MAOMBI |
DHIKRI NA DUA
|
![]() |
|||
Maskani | Qurani | Sunna | Fiqhi | Sera | Tarehe | Dua | Masuala | Fatawa | Dunia |
Uislamu | Dua | Dua | Dua | Dua | Dua | Dua | Dua | Dua | Viungo |
Dhikri: Kumtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu:
Dhikri na dua ni vitendo viwili vinavyofuata na kutiana nguvu, kwani dhikri yenye maana ya kumtaja Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha, kumtukuza, kumtakasa, na kumsifu kwa sifa njema anazozistahiki ni mambo yanayoambatana na dua daima. Mwenyezi Mungu katika Qurani yake tukufu ametufundisha tukitaka kumuomba kwanza tumtangulizie sifa zake tukufu na kuonyesha unyenyekevu wetu kwake na kutegemea kwetu kwake katika kila jambo letu. Kisha ndio tuanze kumuomba mahitajio yetu ya kidunia na kiakhera. Mfano wa dhikri kwa ufupi ni kutaja na kusema maneno fulani kila siku ikiwa kwenye ibada au baada yake au katika munasaba mbali mbali za maisha, ili Muislamu daima awe anamtaja na kumdhukuru Mola wake mchana na usiku. Mfano wa dhikri hizi ni kama zifuatazo: 1- Kumpwekesha Mwenyezi Mungu: Hiki ndicho chanzo na asli ya Tawhidi katika Uislamu, kwani Mitume na Manabii wote wamekuja na ujumbe huu kwa wafuasi wao, nao ni kuhimiza kujua kuwa Mola wao ni Mmoja tu hana mshirika, na ujumbe huu umekusanywa katika jumla ya maneno au ibara inayosema kuwa: "Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu" (La ilaha illa llahu), na hii ina maana kuwa mwanadamu anatakikana ajikumbushe kila mara kuwa hapana anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja tu asiyekuwa na mshirika. 2- Kumtakasa Mwenyezi Mungu: Viumbe vyote mbinguni na ardhini wakiwemo Malaika, Majini, Wanadamu, Wanyama, Ndege, Samaki, Wadudu, na vyote vilivyobakia vinatakiwa vimtakase Mola wao aliowaumba na kuwapa uhai na riziki na kila wanachokihitajia. Nako kumtakasa ni kumuepusha na kumkanushia kila sifa mbaya ambayo hanayo Mola. Kwa ufupi wa maneno kiumbe kinapotamka "Subhana llahi" huwa amesema kuwa ametakasika Mola wangu na sifa hii au na jambo hili. 3- Kumsifu na kumhimidi Mwenyezi Mungu: Huku ni kumtaja Mwenyezi Mungu kwa sifa zake anazozistahiki ambazo amezitaja mwenyewe katika Kitabu chake cha mwisho (Qurani) na kumfundisha Mtumewe awafundishe wanadamu wote kwa jumla, na kwa ufupi ni kusema sifa zote njema zinamstahikia Mola wa walimwengu wote: (Alhamdulilahi rabbil a'lamin) na kutaja majina yake tisini na tisa (99) yaliyokuja kwenye Qurani na Hadithi za Mtume (SAW). 4- Kumtukuza Mwenyezi Mungu: Kumtukuza Mola ni mojawapo ya njia ya dhikri ambayo ina thawabu kubwa kwani hapana anayefaa kutukuzwa isipokuwa Yeye, na ndiye mwenye kustahiki utukufu ulimwenguni na kesho Akhera. Kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa ufupi ni kusema (Allahu Akbaru). Dua (Maombi): Dua ni kumuomba Mwenyezi Mungu kila la kheri hapa duniani na kesho Akhera. Hivi ndivyo anavyohimizwa Muislamu kufanya. Kumkusudia Mwenyezi Mungu peke yake kwa maombi yake na haja zake akiwa anatambua na anajua kuwa wa kuombwa ni Yeye peke yake si mwengine, na kwa hivyo hawezi kuelekeza maombi yake kwa kiumbe chochote mwengine akiitakidi kuwa hicho kiumbe kinaweza kumkidhia haja zake, bali amuelekee Mola wake na kumuomba akiwa na hakika kuwa kila kitu kinatoka kwake, na wote wengine ni sababu tu. Mwenyezi Mungu anatufundisha katika Qurani yake katika Sura tukufu kabisa ambayo kila Muislamu anatakiwa aisome kwenye kila Sala yake, nayo ni Suratul Fatiha kuwa Yeye tu ndiye anayestahiki kuabudiwa kwa haki, na Yeye tu ndiye anayetakwa msaada, na hivi ndivyo Muislamu anavyotakiwa awe katika maisha yake yote - asimtegemee yeyote mwengine isipokuwa Mola wake ambaye ndiye Mola wa walimwengu wote. Nchi za kiislamu
|
|