Baada ya kufariki Adam (AS), Mwenyezi Mungu aliendelea kuteremsha Wahyi kwa Manabii na Mitume wengine kuwakumbusha wanadamu kuwa Yeye ndiye Mola wao aliyewaumba na kuwaleta ulimwenguni na kuwaruzuku, na kuwazindua kuwa Iblisi ni adui wao na atafanya kila linalomkinika kuwapoteza na njia ya haki. Ujumbe huu uliendelea kuwateremkia hawa watu waliochaguliwa kuwaongoza wengine na kuwafikishia ukweli kupitia kaumu mbali mbali kama kaumu ya Nuhu, Ibrahim, Musa, Isa na wengineo.
Mtume Muhammad alikuwa wa mwisho katika mfululizo wa Manabii na Mitume hawa kupokea Wahyi na katika muda wa miaka ishirini na tatu aliteremshiwa Qurani Tukufu kwa ajili ya uwongofu wa mwanadamu wote kwa jumla kinyume na ujumbe wa Mitume iliyokuja kabla yake ambao ulikuwa ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu au kaumu fulani tu kama Wahyi alioteremshiwa Nabii Musa (Taurati), Nabii Daudi (Zaburi), na Nabii Isa (Injili) (rehema na amani ziwe juu yao).
Katika muda wa miaka 23 wakati Muhammad alipokuwa na miaka 40 mpaka alipofikia umri wa miaka 63, Qurani kwa njia ya Wahyi ilikuwa ikimteremkia Mtume (SAW) kutoka kwa Mola wake, na ujumbe huu ulikuwa umekusanya maamrisho na makatazo na maelekezo na simulizi mbali mbali za Umma zilizotangulia kwa ajili ya kuwaongoza Wanadamu duniani.
Ujumbe huu wa mwisho uliteremka kwa lugha ya Kiarabu kwa sababu Mtume Muhammad (SAW) alikuwa ni Mwarabu kama vile Taurati ilivyokuwa kwa Kiibria kwa Mtume Musa na Kiaramia kwa Mtume Isa. Hii ni kwa sababu wale watu wa mwanzo wanaopata ujumbe au risala hii waweze kufahamu madhumuni ya risala hii kutoka kwa Mola wao. Qurani imebakia mpaka leo katika lugha ile ile iliyoteremshiwa ya Kiarabu na watu wote ulimwenguni wanaisoma kwa lugha hii. Lakini wanaamrishwa watu wa mataifa na makabila mengine wajifunze Kiarabu na wafasiri hii Qurani kwa lugha zao ili waweze kufahamu zaidi maneno ya Mwenyezi Mungu.
Qurani Tukufu ndio chanzo cha mwanzo cha Sharia ya Kiislamu, na kutokana na maandishi haya, Waislamu wanajifunza kila aina ya Ibada (Sala, Saumu, Zaka na Hija), na kila aina ya Maingiliano (ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kadhalika). Chanzo cha pili cha Sharia ni Sunna za Mtume Muhammad (SAW) na tofauti baina ya Qurani na Sunnah ni kuwa Qurani ni Wahyi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu na hakuna uwezekano wa kubadilika, na Sunna ni maneno, vitendo vya Mtume Muhammad katika muda wa utume wake, na yale ambayo yamefanywa katika uhai wake bila ya yeye kuyapinga au kuyatoa makosa na yanachukuliwa kuwa ni mambo aliyoyakubali kuendelewa kufanywa.
Leo Qurani baada ya miaka ya zaidi ya elfu na kitu ni yale yale maneno na maandishi yaliyoachwa na Mtume Muhammad kwa Waislamu, nayo husomwa na kuzungumzwa na kusomeshwa na kuhubiriwa na kufasiriwa na kufanyiwa uchunguzi mbali mbali na Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na kila kukicha mambo mengi katika maisha na sayansi yanagunduliwa yakiwa yanakubaliana na yale yaliyokuwemo ndani ya hii Qurani.