|
Kikosi cha A'lqama: Vile vile, Mtume (SAW) alimpeleka Alqama na watu mia tatu kwenda Jidda aliposikia kuwa kuna Mahabushia ambao wamekuja na merikebu zao kuja kuwapiga watu wa Makka na kuwanyanganya mali zao, basi akenda Alqama mpaka kwenye kisiwa walichojificha wakakimbia waliposikia wanakuja. Muhimu yaliyotokea mwaka huu: Katika mwaka huu Maria suriya wa Mtume (SAW) alimzaa Ibrahim katika mwezi wa Dhul-Hijja, wakaingiwa na wivu sana wakeze wengine kwa kuruzukiwa Maria mtoto kutoka kwa Mtume (SAW) na wao wasipate. Aidha, katika mwaka huu Mtume (SAW) alimpeleka Amr bin Al-Aas kwenda kwa watoto wa Al-Julandi kuchukuwa Zaka, basi akachukuwa Zaka kutoka kwa matajiri katika wao na kuwapa maskini katika wao. Mwaka wa tisa: Mwaka wa tisa umeshuhudia mambo mengi, kwani ni mwaka ambao tume nyingi zilikuja kwa Mtume (SAW) kusilimu, na aghlabu ya Waarabu wakaingia katika Uislamu, lakini ni mwaka vile vile uliokuwa mgumu na mzito kwa Waislamu kwani Warumi baada ya mapambano yao na Waislamu katika vita vya Muuta, na kutambua hatari kubwa inayowakabili, walianza kujizatiti na kujitayarisha pamoja na makabila ya kiarabu yaliyokuwa karibu nao na chini ya himaya yao kwenda kuwapiga Waislamu Madina ili kuuzima moto huu unaowaka Bara Arabu nzima na kukaribia kuwaunguza na wao. Mtume (SAW) alipopata habari ya mkusanyiko wa Warumi na nia yao ya kuja kuwapiga vita Waislamu, aliwaambia Waislamu wajitayarishe kwenda kupambana na Warumi na kujizatiti barabara kwa sababu ya ukubwa na nguvu za jeshi la Warumi, na ilikuwa ni desturi yake akitoka kwenda katika shambulizi lolote hatangazi ili maadui washtukie tu kufika kwa jeshi la Mtume (SAW), lakini shambulizi hili alilitangaza mapema na kuwaeleza Waislamu nani wanaokwenda kupambana nao, na kuwa linahitajika jeshi liwe limejitayarisha kidhati kwa watu na silaha, na kwa hivyo akawaamrisha matajiri katika Masahaba wajitolee katika kulizatiti jeshi sawasawa. Masahaba wakubwa na wenye mali nyingi kama Abubakar na Uthman na Umar na AbdulRahman bin Awf na Al-Abbas na Talha na Aasim wote wakatoa mali nyingi kusaidia kulitayarisha jeshi hili, kila mmoja kwa uwezo wake. Aidha, wanawake wakatoa mapambo yao na dhahabu zao kusaidia jeshi, na wengine katika Masahaba maskini wakajitolea na kumwomba Mtume (SAW) awapatie vipando ili na wao waweze kushiriki katika vita, huku machozi yakiwalengalenga, basi Masahaba wengine wakawasaidia kwa kuwapatia vipando. Jeshi lilipokuwa tayari, idadi yao ikiwa elfu thalathini, alimweka Madina Muhammad bin Maslama kama mwakilishi wake, na kumweka Ali bin Abi Talib mwakilishi wake juu ya wakeze. Wengi katika Wanafiki waliomba ruhusa wasende vitani na kutoa nyudhuru mbali mbali, naye akawapa ruhusa wasende vitani, ijapokuwa baadaye Mwenyezi Mungu akamlaumu kwanini akawaachia kwani kuhudhuria kwao kungemdhihirishia nani ni mkweli na nani ni mwongo. Akasema Mwenyezi Mungu: Q. Tauba:43, 45 Aidha, kuna wengine katika Masahaba ambao vile vile hawakuhudhuria vita na ijapokuwa walikuwa hawana udhuru wowote, lakini walibaki nyuma na hawa Mwenyezi Mungu baada ya kuwatia katika mtihani mkubwa mpaka wakataka ardhi ipasuke watumbukie ndani yake, aliteremsha wahyi kuwasamehe. Nao ni Kaab bin Malik, na Muraara bin Ar-Rabii, na Hilal bin Umayya. Jeshi likaondoka na Mtume (SAW) akampa bendera ya kuongoza jeshi zima Abubakar, na bendera ya Muhajirina alimpa Az-Zubeyr, na bendera ya Aus alimpa Usayd bin Khudhayr, na ya Khazraj alimpa Al-Hubab bin Al-Mundhir, na kwenda mpaka walipofika mji wa Thamud waliomkadhibisha Nabii wao Saleh na kumkataa Mwenyezi Mungu, aliwaambia Mtume (SAW) wasiingie mji wao isipokuwa katika hali ya kulia na kusikitika. Wakaupita mji wa Thamud mpaka wakafika Tabuk. Hapo Waislamu wakafanya kambi, na Mtume (SAW) akawahutubia na kuwatia mori na kuwabashiria kheri. Kwa upande mwengine, Warumi waliposikia kuwa Mtume (SAW) ametoka na jeshi lake, waliingiwa na khofu kubwa wakatawanyika ndani ya mipaka yao na Mwenyezi Mungu akawanusuru waja wake na kuwapa ushindi mkubwa wa kisiasa kwani Waarabu wote wakatambua nguvu za Waislamu na kubadilika nyoyo zao kuhusu Warumi na kuelekea nyoyo zao kwenye nguvu mpya ya Uislamu. Mtume (SAW) akabaki na jeshi lake hapo Tabuk kwa muda wa masiku mpaka akaja Yohana mkuu wa Ayla, na wenziwe watu wa Jarbaa na Azruh na Mina kufanya sulhu na Mtume (SAW), naye akawakubalia watoe jizya na atawapa himaya wasiudhiwe na waendelee na maisha yao katika amani. Akawaandikia mkataba wa amani katika safari zao za bara na bahari, na kuwa wataishi kwa wema na hisani baina yao na Waislamu na kila mwaka watalipa jizya. Kisha Mtume (SAW) akawashauri Masahaba zake kuhusu kuvuka mipaka ya Tabuk na kuwafuatia Warumi katika miji yao, lakini Umar akamwambia ikiwa hakuteremshiwa Wahyi kuhusu shambulizi hilo, basi haina haja, na Mtume (SAW) akamjibu ingekuwa ameteremshiwa Wahyi, asingemshauri mtu, basi Umar akamwambia kuwa warudi mwaka huu kwani Warumi wako wengi huko kwao, na Waarabu wa sehemu za Sham bado hawajakuwa na wao, basi Mtume (SAW) akamsikiliza rai yake na kuamrisha jeshi lifunge safari na kurudi Madina. Msikiti wa Madhara: Njiani lilipokuwa jeshi la Mtume (SAW) linarudi kuelekea Madina, alipata habari Mtume (SAW) kuwa Wanafiki wamejenga msikiti uwe dhidi ya msikiti wa Qubaa, na kujaribu kuwafarikisha Waislamu, na walipokuja kumuomba Mtume (SAW) asali ndani yake, na alipowauliza sababu ya kujenga msikiti huu, walidai kuwa wanakusudia mema, lakini Mwenyezi Mungu aliwafedhehesha na kuteremsha Wahyi na kusema: Q.Tauba:107 Mtume (SAW) baada ya kujua nia yao mbaya, aliwaamrisha Waislamu wauvunje msikiti huo, na Wanafiki wakafedheheka na kuhizika. Jeshi likaendelea na safari yake na kurudi Madina kwa salama. Watatu wasamehewa: Mtume (SAW) alipofika Madina alikwenda msikitini kwanza na kusali rakaa mbili na kukaa kusikiliza watu, wakaja Wanafiki ambao hawakuhudhuria vita na kutoa nyudhuru zao, kila mmoja akisema lake, na Mtume (SAW) akiwakubalia kwa dhahiri ya maneno yao na kumwachia Mwenyezi Mungu undani wao. lakini Mwenyezi Mungu akafichua undani wao na kusema: Q.9:90 Ama wale Waislamu watatu ambao hawakuhudhuria vita wala hawakuwa na udhuru wowote, nao ni Kaab bin Malik na Hilal bin Umayya na Murara bin Rabi' walipoulizwa walisema kweli na kwa hivyo Mtume (SAW) akaamuru wasizungumzishwe mpaka Mwenyezi Mungu ateremshe hukumu yake juu yao. Waislamu wakawasusia na kuwapiga pande wakawa hawazungumzi nao kabisa mpaka wakaona dhiki kubwa na kutamani ardhi ipasuke iwameze, na mwisho baada ya kupita siku arubaini, Mtume (SAW) akawaamuru wajitenge na wake zao, na hili likawasababishia dhiki kubwa zaidi, lakini hatimaye baada ya kupita siku hamsini, Mwenyezi Mungu akateremsha Wahyi kuwasamehe, akasema: Q.9:118 Waislamu wakakimbilia kuwabashiria msamaha wa Mwenyezi Mungu walioteremshiwa na watu wote wakafurahi, na furaha ya wale watatu waliosamehewa ikawa haina kifani, na wakawa kama waliozaliwa upya. Mwenyezi Mungu vile vile aliwatolea udhuru wale wengine ambao juu ya kuwa nia yao na matamanio yao ni kushiriki katika vita, lakini walizuilika na nyudhuru mbali mbali za kweli kweli, akasema: Q.91-92 Na Mtume (SAW) akasema alipokaribia Madina: Hakika kuna katika Madina wanaume ambao hamkwenda mwendo wala kukata bonde ila walikuwa pamoja na nyinyi, wamezuiliwa na udhuru. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na wao wako Madina? Akawaambia: Na wao wako Madina.
Baada ya Tabuk, ambalo ndilo shambulizi la mwisho aliloshiriki Mtume (SAW) kabla ya kwenda kukutana na Mola wake, tume nyingi sana zilikuja kwa Mtume (SAW) kwa kutambua kuwa hapana nguvu yoyote itakayoiweza nguvu ya Uislamu, na kwa hivyo Washirikina na Wanafiki wakakata tamaa ya kuweza kuwashinda Waislamu na wakakubali kuingia chini ya utiifu na himaya ya Mtume (SAW) na wafuasi wake. Qurani Tukufu vile vile ilieleza mengi kuhusu vita hivi kwenye sura ya Toba, na kulitaja shambulizi hili na walioshiriki na waliojikimbiza na walioshindwa kushiriki kwa sababu ya udhuru fulani, na mengineyo. Tume ya Thaqif: Kabla ya kuja tume hii ya watu wa Thaqif, alikuja Urwa bin Mas'ud kusilimu kwa Mtume (SAW) na kumuomba arudi kwa watu wake kuwaita kwenye Uislamu, lakini Mtume (SAW) akamwambia watakupiga vita, akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi wananipenda zaidi kuliko wanawali wao. Basi akarudi kwao, lakini alipowaarifu kuwa amesilimu, walimuua. Mwezi ulipopita baada ya mauaji yake, walikutana wakubwa wao na wakashauriana baada ya kuona kuwa hawana nguvu za kupigana na Waarabu wote, basi wakaamua kumpeleka mjumbe kwa Mtume (SAW) na walipomwambia Abduyaleyl bin Amr kwenda, alikataa kwa kuchelea kuwa na yeye vile vile akirudi watamuua, basi akashurutisha ende na wenzake, basi wakachaguliwa watukufu watano katika wao na kumuandamanisha naye. Basi walipokaribia Madina walikutana na Al-Mughira bin Shu'uba, naye alipowaona aliruka na kukimbilia kumbashiria Mtume (SAW) kuja kwao, lakini akakutana na Abubakar kabla hakuingia kwa Mtume (SAW), basi baada ya kumpasha habari ya wajumbe wa Thaqif, alifurahi sana Abubakar na kumuomba Al-Mughira amwachie yeye ambashirie Mtume (SAW) habari hii, basi akamwachia naye akaingia kumbashiria. Mtume (SAW) akawapokea na kuwafahamisha juu ya Uislamu na akaweko katika wao Uthman bin Abil-Aas ambaye alikuwa mdogo wao wote lakini alikuwa na hamu kubwa ya kusoma Qurani na kujifundisha dini, basi akajifundisha na kuhifadhi sehemu nyingi za Qurani. Walipokuwa tayari kurudi, Mtume (SAW) alimtuma Al-Mughira na Abu Sufyan kufuatana nao ili wende wakalivunje sanamu hilo, aliwaandikia risala watu wa Taif, na kuwaamrisha wavunje sanamu lao kubwa liitwalo Al-Lat. Basi uliporudi ujumbe na kuwatishia kuhusu Mtume (SAW) walikuwa tayari kupigana lakini kisha wakaingiwa na khofu na wao wakawaambia kuwa washasilimu basi na wao wakasilimu. Kisha akasimama Al-Mughira kulivunja sanamu lao. Mwisho mwisho wa mwezi wa Dhul-Qaada, Mtume (SAW) alimpeleka Abubakar kwenda kuhiji na watu, basi akatoka na watu mia tatu pamoja na ngamia ishirini na kuelekea Makka. Huku nyuma Mwenyezi Mungu akateremsha Aya za mwanzo za Sura ya Baraa kuvunja mikataba iliyoko baina yao na Washirikina ambao hawakutimiza ahadi zao, na kuwapa muhula wa miezi minne kutembea nchini kwa uhuru, na kuwacha mikataba ya wale ambao hawakuivunja mpaka muda wao utakapotimia. Mtume (SAW) akampeleka Ali bin Abi Talib kumfikishia Abubakar ujumbe huu, na alipokutana naye njiani alimuuliza umeletwa kiongozi juu yangu au mfuasi, na Ali akamjibu kuwa ni mfuasi. Basi baada ya kutimiza hija, alisimama Ali kuwasomea Waislamu wote yale yaliyokuwemo katika Aya hizi, kisha akatangaza: Hatohiji baada ya mwaka huu mshirikina yeyote, wala hatotufu mtu kwenye Al-Kaaba uchi (kama ilivyokuwa wakifanya zama za Ujahili). Akawa Ali akisali nyuma ya Abubakar muda wote waliokuwa pamoja mpaka waliporudi Madina. Mengine muhimu ya mwaka huu: Aidha, katika mwaka huu ulikuja ujumbe wa Bani Asad kuja kusilimu na kumwambia Mtume (SAW) kuwa unaona sisi tumekuja kabla hujatuletea mjumbe yeyote, basi Mwenyezi Mungu akawaambia: Q.Hujurat:17 Vile vile, katika mwaka huu alikufa mkubwa wa Wanafiki Abdullahi bin Ubay bin Saluul, na Mtume (SAW) akatoka na kwenda kumsalia na kumzika na kumuombea maghfira, juu ya kuwa Umar alimkataza kumfanyia haya, kisha Mwenyezi Mungu akamteremshia Wahyi kukataza jambo hili, akasema: Q.Tauba:84 Halikadhalika, alifariki katika mwaka huu Umm Kulthum binti wa Mtume (SAW) na mke wa Uthman bin Affan, na Mtume (SAW) akasikitika sana kwa kifo chake, na akamwambia Uthman: Lau ningekuwa na binti wa tatu ningekuoza. Kwa sababu yeye alikuwa amemuoa Ruqayya binti wa Mtume (SAW) kabla ya huyu, na ndio maana Uthman akaitwa Dhun-Nurayn, yaani mwenye nuru mbili. Mwaka wa kumi: Ulipoingia mwaka wa kumi Mtume (SAW) alimpeleka Khalid bin Al-Walid Yemen kwenda kuwatangazia dini watu wa kabila la Banu Abdil-Madan, na akamuamrisha awaite kwenye Uislamu mara tatu, wakikataa baada ya hapo basi apigane nao. Alipofika Khalid alitawanya wenzake kila upande kila mmoja akitangaza kuwa: Silimuni mtasalimika. Basi wakaingia katika dini ya Mwenyezi Mungu kwa umoja wao, akakaa Khalid anawafundisha Qurani na Uislamu na kumwandikia Mwenyezi Mungu juu ya jambo hili. Mtume (SAW) akampelekea mjumbe kuwa aje na tume kutoka kwao, basi wakaja na kukutanika na Mtume (SAW) na alipowauliza: Mlikuwa mkiwashinda kwa kitu gani wale waliokuwa wakipigana na nyinyi katika zama za Ujahili? Walisema: Tulikuwa tunashikamana wala hatufarikiani, wala hatuanzi kumfanyia yeyote dhulma. Akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu: Mmesema kweli. Aidha, Mtume (SAW) alimpeleka Ali bin Abi Talib kwa kabila la Banu Madh-hij la kiyemeni kulitangazia dini na awaamrishe Sala, wala asitake kitu zaidi kutoka kwao, wala asipigane nao mpaka wao waanza kuwapiga, basi akenda na wenzake mpaka kwao, lakini alipowatangazia Uislamu walikataa na kuanza kumrushia mishale, basi Ali na kikosi chake wakapigana nao mpaka wakawashinda, kisha wakawaita tena waingie Uislamu wakakubali na wakubwa zao wakatoa ahadi kwake ya kumfuata Mtume (SAW) na kusali na kutoa Zaka. Kisha Ali akarudi Makka. Kisha Mtume (SAW) akapeleka Yemen wawakilishi wake, akampeleka Muadh bin Jabal na Abu Musa Al-Ash'ari na kuwaambia: Sahilisheni wala msifanye mambo magumu, na wabashirie kheri wala msiwakimbize. Aidha, akamwambia Muadh bin Jabal: Wewe unakwenda kwa watu wa Kitabu, basi ukiwaendea waite washuhudie kuwa hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na kuwa Muhammad ni Mtume wake, basi wakikutii kwa hilo, waambie kuwa Mwenyezi Mungu amefaridhisha Zaka inayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kupewa maskini wao, na wakikutii kwa hilo, jihadhari na kuchukuwa mali zao bora, na uiche dua ya mwenye kudhulumiwa, kwani hapana baina yake na Mwenyezi Mungu kizuizi. Aidha, katika aliyomwambia Muadh: Ewe Muadh, hakika wewe huenda usikutane na mimi tena baada ya mwaka wangu huu, na huenda ukaupitia msikiti wangu huu na kaburi langu. Muadh akalia kwa kuogopa kufarikiana na Mtume (SAW), na Muadh alikaa Yemen mpaka akafariki dunia Mtume (SAW) kama alivyombashiria, lakini Abu Musa aliwahi kurudi na kuonana na Mtume (SAW) katika hija ya kuaga. Hija ya kuaga: Baada ya kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu karibu kila mahali, na kuondosha ushirikina kote Arabuni, na kukata mizizi ya fitina za Mayahudi, Mtume (SAW) alitia nia kwenda kuhiji na kutangaza azma yake hii kwa watu. Wakajumuika watu wengi kutoka kila upande katika mji wa Madina wakitaka na wao kumfuata Mtume wao (SAW) katika hija hii, basi katika mwezi wa Dhul-Qaada akajitayarisha Mtume (SAW) kwa matayarisho yote ya haji na kuondoka kuelekea Makka. Mtume (SAW) na mahujaji walipofika Dhul-Huleyfa alihirimia kufanya Hija na Umra pamoja na kuleta "labayka-llahuma labayka" mpaka akaingia Makka na kuendelea na ibada za Hija. Mahujaji waliomfuata Mtume (SAW) kwenda kuhiji naye walikaribia elfu tisini. Kisha alipomaliza kuhiji na kuchinja aliwahutubia watu katika uwanja wa Arafa akiwa juu ya nyumbu wake hotuba yake mashuhuri inayojulikana kama hotuba ya kuaga. Hotuba ya Mtume kwa Mahujaji: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, tunamhimidi na kutaka kwake msaada, na tunaomba kwake maghfira na tunatubu kwake, na tunajikinga kwake na shari za nafsi zetu na maovu ya vitendo vyetu. Mwenye kuhidiwa na Mwenyezi Mungu huwa hana wa kumpoteza, na mwenye kupotezwa basi hana wa kumuongoza, na ninashuhudia kuwa hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika na ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja wake na Mtume wake. Ninakuusieni enyi waja wa Mwenyezi Mungu kumcha Mwenyezi Mungu na ninakuhimizeni kumtii Yeye na ninaanza kwa lile ambalo ni kheri. Ama baada ya haya: Enyi watu, nisikilizeni nikubainishieni, kwani mimi sijui pengine nisikutane na nyinyi baada ya mwaka wangu huu katika msimamo wangu huu. Enyi watu, hakika damu zenu na mali zenu ni tukufu kwenu mpaka mtakapokutana na Mola wenu, kama utukufu wa siku yenu hii katika mwezi wenu huu kwenye nchi yenu hii. Tambueni! Je, nimefikisha (ujumbe)? Wakasema: Naam. Akasema: Ewe Mola shuhudia. Basi yule aliyekuwa na amana aifikishe kwa yule aliyempa amana hiyo. Hakika, riba ya zama za Ujahili imeondoshwa, na riba ya kwanza ninayoianzia ni riba ya ami yangu Al-Abbas bin Abdil-Muttalib, na hakika damu (kisasi) ya zama za Ujahili imeondoshwa, na damu (kisasi) ya kwanza ninayoianzia ni damu ya A'mir bin Rabi'a bin Al-Harith. Enyi watu, hakika shetani amekata tamaa kuabudiwa kwenye ardhi yenu hii, lakini yeye ameridhia kutiiwa katika mambo mengine mnayoyadharau katika vitendo vyenu. Basi tahadharini naye juu ya dini yenu. Enyi watu, kuparaganya miezi ni ziyada katika ukafiri, hupotezwa wale wenye kukufuru, huhalalisha (mwezi fulani) mwaka huu na kuuharimisha mwakani ili wabadilishe idadi ya miezi aliyoiharimisha Mwenyezi Mungu, na zama zimerudi kama zilivyokuwa mwanzo siku Mwenyezi Mungu alipoumba mbingu na ardhi, na idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni kumi na mbili katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu siku alipoumba Mwenyezi Mungu mbingu na ardhi, katika hiyo, minne ni mitukufu, mitatu imefuatana na mmoja peke yake: Dhul-Qaada, na Dhul-Hijja na Muharram na Rajab ambao uko baina ya Jumada na Shaaban. Enyi watu, hakika wanawake wenu wana haki juu yenu na nyinyi mna haki juu yao. Wasilainishe magodoro yenu kwa wenginewe, wala wasimuingize mtu mnayemchukia nyumbani kwenu isipokuwa kwa idhini yenu, wala wasifanye machafu, na wakifanya basi Mwenyezi Mungu amekuruhusuni kuwazuia nyumbani mwao na kujitenga nao katika malazi na kuwapiga bila kuwaumiza, na wakiacha na kukutiini, basi ni juu yenu kuwapa riziki na kuwavesha kwa wema, kwani wanawake kwenu ni kama wafungwa hawamiliki kitu juu ya nafsi zao, mumewachukuwa kwa amana ya Mwenyezi Mungu na kuhalalisha tupu zao kwa neno la Mwenyezi Mungu, basi mcheni Mwenyezi Mungu katika wanawake na muwatakie na muwafanyie kheri. Enyi watu, hakika waumini ni ndugu wala haijuzu kwa mtu, mali ya nduguye ila kwa kuridhia mwenyewe, basi msidhulumu nafsi zenu. Wala msirudi baada yangu mkawa makafiri, baadhi yenu wakikata shingo za wengine, kwani mimi nimeacha kwenu kile ambacho mkishikamana nacho hamtapotea baada yangu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mwenendo wangu. Enyi watu, hakika Mola wenu ni Mmoja na baba yenu ni mmoja, nyote nyinyi mnatokana na Adam na Adam anatokana na udongo. Hakika, aliye bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule aliye mcha Mungu zaidi. Hana mwarabu ubora juu ya asiyekuwa mwarabu ila kwa ucha Mungu, basi aliyehudhuria na amfikishie asiyehudhuria. Enyi watu, hakika Mwenyezi Mungu amekwishamgawia kila mrathi sehemu yake ya mirathi, basi haijuzu wasia kwa mrathi, wala haijuzu kufanya wasia zaidi kuliko thuluthi, mwana ni wa (mwenye) malazi, na mzinifu lake ni jiwe (yaani hana kitu). Mwenye kudai baba asiye wake au kujinasibisha na watu wasiokuwa wake, basi huyo ni juu yake laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote, hakubaliwi kutoka kwake siku ya Kiyama toba wala fidia, na amani na rehema ya Mwenyezi Mungu iwe juu yenu . Mwenyezi Mungu katika siku hii akateremsha Aya yake kuwafahamisha Waislamu kuwa dini yao ishakamilika na kuwa kazi ya Mtume wake (SAW) ishatimia, na kuwatanabahisha kuwa huu Uislamu ndio neema kubwa kabisa ambayo mwanadamu aliyopewa na Mola wake, akasema: Q. Al-Maida: 3 Mtume (SAW) alikaa Makka siku kumi, kisha akafunga safari kurudi Madina. Tume zilianza kuja kwa Mtume (SAW) tangu Uislamu ulipoanza kupata nguvu na kuonekana athari yake wazi baina ya watu, lakini katika mwaka wa tisa na kumi, tume zilikuwa nyingi zaidi, na yote ni kwa sababu katika mwaka wa tisa, Uislamu ulipata ushindi mkubwa sana kwa kuingia Makka kibla cha Waarabu wote, na kuwashinda makabila makubwa ya Taif katika vita vya Huneyn. Mwaka wa kumi ulipoingia na Mtume (SAW) akatoka na maelfu kwa maelfu ya Waislamu kwenda kuhiji, makabila mengine yaliyokuwa bado hayakusilimu yaliona kuwa hakuna njia ya kuushinda Uislamu na kuwa nguvu za Waislamu zimekuwa kubwa sana, na kwa hivyo, wengi wao wakaanza kuja kwa Mtume (SAW) kusilimu na kuonyesha utiifu wao kwake. Tume ya Manasara wa Najran: Katika tume zilizokuja kwa Mtume (SAW) ni tume ya Wakristo wa Najran ambao walikuwa ni watu sitini, wakaja na kumletea zawadi Mtume (SAW), na alipowataka wasilimu, walimuambia kuwa sisi tumekuwa Waislamu kabla yenu, na Mtume (SAW) akawajibu kuwa kinachokuzuieni kuwa ni Waislamu ni mambo matatu: Kuabudu kwenu msalaba, na kula kwenu nyama ya nguruwe, na kudai kwenu kuwa Mwenyezi Mungu ana mwana. Wakamuuliza: Na ni nani kama Isa ambaye hana baba? Mwenyezi Mungu akateremsha Aya kuwajibu: Q. Al-Imran:59 na 61 Pamoja na hayo, Wakristo hawa walikataa kumfuata Mtume (SAW) na badala yake wakakubali kulipa jizya, na kutaka wapelekewe mtu mwaminifu kuchukua jizya kila mwaka, basi Mtume (SAW) akampeleka Abu Ubeyda pamoja nao kwenda kukusanya jizya, na ikawa sababu ya kujulikana kwa jina la mwaminifu wa umma huu. Tume ya Dhimam bin Thaalaba: Aidha, alikuja mtu kutoka Ubeduini akiwa nywele zake matimutimu na kuuliza: Ni nani katika nyinyi ni Ibn Abdul-Muttalib? Basi baada ya kuonyeshwa alimkaribia na kumuuliza: Ninakuomba kwa Mwenyezi Mungu uniambie: Je, Mwenyezi Mungu amekuleta kwa wanadamu wote? Mtume (SAW) akamjibu: Ndiyo. Kisha akamuuliza kuhusu Sala na Zaka na Saumu na Hija, na alipomjibu kuwa ndiyo haya yote yameamriwa kufanywa, akamwambia kuwa yeye amemuamini na kumsadiki, na kuwa yeye ni Dhimam bin Thaalaba ameletwa na Banu Saad, basi aliporudi kwa watu wake aliwataka waingie kwenye dini ya Uislamu na wakasilimu na kuwacha kuabudu masanamu. Tume ya Abdul-Qays: Vile vile, ilikuja tume ya Abdul-Qays, Mtume (SAW) akawasifu sana na kusema kuwa ni watu wa kheri hawakulazimishwa kuingia katika Uislamu bali waliingia wenyewe, na alipowaona aliwaombea maghfira na alikuwa mmoja katika wao akiitwa Abdullahi bin Awf na alikuwa ni mdogo wao, basi walipofika walikimbilia kwenda kumuona Mtume (SAW) isipokuwa yeye ambaye alibakia nyuma na kuvaa nguo zake na kuja zake taratibu, naye alikuwa ni mfupi na mbovu wa sura, basi alipokuwa anakuja na Mtume (SAW) anamtazama, alihisi kuwa anamtazama kwa namna alivyo, basi akamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Habari hazijulikani kutokana na ngozi za watu, lakini mtu hujulikana kwa vidogo vyake viwili: moyo wake na ulimi wake. Akasema Mtume (SAW): Hakika, una sifa mbili ambazo Mwenyezi Mungu na Mtumewe wanazipenda: Upole na subra. Tume hii ikamuomba Mtume (SAW) awaamrishe mambo yatakayo watosheleza maana wao wanakaa mbali sana, basi akawaamrisha kumuamini Mwenyezi Mungu mmoja asiye na mshirika na kuamini kuwa Muhammad ni mjumbe wake, na kusali na kutoa Zaka na kufunga mwezi wa Ramadhani na kuwakataza kunywa vinywaji vyenye kulevya. Tume ya Banu Hanifa: Halikadhalika, ilikuja tume ya Banu Hanifa akiwemo Musaylama Mwongo ambaye aliyekuja baadaye na kudai utume baada ya kufa Mtume (SAW), naye alikuwa akisema: Ikiwa jambo hili la Utume atanijaaliya mimi baada yake basi nitamfuata, basi Mtume (SAW) akaja na kusimama mbele ya wenzake ukiwa mkononi mwake kuti la Mtende na kumwambia: ukiniomba kipande hichi sikupi, nami ninakuona yule ambaye niliyemuona, naye alikuwa kaoteshwa kuwa katika mkono wake kuna bangili mbili za dhahabu, zikamtia wasiwasi, akaletewa ufunuo kuwa azipulize, na alipozipuliza ziliruka, akafasiri kuwa waongo wawili watakuja baada yake, ikawa mmoja wao ni huyu Musaylama na wa pili ni Al-Aswad Al-A'nsi aliyetoka Sanaa. Tume hii ya Banu Hanifa ikasilimu. Tume ya Kinda: Pia ilikuja tume ya Kinda akiwemo Al-Ash'ath bin Qays na alikuwa ni mtu mwenye kutiiwa na watu wake, basi walipofika kwa Mtume (SAW) walificha kitu na kumuuliza kitu gani, akawaambia: Ametakasika Mwenyezi Mungu, hayo hufanywa na makuhani, na makuhani na mwenye kufanyiwa ukuhani wamo Motoni, kisha akawaambia kuwa Mwenyezi Mungu amemleta kwa haki na ameniteremshia Kitabu kisichojiwa na upogo la mbele yake wala nyuma yake. Basi wakataka kusikia na Mtume (SAW) akawasomea Aya za Qurani, kisha akasita na kutokwa na machozi, wakamuuliza: Tunakuona unalia? Je, kwa kumuogopa aliyekuleta unalia? Akasema: Hakika khofu yangu kwake imeniliza, amenileta kwenye njia nyofu kama ncha ya upanga, nikiteteleka nayo nitaangamia. Kisha akasoma: Q. 17:86-87 Tume nyenginezo: Kadhalika, Mtume (SAW) alipokea tume kutoka kwa Azd Shanua, na wafalme wa Himyar, na Hamdan na Tajib na Thaalaba na Banu Saad na Banu Fazara na Banu Asad na Banu Uzra na Banu Muhaarib na Ghassan na tume nyingi nyenginezo ambazo zinafika sabini, na zote zilikuwa zikielezwa juu ya Uislamu na wajibu wao kama Waislamu mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtumewe na watu wao. Mwaka wa kumi na moja: Kikosi cha Usama: Baada ya kurudi Madina, hakukaa muda akaanza kukusanya jeshi la kwenda kuwapiga Warumi, na akamchagua Usama bin Zayd bin Haritha kuliongoza jeshi hili, wakiwemo Masahaba wakubwa katika Muhajirina na Maansari kama Abubakar na Umar na Abu Ubeyda na Saad, na ijapokuwa baadhi ya Masahaba walihisi kuwa kijana huyu mdogo ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na saba tu, hafai kuongoza jeshi kubwa kama hilo, lakini Mtume (SAW) alishikilia kuwa lazima Usama ndiye awe amirijeshi wake. Mtume alihamaki sana yalipomfikia maneno hayo na akawaita watu na kuwaambia: Enyi watu, maneno ya wengine katika nyinyi yamenifikia kuhusu kumfanya Usama kuwa amirijeshi, na ikiwa mnatia ila kuhusu kumfanya Usama amirijeshi, basi mlitia ila kabla yake kwa kumfanya babake amirijeshi, na ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa yeye alikuwa ni mwenye kustahiki uamirijeshi, na kuwa mwanawe ni mwenye kustahiki pia, naye alikuwa katika niliokuwa nikiwapenda zaidi katika watu, na huyu ni katika ninaowapenda zaidi katika watu baada yake. Mtume (SAW) akamuamrisha Usama aende mpaka pale alipouliwa babake Zayd bin Haritha na kumwambia ashambulie kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na apigane na wale waliomkataa Mwenyezi Mungu, na atangulize majasusi na achukuwe watu watakaomuonyesha njia, na afanye haraka ili habari zisiwafikie maadui, na ikiwa Mwenyezi Mungu atampa ushindi basi asikae kwao sana, arudi upesi. Watu wengi wakajiunga na jeshi hili na kutoka na Usama mpaka sehemu iitwayo Al-Jurf si mbali sana na Madina, na hapo habari za kuzidiwa Mtume (SAW) na maradhi zikawafikia, na jeshi likabidi kusubiri kidogo kungojea amri ya Mwenyezi Mungu, na alipomkhitari Mwenyezi Mungu mja wake, jeshi likabidi lirudi kushughulikia msiba mkubwa uliowasibu Waislamu.
Kabla ya kushikwa Mtume (SAW) na maradhi yake ambayo yalikuwa ni sababu ya mauti yake, kulikuweko dalili mbali mbali zilizoonyesha kuwa Mtume (SAW) amekaribia ajali yake, kwani katika Ramadhani ya mwaka wa mwisho kabla ya kufa kwake, Mtume (SAW) alikaa msikitini itikafu ya siku ishirini badala ya siku kumi kama ilivyokuwa desturi yake, na mwaka huo Jibril (AS) alimsikiliza Qurani Tukufu mara mbili badala ya mara moja kama ilivyokuwa kawaida yake ya kila mwaka. Aidha, Mtume (SAW) alipofanya Hija yake aliwaambia Mahujaji kuwa huenda ukawa huu ni mwaka wangu wa mwisho kukutana na nyinyi, basi chukueni kwangu namna ya kufanya Hija, na katika hotuba yake ya Hija, Mwenyezi Mungu aliteremsha Aya ya kuonyesha kuwa Uislamu umeshakamilika, akasema: Leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema zangu, na nimeridhia Uislamu kuwa ndiyo dini yenu. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha sura ya ushindi katika siku za Idi, akasema: Q.110:1-5 Vile vile, Mtume (SAW) alitoka kwenda Uhud na kusalia mashahidi waliokufa hapo, na kwenda siku nyengine kwenye makaburi ya Al-Baqi'u na kuwasalimia na kuwaombea maghfira, kisha aliporudi kutoka huko alianza kuumwa na homa kali na kichwa. Akasema Aisha: Alirudi Mtume (SAW) akanikuta kichwa kinaniuma huku ninapiga kelele: Kichwa! Akasema: Bali mimi wallahi ndio ninaumwa na kichwa ewe Aisha. Kisha akasema: Utadhurika na nini ikiwa utakufa nikakuosha na kukuvesha sanda na kukusalia na kukuzika! Akasema Aisha: Wallahi, ninakuona kama kwamba ukifanya hivyo, utarudi nyumbani kwangu na kuoa baadhi ya wanawake wako.. Akacheka Mtume (SAW) na kuendelea maradhi yake lakini pamoja na hayo alikuwa akisimama kufanya wajibu wake wa kupitia wakeze wote na kusalisha watu kwa muda wa siku kumi na moja. Na mwanzo wa kuumwa Mtume (SAW) alikuwa kwa mkewe Maymuna na alikuwa kila siku akiwapitia wakeze kwa mujibu wa zamu zao, mpaka yaliposhitadi maradhi yake, akawa anawauliza wakeze: Kesho mimi niko wapi? Kesho mimi niko wapi? Wakeze wakamfahamu muradi wake, wakamruhusu aende anapotaka, basi akawataka idhini auguzwe katika nyumba ya Aisha, basi akasimama Al-Abbas ami yake na Ali bin Abi Talib na kumsaidia kwenda akiwa amewategemea mpaka akaingia kwa Aisha, na akawa Aisha anamsomea "Suratul-Falaq na Suratun-Naas" na dua nyenginezo na kumpulizia mwilini mwake na kuuchukuwa mkono wake na kumpangusia mwili wake. Siku zake za mwisho: Homa ilimpanda Mtume (SAW) mpaka akawa hashikiki kwa umoto, akasema: Nimwagieni maji viriba saba kutokana na visima mbali mbali ili niweze kwenda kwa watu na kuwausia. Basi wakamkalisha na kumwagia maji mpaka akasema basi, na akajihisi mwepesi. Akaingia msikitini huku amefungwa kichwa chake mpaka akakaa kwenye mimbari na kuwahutubia watu, akasema: Laana ya Mwenyezi Mungu juu ya Mayahudi na Manasara, wamefanya makaburi ya manabii wao kuwa ni mahali pa ibada. Pia akasema: Msilifanye kaburi langu kuwa ni mzimu unaabudiwa. Kisha akawataka watu wachukuwe kisasi chao kwake, ikiwa amempiga mtu basi yeye yuko tayari kupigwa, na ikiwa amemtukana mtu basi yeye yuko tayari kutukanwa. Kisha akateremka kusali Adhuhuri na kupanda tena mimbari na kurudishia maneno yale aliyowaambia watu, akasema mtu: Mimi ninakudai dirhamu tatu, akasema Mtume (SAW) kusema: Ewe Fadhl, mpe. Kisha akasema: Enyi watu, mwenye amana airudishe, wala asiseme fedheha za dunia. Tambueni kuwa fedheha za dunia ni nyepesi kuliko fedheha za Akhera. Akasimama mtu na kusema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, nina dirhamu tatu nilizificha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Akamuuliza: Kwa nini ukazificha? Akajibu: Nilikuwa ninazihitajia. Akasema: Ewe Fadhl, chukuwa kutoka kwake. Kisha Mtume (SAW) akausia kuhusu Maansari na kusema kuwa wameshatimiza wajibu wao, na imebakia kutimiziwa haki zao, na kubalini kutoka wafanya wema katika wao, na muwasamehe waovu katika wao. Watu wanazidi tu na Maansari wanapungua mpaka watakuwa kama chumvi katika chakula. Kisha akasema: Mja amekhiarishwa na Mwenyezi Mungu baina ya hazina za dunia na yale yaliyokuwa kwake, akahiari yale yaliyokuwa kwake. Basi aliposikia haya Abubakar alilia na kutambua kuwa siku zimeshawadia na ajali imeshafika, akasema: Tumekutolea mhanga baba zetu na mama zetu. Akasema Mtume (SAW): Polepole ewe Abubakar! Tazameni hii milango ya msikiti ambayo njia zinaelekea kwake. Ifungeni yote isipokuwa mlango unaoelekea nyumba ya Abubakar, kwani sijui mtu yeyote aliyekuwa mbora kwangu kwa usuhuba na mali yake kuliko yeye, na lau ningetaka rafiki mpenzi asiyekuwa Mola wangu, ningemfanya Abubakar kuwa rafiki mpenzi, lakini ni udugu katika Uislamu na mapenzi. Mtume (SAW) ausia: Kabla ya kufa Mtume (SAW) kwa siku tatu alitaka aletewe kitu aandike jambo ambalo hawataweza kupotea baada yake, naye alikuwa amezidiwa na maumivu siku hiyo, basi Umar akawaambia haina haja, inakutosheni Qurani, wakahitalifiana mpaka Mtume (SAW) akawaambia wende zao. Lakini akawausia wawatoe Bara Arabu Mayahudi na Manasara na Mushrikina, na kuruhusu tume kama walivyokuwa wakiziruhusu kuja, na la tatu lilikuwa ima kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mwenendo wa Mtume wake, au kulipeleka jeshi la Usama, au Sala na wale inayowamiliki mikono yao. Abubakar asalisha watu: Mtume (SAW) alikuwa akisalisha watu siku kumi na moja za maradhi yake, lakini siku nne za mwisho alikuwa anashindwa kwenda kusalisha watu na kwa hivyo alimuamrisha Abubakar kwenda kuwasalisha watu, na ilipokuwa siku ya Jumamosi alitoka Mtume (SAW) akiongozwa na watu wawili na kujiunga na jamaa akawa amekalishwa kushotoni mwa Abubakar, akawa Abubakar anasali kwa kumfuata Mtume (SAW) na watu wanamfuata Abubakar. Kisha siku ya pili yake, Mtume (SAW) akawawacha huru watumwa wake na kutoa sadaka dirhamu saba zilizombakilia na kuzigawa silaha zake kwa Waislamu. Siku ya mwisho ya maisha yake: Alfajiri ya Jumatatu, alipokuwa Abubakar anawasalisha watu, alifungua Mtume (SAW) pazia ya chumba cha Aisha akawatazama wanasali, kisha akacheka. Abubakar akadhani Mtume (SAW) anataka kuja kusali nao akarudi nyuma kujiunga na safu, na Waislamu wakababaishika na Sala yao kwa furaha ya kuwa Mtume (SAW) atakuja kusali nao, lakini aliwaashiria waendelee kisha akaingia ndani ya chumba na kuiteremsha pazia. Kufariki kwake dunia: Mtume (SAW) hakuwahi Sala nyengine baada hiyo, kwani lilipopanda jua la asubuhi na kuanza kuingia mchana alimwita Fatma binti yake na walikuwa wakeze wamemzunguka, akaja Fatma mwendo wake ukiwa kama wa babake mpaka akafika kwa babake. Mtume (SAW) akamwambia: Marhaba ewe binti yangu. Na kumkalisha karibu yake, kisha akamnongoneza neno akalia Fatma, kisha akamnongoneza jengine akacheka. Aisha akamwambia: Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuhusisha kwa siri na wewe unalia! Basi aliposimama kwenda zake, alimwambia: Niambie nini amekuambia. Akamwambia: Mimi siwezi kufichua siri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Lakini baada ya kufa, Aisha alimuuliza tena, akamwambia kuwa mara ya kwanza alimnongoneza kuwa ajali yake imefika akalia, na mara ya pili akamwambia kuwa yeye ndiye atakuwa wa kwanza katika watu wake kumfuata na kuwa atakuwa bibi wa wanawake wote wa kiislamu, akafurahi. Aidha, Mtume (SAW) aliwaita Al-Hasan na Al-Husein na kuwabusu na kuusia kheri kutokana na wao, na kuwaita wakeze na kuwausia, kisha maumivu yakazidi zaidi na kuanza kukata roho. Aisha akamchukua na kukiweka kichwa chake baina ya kifua chake na shingo yake, akatokea AbdulRahman bin Abubakar na msuwaki mkononi, akawa Mtume (SAW) anautazama, na akajua Aisha kuwa anautaka, basi akauchukuwa na kuutafuna na kuulainisha kwa meno yake kisha akampa Mtume (SAW), naye akapiga msuwaki huku akitia mkono wake kwenye chombo na kujifuta uso wake kwa maji akiwa ameegemea kwenye kifua cha Aisha. Baada ya kumaliza kupiga msuwaki, aliinua kidole chake na kutazama kwenye sakafu huku akisema: Pamoja na wale uliowaneemesha katika Manabii na wenye kupenda haki na ukweli na mashahidi na watu wema, Ewe Mola nighufirie na unirehemu, na unikutanishe na Rafiki Aliye juu, ewe Mola Rafiki Aliye juu. Akasema haya mara tatu, kisha akakata roho. "Inna lillahi wa inna ilayhi raaji'uun" إن لله وإن إليه راجعون Kwa hakika, sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye tunarudi Umar afazaika na Abubakar athibiti: Habari ya msiba huu wa kufa kwa Mtume Muhammad (SAW) ilitapakaa kote Madina na pambizoni mwake, na huzuni ikawateremkia Masahaba na kuondoa jinsi ya furaha kwenye nyoyo zao, na kila mtu akawa amefazaika na kubabaika na kumahanika. Umar bin Al-Khattab alipopata habari hii hakuweza kujimiliki nafsi yake, bali alitoa upanga wake na kufoka huku akisema: Amepelekwa kama alivyopelekwa Musa akakaa mbali na kaumu yake siku arubaini kisha akarudi. Wallahi, Mtume wa Mwenyezi Mungu atarudi na itakatwa mikono na miguu yao. Abubakar wakati huu alikuwa hayuko amekwenda As-Sunhu kwa mkewe Habiba bint Kharija bin Zayd, akatoka Salim bin Ubeyd kwenda kumpasha habari, akaja na kuingia katika nyumba ya Aisha na kuufungua uso wa Mtume (SAW), kisha akainama na kumbusu na kulia, kisha akasema: Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mkononi mwake, amekufa. Rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Umzuri namna gani hai na maiti. Ninakutolea muhanga babangu na mamangu, Mwenyezi Mungu asikukutanishie mauti mawili. Kisha Abubakar akatoka na kumtuliza Umar asisikilize, basi akamwacha na kusema baada ya kumsifu Mwenyezi Mungu: Ama baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu, yule miongoni mwenu aliyekuwa akimuabu Muhammad, basi Muhammad amekwishakufa, na yule miongoni mwenu aliyekuwa akimuabudu Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu hakika Yuhai hafi. Amesema Mwenyezi Mungu: Q.3:144 Akasema Umar: Wallahi, kama kwamba sijawahi kuisoma Aya hii katu. Wallahi, nilipomsikia Abubakar anaisoma Aya hii nilijitupa chini juu ya ardhi na kugaragara kwenye mchanga na kujua kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amekwishakufa. Mtume (SAW) azikwa: Baada ya kufa Mtume (SAW) kulitokea hitilafu baina ya Muhajirina na Maansari kuhusu nani atakayemwakilisha Mtume (SAW) katika mambo ya dola na ya Waislamu, hata wakatoa fikra Maansari kuwa awe kiongozi mmoja kutokana na Maansari na mmoja kutokana na Muhajirina, Abubakar akawabainishia kuwa Waarabu wamezowea kuongozwa na Makureshi na kwa hivyo hawatokubali mtu mwengine awaongoze, basi wakakubali. Akasimama Umar bin Al-Khattab na kumchagua Abubakar kuwa Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Muhajirina wakamkubali, na Maansari wakamkubali awe kiongozi wa Waislamu. Akasimama Abubakar na kusema: Enyi watu, Mimi nimewakilishwa juu yenu wala mimi si mbora wenu, basi nikifanya mema nisaidieni, na nikifanya ubaya ninyosheni. Ukweli ni amana, na uwongo ni khiyana, na dhaifu kwenu ni mwenye nguvu kwangu mpaka niiondoshe ila yake inshallah, na mwenye nguvu kwenu ni dhaifu kwangu mpaka niichukuwe kutoka kwake haki ya watu inshallah. Watu hawawachi Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu isipokuwa Mwenyezi Mungu atawapa idhlali, wala hakuenei machafu kati ya watu kamwe isipokuwa Mwenyezi Mungu ataieneza kwao balaa. Nitiini maadamu ninamtii Mwenyezi Mungu na Mtumewe, na nikimuasi Mwenyezi Mungu na Mtumewe, basi sina utiifu kutoka kwenu. Wakati huu wote maiti ya Mtume (SAW) ilikuwa bado juu ya godoro lake tangu Jumatatu alipokufa mpaka Jumanne ndipo alipooshwa na akaingia kumuosha bila kumvua nguo zake Al-Abbas ami yake na watoto wake wawili Al-Fadhl na Qutham ambao walikuwa wakimgeuza na Ali bin Abi Talib akimuogesha na Usama bin Zayd na Shuqraan huru wa Mtume (SAW) wanawatilia maji. Kisha wakamkafini kwa kumvesha sanda nyeupe vipande vitatu na kuweka juu ya godoro lake. Kukatokea hitilafu kuhusu wapi azikwe, akasema Abubakar: Mimi nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu akisema: Hakutolewa roho Nabii mahali isipokuwa huzikwa hapo alipotolewa roho. Basi akaitwa Abu Talha na kuchimba chini ya godoro lake, na kufanya mwanandani kwenye kaburi lake. Kisha wakaingizwa watu kumsalia. Waislamu wakaingia kumi kumi kuja kumsalia Mtume wao (SAW) kila mtu peke yake bila ya Imamu. Kwanza wakaingia jamaa zake, kisha Muhajirina kisha Maansari, kisha wanawake, kisha watoto. Watu wakaendelea kumsalia siku ile ya Jumanne mpaka ukaingia usiku wa kuamkia Jumatano na kuteremka Ali na Al-Abbas na watoto wake wawili Qutham na Al-Fadhl na kumzika. Kisha Bilal akalirushia kaburi lake maji.
|
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|