S&J |
MASUALA
|
![]() |
|||
Maskani | Qurani | Sunna | Fiqhi | Sera | Tarehe | Dua | Masuala | Fatawa | Dunia |
Uislamu | Masuala | Masuala | Masuala | Masuala | Masuala | Masuala | Masuala | Masuala | Viungo |
Maisha yamejaa mambo ambayo mwanadamu hayajui uhakika wake au hukumu zake, na huwa mara nyingi humkanganya na kumbabaisha na kuhitajia mwenye kujua mambo hayo ili amtoe katika ujinga na mbabaiko huo aliokuwa nao. Hii ni kwa sababu hapana mtu anayezaliwa na elimu, na maarifa huja kidogo kidogo kwa kusikia, kuona na kujifunza mpaka afikie daraja ya kuwa mjuzi, na kwa hivyo kila binadamu anatakiwa ajifunze elimu na kuitafuta popote ilipo ili atafautiane na viumbe vyengine na kuwa ndiye kiongozi wao hapa duniani na mwakilishi wa sawa wa Mwenyezi Mungu hapa ulimwenguni. Nabii Adam (AS) baada ya kuumbwa na Mwenyezi Mungu, alimfunza kila kitu anachokihitajia katika maisha yake hapa duniani ili aweze kumwakilisha sawa sawa, na kuweza kuimarisha hii dunia vilivyo. Akaletwa ulimwenguni akiwa anajua majina ya kila kitu na Mwenyezi Mungu akamchagua kuwa ndiye Nabii wa kwanza kwa wanadamu. Kwa sababu hii, mtoto tangu anapozaliwa huanza kuuliza kila kitu ili ajue, na hii ni tabia ameumbwa nayo mwanadamu ili ajifunze na afahamu mambo yanayohusu maisha yake. Kwa hivyo, kuuliza si ujinga na anayetaka kujua mambo lazima aulize, na Mwenyezi Mungu amewapa watu elimu kwa kiasi tofauti tofauti na elimu mbali mbali ili kila mmoja amuulize mwenzake, na yule mwenye elimu na maarifa mengi afundishe wale wasiokuwa na elimu kama yeye. Pamoja na hayo, inataka ifahamike kuwa kila mtu ana upungufu na kuwa hapana mtu anajua kila kitu, kwani hii ni sifa ya Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye ndiye Mjuzi wa kila kitu, lakini wanadamu wanapishana tu kwa elimu, na yule ambaye watu wanamuona kuwa ana elimu sana, basi yuko ambaye amempita kwa elimu na ujuzi na maarifa. Mifano ya Suala na Jawabu katika Qurani: Kuna mifano mingi kwenye Qurani ambayo Mwenyezi Mungu ametuonyesha ndani ya Kitabu chake kitukufu kuhusu masuali mbali mbali ambayo mwanadamu anaweza kuuliza, na katika hayo ni kuuliza kuhusu miezi, kuhusu kilicho halali katika vitu, kuhusu kutoa na kusaidia wengine, kuhusu mayatima, kuhusu hedhi, kuhusu ulevi na kamari, kuhusu vita katika miezi mitukufu, kuhusu ghanima, kuhusu DhulQarnain, kuhusu roho, kuhusu Qiyama, na kuhusu majabali. Tukizingatia masuali haya na jawabu zake tutakuta kuwa yamekusanya kila sehemu ya maisha ya binadamu, kwani miezi kama alivyotueleza Mola ni kitu ambacho kinatunadhimia sisi maisha yetu ya kila siku ya ibada zetu na haji yetu na shughuli zetu nyingine za mwaka mzima, na suala kuhusu nini halali na nini haramu linatufahamisha yote yale ambayo tumehalalishiwa na Mola wetu, na suala kuhusu kutoa na kusaidia linatueleza namna ya kusaidia wenzetu wakiwa ni jamaa zetu au wasiokuwa jamaa zetu katika maskini na mafakiri. Kisha katika suala jengine, Mwenyezi Mungu anatufahamisha namna gani tuishi na mayatima katika sisi na njia bora ya kuwatazama na kuwafanyia wema. Aidha, anatufahamisha namna ya kuishi na wake zetu na kujiepusha nao katika hali ya uchafu na udhia wanapokuwa kwenye hedhi zao, kisha katika suala jengine anatuonya na maovu na mabaya kama ya kulewa na kucheza kamari, mambo ambayo yanamwangamiza mtu akiyashiriki, kwani ulevi unamtoa mtu katika imani na kumsahauzisha Mungu wake na watu wake na kamari humfanya apoteze wakati wake katika mchezo na kumpotezea mali yake na heshima yake na kumtetesha na wenzake. Vile vile, kwenye suala la mapigano katika miezi mitukufu, Mwenyezi Mungu anatufahamisha hukumu ya vita katika miezi hii na kuwa ni dhambi kubwa kufanya hivyo, lakini mkitokea kuhujumiwa basi hamna budi kujitetea na kujihami nafsi zenu, kwani lililokuwa kubwa zaidi kuliko kupigana katika miezi hii, ni kule kuipinga njia ya Mwenyezi Mungu na kumkataa Mola, na kwa hivyo, makafiri wakikupigeni katika miezi hii nanyi msiwawache piganeni nao. Na kuhusu ghanima (ngawira) inayopatikana katika vita, basi ni ya Mwenyezi Mungu na Mtumewe ana haki ya kuifanya atakavyo, kwa hivyo msiipiganie. Aidha, katika suala la DhulQarnain anatufahamisha kuwa kulikuwa huko nyuma umma mbali mbali na waja wa Mwenyezi Mungu waliokuja wakafanya kheri chungu nzima. Kisha Mwenyezi Mungu akataja kuhusu suala la roho na kuwa hapana mtu mwenye kujua kuhusu roho, na kuwa ni jambo lililokuwa katika elimu ya Mwenyezi Mungu tu peke yake, kama vile vile suala la Siku ya Kiyama ambayo hapana kiumbe mwenye kujua lini kitakuja ijapokuwa wakati wowote kinaweza kutokea, na kuhusu majabali ambayo Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atayapasuliapasulia mbali na kuyafanya kama usufi unaopeperuka angani, na kuwa elimu ya mambo haya yaliyofichikana anayajua yeye tu Mola wa walimwengu wote. Nchi za kiislamu
|
|