|
Mwaka wa tano: Shambulizi la Dawmatul-Jandal: Katika mfungo sita wa mwaka huu, baada ya kupita kiasi cha miezi sita tangu yamalizike mashambulizi ya Badr ya pili, alipata habari Mtume (SAW) kuwa mabedui waishio Dawmatul-Jandal karibu na Sham wanawashambulia watu na kuwanyanganya mali yao, na kuwa vile vile wana nia ya kuja kuwahujumu Waislamu Madina. Basi Mtume (SAW) akamweka Siba'a bin Urfatta Al-Ghaffari hapo Madina kama mwakilishi wake, na kutoka na jeshi la watu elfu kwenda kuwashambulia hawa mabedui na kuwatia adabu. Akawa anakwenda usiku na kujificha mchana mpaka wakakaribia mahali walipo hawa maadui. Ilipoingia Magharibi jeshi la kiislamu liliteremka kuwavamia mabedui hao, lakini walikuwa wameshapata habari kuwa wanajiwa, na kwa hivyo Waislamu walipofika pale walipo hawakumkuta mtu isipokuwa wanyama wao na wachungaji wao, basi wakawachukuwa wale wanyama kama ghanima, na kupeleka vikosi vyao huku na huku kujaribu kuwakamata lakini hawakubahatika kuwaona, maana walikuwa wameshakimbia, basi Mtume (SAW) akarudi Madina akiwa amepata ngawira nyingi, na njiani akafanya sulhu na Uyayna bin Hisn Al-Fazari. Baada ya tukio hili, Mtume (SAW) akawa ametekeleza sehemu kubwa ya kuithibitisha dola yake, kwani alikuwa ameshakata mizizi ya fitina ya Mayahudi wa Madina, na kuwanyamazisha Wanafiki, na kuwashitua mabedui na kuwatia khofu Makureshi, na kuonyesha makabila mbali mbali kuwa Waislamu si watu wa kuchezewa, na kuwa mwenye kumnusuru Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atamnusuru vile vile. Shambulizi la Handaki: Mayahudi wa Banun-Nadhiir waliotolewa na Mtume (SAW) Madina kwa khiyana yao ya kutaka kumuua Mtume (SAW), walikuwa wakisubiri kwa hamu na kungoja nini makabila mengine ya kikafiri yatafanya dhidi ya Waislamu ili wapate kurudi zao Madina. Lakini walipoona kuwa badala ya kupungua nguvu zao Waislamu, zilikuwa zikizidi siku baada ya siku, waliona kuwa hapana budi isipokuwa wapange njama pamoja na makabila mengine ya kiarabu yaliyokuwa dhidi ya Waislamu, ili wachange nguvu na kuwamaliza Waislamu moja kwa moja. Wakajikusanya kiasi ya viongozi ishirini wa kiyahudi na mabwana wa kabila la Banun-Nadhiir na kuwaendea Makureshi Makka kwa mas-ala haya. Makureshi ambao tokea hapo walikuwa na shauku ya kutaka kupigana na Waislamu na kutimiza ahadi yao ambayo wameivunja waliposhindwa kuhudhuria vita vya Badr vya pili, walikubali fikra hii upesi upesi. Baada ya hapo, Mayahudi waliliendea kabila la Ghattafaan na kulishawishi vile vile, na wao wakakubali. Kisha wakayaendea makabila mengine ya kiarabu na kuyatia maneno na hayo pia yakakubali. Yakawa yamekusanyika makabila ya kikafiri ya kiarabu na kiyahudi kutaka kuuangamiza Uislamu moja kwa moja. Makureshi wakakusanya marafiki zao ikawa idadi yao kama elfu nne, na Ghattafaan wakatoka na jeshi la maelfu ya watu: Banu Fazara walikuwa na wapandi farasi elfu, wakiongozwa na Uyayna bin Hisn ambaye Mtume (SAW) alifanya naye sulhu na kummegea ardhi alishie wanyama wake, naye akasahau hisani hii, akajiunga na maadui. Banu Mura wakiwa ni watu mia nne wakiongozwa na Al-Harith bin A'uf, na Banu Ashja'a wakiongozwa na Mis'ir bin Rukhayla, na Banu Suleym wakiongozwa na Sufyan bin Abd Shams, na Banu Asad wakiongozwa na Tulayha bin Khuwaylid, ikiwa idadi ya jeshi lote la Makafiri ni watu elfu kumi. Mtume (SAW) ilipomfikia habari hii, pale pale aliliita baraza lake kuu la mashauri na kushauriana nao kuhusu njia za kuweza kuihami Madina kutokana na hujumu na uadui huu, na baada ya kushauriana na kujua kuwa wanakabiliana na jeshi kubwa sana, alitoa rai Salman Al-Faarisi ya kuchimba handaki, na kuwaeleza kuwa Mafursi (Mairani leo) katika vita vyao hufanya haya, na hili lilikuwa ni jambo geni kwa Waarabu, kwani Waarabu walikuwa wakipigana uso kwa uso tu. Basi Mtume (SAW) kwa uhodari wake wa vita akaamua wachimbe sehemu ya kaskazini ya Madina ambayo ilikuwa tupu, haikuzungukwa na majabali, wala majumba, wala mashamba, na ambako akitarajia maadui watakuja kutokea upande huo. Kwa hivyo, Mtume (SAW) akakusanya kiasi Masahaba elfu na kuwagawa kumi kumi, kila kumi wachimbe sehemu moja upana wa dhiraa arubaini, na akawa Mtume (SAW) mwenyewe anawasaidia, ikawa wanachimba mchana mzima, kisha jioni hurudi kwa wake zao, na ilikuwa hali ya hewa ni baridi na chakula ni kidogo sana, wakawa wanafanya kazi katika hali ya machofu na njaa, na huku Mtume (SAW) akiwashajiisha kwa kuwaambia: Ewe Mola hapana maisha isipokuwa maisha ya Akhera, basi waghufirie Maansari na Muhajira, na wao wakimjibu: Sisi ndiwo tuliomkubali Muhammad kwa jihadi muda wote tutakaobakia. Waislamu walipokuwa wakichimba kwa hima na hamasa, walipambana na matatizo mengi ya njaa, na ugumu wa ardhi, na hali ya hewa, na Mtume (SAW) alikuwa akiwasaidia na kuwapa moyo, na wakaona Waislamu miujiza mikononi mwa Mtume (SAW), kwani mara moja waliletewa chakula, Mtume (SAW) akawakusanya Masahaba zake wote elfu na kula chakula hicho, kila wakila hakimaliziki mpaka wakashiba wote na kutoshelezeka. Halikadhalika, mara moja alipita mwanamke na tende, Mtume (SAW) akazichukua na kuzitupatupa juu ya nguo, kisha akawaita wachimba handaki na kuwapa, wakala mpaka wakashiba, tende ziko pale pale zinazidi tu. Aidha, mara nyengine walipokuwa wakichimba walikutana na jabali likawashinda kulivunja basi wakamwambia Mtume (SAW) naye akenda na kushika sururu na kusema: Bismillahi na kulipiga dharuba moja kubwa, kisha akasema: Allahu Akbar! Nimepewa funguo za Sham na wallahi hivi ninayaona majumba yake mekundu. Kisha akalipiga mara ya pili na kulimegua kipande chengine, na kusema: Allahu Akbar! Nimepewa Ufursi (Iran), na wallahi hivi sasa ninayaona majumba meupe ya Madain. Kisha akapiga mara ya tatu, na akasema: Bismillahi. Likavunjika lililobakia. Akasema: Allahu Akbar! Nimepewa funguo za Yemen, na wallahi hapa nilipo ninaona milango ya San'a. Basi wakaendelea na kuchimba kwao mpaka walipomaliza kama vile alivyotaka Mtume wao. Baada ya kumalizika kuchimbwa handaki, Mtume (SAW) alitoka na jeshi la watu elfu tatu, na kumwakilisha Madina Ibn Umm Maktum, na kumpa bendera ya Muhajirina Zayd bin Haritha, na bendera ya Maansari Saad bin Ubada, na akaamrisha wanawake na watoto kuwekwa ndani ya ngome, na kuja kuwakabili maadui wakiwa wamelipa mgongo jabali Sal'i, na usoni mwao handaki kizuizi baina yao na baina ya jeshi la Makafiri. Makafiri walipofika Madina, walishangazwa sana na waliyoyaona, kwani walijikuta ukingoni mwa handaki kubwa na mbele yao jeshi la kiislamu linawasubiri. Jambo hili lilikuwa ni geni kwao na hawakulitarajia kamwe, na kwa hivyo wakawa hawajui wafanye nini ili waweze kuwahujumu Waislamu. Wakabaki Washirikina kuzunguka huku na huko kutazama kama kuna sehemu watakayoweza kupita, na kama iko njia ya kujenga daraja au kuruka, lakini handaki lilikuwa limechimbwa kwa uhodari mkubwa, na Waislamu walikuwa wamekaa tayari kumpiga au kumrushia mshale yeyote atakayejaribu kuruka au kukiuka handaki. Washirikina wakawa hawana la kufanya isipokuwa kungojea, na kudhani kuwa kusubiri kwao kutawafanya Waislamu wasalimu amri, lakini kwa kuwa hawakujitayarisha kwa jambo hili na wamekuja kulishtukia tu, waliona kuwa hawatoweza kukaa muda mkubwa sana na kwa hivyo, vijana katika wao wakawa wana pupa wanataka kufanya jambo. Kikatoka kikundi cha vijana wa kikureshi akiwemo Ikrima bin Abi Jahl na Dhiraar bin Al-Khattab na Amr bin Abd Wadd na wengineo, na kujaribu kuvuka handaki, lakini Ali bin Abi Talib pamoja na kundi la Waislamu likawaendea, na Ali akasimama kupigana na Amr mpaka akamuua, wenzake walivyoona Amr ameuliwa na yeye alikuwa ni katika mashujaa wa kikureshi, walikimbizana na kurudi upesi kwa Makafiri wenzao. Vita vikaendelea baina ya Waislamu na Washirikina kwa kurushiana mishale tu, na wakapigana siku nzima mpaka ukaingia usiku na kukosa Sala siku ile, jambo ambalo lilimkasirisha sana Mtume (SAW) kufikia hadi kuwalaani Washirikina, akasema: Mwenyezi Mungu ajaze nyumba zao na makaburi yao Moto kama walivyotushughulisha na Sala ya katikati mpaka likazama jua. Imesimuliwa na Bukhari-2/590 Na wakati Washirikina walipokuwa wanaendelea kuwazunguka Waislamu, na kuwatupia mishale, alikuja Huyay bin Akhtab, bwana wa Banun-Nadhiir na kumwendea Kaab bin Asad, bwana wa Banu Quraydha na kujaribu kumshawishi avunje mkataba waliokuwa nao na Mtume (SAW) na wajiunge na Washirikina katika kuwapiga vita Waislamu, na juu ya kwamba mwanzo alikataa sana, lakini Huyay aliweza mwisho kumkinaisha kwa kumuonesha kuwa Waislamu wamekwisha, na hivi sasa nimekuja na makabila yote ya kiarabu tayari kuwamaliza Waislamu. Mtume (SAW) alipopata habari ya khiyana wanayotaka kuifanya Mayahudi hasa katika hali nzito kama hii iliyowakabili, alitumiza watu kwenda kuhakikisha, na alipoyakinisha alituma watu kwenda kuwahami watoto na wanawake waliowachwa nyuma Madina, na akataka kumpelekea watu Uyayna kufanya naye sulhu, na ampe thuluthi (sehemu moja katika tatu) ya matunda ya Madina, ili aondoke na kabila lake la Ghattafaan, lakini Maansari wakamwambia ikiwa si amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu, basi sisi hatutaki, kwani wao walikuwa hawapati hata kidogo ya matunda yetu tulipokuwa sisi ni Makafiri, watakuja kupata leo, baada ya kuwa sisi Waislamu? Kisha tena Mwenyezi Mungu katika kutaka kuwanusuru Mtume wake na Waislamu, alimtia imani mmoja katika kabila la Ghattafaan, anayeitwa Nuaim bin Masuud Al-Ashja'i, na kuja kwa Mtume (SAW) na kumwambia kuwa mimi nimesilimu kisiri na watu wangu hawajui, basi niamrishe nifanye nini ili niweze kukusaidia. Mtume (SAW) akamwambia: Wewe ni mtu mmoja, kitu gani utaweza kufanya? Lakini fanya khiyana kwa ajili yetu utakavyoweza, kwani vita ni hadaa Mwenyezi Mungu awanusuru waja wake: Nuaim akatoka na kuwaendea Banu Quraydha ambao walikuwa ni marafiki zake na kuwaambia: Enyi Banu Quraydha, nyinyi mnajua mapenzi yangu kwenu na khofu yangu juu yenu, nami nitakuambieni jambo msiseme kuwa mimi nimekuambieni. Wakasema: Naam. Akasema: Mmeona yaliyowatokea Banu Qaynuqaa na Banun-Nadhiir, ya kutolewa nchi na kuchukuliwa mali yao na nyumba zao, na Makureshi na Ghattafaan si kama nyinyi, kwani wao wakiiona fursa wanaichukua, la si hivyo watarudi nchini mwao. Ama nyinyi mnaishi na huyu mtu - yaani Mtume - wala nyinyi hamna nguvu ya kupigana naye peke yenu, basi mimi ninaona msiingie katika vita hivi mpaka mhakikishe kutokana na Makureshi na Ghattafaan kuwa hawatokuacheni wakenda zao kwao, basi mchukue kutoka kwao watukufu wao sabiini kama dhamana. Basi Banu Quraydha wakaona rai yake kuwa ni nzuri, na wakamkubalia. Kisha Nuaim akatoka na kuwaendea Makureshi na kukutana na viongozi wake na kuwaambia: Nyinyi mnajua mapenzi yangu kwenu, nami nitakuambieni jambo lakini msiseme kuwa nimekuambieni. Wakasema: Haya. Akawaambia: Kwa hakika Banu Quraydha wamejuta kwa yale waliyomfanyia Muhammad na wanaogopa mtarudi muwawache na yeye, wakamwambia: Je, utaridhia tuchukue kundi la watukufu wao tukupe wewe, na wewe uturudishie ubawa wetu uliouvunja? (yaani Banun-Nadhiir). Basi akawakubalia hilo. Na hivi wataleta watu kwenu kuhusu jambo hili, basi wakija kutaka dhamana msiwape. Kisha akenda kwa Ghattafaan na kuwaambia maneno kama hayo. Basi ulipoingia usiku wa kuamkia Jumamosi, alipeleka Abu Sufyan ujumbe kwa Banu Quraydha kuwataka wawasaidie katika mapigano yao na Muhammad. Banu Quraydha wakajibu kuwa sisi hatuwezi kupigana siku ya Jumamosi (maana siku yao tukufu) na hayakutufika haya isipokuwa kwa kutoiheshimu siku hii, na vile vile hatutapigana isipokuwa mtupe dhamana ya watu kutoka kwenu ili msije mkaondoka na kutuwacha na kurudi makwenu. Basi Makureshi na Ghattafaan wakahakikisha maneno ya Nuaim na kuingiwa na khofu na kuvunjika moyo, na wakawapelekea salamu Banu Quraydha kuwa sisi hatukuleteeni mtu, basi wakasema kuwa ametuambia kweli Nuaim. Mtume (SAW) akamwelekea Mola wake na kumuomba dua amnusuru dhidi ya Makafiri, akasema: Ewe Mola Mteremshi Kitabu, Mwepesi wa kuhisabu, Washinde Makundi. Ewe Mola, washinde na uwasukesuke. (Bukhari: Jihad 1/411) Mwenyezi Mungu akamuitikia Mtume wake dua yake, na kuwaletea maadui upepo mkali wa baridi na kupeperusha mahema yao na kuwatia khofu katika nyoyo zao, mpaka wakaamua bora waondoke na kurudi makwao kabla ya kupambazuka. Basi Mtume (SAW) aliposikia zogozogo upande wa Washirikina, alimtuma Hudhaifa bin Al-Yamaan akachunguze na awaletee habari zao, na juu ya kuwa hali ilikuwa ni ya hatari kabisa na hali ya hewa ilikuwa mbaya sana, lakini alitoka Hudheifa na kwenda kwa Makafiri na kurudi na habari yakini kuwa Washirikina wanajitayarisha kuondoka. Kushindwa kwa Makundi ya Washirikina Abu Sufyan akiwa ndiye kiongozi wa mapote yote ya Washirikina aliwaamrisha wajitayarishe na kuwahadhirisha asije adui akaingia kati yao, hasa ulivyokuwa usiku ni wa giza totoro, na watu wako katika hali ya mchafuko, basi akawasimamia waondoke na kumuamrisha Khalid bin Al-Walid na kikosi kukaa nyuma ili awahami wasije wakavamiwa, wakaamka asubuhi Waislamu na kukuta maadui washaondoka, na ikawa Mwenyezi Mungu amewarehemu Waislamu na vita ambavyo vingewaangamiza moja kwa moja, akawa amemtimizia Mtume wake ahadi yake na kulipa nguvu jeshi lake na kumnusuru mja wake na kuwashinda mapote yaliyokusanyika kumpiga peke yake, wakahizika Washirikina na kurudi zao makwao. Vita vya handaki au kama vinavyojulikana mara nyengine kwa jina la vita vya mapote, vilikuwa ni vita muhimu sana katika tarehe ya Uislamu, ijapokuwa hakukupatikana hasara nyingi ya mali na watu, kwani waliokufa upande wa Waislamu ni watu sita tu kwa mishale, na kumi upande wa Washirikina, lakini Washirikina walitambua kuwa baada ya mkusanyiko wa majeshi yote haya hatukuwaweza Waislamu, basi hatuna uwezo wa kuwashinda tena. Na akasema Mwenyezi Mungu kuwakumbusha Waislamu neema hii aliyowapa na kuwakirimu kwa ushindi mkubwa baada ya kuwa walikuwa katika hatari kubwa na kifo cha dhahiri. Q. Ahzaab:9-13. Shambulizi dhidi ya Banu Quraydha: Mtume (SAW) aliporudi Madina na kuvua nguo zake za vita, alimjia Jibril (AS) na kumwambia: Ushaweka silaha yako? Kwani Malaika bado hawakuweka silaha zao, kwa hivyo inuka na wenzako mwende kwa Banu Quraydha, nami ninakwenda mbele yako nikazitetemeshe ngome zao na niingize khofu ndani ya nyoyo zao. Akenda Jibril (AS) akifuatwa na kundi la Malaika. Banu Quraydha ni kabila la mwisho la kiyahudi lililokuwepo Madina wakati wa vita vya mapote (makundi), na wao kinyume na mkataba waliofanya na Mtume (SAW) wa kuishi kwa amani, walifanya khiyana kama wenziwao waliopita kina Banun-Nadhiir na Banu Qaynuqaa, na kuvunja mikataba na kutupa ahadi kama ilivyo desturi yao Mayahudi siku zote. Katika vita hivi vya handaki, Mayahudi hawa walikuwa tayari kushirikiana na Washirikina katika kuwamaliza Waislamu na kuwaangamiza moja kwa moja, na kwa hivyo Mwenyezi Mungu akamuamuru Mtume wake asiweke silaha yake chini kwa kuwa washirikina wameshindwa na kuondoka, kwani hawa waliobaki nyuma ni hatari zaidi na waovu zaidi, kwa sababu hawa ni wale kikulacho ki maungoni mwako. Mtume (SAW) akamuamuru mtu atangaze kwa Masahaba zake kuwa: Mwenye kusikia na kutii, basi asisali Alasiri isipokuwa kwa Banu Quraydha! Kisha akamweka Ibn Umm Maktum kama mwakilishi wake Madina na kumpa bendera Ali bin Abi Talib na kuelekea kwenye ngome za Banu Quraydha. Waislamu wakachomoza kila upande kila mmoja kabeba silaha yake na kujibu mwito wa Mtume wake na kukimbilia kumfuata kwenye ngome za Banu Quraydha mpaka ikafika idadi yao watu elfu tatu, na kuzizunguka ngome zao. Banu Quraydha walipoona jeshi la Waislamu linakuja waliingiwa na khofu kubwa sana kwa kujua kuwa hawana njia ya kumkimbia Mtume (SAW) na Masahaba zake, baada ya khiyana waliomfanyia wakati alipokuwa katika hali ya hatari kubwa ya kumalizwa na majeshi ya Makafiri. Kwa hivyo, wakajifungia ndani ya ngome zao wakidhani kuwa zitawakinga na ghadhabu za Mwenyezi Mungu kwa kwenda kinyume na Mtume wake ambaye wanayakini kuwa ndiye aliyetajwa katika vitabu vyao. Waislamu wakabakia hapo siku ishirini na tano mpaka Mayahudi wakahisi kuwa hapana hila ya kuvikimbia vita hivi, vimewaandama vimewaandama tu, na ikiwa wataendelea kujificha ndani ya ngome zao, mwisho wataishiwa na vyakula na kufa kwa njaa. Mkubwa wao Kaab bin Asad akawaambia kuwa wachague mojawapo ya mambo matatu: Ima wasilimu na waingie katika dini ya Muhammad ili wasalimike wao na mali yao na wake zao na watoto wao, hasa ilivyokuwa wao wana yakini kuwa huyu ndiye Mtume aliyeletwa na kutajwa kwenye vitabu vyao, au waue watoto na wake zao wenyewe kwa mikono yao, kisha wamtokee Muhammad na panga zao, wapigane naye mpaka wamshinde au wafe wote, au wamhujumu Muhammad na Masahaba zake siku ya Jumamosi, siku ambayo hawatarajii kuwa watawahujumu. Watu wake wakazikataa rai zote hizi tatu. Walivyoona mambo yamewatatiza, waliwaambia Waislamu kuwa wako tayari kutoka nchi kama Banun-Nadhiir na kuchukua mali na kuacha silaha, Mtume (SAW) akawakatalia. Wakaomba basi watoke peke yao bila ya mali wala silaha, na hili pia Mtume (SAW) hakuliridhia, bali akawaambia kuwa lazima wakubali hukumu yake atakayoitoa juu yao, ikiwa ni nzuri au mbaya. Basi wakamuomba awaletee Abu Lubaba wamshauri, naye alikuwa ni katika kabila la Aus na Banu Quraydha hapo nyuma walikuwa ni marafiki zao, na mali zake na ukoo wake ulikuwa unaishi katika mitaa yao. Basi alipokwenda walimshauri kuhusu kukubali hukumu ya Mtume (SAW), akawaashiria kwa mkono wake shingoni kuwa hukumu ya Mtume (SAW) juu yao ni kifo tu. Kisha pale pale akatanabahi kuwa amemkhini Mwenyezi Mungu na Mtumewe, akaondoka na kuelekea kwenye msikiti wa Mtume (SAW) na kujifunga kamba na nguzo ya msikiti, na kuapa kuwa asifunguliwe isipokuwa na mwenyewe Mtume (SAW), na kuwa hatoingia ardhi ya Banu Quraydha abadan. Mtume (SAW) aliposikia habari hii, alisema kuwa lau angemjia na kumuomba amuombee maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu angemuombea, lakini maadamu yeye amefanya alilolifanya, basi si Mimi nitakayemuondosha mahali alipo mpaka Mwenyezi Mungu amsamehe madhambi yake. Huku nyuma Ali bin Abi Talib akapaza sauti yake na kusema: Enyi kikosi cha imani, wallahi nitaonja aliyoonja Hamza, au nitaziteka ngome zao. Hapo Mayahudi wakaingiwa na kihoro na kukubali hukumu ya Mtume (SAW). Kwa hivyo, Mtume (SAW) akaamrisha wakamatwe wanaume na wafungwe mikono yao na kuwekwa chini ya usimamizi wa Muhammad bin Maslama, na wanawake na watoto watengwe kando. Aus walivyoona hivi, walisimama na kumwambia Mtume (SAW): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, umewafanyia Banu Qaynuqaa yale ambayo unajua umewafanyia, nao walikuwa ni marafiki wa ndugu zetu Al-Khazraj, na hawa ni marafiki zetu sisi, basi wafanyie wema. Akasema: Je, hamridhii awahukumu mmoja wenu? Wakasema: Kwani! Akasema: Basi hukumu hiyo ni ya Saad bin Mua'dh. Wakasema: Tumeridhia. Mtume (SAW) akaagizia aitwe Saad bin Muadh ambaye alikuwa amebaki Madina hakuja nao kwa Banu Quraydha kwa sababu ya majeraha aliyoyapata katika vita vya handaki, na alipokuwa anakwenda kwa Mtume (SAW) wakawa wanamwambia: Ewe Saad, wafanyie uzuri marafiki zako na uwafanyie wema, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuachia uwahukumu ili uwafanyie hisani. Akanyamaza kimya asiseme neno, lakini walipozidi kumkera, akawaambia: Umewadia wakati kwa Saad asijali kwa Mwenyezi Mungu lawama ya mtu yeyote. Basi waliposikia hayo walijua kuwa hapana msamaha. Saad alipofika kwa Mtume (SAW) alimwambia: Wahukumu Ewe Saad! Masahaba wakamwambia: Hawa watu wamekubali hukumu yako. Akasema: Na hukumu yangu itapita juu yao? Akaambiwa: Naam. Akasema: Na juu ya Waislamu? Wakasema: Naam. Akasema huku amemkabili Mtume (SAW): Na juu ya huyu hapa? Huku uso wake uko chini kwa kumheshimu na kumtukuza. Akasema: Naam na juu yangu. Akasema: Basi Mimi nimewahukumu wanaume wao wauliwe, na wanawake na watoto wachukuliwe mateka, na mali yao igawanywe. Akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu: Kwa hakika umewahukumu kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu inayotoka mbingu ya saba. Basi Mtume (SAW) akawakusanya na kuamrisha hukumu ipitishwe, wakachukuliwa na kufungwa ndani ya nyumba ya mwanamke mmoja wa kina Bani An-Najjar, na kuchimbwa mahandaki kwenye soko la Madina na kukatwa vichwa vya wanaume katika wao, na yakachukuliwa mali yao na kugawiwa walioshiriki katika shambulizi la Banu Quraydha, sehemu moja kwa maaskari wa miguu, na sehemu tatu kwa maaskari wa farasi, baada ya kuchukuwa sehemu moja katika tano yeye mwenyewe Mtume (SAW), na wakachukuliwa wanawake wao na kuuzwa baadhi yao kwenye soko huko Najd, na kununua badala yake farasi na silaha, na Mtume (SAW) akamchagua Rayhana katika wanawake wao kama suriya wake. Katika shambulizi hili, hakuuliwa Muislamu isipokuwa mmoja Khalaad bin Suweid ambaye alirushiwa jiwe la kusagia unga na mwanamke wa kiyahudi likamuua, na ndiye mwanamke pekee aliyeuliwa baada ya kumalizika shambulizi hili. Kwa upande mwengine, Saad aliporudi Madina kujiuguza haukupita muda yakatumbuka majeraha yake na kumwagika damu akafariki dunia. Saad bin Muadh alikuwa akipendwa sana na Mtume (SAW) na alikuwa yeye kwa Maansari kama Abubakar kwa Muhajirina, na Mtume (SAW) alimbashiria Pepo. Waislamu walipokwenda kumzika, baadhi ya Wanafiki walisema: Ni jepesi sana jeneza lake, Mtume (SAW) akasema: Hakika Malaika walikuwa wakilibeba. Na imesimuliwa katika Sahihi Bukhari na Muslim kutokana na Jabir kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Arshi ya Mwenyezi Mungu imetikisika kwa kufa Saad bin Muadh. Bukhari 1/536 na Muslim 2/294 Huku alibakia Abu Lubaba amejifunga kwenye nguzo ya msikiti siku sita, huja mkewe wakati wa Sala na kumfungua akasali kisha akarudi kumfunga mpaka ulipoteremshwa Wahyi kutoka kwa Mola wake kumsamehe makosa yake haya, ndipo walipokuja watu kumfungua, lakini akakataa mpaka alipokuja Mtume (SAW) akamfungua. Qurani Tukufu inaeleza kuhusu toba yake ikasema:Toba:102 Kuuliwa kwa Abu Raafi': Baada ya kumalizika shambulizi la Banu Quraydha, walitaka idhini Al-Khazraj kutoka kwa Mtume (SAW) kumuua Abu Raafi' Salaam bin Abil-hakiik ambaye ni katika Mayahudi waliokuwa wakimkera na kumuudhi Mtume (SAW) na kuwasaidia Washirikina kuwapiga vita Waislamu kwa hali na mali. Na ilivyokuwa Aus walipata sharafu ya kumuua Kaab bin Al-Ashraf Yahudi mwengine aliyekuwa vile vile akimkera Mtume (SAW), wao walitamani wapewe fursa hii ili wapate fadhila ya kumuondoshea Mtume wao dhiki na jeuri ya mtu huyu. Mtume (SAW) akawapa ruhusa kumuua Abu Raafi' peke yake, na kuwakataza kuwaua wanawake na watoto, basi wakatoka wanaume watano wa kikhazraj wakiongozwa na Abdullahi bin A'tiik na kuelekea Khaybar kwenye ngome ya Abu Raafi'. Ulipoingia usiku waliingia kwenye ngome na kupanda juu kwa Abu Raafi' na kungojea mpaka walipotoka watu waliokuwa wakipitisha usiku naye, walimuingilia na kumuua, kisha wakakimbia kurudi kwa Mtume (SAW), lakini walipokuwa wakishuka ulivunjika mguu wa Abdullah bin A'tiik na wakambeba mpaka kwa Mtume (SAW), basi alipomuona alimwambia anyoshe mguu wake na akauweka mkono wake na kuupangusa mguu ukawa kama haukupatikana na chochote. Shambulizi la Khaybar: Ulipoingia mwaka wa saba, Mtume (SAW) aliwaamrisha Waislamu wajitayarishe kuwashambulia Mayahudi wa Khaybar ambao waliwachochea sana Waarabu wawapige Waislamu katika vita vya handaki. Ili kuondosha shari yao na kuukata mzizi wa fitina moja kwa moja, alikusanya Mtume (SAW) Mabedui ambao walikuwa pamoja naye katika mapatano ya Hudaybia na kuwaambia kuwa asitoke mtu kufuatana naye katika vita hivi ila mwenye kutaka kupigana jihadi, basi hawakumfuata isipokuwa wale waliomuunga mkono chini ya mti, katika mkataba wa Ridhwaan, ambao idadi yao ilikuwa elfu moja mia nne. Basi baada ya kumwakilisha Siba'a Al-Ghafari hapo Madina, alitoka na jeshi lake na kuelekea Khaybar, akiwa amemchukua katika wakeze Umm Salama. Wanafiki wakawapelekea habari Mayahudi kuwa Waislamu wako njiani wanakuja kuwashambulia, basi Mayahudi wakawapelekea habari kabila la Ghattafaan liwasaidie, na kuwa watawapa nusu ya mavuno ya Khaybar wakiwashinda Waislamu, basi wakatoka kwenda kuwasaidia, lakini walipofika masafa fulani walisikia kama fujo na ghasia, wakadhani kuwa Waislamu wamekwenda kuwashambulia wake zao na mali zao, basi wakarudi mbio na kuwawacha mkono Mayahudi. Mtume (SAW) aliwaita dalili wake wawili wa njia na kuwauliza njia bora ya kuingia Khaybar kwa upande wa kaskazini ili wawazuie wasikimbilie Sham wakiwashambulia, na vile vile kuwazuia Ghattafaan wasiweze kuwafikia. Basi wakamwambia kuna njia nne zote zinawafikisha Khaybar, basi Mtume (SAW) baada ya kutajiwa majina yake, akaichagua moja na wakaifuata hiyo. Njiani, Waislamu wakawa wanaleta takbiri kwa sauti kubwa, Mtume (SAW) akawaambia: Jihurumieni nafsi zenu, kwani nyinyi hamumwiti kiziwi wala asiyekuwepo, nyinyi kwa hakika mnamwita msikivu aliye karibu. Mji wa Khaybar: Jeshi la Mtume (SAW) lilipofika karibu na mji wa Khaybar ambao uko mbali na Madina kwa meli thamanini au mia, lilifanya kambi na kula na kusali na kulala hapo. Alfajiri yake, Mtume (SAW) pamoja na Waislamu walisali Sala ya Asubuhi na gizagiza likaondoka jeshi kuingia Khaybar. Baadhi ya Mayahudi walikuwa wametoka kwenda kwenye mashamba yao, lakini walipoliona jeshi linaingia wakapiga kelele: Muhammad! na kukimbia kurudi kwenye ngome zao. Mtume (SAW) akasema: Allahu Akbar! Imeharibika Khaybar! Allahu Akbar! Imeharibika Khaybar! Nao mji wa Khaybar ulikuwa umegawanyika sehemu mbili: Sehemu moja ilikuwa ina ngome tano na sehemu ya pili ina ngome tatu. Ngome tano katika sehemu ya kwanza ni Na'im na Az-Zubeyr na An-Nizaar na As-Sa'ab bin Mu'adh na Ubay, na sehemu ya pili kulikuwa na Al-Qamuus na Al-Wattiih na As-Sulaalim. Mtume (SAW) akaanza na zile ngome tano. Ikawa anakwenda Mtume (SAW) na baadhi ya vikosi vyake na kuacha vikosi vyengine nyuma. Baada ya kwenda Ali bin Abi Talib kwenye ngome ya Naim na kuwataka Mayahudi wasilimu, Mayahudi walikataa na kwa hivyo vita vikapiganwa kuiteka ngome hii na vikaendelea kwa muda wa siku nyingi na wengi katika viongozi wa kiyahudi wakauliwa walipokuwa wanapambana na Ali bin Abi Talib na Zubeir bin Al-Awwam. Mwishowe Mayahudi wakavunjika moyo na kukimbilia ngome ya pili, na kuwaachia Waislamu ngome hiyo. Ngome ya pili kutekwa ni ngome ya As-Saab bin Muadh, na shambulio hili liliongozwa na Hubaab bin Al-Mundhir Al-Ansari na kuizunguka kwa muda wa siku tatu mpaka wakaweza kuiteka, na kila ikitekwa ngome, Mayahudi walikuwa wakikimbilia ngome nyengineyo, mpaka zikatekwa zote za upande mmoja. Mayahudi wakajikusanya kwenye ngome zilizobakia za upande wa pili, lakini Waislamu wakawafuata na kuwazunguka kwa muda wa siku ishirini. Kisha Mwenyezi Mungu akamjaalia Ali bin Abi Talib aweze kuiteka ngome ya Al-Qamuus na humo akatekwa Safia bint Huyay ambaye Mtume (SAW) baada alikuja kumuoa. Ngome zote zikawa zishatekwa isipokuwa mbili tu, nazo ni ngome ya Al-Wattiih na As-Sulaalim, na Mayahudi walipohisi kuwa kuna hatari ya kumalizwa, waliona bora wafanye mkataba na Mtume (SAW) ili watoke kwa salama na wake zao na watoto wao. Basi wakamuomba watoke na nguo zao za mwilini tu bila kuchukuwa kitu chochote, na Mtume (SAW) akawakubalia. Kisha wakamuomba wabakie Khaybar kwa sharti kuwa mavuno yote yatakayopatikana hapo wagawanye na Waislamu nusu kwa nusu, basi Mtume (SAW) akawakubalia vile vile. Mayahudi wa Fadak waliposikia haya, walimuomba Mtume (SAW) awakubalie na wao jambo kama hilo bila ya kupigana, basi akawakubalia na ikawa Fadak ni ghanima ya Mtume (SAW) peke yake, kwa sababu haikutekwa kwa vita. Halikadhalika, Mayahudi wa Taymaa wakaomba waachiwe waishi katika nchi yao na wao walipe jizya, basi Mtume (SAW) akawakubalia. Jaribio la kumtilia sumu Mtume (SAW) Katika shambulizi hili, Waislamu hawakupata hasara sana, maana waliokufa katika wao ni wanaume kumi na tano tu, lakini katika Mayahudi waliuliwa tisini na tatu. Ama faida waliyoipata ni kubwa sana, maana waligawanyiwa ardhi ya Khaybar ambayo ilikuwa imejaa mitende na matunda mengine, na mali na silaha nyingi sana. Pamoja na hayo, kulitokea jaribio la kutaka kumuua Mtume (SAW) kwa njia ya kumtilia sumu katika chakula, na hili jaribio alilifanya mwanamke wa kiyahudi aliyekuwa akiitwa Zaynab ambaye alimtayarishia Mtume (SAW) na Masahaba zake mbuzi wa kuchoma na kumjaza sumu, basi alipotaka kutia mdomoni Mtume (SAW) akaletewa Wahyi kuwa ana sumu akajizuiya kumla, lakini sahaba wake mmoja aitwaye Bishr bin Al-Barraa alikuwa keshaila nyama, basi akafa. Mtume (SAW) akamwita na kumuuliza kwanini akafanya hivi, naye akasema kuwa ikiwa yeye ni Nabii, basi haitomdhuru, na ikiwa ni mwongo, basi Mwenyezi Mungu atatuondoshea. Mtume (SAW) akamsamehe, lakini baada ya kufa Bishr, aliamuru auliwe kwa kulipiza kisasi cha Bishr. Aidha, Mtume (SAW) aliwaua watoto wawili wa Abul-Haqiiq ambao, juu ya mkataba waliofanya Mayahudi na Mtume (SAW) wa kutochukua chochote katika mali yao, watoto hawa walificha mali nyingi, basi baada ya kugundulikana alimuamuru Muhammad bin Maslama ambaye ndugu yake aliuliwa Khaybar awaue. Kuolewa kwa Safia: Baada ya shambulizi la Khaybar, na kutekwa Safia bint Huyay, mtoto wa mkubwa wa Banin-Nadhiir, alimuoa Mtume (SAW) Safia na kumpa mahari kwa kumjaalia si kijakazi tena bali ni mmojawapo wa mamama wa Waislamu. Kutekwa kwa Wadil-Quraa: Mtume (SAW) alipomaliza kuiteka Khaybar, aliwapelekea habari Mayahudi wa Wadil-Quraa na kuwataka wasilimu au wasalimu amri na kukubali kushindwa, nao wakakataa, basi Mtume (SAW) akenda na jeshi lake na walipofika Mayahudi walikuwa tayari wanawasubiri, wakaanza kuwarushia mishale akauliwa mmoja katika Waislamu. Mtume (SAW) akanadhimu jeshi lake na kumpa bendera Saad bin Ubada, na bendera Hubaab bin Al-Mundhir, na nyengine Sahl bin Hanif, na nyengine Abaad bin Bishr, na kuwataka tena wasilimu nao wakakataa, na akatoka mmoja katika Mayahudi ili apigane na mmoja katika Waislamu, akajitokeza Az-Zubeyr bin Al-Awwaam na kumuua, kisha akaja mwengine ambaye vile vile alimuua, kisha akajitokeza mwengine, akasimama Ali bin Abi Talib akapigana naye na kumuua, mpaka wakauliwa Mayahudi kumi na moja. Ilipoingia siku ya pili, Mayahudi wakasalimu amri na kuwapa Waislamu kila walichokuwa nacho, zikawa ghanima nyingi. Mtume (SAW) akazichukua na kuzigawa baina ya Masahaba walioshuhudia vita hivi. Kisha Waislamu wakakaa kwa muda wa siku nne hapo na wakapatana na Mayahudi wabakie kwenye kijiji chao na mashamba yao, na mavuno yatakayopatikana wagawane nusu kwa nusu kama walivyokubaliana na watu wa Khaybar. Walipokuwa wanarudi Madina walilala njiani ukiwa usiku ushakuwa mwingi sana, basi Mtume (SAW) akamwambia Bilal awaamshe, lakini Bilal alichukuliwa na usingizi akashindwa kuamka mpaka jua likachomoza wakakosa Sala ya Alfajiri. Mtume (SAW) akawa wa kwanza kuamka, na baada ya kuwaamsha wengine walikwenda mwendo kidogo, kisha akawaamrisha ikasimamishwa Sala na wakasali kadhaa. Kuharimishwa Mut'a na Punda: Aidha, baada ya ushindi wa Khaybar, Waislamu walikatazwa kuoa ndoa ya Mut'a, ambayo ni ndoa ya muda iliyokuwa ikifanyika katika zama za Ujahili, nayo ni kwa mwanamume kumuoa mwanamke kwa muda fulani tu, kisha akimwacha. Halikadhalika, Waislamu wakakatazwa kula nyama ya punda ambayo kabla yake walikuwa wakila. Waliohamia Habasha warudi: Waislamu waliporudi Madina na ghanima zao na ushindi mkubwa walioupata huko Khaybar, furaha yao ilizidi ilipokutanika na furaha ya kurudi kwa ndugu zao Waislamu kutoka Habasha, na Mtume (SAW) akafurahi sana kumpokea binamu yake Ja'afar bin Abi Talib mpaka akasema: Wallahi, sijui nifurahi kwa lipi? Kwa kuiteka Khaybar au kwa kurudi Ja'afar? Ja'afar alirudi pamoja na Umm Habiba bint Abi Sufyan ambaye Mtume (SAW) alimposa kwa An-Najashi akiwa bado yuko Habasha, na alipokubali alitoa An-Najashi dinari mia nne kama mahari yake. Aidha, alikuja pamoja naye Abu Musa Al-Ash'ari na jamaa zake, na Mtume (SAW) kwa furaha yake aliwapa wote waliokuwemo ndani ya merikebu hii, sehemu ya ghanima zilizopatikana Khaybar. Al-Hajjaj awahadaa Makureshi: Baada ya kumalizika shambulizi la Khaybar, aliomba ruhusu Al-Hajjaj bin I'laatt kutoka kwa Mtume (SAW) kwenda Makka kukusanya mali yake ambayo ilikuwa mikononi mwa wafanyibiashara wa huko Makka, naye akichelea isipotee mali yake baada ya kusilimu. Basi Mtume (SAW) akamruhusu na akafunga safari kwenda Makka. Alipofika Makka aliwakuta Makureshi wamo katika kutafuta habari za Mtume (SAW) baada ya kusikia kuwa ametoka kwenda kushambulia Khaybar, basi walipomuona Al-Hajjaj anaingia walijua kuwa watapata habari za Muhammad kutoka kwake. Makureshi walipomuuliza aliwaambia kuwa Waislamu wameshindwa vibaya sana, na Masahaba wengi wameuliwa, na Muhammad mwenyewe amekamatwa mateka na Mayahudi. Makureshi, kwa kuwa walikuwa hawajui kuwa amesilimu, walifurahishwa sana na habari hii, na alipowaambia wamsaidie kumkusanyia mali yake iliyoko mikononi mwa wafanyibiashara, ili awahi kwenda Khaybar kufanya biashara, basi wakamsaidia upesi upesi akapata mali yake yote. Akaja Al-A'bbas bin AbdulMuttalib na kumuuliza habari aliyoisikia, naye akamwambia asubiri mpaka amalize kukusanya mali yake, kisha wakutane nje, basi walipokutana, akamwambia kuwa amemwacha mtoto wa ndugu yake bwana arusi amemuoa binti wa mfalme wa Khaybar, na kuwa ameshaiteka Khaybar na wamepata ghanima nyingi sana, lakini asiseme mpaka zipite siku tatu. Basi baada ya kupita siku tatu, Al-Abbas alivaa nguo zake nzuri na kujitia manukato na kutoka kwenye Al-Kaaba na kutufu. Makureshi wakamwambia kuwa kufanya hivi ni kujaribu kustahmili msiba mkubwa uliomfika. Naye akawajibu kuwa yeye anawaapia kuwa Muhammad ameshaiteka Khaybar na hivi sasa ni bwana arusi wa binti ya mfalme wao na kuwa amepata mali mingi huko Khaybar. Wakamuuliza ni nani aliyempasha habari hizo, naye akawajibu kuwa yule aliyewaambia kuwa Muhammad amekamatwa, na kuwa yeye alikuja kwao akiwa Muislamu na kuchukuwa mali yake na kwenda zake kwa Muhammad na Masahaba zake. Makureshi wakasema: Ametuponyoka adui wa Mwenyezi Mungu, na wallahi lau tungejua angekiona chake. Kisha haukupita muda Makureshi wakapata habari ya Mtume (SAW) ya kuiteka Khaybar.
|
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|