. Alikuwa haogopi lawama ya mtu yeyote katika kusema haki, na wala hasemi isipokuwa haki akiwa radhi au amehamaki. Daima alikuwa ni mwenye bashasha, mwepesi kuingiliana na watu, hana hasira za upuuzi wala si mkorofi. Hapendi kupiga kelele wala kutukana watu wala kulaumu mtu. Hampi mtu sifa asiyokuwa nayo wala hamtii aibu. Hazungumzi isipokuwa kuhusu yale ambayo anahisi yatampatia thawabu, na hajishughulishi na mambo yasiyomhusu. Chakula akikipenda hukila na akiwa hakipendi hukiacha bila kukitia ila. Akiitukuza sana neema hata ikiwa ndogo na kuitaja kwa watu. Ameepukana na kiburi na ria hafanyi jambo kwa kujionyesha bali hufanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa kutaka radhi zake. Akiwasaidia wakeze nyumbani kwake na kufanya kazi za nyumbani, akishona kiatu chake na nguo yake, na kukama mbuzi wake maziwa, na kujitumikia nafsi yake. Alikuwa akiishi kwa wema na wakeze na wanawe na watumishi na watumwa wake, na alikuwa hawatukani wala kuwalaumu watumishi na watumwa wake wakikosea jambo. Naye akisema kuwaambia masahaba zake: Mbora katika nyinyi ni yule aliye bora kwa ahli yake na mimi ni mbora wenu kwa ahli yangu. Alikuwa daima akiwapitia masahaba zake na kuwauliza na kuuliza hali zao na kukaa na watu kwa wema bila kujitafautisha nao. Akiwaheshimu watu wote na kuwatanguliza wale wenye kuheshimiwa na watu wao na kuwapa ukubwa juu yao. Mambo yake yote yalikuwa wastani. Akipenda haki na kuipigania na kumpenda mwenye kupigania haki, na mbora kwake ni yule mwenye kuwanasihi wenzake zaidi na kuwasaidia na kumcha Mola wake. Alikuwa mfano mzuri na ruwaza njema na mithali kubwa kwa wanadamu wote, maana aliweka mifano chungu nzima katika maisha yake kwa wanadamu kuigiza. Alikuwa imamu wa wacha Mungu, amirijeshi shujaa na kiongozi bora, baba mwema na mume mzuri, rafiki mpenzi na jirani mwema, mfanyibiashara muaminifu na hakimu muadilifu, mwalimu mzuri na mwenye kumcha Mola wake katika kila hali. Mpole kwa watu wake, karimu kwa wa karibu na wa mbali, mwingi wa subra na mstahmilivu. Akasema Mtume (SAW) kujieleza nafsi yake: Amenifunza Mola wangu adabu, akanifundisha vyema adabu. Rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie mja wake na kipenzi chake Muhammad, mbora wa wanadamu wote, amin. Waliokuwa wakishabihiana na Mtume (SAW). Katika watu ambao wamefanana na Mtume (SAW) kimaumbile ni hawa:
Al-Hasan bin Ali bin Abi Talib, mjukuu wake mtoto
wa Fatma Wazazi wake: Baba na mama wa Mtume (SAW) walikuwa ni watu watukufu waliotokana na koo tukufu za Makka, kwani wote wawili walikuwa ni Makureshi, na wanakutana kwa babu yao aitwaye Kilaab.
1. Babake
akiitwa Abdullahi bin AbdulMuttalib bin Hashim bin Abdi Manaf bin Qusay
bin Kilaab. Amekufa akiwa Wazee wake wa kunyonyesha: Waarabu walikuwa na desturi wakishawazaa watoto wao huwatoa kwa wanawake wanaoishi jangwani ili wawanyonyeshe na wawalee katika hali ya hewa safi wapate kuinukia wakiwa na nguvu. Kwa hivyo, Mtume (SAW) alinyonyeshwa na mamake Aamina muda mdogo tu, kisha akaja Halima As-Saadia na kumchukuwa kwenda kumnyonyesha huko Ubeduini.
1.
Mamake wa kumnyonyesha ni Halima bint Abi Zuayb
Al-Harith bin Abdillahi AsSaadia na mumewe ni Al-Harith bin
2.
Mamake mwengine aliyemnyonyesha baada ya kunyonyesha na
mamake mzazi na kabla ya kuchukuliwa na Halima ni Ami zake: AbdulMuttalib babu yake Mtume (SAW) alioa wake wengi na akapata kutokana na wake hao watoto chungu nzima, mmoja wao akiwa ni Abdullahi babake Mtume (SAW). Ndugu zake Abdullahi kwa baba walikuwa ni:
Mashangazi zake: Mashangazi wa Mtume (SAW) ni hawa wafuatao:
Wajomba zake: Katika wajomba zake Mtume (SAW) ndugu wa mamake ni Abd Yaghuth na Al-Aswad na vile vile Saad bin Abi Waqaas ambaye alikuwa Mtume (SAW) akijifakhirisha naye kwa kusema huyu mjomba wangu na nani mwenye mjomba kama wangu. Nduguze wa kunyonya: Kwa kuwa Mtume (SAW) alinyonyeshwa na Halima na Thuwayba, alikuwa na ndugu wa kunyonya huku na huku: Nduguze kwa Halima ni hawa watoto wa Halima wafuatao:
Nduguze kwa Thuwayba ni hawa wafuatao, ambao walinyonya kwa huyu bibi:
Binamu zake: Mtume (SAW) alikuwa na binamu wengi, kwani ami zake walikuwa wengi vile vile, na katika hao ni: Ali na Jaafar na A'qiyl na Talib watoto wa Abu Talib, na Abdullahi na Qutham na Al-Fadhl watoto wa Al-Abbas, na Abu Sufyan na Nawfal na Rabi'a watoto wa Al-Harith, na Abdullahi mtoto wa Zubeyr, na Hind mtoto wa Qutham, na Ammara mtoto wa Hamza, na Murra mtoto wa Hajal, na Utba mtoto wa Abi Lahab. Binamu zake Mtume (SAW)
Watoto wa shangazi zake wa kiume: Katika watoto wa mashangazi zake wa kiume ni Ubeydillah na A'mir watoto wa Umayma na Abu Salama na Tuleyb na Abdullahi, na Az-Zubeyr mtoto wa Safia. Watoto wa shangazi zake wa kike: Katika watoto wa kike wa shangazi zake aliyekuwa mashuhuri sana ni Zaynab bint Jahsh ambaye ni mtoto wa shangazi lake Umayma, naye aliolewa na Zayd bin Haritha mtoto wa Mtume (SAW) wa kulea ambaye alimpa jina lake na kumwita Zayd bin Muhammad kisha Mwenyezi Mungu akalikataza jambo hili na kuiondoa ada hii kwa kumwambia Mtume (SAW) amuoe huyu Zaynab na kuwa ndiye mke ambaye Mtume (SAW) aliamrishwa na Mwenyezi Mungu amuoe ndani ya Qurani. Watoto wengine wa kike wa Umayma ni Umm Habiba na Jamna. Wake zake (SAW) : Mtume (SAW) alioa wake kumi na moja, nao ni Khadija bint Khuwaylid na Sauda bint Zam'a na Aisha bint Abubakar Assiddiq na Hafsa bint Umar bin Al-Khattab na Zaynab bint Khuzayma (Ummul-Masakiin) na Hind (Ummu Salama) na Zaynab bint Jahsh (bint wa shangazi lake Umayma) na Juwayria bint Al-Harith na Safiya bint Huyay na Ramla (Umm Habiba) bint Abu Sufyan na Maymuna bint Al-Harith. Katika hawa sita walikuwa ni Makureshi, mmoja alikuwa ni mwanamke wa Kiyahudi, na wengine wanawake wa makabila mengine ya Kiarabu. Wawili walikufa akiwa Mtume (SAW) bado yu hai, nao ni Khadija na Zaynab bint Khuzayma, na tisa walimkalia eda. 1- Khadija bint Khuwaylid aliolewa na Mtume (SAW) akiwa na umri wa miaka arubaini na Mtume (SAW) miaka ishirini na tano. Alikuwa ndiye mke wa kwanza kwa Mtume (SAW), lakini yeye alikuwa keshaolewa mara mbili, mara ya kwanza na Abu Hala na akazaa naye mtoto wa kiume aitwaye Hind, kisha akaolewa na U'tayyiq na kuzaa naye mtoto wa kike aitwaye Hind vile vile. Ameishi Mtume (SAW) na Khadija miaka ishirini na tano, na akafariki akiwa na umri wa miaka sitini na tano kabla ya kuhamia Mtume (SAW) Madina kwa miaka mitatu. Amezaa na Mtume (SAW) watoto sita isipokuwa mmoja tu ambaye amezaliwa na Maria suriya wake. Alipokuwa na Khadija alikuwa hana mke mwengine na aliishi naye peke yake na kutuwachia mfano wa vipi mtu anaishi na mke mmoja peke yake, kisha alipokufa alioa wake wengi na kutuwachia mfano wa vipi mtu anaishi akiwa na wake wengi. Khadija alikuwa bibi mtukufu wa kikureshi na alisimama na Mtume (SAW) kwa hali na mali na hapana mke aliyekuwa akimuenzi zaidi kuliko bibi huyu. Mtume (SAW) alisema: Mabibi wa wanawake wa watu wa Peponi ni Maryam kisha Fatma kisha Khadija kisha Asiya. 2- Sauda bint Zam'a ni mke wa pili baada ya kufa Khadija, naye alikuwa kwanza ameolewa na Sakraan Al-Aamiri na wakahamia Habasha, kisha alipokufa mumewe akaolewa na Mtume (SAW) katika mwezi wa Ramadhani mwaka wa kumi baada ya kupewa utume akiwa bado yuko Makka, na akaishi naye na kumkalia eda Mtume (SAW) na kufariki mwaka wa 54 wa Hijra katika Ukhalifa wa Umar bin Al-Khattab. Alikuwa Sauda bibi mtukufu wa kikureshi na katika waliosilimu mwanzo mwanzo pamoja na mumewe Sakran, kisha wakaondoka kwenda Habasha yalipozidi mateso ya Washirikina juu ya Waislamu na kukaa muda mkubwa huko, kisha wakarudi Makka na akafariki mumewe hapo. Wakati huu alikuwa Mtume (SAW) amefiliwa na mkewe Khadija, basi akaja Khawla bint Hakim na kumuuliza kama anataka kuoa. Mtume (SAW) alipomuuliza ni nani huyo mke, alimjibu kama anataka mke aliyekwisha kuolewa basi ni Sauda, na kama anataka bikra basi ni Aisha. Kwa hivyo, akakubali na akamuoa Sauda na kumposa Aisha maana alikuwa bado mdogo. Alikuwa Sauda mtu mzima sana na kwa hivyo aliitoa siku yake kumpa Aisha na kumfurahisha Mtume (SAW) alipojiona keshakonga na kwa hivyo alikuwa akipendwa sana na Aisha. 3- Aisha bint Abibakar: Aliposwa na Mtume (SAW) baada ya kufa Khadija kwa miaka mitatu kabla ya kuhamia Madina, naye wakati huo alikuwa na umri wa miaka sita, kisha alipohamia Mtume (SAW) Madina, akiwa Aisha ameshatimia miaka tisa na keshabaleghe, alikuja Abubakar na mwanawe Aisha na kumkabidhi Mtume (SAW) mkewe. Wakati huu Mtume (SAW) alikuwa na umri wa miaka hamsini na nne. Mtume (SAW) aliishi na Aisha kwa muda wa miaka tisa, na alipofariki dunia Mtume (SAW) alikuwa Aisha ni mwenye umri wa miaka kumi na nane, naye alifariki katika mwezi wa Ramadhani na kuzikwa Al-Baqi'u huko Madina akiwa na umri wa miaka sitini na sita. Hakuoa Mtume (SAW) mwanamke mwengine aliyekuwa bikra isipokuwa huyu, na alikuwa akimpenda sana kwa kupenda kwake dini na kwa kufahamu kwake Qurani na Sunna na Fiqhi, na kwa kuwa ni binti wa sahibu yake mpenzi. Aisha alipokea Hadithi nyingi na alikuwa mwanachuoni mkubwa wa kujua mambo mengi ya dini hata masahaba walikuwa wakichukuwa elimu kutoka kwake. 4- Hafsa bint Umar bin Al-Khattab: aliolewa na Mtume (SAW) baada ya kufa mumewe Khuneys katika vita vya Badr, alikwenda babake Umar kwa Uthman kumtaka amuoe mwanawe akiwa wakati huo amefiliwa na mkewe Ruqayya akakataa. Basi akatoka na kwenda kwa Abubakar kumtaka yeye amuoe mwanawe, na yeye alinyamaza kimya wala hakumjibu kitu, basi hili likamkasirisha sana Umar na kwenda kwa Mtume kumshtakia. Mtume (SAW) akamwambia: Huenda Mwenyezi Mungu akamruzuku Uthman aliye bora kuliko Hafsa na akamruzuku Hafsa aliye bora kuliko Uthman. Basi Mtume (SAW) akamuoa Hafsa na akamuozesha Uthman binti yake Umm Kulthum. Hafsa alikuwa mdogo wa Mtume kwa miaka thalathini na tano (35) maana alizaliwa kabla ya Mtume (SAW) kupewa Utume kwa miaka mitano na wakati huo Mtume (SAW) alikuwa na umri wa miaka thalathini na tano. Mtume (SAW) alimuoa Hafsa mwaka wa tatu baada ya Hijra na wakati huo alikuwa Hafsa keshapindukia umri wa miaka ishirini. Alikuwa akisifika kwa kusali sana na kufunga sana na alikuwa ni mwanamke mwenye akili na hodari wa kuhifadhi Aya za Qurani na Hadithi za Mtume (SAW), naye ndiye aliyepata sharafu ya kukabidhiwa msahafu wa kwanza na babake Umar tangu Ukhalifa wa Abubakar baada ya kumalizika kuandikwa na Zayd bin Thabit, na kuuweka mpaka Ukhalifa wa Uthman bin Affan ndipo alipouchukuwa kuandika nakala nyengine kutokana na msahafu huo na kuzitawanya miji mbali mbali ya kiislamu. Alifariki Hafsa katika mwezi wa Shaaban mwaka wa 45 baada ya Hijra akiwa ameshatimia umri wa miaka sitini na kuzikwa Al-Baqi'u hapo Madina. 5- Zaynab bint Khuzayma (Ummul-Masakiin): Kabla ya kuolewa na Mtume (SAW) alikuwa kaolewa na Abdullahi bin Jahsh, na baada ya kufa katika vita vya Uhud, Mtume (SAW) alimuoa yeye katika mwaka wa nne wa Hijra. Hakuishi sana na Mtume (SAW) kwani alifariki muda mdogo tu baada ya kuolewa na Mtume (SAW), na yeye na Khadija katika wakeze Mtume (SAW) ndiyo waliomtangulia na wengineo waliobakia 9 walimkalia eda. Alikuwa ni mwanamke mwema sana na akipenda kusaidia maskini mpaka akapewa jina la mama wa maskini (ummul-masakiin). 6- (Ummu Salama) Hind bint Abi Umayya: Mumewe kabla ya kuolewa na Mtume (SAW) ni Abu Salama Abdullahi bin Abdul Asad, naye alinyonya pamoja na Mtume, na kwa hivyo ni nduguye wa kunyonya. Alipofariki Abu Salama (RA) kwa majeraha aliyoyapata katika vita vya Uhud, Mtume (SAW) alimposa na kumuoa. Ummu Salama pamoja na mumewe ni katika watu wa kwanza waliosilimu hapo Makka, na kwa sababu ya mateso makubwa ya makafiri wa Makka, iliwabidi wahamie Habasha pamoja na kundi la mwanzo lililohamia huko. Baadaye walirudi Makka lakini walikuta mambo yako vile vile na kwa hivyo, Mtume (SAW) akawaamrisha wahamie Madina, lakini njiani alizuiliwa na kabila lake la Bani Makhzumi na kuwekwa mbali na mumewe na kuwachwa mumewe ende Madina. Wakati huo huo lilikuja kabila la mumewe wakamnyang'anya mtoto wake na akawa yuko peke yake. Ummu Salama aliishi mbali na mumewe na mwanawe karibu mwaka mzima, kisha baada ya mtu katika kabila la Banu Umayya kuzungumza na watu wake, walimpa ruhusa kwenda kujiunga na mumewe. Watu wengine vile vile wakatoka kwenda kuzungumza na watu wa kabila la mume wangu na wao wakakubali kumrudishia mwanawe, ndipo alipofanya safari peke yake kuelekea Madina. Njiani katika sehemu inayoitwa Taniim kiasi meli 3 kutoka Makka akakutana na Uthman bin Talha ambaye bado alikuwa si Muislamu, akamsaidia kumuongoza katika safari yake kwenda Madina. Alipofika kijiji karibu na Qubaa kiasi meli 2 kufika Madina, alimwacha hapo maana ndipo alipo mumewe, na kurudi zake. Ummu Salama alikutana na mumewe na kuishi naye Madina pamoja na jamii ya kiislamu. Alishiriki katika vita vya Badr, na vita vya Uhud na mashambulizi mengine dhidi ya Banu Abdul Asad ambayo alishiriki katika vita hivi na kujeruhiwa. Alimuuguza mumewe mpaka siku moja akaja Mtume (SAW) kumuangalia na kukaa naye kwa muda mrefu kidogo. Kisha Abu Salama akafariki dunia. Baada ya kumaliza eda, alikuja Abubakar kumposa na kadhalika Umar, lakini alikataa. Kisha akaja Mtume (SAW) kumposa, naye akamwambia kuwa yeye ni mtu mzima, ana wivu sana na ana watoto wengi. Mtume (SAW) alimwambia kuwa kuhusu wivu wake atamwombea Mungu amuondoshee, na kwa kuwa ni mtu mzima, yeye ni mtu mzima zaidi, na kuhusu watoto wako, wao wana Mwenyezi Mungu na Mtumewe. Basi Ummu Salama akakubali kuolewa na Mtume (SAW) katika mwezi wa Shawwal mwaka wa 4 wa Hijra, akiwa na umri wa miaka 29. Aliishi naye kwa wema na hisani na kuishi kwa ucha Mungu na kuhifadhi Qurani nzima kama Aisha na Hafsa. Yeye ni katika wake waliomuona Jibril alipokuja kwa Mtume (SAW) kwa sura ya Dihya al Kalbi kuonyesha cheo chake kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Mara nyingi Mtume (SAW) alikuwa akimchukuwa katika safari zake, na kwa hivyo alihudhuria Hudaybiya na Khaybar na ilipotekwa Makka, na Taif na vita vyenginevyo dhidi ya Hawazin na Thaqif. Aidha, alikuwa naye katika Hija yake ya mwisho. Alikuwa na watoto wanne: Salama, Umar, Zaynab na Durra. Aliishi na Mtume (SAW) kwa muda wa miaka 7 mpaka alipofariki dunia katika mwaka wa 10 wa Hijra. Aliendelea kuishi muda mkubwa baada ya kufa Mtume (SAW) mpaka mwaka wa 61 wa Hijra, akiwa na umri wa miaka 84. Alisaliwa na Abu Hureira na kuzikwa. 7- Zaynab bint Jahsh (bint wa shangazi lake Umayma): Alikuwa mwanzo ameolewa na Zayd bin Al Haritha, huru na mtoto wa kulea wa Mtume (SAW), na juu ya kuwa Zainab hakutaka kuolewa na Zayd kwa sababu ya kuwa alikuwa mtumwa, Mwenyezi Mungu aliamrisha akubali ndoa hiyo kwa hekima yake aliyotaka kuipitisha, kwani hapo mwanzo ilikuwa Waarabu hawawezi kuoa wake wa watoto wao wa kulea, kwa kuchukulia kuwa ni kama watoto wao hasa, lakini Mwenyezi Mungu alipotaka kuibatilisha hukumu hii ya kijahili, na kuweka Sharia yake, alimuamrisha Zainab akubali ndoa hii, kisha kwa namna ya maisha baina yake na Zayd yalivyokwenda ilimbidi asiweze kuishi naye, na mwishowe ikalazimu amwache na Mtume (SAW) amuoe yeye Zainab kuweka hukumu na sharia mpya. 8- Juwayria bint Al-Harith: Ni mtoto wa Al Harith, mkubwa wa kabila la Banu Mustaliq. Alikuwa katika mateka wa vita baina ya Waislamu na Banu Mustaliq, na alipokwenda kumuona Mtume kuhusu mas-ala ya kujikomboa, Mtume (SAW) akamwambia: "Sikuambii lililokuwa bora kuliko hilo?" Basi akamchukuwa yeye na kumuoa katika mwaka wa 6 H, mwezi wa Shaabani, akiwa Mtume (SAW) ni mwenye umri wa miaka 58 na yeye akiwa na miaka 20 muda mdogo tu baada ya kuolewa Zaynab bint Jahsh. Baada ya kumuoa Juwayria, Mtume (SAW) aliruwadishia Banu Mustaliq ghanima (ngawira) zao zote na kuwawacha mateka wao, na kwa hivyo ikalifanya kabila lote kusilimu. Kwa hivyo, Juwayria alikuwa ni mke wa baraka kubwa kwa watu wake. Baada ya Mtume (SAW) kumuoa alimbadilisha jina, kwani jina lake lilikuwa Barra kabla ya kumuoa. Mtume akamwita Juwayria. 9- (Umm Habiba) Ramla bint Abu Sufyan: Aliolewa mwanzo na Abdullahi bin Jahsh na kuhama naye kwenda Habasha pamoja na Waislamu wengine kukimbia mateso ya makafiri wa Makka. Huko mume akaingia kwenye dini ya kinasara na kuishi huko mpaka kufa kwake, lakini Ramla alibakia katika Uislamu na kuishi huko mpaka Mtume (SAW) alipompeleka Amr bin Umayya na risala kwa mfalme wa huko Najashi, na akamwandikia kutaka kumuoa Ramla. Basi akamuoza na kumpa mahari yake 400 dinari za dhahabu. Umm Habiba alibakia huko Habasha miaka sita mengine mpaka Waislamu walipoweza kurudi Madina na kukutana na Mtume (SAW) katika mwaka wa 7 H. Wakati huu Mtume (SAW) alikuwa na miaka 60 na Umm Habiba miaka 35. Umm Habiba aliishi miaka 4 na Mtume (SAW) mpaka alipofariki na kumkalia eda. Kisha aliishi miaka 33 mengine baada ya kufa Mtume (SAW), akiwa na umri wa miaka 72 katika mwaka 44 H. Alikuwa ni bibi mcha Mungu. 10- Safiya bint Huyay alikuwa ni mwanamke mtukufu wa kabila la kiyahudi la Bani Nadhir. Aliolewa na Mtume (SAW) baada ya kushindwa kabila lake katika vita vya Khaybar baina yao na Waislamu, na kuuliwa mumewe katika vita hivyo, na kuchukuliwa mateka. Mtume (SAW) akamchukuwa yeye na kumtaka aingie katika Uislamu. Aliposilimu alimwacha huru na kumuoa yeye, na kujaaliya mahari yake kuwa ni kule kuwachwa kwake huru. Mtume (SAW) alipomuoa Safiya katika mwaka wa 7 H, umri wake ulikuwa ni miaka 60, na yeye ni mwenye umri wa miaka 17. Safiya unarudi ukoo wake kwa Harun na Musa (AS), na babake alikuwa ndiye mkubwa wa kabila la Bani Nadhir. Safiya aliishi na Mtume (SAW) kwa muda wa miaka 4. Alipofariki Mtume (SAW) alikuwa Safiya ana miaka 21 tu, na aliishi bila ya kuolewa kwa muda wa miaka 39 mengine. Alifariki akiwa na umri wa miaka 60 katika mwaka 50 H. 11- Maymuna bint Al-Harith: Barra, kama alivyokuwa akijulikana mwanzo, alikuwa ni ndugu wa Lubaba (Ummul-Fadhl) mke wa ami yake Mtume (SAW) Al Abbas. Aidha, katika ndugu zake wengine ni Zainab bint Khuzayma, na Asmaa bint Umays, na kwa hivyo alikuwa na uhusiano na Mtume (SAW). Aliolewa na Mtume (SAW) katika mwaka wa 7 H, akiwa Mtume (SAW) ana umri wa miaka 60 na yeye akiwa na umri wa miaka 36. Baada ya kufa Mtume (SAW), Maymuna aliendelea kuishi Madina kwa muda wa miaka 40 mengine. Alifariki akiwa na umri wa miaka 80 katika mwaka 51 H, akiwa ni mke wa mwisho wa Mtume (SAW) kufariki dunia. Aliusia azikwe Saraf, pale ambapo Mtume (SAW) alimuoa. Suriya zake: Maria al-Qiptiya pamoja na nduguye Sirin walikuwa ni wanawake alioletewa zawadi Mtume (SAW) kutoka kwa Muqawqis, mfalme wa Misri. Alifika Madina baada ya Mtume (SAW) kurudi kutoka kufanya mkataba wa Hudaybiah. Alimweka Maria na kumtoa Sirin kwa mshairi wake Hassan bin Thabit. Aliishi na Mtume (SAW) na kumzalia mtoto mmoja wa kiume Ibrahim, lakini mtoto hakuishi sana, maana alifariki akiwa bado mdogo. Aidha, Mtume (SAW) alikuwa na suriya mwengine akiitwa Rayhana. Watoto wake (SAW): Mtume (SAW) hakupata watoto kutokana na wakeze wote isipokuwa Khadija bint Khuwaylid (RA), naye alizaa naye watoto sita: Zeinab, Ruqayya, Umm Kulthum, Fatima, Al-Qassim, Abdallah (Attayyib, Attahir). Aidha, kutokana na masuriya wake, alipata mtoto kutokana na Maria Al-Qiptiya, naye ni mwana wa kiume mmoja Ibrahim. Katika watoto wake hawa, wa kiume wote walifariki wakiwa bado wadogo, nayo ni dalili moja ya kuwa hakuna Mtume atakayekuja baada yake, kwani mara nyingi utume ulikuwa ukiendelezwa kutokana na kizazi kimoja cha Mitume, kama tunavyoona katika kizazi cha Nabii Ibrahim (AS). Ama watoto wa kike ambao hawaendelezi ukoo, walibakia kuwa wakubwa na kuolewa na kuzaa watoto chungu nzima. Watoto wa Mtume (SAW)
Al-Qasim: Mtoto wa kwanza wa kiume wa Mtume (SAW) alikuwa ni Al-Qasim, naye alizaliwa kabla ya Mtume Muhammad (SAW) kupewa utume kwa miaka 11, akiwa Mtume (SAW) ana miaka 29, na kwa kuwa ni desturi ya Waarabu kumpa mtu jina la yule mtoto mkubwa, kwa hivyo Mtume (SAW) alikuwa akijulikana kwa jina la Abul-Qasim, jina ambalo akilipenda sana na Masahaba zake wakipenda kumuita kwa jina hili. Kwa mujibu wa Ibn Saad, Al-Qasim alilelewa na kufikia umri wa miaka 2 kisha akafariki dunia. Na ijapokuwa Ibn Faris anaongeza kusema kuwa pengine alifikia umri wa kuweza kutambua mambo, Al Qasim alifariki dunia kabla ya Mtume (SAW) kupewa utume. Mtume (SAW) alimpenda sana mwanawe huyu, lakini Mwenyezi Mungu ana hekima yake katika kumchukuwa mja wake huyu, kwani mara nyingi utume hupokewa na kizazi chake, na kwa hivyo kufa Al-Qasim ni ishara moja ya kuwa hapatokuwa na Mtume baada ya Muhammad (SAW). Zainab (RA): Mtoto wa pili kuzaliwa wa Mtume Muhammad (SAW) ni Zainab, naye alizaliwa miaka 10 kabla ya Mtume (SAW) kupewa utume, akiwa Mtume Muhammad (SAW) ana umri wa miaka 30. Zainab aliishi kuwa mkubwa na kuolewa na binamu yake Abul A'as. Ulipokuja Uislamu na Zainab akasilimu, mumewe alikataa kumfuata kwenye dini hii mpya, na juu ya kuwa makafiri walimshikilia amwache Zainab, Abul A'as alikataa. Zainab alihama na kwenda Madina na kumwacha mumewe Makka. Katika vita baina ya Waislamu na makafiri wa Makka, Abul A'as alikamatwa, lakini Zainab alimpa himaya, na akapeleka kidani chake kumkomboa. Abul A'as baadaye alisilimu na kuishi na mkewe Zainab, na walikuwa na watoto wawili, wa kiume aliyekuwa akiitwa Ali na wa kike aliyekuwa akiitwa Umamah. Huyu Umamah baada ya kufa Fatima (RA), mke wa Ali bin Abi Talib, aliolewa na Ali (RA) kutokana na wasia wa mwenyewe Fatima kuwa akifa amuowe Umamah, basi alimuoa na kuishi naye kwa wema na hisani. Zainab aliishi kufikia umri wa miaka 20 na kitu, alifariki katika mwaka wa 8 wa Hijrah. Mtume (SAW) alimsalia na kumzika mwenyewe.
Ruqayya (RA): Ruqayya ni mtoto wa tatu wa Mtume (SAW), naye alizaliwa baada ya kuzaliwa Zainab kwa miaka 3, akiwa Mtume (SAW) ana umri wa miaka 33. Kabla ya utume aliolewa na Utba mtoto wa Abu Lahab, lakini ulipokuja utume na ukaweko uadui mkubwa baina ya Abu Lahab na Mtume (SAW) alimwamrisha Utba amwache Ruqayya. Ruqayya kisha akaolewa na Uthman bin Affan (RA), sahaba mkubwa na ni jamaa yake Mtume (SAW). Ruqayya na mumewe Uthman, kwa sababu ya mateso ya makafiri wa Makka walilazimika kuhama Makka na kwenda Habasha, na huko akapata mtoto wa kiume, lakini hakuishi sana. Baadaye wakahamia Madina. Katika vita vya Badr vilivyopiganwa huko Madina, Ruqayya alishikwa na maradhi akafariki dunia akiwa bado msichana wa miaka ishirini na kitu. Wakati huo jeshi la kiislamu lilikuwa linarudi kutoka vitani na kuja Zayd bin Al Haritha (RA) kutangaza ushindi mkubwa walioupata katika vita hivyo vya Badr. Mtume (SAW) alisikitishwa sana na kifo cha mwanawe huyu. Ummu Kulthum (RA): Ummu Kulthum alikuwa ni mtoto wa tatu wa Mtume (SAW). Yeye kama nduguye Ruqayya aliolewa na mtoto wa Abu Lahab aliyekuwa akiitwa Utaiba, lakini baada ya kuja Uislamu aliwalazimisha wanawe wawache watoto wa Mtume (SAW), na kwa hivyo Utaiba akamwacha Ummu Kulthum. Baada ya kufa nduguye Ruqayya, Mtume (SAW) alimuozesha Ummu Kulthum kwa Uthman, lakini naye hakuishi muda mrefu kwani alifariki akiwa bado mdogo kabla ya kufikia miaka ishirini. Mtume (SAW) alihuzunishwa sana na kifo cha Ummu Kulthum. Alimsalia na kumzika mwenyewe katika mwaka wa 9 wa Hijrah. Hakuacha watoto wowote. Abdullah: Abdullah alizaliwa baada ya Mtume (SAW) kupata utume, na kwa hivyo akaitwa "Attayyib" na "Attahir" kwa sababu amezaliwa kwenye Uislamu. Amekufa bado mdogo na Makureshi wakamstihzai na kumwambia kuwa atakuwa kibubutu, maana hana watoto wa kiume wa kuendeleza kizazi chake, basi Mwenyezi Mungu akamteremshia Suratul Kawthar:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mjawa wa Rehema,
Mwingi wa Rehema. Fatima (RA): Fatima alikuwa ndiye mtoto wa mwisho wa kike wa Mtume (SAW). Naye alirithi sifa nyingi za Mtume (SAW) na ndiye aliyekuwa kipenzi chake sana. Alikuwa mcha Mungu sana na alimsaidia sana babake katika kueneza Uislamu, na katika kusaidia maskini. Aliolewa na binamu yake Mtume (SAW) mtoto wa ami yake Abu Talib, Ali bin Abi Talib. Mtume (SAW) alikuwa akimpenda sana binamu yake huyu. Fatima alipata watoto wa tano kutokana na ndoa hii. Alimzalia Ali (RA) watoto hawa wafuatao: Al Hassan na Al Hussein na Muhsin na Ummu Kulthum na Zainab. Muhsin alikufa akiwa bado mdogo. Al Hassan na Al Hussein walioa na kuzaa watoto wengi. Ummu Kulthum aliolewa na Umar bin Al Khattab, na Zainab aliolewa na kuzaa watoto. Fatima alifariki akiwa na umri wa miaka 29 katika mwaka wa 11 wa Hijra, baada ya kufa kwa babake kwa miezi sita tu. Ibrahim: Ibrahim ndiye mtoto pekee wa Mtume (SAW) aliyekuwa hakuzaliwa na Khadija (RA). Mama yake alikuwa ni Maria Al-Qibtia, suriya wa Mtume (SAW). Yeye alikuwa ndiye mtoto wa mwisho wake, na alizaliwa Madina mwaka wa 8 wa Hijra. Ibrahim hakuishi sana na alikufa akiwa bado mdogo mwenye umri wa miezi 15 au 17. Mtume (SAW) alihuzunika sana kwa kifo chake kwani alikuwa mtoto wake wa kiume wa mwisho kufariki dunia. Mtume (SAW) alikuwa na watumwa wengi ambao aliwapata ima kwa kupewa zawadi au kwa kuwapatamateka katika vita au kuwanunua kwa nia ya kuwawacha huru baada ya kuwa watumwa wa watu wengine. Katika hao: A- Wanaume:
1- Zayd bin Haritha
alipewa zawadi na mkewe Khadija akamwacha huru na kumwita Zayd bin
Muhammad, kisha akamuoza binti wa shangazi lake Zaynab na baada ya
kumwacha, akamuoza Baraka mlezi wake Mtume (SAW). B- Wanawake:
1-Baraka
(Umm Ayman), mke wa Zayd bin Haritha na mamake Usama, na ni
mlezi wake Mtume (SAW) alipokuwa mchanga kabla hajachukuliwa na Halima
Assaadiya.
2- Salma (Umm Raafi'), mke wa
Abu Raafi' mmoja katika watumwa wa Mtume (SAW), Hawa ni watumwa wa Mtume (SAW) ambao wote aliwaacha huru wakawa ni huru wake. Watumishi wake:(SAW): Watumishi wake ni hawa wafuatao:
1- Anas bin
Malik na
Thaalaba bin AbdulRahman, na
anaeleza Anas kuwa amemhudumikia Mtume (SAW) miaka kumi hakusikia kwake
neno baya au kuona uovu wowote ule.
Waadhini wa Mtume (SAW): 1- Bilal bin Rabah: Watu wengi wanajua kuwa Bilal bin Rabah alikuwa ni muadhini wa Mtume (SAW), naye alikuwa ni mwanachuoni mkubwa wa Fiqhi na Hadithi. Alikuwa ni mtumwa wa kihabushia, aliyemilikiwa na Umayya bin Khalaf na kumtesa kwa ajili ya kusilimu kwake, kisha akanuliwa na Abubakar Assiddiq na kumuacha huru ili kupata ridha ya Mwenyezi Mungu. 2- Ibn Ummi Maktum: Muadhini mwengine wa Mtume (SAW), naye alikuwa kipofu, na mara nyingi Mtume (SAW) akimwacha Madina kuwa mwakilishi wake akiwa anakwenda vitani, naye amewahi kushiriki katika vita vya Al-Qadisiya na kupigana na kurudi Madina. Amekufa katika ukhalifa wa Umar bin Al-Khattab. Waandishi wa Mtume (SAW): Mtume (SAW) alikuwa hajui kuandika wala kusoma, na hii ni katika miujiza yake aliyopewa, kwani pamoja na kuwa hajui kusoma wala kuandika, alikuwa ni mtu mwenye akili na elimu na maarifa mengi kuliko wanadamu wote duniani, kwani aliyemfundisha na kumtoa ujingani na kumpa elimu na maarifa ya mambo mbali mbali ni mwenyewe Mwenyezi Mungu aliyetukuka. Kwa sababu hii, Mtume (SAW) alikuwa na waandishi wake ambao walikuwa wakimwandikia Qurani inapoteremshwa, au mikataba mbali mbali baina yake na makabila mengine au Washirikina au Mayahudi, au risala zake alizokuwa akiwapelekea wafalme na viongozi mbali mbali duniani. Waandishi hawa walikuwa wengi sana, wengine walikuwa daima na yeye, na wengine walimuandikia muda fulani tu, na katika hao ni:
1- Zayd bin
Thabit Al-Ansari
mwandishi wake mkubwa wa Wahyi unapoteremka, na wa risala zake. Alikuwa
mwanachuoni mkubwa sana Madina na alikuwa akitoa fatwa na kuhukumu na
kueleza mambo ya mirathi na visomo vya Qurani, katika zama za Umar na
Uthman na Ali, na alikuwa mjuzi wa mambo mengi sana hata alipokufa,
alisema Ibn Abbas: Leo imekwenda elimu, huku akionyesha kaburi lake. Wawakilishi wa Mtume (SAW): Mtume (SAW) alikuwa na desturi akiondoka Madina kwenda popote, lazima aweke mtu kumwakilisha yeye hapo Madina. Naye mara nyingi alikuwa akitoka yeye mwenyewe kwenda kuhudhuria vita mbali mbali vilivyokuwa vikitokea baina ya Waislamu na Makafiri, au Washirikina, au Mayahudi, na mara zote alikuwa na watu akiwaweka kama wawakilishi wake. Wafuatao ni wawakilishi wa Mtume (SAW) katika munasaba mbali mbali. Wawakilishi wake Madina:
1- Saad bin Ubada katika shambulizi
la Al-Abwaa
1-
Al-Muhajir bin Abi Umayya - mwakilishi wake juu ya Kinda na
As-Sadaf Majemadari wake:
1- Hamza bin AbdulMuttalib katika
shambulizi la Al-Abwaa Watarishi wa Mtume (SAW): Baada ya mkataba wa sulhu wa Hudaybiya, na kusita vita kwa muda baina ya Washirikina na Waislamu, alituma Mtume (SAW) wajumbe kwenda kwa wafalme na wakubwa wa makabila na viongozi mbali mbali kuwapelekea risala na kuwaita kwenye dini ya Mwenyezi Mungu, na hawa wafuatao ni wajumbe waliopelekwa kwa wakuu hao:
1- Amr bin Umayya Adh-Dhamri
kumpelekea risala An-Najashi mfalme wa Habasha Wasimamizi wa kukusanya Zaka wa Mtume (SAW): Zaka ni mojawapo ya nguzo za Uislamu, nayo ina umuhimu kama Sala na Saumu na Hija, na kwa hivyo Mtume (SAW) alikuwa amewaweka watu fulani kusimamia ukusanyaji wa Zaka kutoka kwa makabila na miji mbali mbali, na katika hao ni:
1- Ziyad bin Labid Al-Bayadhi -
Hadhramaut Viongozi wa watu katika msimu wa Hija: 1- Abubakar Assiddiq - Hija ya mwaka wa 9 Mavazi yake (SAW): Mtume (SAW) alikuwa akivaa mavazi kutoka nchi mbali mbali kwani alikuwa na mavazi yanayotoka Yemen na Sham na Hadhramaut na Hijaz na kwengineko, na yalikuwa mavazi yake meupe na mengine ya rangi mbali mbali kama nyekundu na manjano na meusi na kijani, lakini akipenda zaidi kuvaa nguo nyeupe. Katika mavazi yake ya kawaida ni kanzu na kofia na kikoi na juba na kilemba na guo la kujitupia na kujifunika nalo siku za baridi. Alikuwa akivaa kanzu fupi yenye kuteremka chini ya magoti lakini haifiki kwenye vifundo vya miguu, na akivaa kikoi na juba jeusi au kijani au jekundu, na mara nyengine akijifunika guo kujikinga na baridi katika majira ya baridi. Pamoja na kuwa Mtume (SAW) alikuwa akivaa nguo za rangi mbali mbali, lakini alikuwa hapendi marangirangi, na akipendelea sana kuvaa nguo nyeupe, na akihimiza watu wavae nyeupe hasa siku ya Ijumaa na kuvaa za rangi siku za Idi. Pia Mtume (SAW) alikuwa akivaa pete ya chuma iliyozungurishiwa fedha na juu yake imeandikwa: Muhammadun Rasuulullah. Aidha, alikuwa Mtume (SAW) akivaa viatu vya ngozi vyenye ukanda wa kufungia kwa juu ya mundi wa mguu, na alikuwa akizielekeza kanda zote upande wa kulia wakati wa kufunga, na vile vile alikuwa akivaa viatu vya ngozi hafifu na kusalia navyo, na kupangusia juu yake bila ya kuvivua ikiwa amekwishatawadha kabla. Vile vile, katika vitu alivyokuwa akivitumia ni kitana cha pembe ambacho akichania nywele zake na akitumia sana mafuta kupaka nywele zake na alikuwa na kioo akijitazamia na kichupa cha wanja ambao akijitia usiku usiku kabla ya kulala, na akipenda sana kutumia manukato na manukato yake yalikuwa ni miski na ambari, na akijifukiza kwa kafuri, na mara nyingi sana akitumia msuwaki wa mti kwa kupigia msuwaki meno yake baada ya kula na kulala na kabla ya kutawadha. Chakula chake (SAW): Mara nyingi chakula cha Mtume (SAW) na wakeze kilikuwa ni tende na maji tu, na wakikaa mara nyengine mwezi mmoja au miwili bila nyumba za wakeze kutoka moshi kwa kukosa cha kupika. Pamoja na hayo, alikuwa Mtume (SAW) akipenda katika vyakula asali na vitu vitamu na tende mbivu na akipenda tharid (mkate unaoroanishwa ndani ya mchuzi) au tende na maziwa ya kuganda na samli iliyochanganywa na kupikwa pamoja. Aidha, amekula Mtume (SAW) mkate wa ngano na shairi na nyama ya mbuzi na ngamia na maziwa na matunda kama vitango na boga na samaki, lakini mara nyingi alikuwa akikosa chakula na kubakia na njaa muda mkubwa, wala hakujawahi kutupwa chakula nyumbani kwake, au kujaza tumbo lake kwa vitu viwili wakati mmoja. Silaha zake (SAW): Katika silaha alizokuwa akimiliki Mtume (SAW) ni panga na ngao na mikuki na mishale na pinde na vizibao na kofia za kujikinga vitani, na aghlabu ya silaha hizi alizipata ngawira katika vita vyake alivyokuwa akipigana na Mayahudi na Washirikina, kwani alikuwa na panga tisa na ngao tatu na mikuki mitatu na pinde tano na vizibao saba na kofia mbili za kinga. Vile vile, alikuwa na bendera nyeupe na nyeusi ambazo daima akitoka kwenda vitani huwapa viongozi wa jeshi lake kushika, na alikuwa na hema ambalo akifungiwa akifika kwenye uwanja wa vita ili aongoze na kutazama vita vinavyokwenda. Aidha, Mtume (SAW) alikuwa na fimbo akiitumia na gongo akilishika wakati wa kutoa hotuba juu ya mimbari. Wanyama wake (SAW): Mtume (SAW) alikuwa na wanyama mbali mbali, kwani alikuwa akimiliki farasi na ngamia na mbuzi na punda na nyumbu, ambao wengine alinunua na wengine aliwapata ghanima katika vita, na wengine alipewa zawadi na wafalme au viongozi wa makabila. Alikuwa na farasi kumi na tisa na nyumbu wanne na punda wawili na ngamia wawili aliyekuwa akiwapanda mara nyingi katika safari zake, na alikuwa na ngamia jike ishirini wa kukamwa maziwa na mbuzi saba akipata maziwa kutokana nao. Nyumba zake (SAW): Mtume (SAW) alikuwa na nyumba tisa alizowajengea wakeze karibu na msikiti wake hapo Madina, na zilikuwa ni vyumba tu vilivyojengwa kwa majani ya mtende na nyengine kwa matofali ya udongo, na vilikuwa ni vidogo na sakafu yake unaweza kuishika kwa mkono, na mlangoni kulikuwa na pazia ya ngozi nyeusi yenye urefu wa dhiraa tatu kwa dhiraa moja na kitu. Mtume (SAW) ni mfano mwema: Mwenyezi Mungu aliyetukuka alipokuwa tayari kukamilisha dini na neema zake kwa wanadamu, aliwachagulia Uislamu kuwa ndio dini na mwenendo wa maisha kwa waja wake, na akamteua mja wake mwema na mbora wa wanadamu wote ili aje ulimwenguni kuishi maisha makamilifu ya kibinadamu kulingana na njia na mwenendo wa kiislamu ili watu waone mfano na wafuate mfano huo, akasema Mola wao aliyetukuka: Mna katika Mtume wa Mwenyezi Mungu mfano mwema, kwa yule mwenye kumtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Kwa hivyo, Mtume (SAW) tangu kuzaliwa kwake kwendea utotoni mwake kupitia ujana wake mpaka kufikia utuuzima wake ni mifano mema mitupu aliyotuachia ili sisi wanadamu tuweze kufuata na kuishi maisha mazuri hapa duniani na kesho Akhera. Mtume (SAW), japo alikuwa ni mbora wa wanadamu wote, alizaliwa akiwa ni yatima hana baba wa kumtazama na kumhangaikia, na hakukaa muda akafiliwa na mamake na kukosa wa kumlea na kumuangalia, na akabaki kutazamwa na babu yake kwa muda mfupi kisha ami yake, tukio ambalo lilimfanya akose mapenzi ya baba na mama na kuishi maisha ya kiyatima. Mfano huu mkubwa kabisa unatufahamisha kwamba kuwa yatima haina maana kukosa riziki au kuishi maisha ya taabu kama watu wengi wanavyofikiri, kwani mwenye kuruzuku ni mwenyewe Mola aliyetukuka na kwa hivyo kila mwanadamu amedhaminiwa riziki yake na Mola wake tangu alipokuwa ndani ya matumbo ya mamake. Mtume (SAW) alipokuwa mdogo aliinukia kuwa mtoto mwema mwenye utulivu na akhlaki njema na tabia nzuri na alipata malezi na uangalizi mzuri kutoka kwa mlezi wake ami yake ambaye alikuwa bwana wa kabila lake na mtu aliyekuwa akiheshimiwa sana na watu wake na kutukuzwa, na kwa hivyo akainukia kuwa mtoto wa kheri anayetokana na ukoo mtukufu, na haya ni kwa uteuzi mtukufu wa mwenyewe Mola ili kutufundisha sisi wanadamu kuzikuza koo zetu katika fadhila na mambo mema na kujiepusha na maovu na machafu ili zipate heshima na utukufu, na tangu utotoni mwake alijifundisha kuchunga mbuzi alipokuwa kwa mamake wa kumlea Halima, kisha akawa anafanya kazi hii kwa watu wa Makka na kulipwa vijipesa kidogo. Mtume (SAW) alipokuwa barobaro alishiriki katika mkataba uliofanywa na makabila ya kikureshi baada ya kutokea vita kwa sababu ya kuhujumiwa msafara kwa dhulma, na ukaandikwa mkataba huu kuhifadhi haki za watu na kuwaepusha na dhulma na jeuri za madhalimu, jambo ambalo alikuwa na fahari nalo sana. Kisha akatoka na ami yake kwenda katika msafara wa biashara huko Sham na kuona watu vipi wanaishi huko nje ya nchi yake, jambo ambalo lilimsaidia baadaye kumfanyia biashara Khadija alipomuomba amfanyie biashara zake, hasa baada ya kuonyesha uaminifu mkubwa na ukweli katika maneno yake na vitendo vyake na ahadi zake. Mtume (SAW) alipofikilia umri wa miaka ishirini na tano alimuoa Khadija ambaye alikuwa ni bibi mtukufu sana wa kikureshi, na juu ya kuwa kulikuwa na tofauti kubwa ya umri baina yao, Mtume (SAW) alimuoa bibi huyu na kutuonyesha sisi Waislamu kuwa umri si pingamizi baina ya mume na mke, na lililokuwa muhimu ni kupata mke mwema na mwenye sifa nzuri. Maisha yake na Khadija yalikuwa ni mfano kwetu sisi kutuonyesha namna gani mume anaishi na mke mmoja tu, kwani wakati alipokuwa na Khadija hakuoa mke mwengine na aliishi naye mpaka akafariki. Mtume (SAW) alipokuwa na umri wa miaka thalathini na tano, kulitokea tukio muhimu sana katika maisha yake, kwani Makureshi waliivunja Al-Kaaba kwa nia ya kuijenga upya, na walipokuwa tayari kuliweka jiwe jeusi ambalo ndilo jiwe la msingi, walihitalifiana kuhusu nani atapata sharafu na heshima ya kuliweka jiwe hili mahali pake, na baada ya kugombana na kukaribia kupigana, walikubali kumwachia hukumu mtu wa kwanza atakayeingia kwenye mlango wa msikiti wa Makka. Mwenyezi Mungu kwa hekima yake akajaaliya kuwa aliyetokea ni Mtume (SAW) ambao wao pale pale waliridhika kwa kumjua kuwa ni mkweli na muaminifu, sifa ambazo yeye alikuwa akijulikana nazo kabla ya kupewa utume, na kwa hivyo akapata nafasi ya kutoa hukumu iliyokuwa na hekima kubwa, kwani aliweka guo lake na kuliweka jiwe katikati yake na kuamrisha wakubwa wa kabila za kikureshi kukamata nchani mwa guo lake na kuinua pamoja mpaka mahali pa kuwekwa hilo jiwe, kisha yeye akaliinua na kuliweka mahali pake, na wote wakaridhia na kufurahi na akaweza kusitisha vita ambavyo vingezuka baina ya makabila haya. Mtume (SAW) alipata matatizo na misukosuko mingi baada ya kupata utume na aliishi yeye na wafuasi wake katika taabu na shida na kukandamizwa mpaka alipowaamrisha Waislamu wahame na kwenda Habasha, nchi ambayo watapata amani na wataweza kufanya ibada zao kwa usalama, jambo lililotuonyesha njia ya kufanya wakati wowote Waislamu wanapopata mateso na kudhikiwa wasifanye ibada zao na kunyimwa uhuru wa kuabudu. Huku kuhama kutoka nchi kwenda nchi kuna fadhila kubwa ikiwa mtu anawacha nchi yake kwa ajili ya kuihifadhi dini yake, hata ikiwa ile nchi anayoikimbilia si ya kiislamu lakini inampa uhuru wa kufanya ibada yake na kutangaza dini yake. Mtume (SAW) alilazimika kuhamia Madina baada ya dhulma kuwa nyingi Makka na kutoka nchi ambayo ilimnyima haki ya kuabudu Mola wake na kwenda kwenye nchi ya kigeni ambayo ilimkaribisha na kumpokea na kumpa nafasi ya kueneza dini yake na kusimamisha dola yake. Baada ya kusimamisha dola ya kiislamu, Mtume (SAW) alianza kuteremshiwa na Mola wake hukumu na sheria za maisha ya jamii ya kiislamu na namna ya kuishi Waislamu na wasiokuwa Waislamu wakiwa ni Makafiri au Mayahudi au Manasara au watu wengineo wenye kufuata mila nyenginezo. Mtume (SAW) aliendelea kutangaza dini ya Mwenyezi Mungu na kujaribu kuwavutia makabila na watu mbali mbali kuingia katika dini ya Mola wake, kwa kufanya mikataba na kupanga udugu na urafiki na kuoa katika makabila mbali mbali na kuweka uhusiano mwema baina ya watu na majirani na hata baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, lakini upinzani ulikuwa mkubwa ndani ya nchi na nje yake, na wakawa Mayahudi waliokuwa wakiishi Madina kwa upande mmoja na makabila ya kiarabu na Makureshi kwa upande mwengine, wanatumia kila mbinu na vitimbi ili kuwapiga Waislamu na kuwazuiya wasiineze dini yao, jambo ambalo lilimfanya Mtume (SAW) achukuwe msimamo dhidi ya wapinzani hawa, na kusimamisha vita dhidi yao alipopewa idhini na Mola wake, na kutuonyesha kwamba mambo yakipindukia mpaka Waislamu wanatakiwa wasimame kuizuiya dhulma isitendeke hata ikiwa kwa vita na kupigana. Mtume (SAW), baada ya kupigana vita ishirini na nane katika nyakati mbali mbali na kupeleka vikosi vyake sehemu mbali mbali kuonya au kutia adabu wale ambao wanajaribu kuzuiya neno la Mwenyezi Mungu lisitangazwe, aliwafundisha Waislamu mambo mengi yanayohusu maisha yao, katika mas-ala ya ibada kama Sala na Zaka na Saumu na Hija au maingiliano mengineyo ya kimaisha yakiwa ya kijamii au kindoa au kibiashara au kisiasa au ya kimahusiano ya kitaifa na kimataifa. Katika mfano mzuri aliotuonyesha katika mas-ala ya ndoa ni kuoa kwake Madina wake wengi na namna ya kuishi nao kwa uadilifu na mapenzi na vipi kusawazisha baina yao katika makazi na malazi na chakula na mavazi. Kwa hivyo, Mtume (SAW) aliishi miaka ishirini na tatu ya utume akiwa ni mithali njema na mfano mzuri kwa wanadamu wote wa namna ya mtu kuishi akiwa yatima au maskini au tajiri au mfanyikazi au mfanyibiashara au mwalimu au imamu au kiongozi wa jeshi au mkuu wa nchi. Mtume (SAW) aliishi akiwa mtoto mwema na jirani mzuri na mfanyikazi mwenye bidii na mfanyibiashara muaminifu na kiongozi muadilifu na mume mtulivu na baba mrehemevu na rafiki mwema na mpiganiaji haki mstahmilivu, na bila shaka amesema kweli Mwenyezi Mungu Mola wetu aliposema: Mna mfano mzuri kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. |
|
|||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|