Viungo

Fatawa

Masuala

Dua

Tarehe

Sira

Fiqhi

Sunna

Qurani

Maskani

Habari

Elimu

Afya
Nchi
Michezo
Vyakula
Riyadha
Masomo
Nasiha
Kamusi
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
      

 

      SERA

 

MAISHA YA MTUME

 

       
       
       
       

 
13-
 
Hotuba ya Mtume baada ya ushindi
14-
 
Ansari wakhofu Mtume asirudi Madina
15-
 
Masanamu yavunjwa
16-
 
Shambulizi la Huneyn
17-
 
Washirikina watiwa mbioni
18-
 
Shambulizi la Taif
19-
 
Ghanima za Huneyn zagawanywa
20-
 
Kuja kwa ujumbe wa Hawazin
21-
 
Umra ya Ju'rana
22-
 
Vikosi vyapelekwa na tume zapokewa
23-
 
Kikosi cha Bishr bin Sufyan
24-
 
Tume ya Al Walid bin U'qba


1-
  
Kutangaa kwa Uislamu
2-
  
Mtume apeleka risala kwa Najashi
3-
  
Kutekwa kwa Makka
4-
  
Abu Sufyan akutana na Mtume
5-   Mtume ajitayarisha kwenda Makka
6-   Waislamu wafunga kambi Marudh-Dhahran
7-   Abu Sufyan akiri nguvu za Waislamu
8-   Jeshi la Mtume laingia Makka
9-   Mtume asali ndani ya Al Kaaba
10- Mtume asamehe Makureshi
11- Ufunguo wa Al-Kaaba warudishiwa wenyewe
12-
Bilal aadhini juu ya Al Kaaba
 

 

Kutangaa kwa Uislamu:

            Baada ya mapatano ya Hudaybiya, Waislamu walikuwa wamemakinika na hawana kinachowatia wasiwasi wala khofu, kwa sababu Makureshi ambao ndio waliokuwa ni nguvu yenye kuogopewa na kuheshimiwa na Waarabu wote, sasa hawana ugomvi nao na walikuwa na haki ya kutangaza dini yao kote Arabuni. Kwa hivyo, Mtume (SAW) akaamua kuwapelekea risala wafalme wa nchi mbali mbali zilizokuwa zikijulikana wakati ule na kuwaarifu kuhusu Uislamu, na ilivyokuwa ni desturi ya wafalme kutumia pete yenye mihuri yao katika mawasiliano yao, basi Mtume (SAW) alitengeneza yake ikaandikwa:

Muhammadun Rasuulullah

"محمد رســـــــــــول اللــه " 

            Ulipoingia mwaka wa saba, Mtume (SAW) akachagua watarishi wake na kuwatuma kupeleka risala zake kwa wafalme mbali mbali, na hizi zifuatazo ni risala zake kwa hawa wafalme

Mtume (SAW) apeleka risala kwa Najashi: 

            Amesimulia Al-Bayhaqi kutokana na Ibn Is-haq kuwa Mtume (SAW) amepeleka risala hii kwa mfalme wa Habasha An-Najashi Al-Ass-hum na kumwambia: Hii ni risala kutoka kwa Muhammad Nabii kwenda kwa Najashi Al-Ass-hum, Mtukufu wa Habasha. Amani kwa yule aliyefuata uongofu, na akamwamini Mwenyezi Mungu na Mtumewe, na ninashuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake, hana mshirika, hakuwa na mke wala mwana, na kuwa Muhammad ni mja wake na mjumbe wake, na nikauita mwito wa Uislamu, kwa Mimi ni Mtume wake, basi silimu utasalimika (Enyi watu wa Kitabu, njooni kwenye neno la sawa baina yetu na nyinyi, ya kuwa tusimwabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na kitu chochote, wala baadhi yetu tusiwafanye wengine waola badala ya Mwenyezi Mungu, na wakikataa basi semeni shuhudieni kuwa sisi ni Waislamu), na ukikataa basi ni juu yako dhambi za Manasara katika watu wako

            Risala ya Mtume (SAW) ilipomfikia Najashi aliisoma na kusilimu na akamjibu Mtume (SAW) risala yake na kumwambia: Kwa Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Najashi Ass-hum. Amani juu yako ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na rehema yake na baraka zake, Mwenyezi Mungu ambaye hapana mola isipokuwa Yeye. Ama baada ya salamu: Risala yako imenifikia ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu katika uliyoyataja kuhusu Isa, na ninaapa kwa Mola wa mbingu na ardhi, kuwa Isa hazidi kuliko hayo uliyoyataja, naye ni kama hivyo ulivyosema, na tumejua yale uliyoletewa kwetu nayo, na tumempokea binamu wako na masahaba zako, na ninashuhudia kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu msema kweli mwenye kusadikiwa, nami nimekukubali na nimemkubali binamu wako na nimesilimu katika mikono yake kwa Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.

            Na alipokufa Najashi katika mwaka wa tisa wa Hijra, Mtume (SAW) alitangaza kifo chake na kumsalia Sala ya maiti aliyekuwa hayupo mbele yake, kwani alikufa Habasha.

Kutekwa Makka: 

            Mji wa Makka ulikuwa tangu zamani ndio mji wenye umuhimu mkubwa sana wa kidini kwa Waarabu, kwa sababu ya uhusiano wake na Al-Kaaba, nyumba ya kwanza kabisa iliyojengwa na Nabii Ibrahim na Nabii Ismail kwa ajili ya kuabudiwa Mwenyezi Mungu Mmoja, na kwa hivyo, Waarabu walikuwa wakiona kuwa wenye kuutawala mji huu mtukufu kwa Waarabu wote ndio wenye kustahiki heshima ya Waarabu wote.  

            Mtume (SAW) alikuwa akijua jambo hili na alikuwa akitamani sana Makka iingie chini ya utawala wa Waislamu, lakini kwa sababu ya ahadi na mkataba wa amani walioandikiana na Makureshi, alikuwa hawezi kuvunja ahadi hii na hawezi kuishambulia Makka kivita kwa sababu ya utukufu wake na kujaaliwa kwake na Mwenyezi Mungu kuwa ni mahali pa amani, lakini Mwenyezi Mungu akitaka kupitisha amri yake, huleta sababu ili jambo linalotaka kufanywa lifanyike, na kwa hivyo kukazuka jambo ambalo likasababisha kutekwa kwa Makka

            Kama tulivyoeleza nyuma, wakati Mtume (SAW) alipofanya sulhu ya Hudaybia na Makureshi, makabila fulani yakajiunga upande wa Waislamu na makabila mengine yakajiunga na Makureshi. Katika hayo, Khuza'a likajiunga na Waislamu, na Banu Bakr likajiunga na Makureshi, na kuwa kukitokea vita vyovyote, Waislamu watawasaidia Khuza'a na Makureshi watawasaidia Banu Bakr. Watu wakaishi kwa amani kwa muda wa miezi kumi na saba au na nane, kisha Banu Bakr wakawachokoza Khuza'a na kuua watu wao na wakawasaidia katika vita hivi Makureshi.

            Akatoka A'mr bin Salim Al-Khuza'i na kwenda Madina kumpasha Mtume (SAW) habari ya mambo yaliyotokea, na Mtume (SAW) akamwambia: Umenusuriwa Ewe A'mr bin Salim. Kisha akaja Budayl bin Warqaa Al-Khuza'i na baadhi ya watu wa kabila lake kumshtakia Mtume (SAW) na kumueleza waliyoyafanya Makureshi ya kuvunja mkataba ulioko baina yao

Abu Sufyan akutana na Mtume: 

            Baada ya kuguta Makureshi na kutambua kuwa wamefanya makosa kwa kuvunja ahadi baina yao na Waislamu, walifanya haraka kumpeleka kiongozi wao Abu Sufyan kwa Mtume (SAW) ili kuuthibitisha mkataba uliokuweko baina yao, lakini Mtume (SAW) hakumjibu neno. Kisha akenda kwa Abubakar kujaribu kumwambia azungumze naye, lakini pia alikataa, na kadhalika Umar na Ali, wote wakakataa, basi Abu Sufyan akapanda ngamia wake na kurudi Makka, na huko Makureshi walipomuuliza aliwaeleza yaliyotokea na kuwa hakufaulu kumkinaisha Mtume (SAW) wala Masahaba zake kuhusu kukubaliana tena juu ya mkataba wao.

Mtume (SAW) ajitayarisha kwenda Makka: 

            Kwa hivyo, katika mwezi wa Ramadhan mwaka wa nane wa Hijra, Mtume (SAW) aliwaambia Masahaba zake wajitayarishe kwenda Makka, na akamuomba Mwenyezi Mungu habari hizi zisiwafikie Makureshi. Mmoja katika Masahaba aitwaye Haattib bin Abi Balta'a ilimuingia khofu kwa kuwepo mkewe na mwanawe huko Makka, akaandika barua kuwapelekea Makureshi kuwaarifu kuja kwa Waislamu, lakini Mwenyezi Mungu akamfichulia jambo hili Mtume (SAW) na akamtuma Ali bin Abi Talib na Az-Zubeir bin Al-Awwam kumfuata mwanamke kijakazi aliyepewa barua hiyo, na walipompata njiani alikataa kuwa amepewa barua yoyote, basi Ali akamwambia kuwa Mtume (SAW) hasemi uwongo na utaitoa barua au tutakuvua nguo zote, basi akaogopa na kuitoa, ikawa Makureshi hawakupata habari yoyote ya kutoka Waislamu kuelekea Makka

            Mtume (SAW) aliondoka Madina na Masahaba elfu kumi na kumweka Madina kama mwakilishi wake Abu Ruhm Al-Ghafaari, wakiwa wote wamefunga saumu ya Ramadhani. Kisha njiani akakutana na ami yake Al-Abbas na mkewe na wanawe wanaelekea Madina kusilimu, na akakutana alipofika Al-Abwaa na binamu yake Abu Sufyan bin Al-Harith, na mtoto wa shangazi lake Abdullahi bin Umayya wamekuja kutaka radhi na kusilimu, akawa hataki kuwapokea kwa sababu ya udhia mkubwa waliokuwa wakimfanyia, lakini baada ya kuombewa na Umm Salama na kuelekezwa na Ali, walikwenda tena na kumuomba akawapokea. Waislamu walipofika Al-Kadid, Mtume (SAW) alitaka aletewe maji na akanywa kufungua saumu na Waislamu wakafanya kama alivyofanya.

Waislamu wafunga kambi Marudh-Dhahran: 

            Mtume (SAW) na jeshi lake waliingia usiku Marudh-Dhahran, wakafunga kambi hapo, na Mtume (SAW) akawaamrisha wawashe moto na ikawa mioto elfu kumi inawaka. Abu Sufyan ambaye alikuwa akitoka kutafuta habari za Mtume (SAW) na alikuwa pamoja na Hakim bin Hizam na Budayl bin Warqaa.

Huku ami yake Mtume (SAW) Al-Abbas baada ya kusilimu alipanda nyumbu wa Mtume (SAW) na kutoka kutafuta wakata kuni au mtu yeyote ambaye atakayeweza kuwafikishia Makureshi habari ya kuja kwa Mtume (SAW) ili waje kutaka amani kwake kabla ya kuingia Makka.

            Mara Al-Abbas akasikia sauti ya Abu Sufyan akijadiliana na Budayl kuhusu mienge ya moto waliyoiona. Akasema Abu Sufyan: Sikuwahi kuona mioto mingi wala askari wengi kama usiku huu wa leo. Budayl akamwambia: Hili wallahi ni kabila la Khuza'a limekasirishwa na vita walivyofanyiwa. Akajibu Abu Sufyan: Khuza'a ni wachache zaidi na wanyonge zaidi kuweza kuwa na moto kama huu au maaskari kama hawa. Basi alipoitambua Al-Abbas sauti ya Abu Sufyan alimwita: Abu Handhala? naye akaitambua sauti ya Al-Abbas na kumwitikia: Abul-Fadhl? Al-Abbas akamjibu: Ndiyo. Akamwambia: Una nini? Akamwambia: Huyu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na watu wake

            Abu Sufyan akamuuliza: Nifanye nini? Al-Abbas akamjibu: Wallahi, akikupata atakukata kichwa chako, basi bora upande nyuma yangu juu ya nyumbu huyu ili nikupeleke kwa Mtume (SAW) nikutakie amani. Basi akapanda nyuma yake na kwenda kwa Mtume (SAW). Walipokuwa wanakwenda walipita mioto mingi ya Waislamu wakawa Waislamu wanaulizana ni nani huyu, lakini wanapomuona nyumbu wa Mtume (SAW) na ami yake juu yake, basi wanajua kuwa ni Al-Abbas, mpaka walipopita kwenye moto wa Umar bin Al-Khattab naye ndiye aliyekuwa mkubwa wa walinzi usiku ule, akauliza na alipomuona Abu Sufyan akasema: Abu Sufyan, adui wa Mwenyezi Mungu. Alhamdulilah kwa kukupata bila ya mkataba wala ahadi. Kisha akatoka kumkimbilia Mtume (SAW) na nyumbu vile vile akakimbia akampita, akafika Al-Abbas na Umar akaingia na kusema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, huyu Abu Sufyan niachie nimkate kichwa chake. Naye Al-Abbas akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nimemuingiza chini ya himaya yangu.  

            Mtume (SAW) alipoona Umar na Al-Abbas wanashindana kuhusu Abu Sufyan, alimwambia amchukuwe na akae naye mpaka asubuhi kisha amlete kwake. Basi asubuhi yake alipoletwa kwa Mtume (SAW) walizungumza kisha akasilimu. Al-Abbas akamwambia Mtume (SAW) kuwa Abu Sufyan ni mtu anayependa mambo ya fakhari, basi mjaaliye kitu chochote. Akasema: Atakayeingia kwenye nyumba ya Abu Sufyan atakuwa katika amani, na mwenye kujifungia nyumbani mwake atakuwa katika amani, na mwenye kuingia kwenye msikiti mtukufu atakuwa katika amani.

Abu Sufyan akiri nguvu za Waislamu: 

            Asubuhi ya Jumaane, tarehe 17 ya mwezi wa Ramadhani, Mtume (SAW) alimwamrisha Al-Abbas amzuiliye Abu Sufyan juu ya kilima katika sehemu nyembamba ya bonde ili aone vikosi vya kiislamu vikipita. Ikawa kila kabila likipita na bendera yake huuliza ni nani hao, na akijibiwa kuwa ni kabila fulani, husema limenihusu nini mimi, na akaendelea hivyo hivyo akiuliza na kujibiwa mpaka akapita Mtume (SAW) na kikosi chake cha kijani akifuatana na kundi kubwa la Muhajirina na Maansari, haoni kwao chochote isipokuwa mavyuma vilivyowazunguka. Akasema: Subahanallahi ewe Abbas, ni nani hawa? Akamjibu: Huyu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Muhajirina na Maanasari. Akasema: Hapana yeyote mwenye kuwaweza hawa wala mwenye nguvu dhidhi yao. Kisha akasema: Wallahi, ewe Abul-Fadhl, hakika ufalme wa mtoto wa ndugu yako leo umekuwa mkubwa. Al-Abbas akamwambia: Ewe Abu Sufyan, huo ni utume. Akasema: Basi ni jambo jema lilioje hilo. Al-Abbas akamwambia: Kimbilia watu wako upate kuwaokoa

Rudi Juu

Jeshi la Mtume laingia Makka

            Jeshi lilipokuwa tayari kuingia Makka, Mtume (SAW) alimuamuru Khalid bin Al-Walid na kikosi chake kilichokusanya makabila ya Aslam na Sulaym na Muzayna na Juhayna na kabila nyenginezo za kiarabu kuingia kutokea chini ya Makka, na mwenyewe Mtume (SAW) akaingia na jeshi lake kutokea kwa juu ya Makka, akiwa ameinamisha kichwa chake kumnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa kumpa ushindi huu mkubwa, huku ikishikiliwa bendera yake na Az-Zubeyr bin Al-Awwam, na akamuamuru Abu Ubeyda bin Al-Jarrah aingie na watu wake bila silaha kupitia katikati ya bonde la Makka, na akawaamrisha maamirijeshi wake wasipigane isipokuwa na wale watakaowapiga, na wakiwapiga basi wamalizeni.

            Mtume (SAW) akaingia Makka juu ya ngamia wake na nyuma yake amempandisha Usama bin Zayd mpaka akaingia msikiti mtukufu na kulielekea jiwe jeusi na kulibusu. Kisha akatufu Al-Kaaba mara saba akiigusa nguzo ya yamani na jiwe kwa kigongo alichokuwa nacho mkononi, na wakati huo Al-Kaaba ilikuwa imezungukwa na masanamu mia tatu na sitini (360), kwa hivyo alikuwa Mtume (SAW) kila akilipita sanamu hulichocha kwa kigongo alichokuwa na kusema: Haki imekuja na batili imeondoka. Kisha akaamrisha itolewe miungu kwenye Al-Kaaba, na hii ndio siku ya kwanza kusafishwa Al-Kaaba kutokana na hii miungu ya uwongo, na kutoweka ibada ya masanamu katika Bara Arabu.

Mtume (SAW) asali ndani ya Al-Kaaba:

            Baada ya kutolewa masanamu, Mtume (SAW) akaingia ndani ya Al-Kaaba pamoja na Usama na Bilal na kufunga mlango, kisha akaelekea ukuta unaokabiliana na mlango na kusali hapo, kisha akaizunguka kwa ndani na kuleta humo takbiri na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Huko nje, Makureshi wakajikusanya na kujazana ndani ya msikiti kusubiri nini atafanya Mtume (SAW). Mlango wa Al-Kaaba ukafunguliwa akatoka Mtume (SAW) na kushikilia mlango na watu wako kwa chini yake, akasema: Hapana mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika, amesadikisha ahadi yake, na amemnusuru mja wake, na amewashinda makundi (ya majeshi) peke yake.

Mtume (SAW) asamehe Makureshi:

            Mtume (SAW) akasali kwenye Maqaamu Ibrahim na kwenda kwenye Zamzam na kunywa maji yake, kisha akakaa msikitini na watu wote wanamtumbulia macho kutazama nini atawafanya Washirikina wa Makka. Mtume (SAW) akasema: Enyi Makureshi! Hakika Mwenyezi Mungu amekuondosheni hamasa ya Ujahili na kujitukuza kwa jadi. Watu wote wanatokana na Adam, na Adam anatokana na udongo, kisha akasoma Aya hii: Q.49:13

            Kisha akasema: Enyi jamii ya Makureshi! Nini mnaona mimi nitakufanyeni? Wakasema: Kheri. Ndugu mtukufu na mtoto wa ndugu mtukufu. Akasema: Basi mimi ninakuambieni kama Yusuf alivyowaambia nduguze: Hapana lawama juu yenu leo. Nendeni zenu kwani nyinyi ni huru. Kisha akataja watu fulani ambao vichwa vyao vilikuwa halali kukatwa wakipatikana kwa uovu wao mkubwa walioufanya dhidi ya Mtume (SAW) na Uislamu, lakini wengine wakabahatika kuombewa na wakasamehewa na kusilimu, na wengine wakauliwa.

            Aidha, Mtume (SAW) alieleza siku hiyo baadhi ya hukumu mbali mbali za dini ya Uislamu, na alipomaliza watu wakaanza kwenda kutoa ahadi kwake ya kumkubali kuwa ni Mtume na kusilimu, na katika waliosilimu hapo Muawiya bin Abi Sufyan na Abu Quhafa babake Abubakar Assiddiq, akafurahi sana Mtume (SAW) kwa hilo.

            Baada ya kumaliza kuchukuwa ahadi kutoka kwa wanaume, Mtume (SAW) alichukuwa ahadi kutoka kwa wanawake ya kuwa hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatawaua watoto wao, wala hawatazua uwongo kwa makusudi, wala hawatamuasi Mtume (SAW).

Ufunguo wa Al-Kaaba warudishwa kwa wenyewe:

             Kisha alikaa Mtume (SAW) katika msikiti, akasimama Ali bin Abi Talib na ufunguo wa Al-Kaaba mkononi mwake na kumwambia Mtume (SAW): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tukusanyie kazi ya kuitazama Al-Kaaba na kuwapa maji mahujaji. Mtume (SAW) akasema: Yuko wapi Uthman bin Talha. Alipoitwa alimwambia: Shika ufunguo wako ewe Uthman, leo ni siku ya wema na uaminifu.

Bilal aadhini juu ya Al-Kaaba:

            Ulipowadia wakati wa Sala, Mtume (SAW) akamuamrisha Bilal kupanda juu ya Al-Kaaba na kuadhini, na hii ilikuwa ni siku muhimu sana kwa Waislamu kwani Makka kama tunavyojua ndio msingi na chanzo cha din ya Nabii Ibrahim, na ni mahali ambapo ipo nyumba ya kwanza iliyojengwa kwa sababu ya kumuabudu Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, ushindi huu wa kuiteka Makka ni ushindi mkubwa kabisa kwa Waislamu

            Baadaye, Mtume (SAW) aliingia kwenye nyumba ya Umm Hani bint Abi Talib nduguye Ali bin Abi Talib na kuoga na kusali humo ndani.

Hotuba ya Mtume (SAW) baada ya ushindi:

            Siku ya pili baada ya kuiteka Makka, Mtume (SAW) alisimama kuwahutubia watu. Akamshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu na kumtukuza kama anavyostahiki, kisha akasema: Enyi watu, hakika Mwenyezi Mungu ameitukuza Makka siku alipoumba mbingu na ardhi, kwa hivyo ni tukufu kwa kuitukuza Mwenyezi Mungu mpaka siku ya Kiyama, basi haijuzu kwa mtu anayeamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho kumwaga damu ndani yake, au kuukata mti ndani yake, na ikiwa mtu anataka ruhusa kupigana na Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi semeni: Hakika Mwenyezi Mungu amemruhusu Mtume wake wala hakukuruhusuni nyinyi, na kwa hakika mimi nimeruhusiwa saa katika mchana mmoja, na utukufu wake usharudi leo kama utukufu wake wa jana, basi naamfikishie mwenye kuwepo yule aliyekuwa hayupo.

Wasiwasi wa Maansari juu ya kurudi Mtume (SAW) Madina:

            Maansari waliingiwa na wasiwasi baada ya Mtume (SAW) kuiteka Makka na kuhisi kuwa maadamu sasa amesharudi kwao, hatotaka tena kurudi Madina, na wakawa wanazungumza baina yao kuhusu mas-ala haya. Mtume (SAW) akawauliza nini wanachozungumza naye wakati huu alikuwa amesimama juu ya jabali la Safa anamuomba Mwenyezi Mungu, wakasema: Si neno. Lakini Mtume (SAW) akawashikilia, na wao wakamwambia, basi akawaambia: Ninajikinga kwa Mwenyezi Mungu, uhai ni uhai wenu na mauti ni mauti yenu.

Masanamu yavunjwa:

            Mtume (SAW) akabakia Makka baada ya kuiteka kwa muda wa siku kumi na nane, akipunguza Sala, na kuwafundisha watu juu ya Uislamu, na kuwapeleka watu kuvunja masanamu yaliyokuweko Makka na pembezoni mwa Makka. Yakavunjwa masanamu yote, na akamtuma mtu atangaze kuwa yeyote mwenye sanamu nyumbani alivunje.

            Kisha akamtuma Khalid bin Al-Walid na wapanda farasi thalathini kwenda kulivunja sanamu kubwa la Makureshi liitwalo Al-Uzza, akenda na kulivunja, na akamtuma A'mr bin Al-A'as kwenda kuvunja sanamu la Huzayl liitwalo Suwa'a, akenda na kulivunja, na akamtuma Saad bin Zayd na wapanda farasi ishirini kwenda kuvunja sanamu la Kalb na Khuza'a liitwalo Manaat, akenda na kulivunja, ikawa Makka imetahirishwa na masanamu waliokuwa wakiyaabudu Washirikina.

Shambulizi la Huneyn:

            Baada ya kutekwa Makka na kuvunjwa masanamu kila upande, aghlabu ya Waarabu walimkubali Mtume (SAW) na kuingia katika Uislamu, lakini makabila mawili ya kiarabu yalikataa kushindwa na kumfuata Mtume (SAW), na kwa hivyo, wakajitayarisha kupigana naye kwa kuchukulia kuwa maadamu keshawashinda jamaa zake Makureshi, hapana litakalomzuia kwenda kuwapiga wao

            Makabila haya, Hawazin na Thaqif, walikutana viongozi wao na kushauriana juu ya jambo hili na kufikia uamuzi kuwa watoke kwenda kuwahujumu Waislamu kabla Muhammad na jeshi lake kuja kuwahujumu wao, na kwa hivyo wakamchagua Malik bin A'uf awe kiongozi wao, naye akatoa shauri watoke watu wote pamoja na wake zao na watoto wao na wanyama wao kwenda vitani ili hamasa ya wapiganaji izidi na wasiweze kukimbia kwa kuwaogopea wake zao na watoto wao.

            Fikra hii haikumfurahisha Durayd ambaye alikuwa ni mmoja katika viongozi wao mkubwa mwenye rai nzuri daima na mpiganaji vita hodari, na akamwambia Malik kuwa mwenye kushindwa hapana jambo litakalomzuia asikimbie, na kuwa mpiganaji hafaliwi isipokuwa na silaha yake, lakini Malik asisikilize rai yake na kwa hivyo kukaamuliwa watu wote na mali yote ichukuliwe vitani

            Mtume (SAW) alipopata habari hii alifurahi sana, na akasema kuwa hizo ni ghanima za Waislamu inshallah. Akamweka Makka I'taab bin Usayd kama mwakilishi wake na akatoka na watu elfu kumi na mbili, elfu kumi aliokuja nao kutoka Madina, na elfu mbili walimfuata kutoka Makka, katika watu waliosilimu ilipotekwa Makka, na Waarabu wengine pembezoni mwa Makka. Waislamu wengine walipojiona ni wingi sana walisema kuwa hatutoshindwa leo kwa uchache wetu, na wakasahau kuwa wangapi kidogo waliwashinda wengi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu

            Waislamu walipofika Huneyn, yalikuwa makabila ya Hawazin na Thaqif na makabila mengine ya Qays Aylan yameshafika na kujitawanya katika sehemu mbali mbali kwenye mabonde na milima na mapitio ya njia mbali mbali kuwasubiri Waislamu waje, na kupewa amri wawapige mishale watapotokea na kuwavamia kwa pamoja.

            Mtume (SAW) alimpa bendera ya Muhajirina Ali bin Abi Talib, na bendera Al-Khazraj Hubab bin Al-Mundhir, na bendera ya Aus akampa Usayd bin Hudhayr, na kuwapa makabila mengine bendera zao, na ilipoingia asubuhi, Mtume (SAW) aliwaamrisha wateremke kwenye bonde la Huneyn, lakini walipofika kwenye mapitio ya majabali kuingia kwenye bonde, Waislamu walipigwa na mshangao kwa mishale mingi iliyokuwa ikiwateremkia, wakaanza kufazaika na kukimbizana na kurudi nyuma, jambo ambalo liliwapa Makafiri nafasi ya kuwafuata na kuwapiga na kuwaua

            Kizaazaa kikaingia na khofu ikazagaa na kila mtu akawa hajui afanye nini au akimbie wapi. Mtume (SAW) akajitenga upande wa kulia na kuthibiti sehemu moja na kuanza kuwapigia kelele Waislamu wathibiti, lakini kuwepo kwa watu ambao ndio kwanza wameingia Uislamu na imani zao ni dhaifu kulileta mchafuko mkubwa kabisa mpaka Mtume (SAW) alipomwambia Al-Abbas ami yake ambaye alikuwa amesimama naye apige kelele kuwaita Masahaba zake katika Muhajirina na Maansari, naye ni mtu ambaye alikuwa na sauti kubwa kabisa, basi akautoa ukelele mmoja mkubwa kuwaita Masahaba zake Mtume (SAW) walioshuhudia mkataba wa Ridhwan na waliposikia tu wote wakawa wanarudi kwa nguvu moja kuiendea sauti ilipo

            Haukupita muda mara Masahaba wakawa washamzonga Mtume (SAW) na wako chini yake wanapigana kwa ushujaa mkubwa kabisa. Mtume (SAW) akachukuwa mkononi mwake gao la mchanga na kuurusha, na hapo hapo Mwenyezi Mungu akajaalia mchanga ule kuingia machoni mwa kila aliyekuwepo katika Makafiri na kubabaishika, wakawa Waislamu wanawafuata kuwapiga na kuwaua na wao wanakimbizana na kutupa wake zao na watoto wao na mali zao na wanyama wao na kila kitu kukimbilia roho zao

            Fazaa kubwa ikaingia, waliokimbia wakakimbia na waliokamatwa wakakamatwa katika makafiri, na mateka wakawa wengi katika wanawake na watoto, na Waislamu wakapata kiasi cha wanawake elfu sita na ngamia elfu ishirini na nne, na zaidi ya mbuzi elfu arubaini na wakia elfu nne za fedha, na mali yote hayo yakakusanywa mahali paitwapo Ju'rana.

            Mwenyezi Mungu akawasumbulia Waislamu na kuwazindua kuhusu hakika muhimu ya kivita katika Aya zake tukufu zisemazo: Q.9:25-26. 

Rudi Juu

Washirikina watiwa mbioni

            Baada ya mambo kubadilika, na ushindi wa Makafiri kugeuka kuwa kushindwa, walitawanyika Washirikina na kukimbilia sehemu mbali mbali. Kundi likakimbilia Awtaas, na kundi likenda Nakhla, na kundi likaelekea Taif. Mtume (SAW) akapeleka vikosi vyake kufuata makundi haya, na kikatoka kikosi kikiongozwa na Abu A'amir Al-Ash'ari kulifuatia kundi lililokimbilia Awtaas na baada ya kupambana na kupigana lilishindwa kundi la Washirikina, lakini kiongozi wa kikosi cha Waislamu akauliwa, akarudi na kikosi hiki Abu Musa Al-Ash'ari ambaye alichukua uwongozi baada ya kufa Abu A'amir na ghanima nyingi

            Kikosi cha pili kilifuatia kundi lililokwenda Nakhla na kuweza kumpata Durayd na kumuua, naye aliuliwa na Rabi'a bin Rafi', na kundi la tatu lililokimbilia Taif, alitoka Mtume (SAW) mwenyewe na jeshi lake kulifuatia ili kumaliza fitna ya Hawazin na wale waliokuwa pamoja nao

Shambulizi la Taif:

            Maalik An-Nassri ambaye aliyekuwa akiongoza jeshi la Hawaazin na Thaqif alikimbilia Taif na jeshi lake na kuingia kwenye ngome lao kubwa na kukusanya vyakula vyao na mali zao ndani humo. Mtume (SAW) alimpa bendera Khalid bin Al-Walid na kumuamrisha awe mbele na kikosi cha watu elfu moja na kuelekea Taif. Walipofika Taif, walikuta ngome imefungwa na watu wote wamo ndani yake, basi akaamrisha ngome izungukwe, lakini Waislamu wakajishtukia wanapigwa mishale kama mvua kutoka kila upande, na wengi wakajeruhiwa na kiasi kumi na mbili wakauliwa.

            Mtume (SAW) alipoona hivi, aliamrisha jeshi lirudi nyuma kidogo mahali ambapo wakirusha mishale itakuwa haiwezi kuwafikia. Hapo wakakaa muda wa masiku chungu nzima, na kujaribu kuivunja ngome kwa kuirushia mizinga ya mawe, na kutengeneza magogo ya kutoboa ukuta wake lakini wasifaulu. Khalid bin Al-Walid akajaribu kuwashawishi Makafiri watoke kupigana uso kwa uso kama ilivyo desturi ya Waarabu, lakini vile vile wakakataa na kugoma na kuwaambia sisi hatutoki humu na tuna chakula cha kututosha miaka, basi subirini huko nje, kikituishia chakula tutatoka tuje kupigana na nyinyi mpaka tufe sote.

            Mtume (SAW) akaamrisha mashamba yao na mitende yao ikatwe, basi Waislamu wakakata mitende chungu nzima mpaka waliokuwa katika ngome wakapiga kelele na kumuomba Mtume (SAW) aiwache asiikate kwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ujamaa, basi Mtume (SAW) akaiacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ujamaa. Kisha Mtume (SAW) akamuamrisha mtu anadi kuwa mwenye kutoka yeyote atakuwa kwenye amani, basi watu kumi na kitu wakateremka na kuja kwa Mtume (SAW) na yeye akawasamehe na kuwapa amani na kuwaamrisha kila Muislamu amsaidie mmoja wao.

            Mambo yalipokuwa magumu na siku zilipozidi kusonga, Mtume (SAW) alimshauri Naufal bin Muawiya juu ya jambo hili la ngome, akamwambia kuwa wao ni kama mbweha katika mashimo lake, ukimngojea utamkamata na ukimwacha hatakudhuru, basi Mtume (SAW) akaamua aondoke na kumuamrisha Umar bin Al-Khattab kuwatangazia watu, basi alipowatangazia watu wakaona taabu sana kuwa wataondoka bila ya kuiteka. Mtume (SAW) akawaamrisha wakae na kupigana, lakini walipojaribu siku ya pili walirushiwa mishale wakaumia chungu nzima, basi Mtume (SAW) akawatangazia tena kuondoka wakafurahi, na wakamwambia awalaani Thaqif, basi akasema: Ewe Mola, waongoe Thaqif na uwalete wakiwa Waislamu.

Ghanima za Huneyn zagawanywa:

            Baada ya kurudi kutoka Taif na kufika Ju'rana palipokusanywa ngawira za Huneyn, alikaa masiku chungu nzima anasubiri labda watu wa Taif watakuja lakini hawakutokea, basi akaanza kuzigawanya ghanima baada ya kuzihesabu na kutoa khumsi (sehemu moja katika tano) yake, akawapa wale waliokuwa hawakusilimu bado na wengine waliosilimu lakini imani zao bado ni dhaifu na ndio kwanza wameingia kwenye dini ya Uislamu, akawapa mali nyingi.

            Akampa Abu Sufyan na wanawe wawili Muawiya na Yazid kila mmoja wao ngamia mia na wakia arubaini za dhahabu, na akawapa Hakim bin Hizam na U'yayna bin Hisn na Al-Abbas bin Mirdaas na Al-Aqraa bin Haabis na Al-Harith bin Al-Harith na wengineo katika viongozi wa Makureshi ngamia mia mia kila mmoja, na akampa Safwaan bin Umayya mamia ya ngamia kwa kuwa bado alikuwa hajasilimu na alisaidia katika vita kwa silaha, na hili likamfanya asilimu. Kisha wengineo wakapewa ngamia hamsini hamsini, na arubaini arubaini mpaka makabila ya Waarabu wakamkusanyikia kila mmoja anataka na yeye apewe, basi akachukuwa katika sehemu yake na kuwapa.

            Kisha baada ya kuwapa hawa wenye imani dhaifu na wasiokuwa Waislamu katika wao, akamwita Zayd bin Thabit na kumwambia awagawie watu wengine kila mmoja ngamia wanne na mbuzi wanne katika majeshi wasiokuwa na farasi na wale wenye farasi wakapewa ngamia kumi na mbili na mbuzi mia na ishirini, lakini Maansari wakawa hawakupewa kitu, na hili likawastaajabisha sana na wengine wakaanza kusema kuwa Mtume (SAW) amepata watu wake Makureshi na sisi anatuacha tuliopigana nao na panga zetu mpaka sasa zinatoja damu zao, basi aliposikia maneno haya aliamuru wakusanywe Maansari tu peke yao na baada ya kukusanyika aliwauliza: Enyi Maansari, maneno gani haya ambayo yamenifikia kuhusu nyinyi? Je, sijakukuteni mmepotea, Mwenyezi Mungu akakuhidini kwangu, na masikini, Mwenyezi Mungu akakutajirisheni kwangu, na maadui, Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zenu kwangu

            Hakika Makureshi ndio mwanzo wanatoka kwenye ukafiri na msiba, nami nilitaka kuwaliwaza na kuwavutia. Je, mumekasirika enyi Maansari ndani ya nafsi zenu kwa jambo dogo la dunia nililowavutia watu ili wapate kusilimu, na nikakutegemezeni juu ya Uislamu wenu ulio thabiti ambao hautikisiki? Je, hamridhii enyi jamii ya Maansari, wende watu na mabuzi na magamia, nanyi mrudi na Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenye msafara wenu? Basi naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mkononi mwake, lau isingekuwa hijra (kuhama kutoka Makka kwenda Madina), ningekuwa mimi mmoja katika Maansari, na lau watu watafuata njia katika majabali na wakafuata Maansari njia nyengine katika majabali, basi ningefuata njia ya Maansari. Ewe Mola, warehemu Maansari na watoto wa Maansari na wajukuu wa Maansari. Maansari wakabwaga lio mpaka zikaroa ndevu zao, wakasema: Tumeridhia Mtume wa Mwenyezi Mungu kuwa ndio sehemu yetu, kisha akaondoka Mtume (SAW) na watu wakatawanyika.

Kuja kwa Ujumbe wa Hawazin:

            Zikapita kama siku kumi na kitu baada ya kugawanywa ghanima za watu wa Hawazin na Thaqif, kisha ukaja ujumbe wa kabila la Hawazin kusilimu, wakiwa ni watu kumi na nne wakiongozwa na Zuhayr bin Surad, wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, katika mliowateka kuna mamama na madada na mashangazi na mamama wadogo nao ni hizaya ya watu, na akasema Zuhayr: Kuna kwenye kundi mashangazi zako na mamama zako na wanawake wengine waliokulea. Kwani katika walioshiriki kupigana na Waislamu katika vita vya Huneyn ni Bani Saad ambalo ni kabila lililomlea na kumnyonyesha Mtume (SAW) alipokuwa mchanga.

            Mtume (SAW) akasema: Hakika mazungumzo ninayoyapenda zaidi ni yale yaliyo ya kweli zaidi, basi chagueni moja katika mafungu mawili: Ima wanawake na watoto wenu, au mali zenu. Wakasema: Hatukuwa tunalinganisha sharafu na kitu chochote, turudishie wake zetu na watoto wetu, kwani tunawapenda zaidi wala hatutozungumza juu ya mbuzi na ngamia. Basi Mtume (SAW) akawaambia: Ama mali yangu na ya Bani AbdulMuttalib basi ni yenu, nami nikisali Adhuhuri simameni museme: Sisi tunawaomba Waislamu kupitia kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na tunamuomba Mtume wa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Waislamu aturudishie wake na watoto wetu.

            Mtume (SAW) akawaambia Masahaba zake: Hawa ndugu zenu wamekuja hali ya kuwa wametubu, nami nimeona niwarudishie wake zao na watoto wao, basi mwenye kutaka kuwarudishia kwa ridhaa yake naafanye, basi Masahaba zake wakasema: Vyote tulivyokuwa navyo ni vya Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kwa hivyo wakarudisha wanawake na watoto waliokuwa mikononi mwao. Ama baadhi ya mabedui kama Al-Aqraa na U'yayna na Al-bbas bin Mirdas, walikataa kurudisha mpaka Mtume (SAW) alipowaahidi kuwa atawapa badala yake mali basi wakarudisha wote isipokuwa Uyayna ambaye mwishowe vile vile alimtoa mwanamke kizee aliyekuwa naye.

            Aidha, Mtume (SAW) aliwauliza Hawazin kuhusu Maalik, na kuwaambia kuwa ikiwa atakuja kusilimu, basi nitamrudishia mali yake na watu wake, na nitampa ngamia mia, basi alipopata habari hii Maalik, alitoka kwenye ngome usiku kimya kimya na kwenda kwa Mtume (SAW) kusilimu, naye akamrudishia watu wake na mali yake na kumpa ngamia mia, na kumfanya ndiye mkubwa wa wale waliosilimu katika Hawazin.

Umra ya Ju'rana: 

            Kwa jumla Mtume (SAW) alikaa Juurana siku kumi na tatu, na baada ya kuwarudishia Hawazin wake na watoto wao, na kumwakilisha Maalik awe ndio kiongozi wa Waislamu katika wao, alijitayarisha Mtume (SAW) pamoja na Waislamu kwenda Makka kufanya Umra na baada ya kumaliza kufanya Umra, aliondoka kurudi Madina kwa amani akiwa amemaliza fitina ya makabila ya Waarabu ambayo yalikuwa yakimsumbua sana kabla ya vita vya Huneyn, kwani makabila ya Thaqif na Hawazin yalikuwa ni yenye nguvu na mali nyingi, na Mwenyezi Mungu akajaaliya wakaja na kila kitu chao katika vita vya Huneyn na kwa hivyo baada ya kushindwa na kuchukuliwa mali zao, walivunjika nguvu na wakawa hawana lao jambo, hasa ilivyokuwa kiongozi wao na kundi katika wao waliingia katika Uislamu na kuwa pamoja na Mtume (SAW).

Vikosi vyapelekwa na tume zapokewa:

            Baada ya kurudi Madina, Mtume (SAW) alimpeleka Qays bin Saad pamoja na watu mia nne kwenda Yemen kuwatangazia Uislamu, akaja mmoja katika wao na kumwambia Mtume (SAW) kuwa yeye atawazungumzia watu wake juu ya Uislamu, na yeye aliamuru jeshi lirudi, basi akaamrisha jeshi lirudishwe, na yule mtu akenda kwa watu wake na kuwatangazia Uislamu, kisha akarudi na watu kumi na tano wakapokelewa na Saad bin Ubada na kumpa ahadi Mtume (SAW) ya kumkubali na kukubali dini ya Uislamu

Kikosi cha Bishr bin Sufyan:

            Mtume (SAW) alimpeleka Bishr kwa Banu Kaab kukusanya Zaka, wakazuiliwa na Banu Tamim majirani zao wasitoe Zaka, basi Mtume (SAW) akamtuma Uyayna na kikosi cha watu hamsini wakapigana nao na kuteka wanaume kumi na moja na wanawake ishirini na moja na watoto thalathini, na kuja nao Madina. Mtume (SAW) akasema wawekwe katika nyumba ya Ramla bint Al-Harith

            Kisha wakaja wakubwa Banu Tamim na kumpigia kelele Mtume atoke kuja kuonana nao. Mtume (SAW) alitoka nyumbani kwake akiwa amekasirika, basi Mwenyezi Mungu akakataza tabia hii na kusema:

                                                                                            Q. Hujurat:5.

            Kisha Mtume (SAW) alikwenda kusali Adhuhuri na baada ya Sala alikaa kuwasikiliza, na wao wakakaa mbele yake kujifakhirisha, na kujisifu kwa mashairi, naye Mtume (SAW) akamuamrisha Hassan bin Thabit awajibu na baada ya kuwajibu walikubali kusilimu na Mtume (SAW) aliwarudishia wake zao na watoto wao na kuwapa zawadi na wakakaa muda kusoma Qurani na kujifunza dini.

Tume ya Al-Walid bin Uqba:

            Aidha, Mtume (SAW) alimpeleka Al-Walid bin Uqba kwenda kwa Banul-Musttaliq kukusanya Zaka, na alipofika aliwakuta watu ishirini katika wao wametoka na ngamia zao na silaha zao, na kwa kuwa kulikuwa na uadui baina yao katika zama za Ujahili, alidhani kuwa wanakuja kumpiga, basi akakimbia na kurudi Madina na kumueleza Mtume (SAW). 

            Basi Mtume (SAW) akamtoa Khalid bin Al-Walid na kikosi chake kwenda kuhakikisha jambo hili, lakini alipofika walimpokea na kumuonyesha utiifu, basi alipoelezwa Mtume (SAW) habari hii, alimpeleka mtu mwengine kwenda kukusanya Zaka badala ya Al-Walid.

Rudi Juu

Matukio ya Tarehe ya Kiislamu kwa Ufupi

Mwaka wa Kikristo Mwaka wa Kiislamu

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
570 K.I 53 B.H. Makka ilihujumiwa na Abraha, akiwa na jeshi kubwa pamoja na tembo (ndovu) ili kuja kuibomoa Kaaba hapo Makka, lakini Mwenyezi Mungu alimuangamiza kwa kumletea ndege waliobeba vijiwe kutoka Motoni.

Abdullah, baba yake Mtume Muhammad (SAW) alifariki dunia.

Mtume Muhammad (SAW) alizaliwa hapo Makkah  katika mwezi wa Rabi-al-Awwal tarehe 12, siku ya Jumatatu.

  51 B.H. Kuzaliwa kwa Abu Bakr Assiddiq (RA)
  48 B.H. Kufariki kwa Amina bint Wahb, mamake Mtume (SAW)
  47 B.H. Kuzaliwa kwa Uthman bin Affan (R.A.)
  46 B.H. Kufa kwa Abdul Muttalib, babu wa Mtume (SAW)
  41 B.H. Mtume Muhammad alichukuliwa safari na ami yake Abu Talib kwenda Syria.

Kuzaliwa kwa Omar bin al-Khattab (R.A.)

591 K.I.   Kisra II aliteuliwa kuwa mfalme wa Masassani
595 K.I. 28 B.H. Mtume Muhammad (SAW) alimuoa Khadijah (RA), mwanamke mtukufu wa Kikureshi, na mfanyi biashara mkubwa.
  20 B.H. Kuzaliwa kwa Ali bin Abi Talib (R.A.)
610 K.I. 14 B.H. Herakle alitawala Kostantinia (Uturuki leo)

Mtume Muhammad (SAW) aliletewa Jibril (AS) kwa mara ya kwanza kumteremshia Wahyi na kumfundisha Qurani. (Q. 96:1-5)

Khadijah na Ali na Abubakar walikuwa watu wa kwanza kuukubali Uislamu.

  9  B.H. Waislamu walihamia Uhabushia (Ethiopia leo)
  8  B.H. Hamza (R.A.), ami yake Mtume (SAW) aliukubali Uislamu, na kadhalika Omar (R.A.) aliingia katika dini ya Uislamu.
  7  B.H. Kabila la Bani Hashim linapigwa pande na Quraish na kutengwa katika Shuab Ali.
  4  B.H. Mwisho wa kupigwa pande Banu Hashim
Kufariki kwa Abu Talib, na Khadijah, mke wa Mtume (SAW).
  3  B.H. Mtume (SAW) anazuru Taif
Kundi la mwanzo la watu wa Madina waliukubali Uislamu
  2  B.H. Mkataba wa kwanza wa Aqaba.
Mtume (SAW) alipelekwa safari ya Israa and Miraji. Israa kutoka Makka mpaka Jerusalemu, na Miraji kutoka Jerusalemu kwenda mbinguni kupokea amri ya Sala na kuonyeshwa mambo ya huko.
  1  B.H. Mkataba wa pili wa Aqaba.
614 K.I.   Jerusalem ilitekwa na Masassani
622 K.I. 1 A.H. Mtume Muhammad (SAW) na wafuasi wake walihamia Madina.

Mwanzo wa mwaka wa kiislamu na kuanza kwa tarehe ya kiislamu, tangu kuhama Mtume (SAW) kwenda Madina katika 1.1.01 A.H., siku ya Ijumaa katika mwezi wa Julai 16, 622 C.E.

Mtume Muhammad (SAW) aliweka msingi wa msikiti wa Quba.  Aidha, msikiti wa Mtume wa Madina ulianza kujengwa.

Waislamu walipewa amri ya kuadhini, na Bilal (R.A.) alikuwa muadhini wa kwanza wa Mtume (SAW).

  2 A.H. Qibla kilibadilishwa badala ya Waislamu kuelekea msikiti wa Al Aqsa waliamrishwa waelekee msikiti mtukufu wa Makka

Waislamu waliamrishwa kufunga mwezi wa Ramadhani.

Vita vya Badr vilipiganwa katika mwezi wa Ramadhani tarehe 17 ya Ramadhan ya mwaka wa pili 2 wa Hijra

Fatima (R.A.) aliolewa na Ali (R.A.)

  3 A.H. Vita vya Uhud
  5 A.H. Vita vya Khandaq
Mtume Muhammad (SAW) alimuoa Zainab bint Jahsh, mtalaka wa Zayd, huru wake na mtoto wake wa kulea.
  6 A.H. Mkataba wa amani wa Hudaybiya
Khalid bin Walid na Amr bin al-Aas waliingia kwenye Uislamu, baada ya mkataba.
Mfalme Najashi wa Habasha (Ethiopia) aliingia kwenye Uislamu.
Mfalme wa Maqipti alimpelekea Mtume (SAW) Maria na nduguye Sirin kama zawadi kutoka kwake. Maria aliingia kwenye Uislamu na Mtume (SAW) akamfanya kuwa suriya wake.
Badhan, mkubwa wa Kifursi hukoYemen, aliingia kwenye Uislamu.
  7 A.H. Vita vya Khaybar vilipiganwa.
Mtume (SAW) alifanya Umrah pamoja na Masahaba zake
Mtume (SAW) alimuoa Safiya, mwanamke wa Kiyahudi baada ya kulishinda kabila lake katika vita, na yeye kuukubali Uislamu.
  8 A.H. Makkah ilitekwa,  na Mtume (SAW) aliingia Makka kama mshindi na kusimama kwenye Al Kabah siku ya Ijumaa tarehe 20 ya mwezi wa Ramadhani na kuamrisha kuvunjwa kwa masanamu.
  9 A.H. Vita vya Tabuk
Mtume (SAW) alipeleka Masahaba zake kwenda kuhiji, wakiongozwa na Abu bakr (RA).
Wasiokuwa Waislamu walikatazwa kuingia kwenye msikiti mtukufu wa Makka kuanzia tarehe hii.
  10 A.H. Hija ya mwisho ya Mtume (SAW) ya kuagaa aliyoifanya pamoja na Waislamu 100,000 na kutoa hotuba yake mashuhuri hapo.
632 K.I. 11 A.H. Mtume Muhammad (SAW) alifariki dunia katika mji wa Madina siku ya Jumatatu, tarehe12 ya mwezi wa Rabi-al-Awwal, akiwa na umri wa miaka 63.
Abu Bakr alichaguliwa kuwa ndiye Khalifa wake wa kwanza.

Hamza na Umar wasilimu

Kuitangaza dini kweupe

Kufikisha Ujumbe kisiri

Bishara ya Utume

Safari ya Sham

Nasaba ya Mtume

Zama za Ujahili Bara Arabu

Shambulizi la Uhud Banu Qaynuqaa Kupanga Udugu Mapatano ya Aqaba Israa na Miraji Majini wanapokea Ujumbe

Mkataba wa dhulma

Waislamu waingia Makka Kutangaa kwa Uislamu Shambulizi la Khaybar Kushindwa kwa Ahzaab Mwaka wa Tano Mwaka wa Nne Abu Sufyan ajinaki
ukurasa 8 Muhtasari Siku za Mtume za mwisho Mtume (SAW) apokea tume Abubakar (RA) ahiji Kikosi cha A'lqama Washirikina watiwa mbioni